Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 20 Agosti 2026 amekutana na kuzungumza na Rais Joseph Aoun wa Lebanon. Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 20 Agosti 2026 amekutana na kuzungumza na Rais Joseph Aoun wa Lebanon.  (@Vatican Media)

Rais wa Lebanon Akutana na Papa Leo XIV Mjini Vatican: Amani ya Kudumu

Viongozi hao wamejikita zaidi katika kujadili “Mkataba wa Mfumo wa Pande Tatu” “Trilateral Framework Agreement” uliotiwa saini mjini Washington na Marekani, Israel, na Lebanon kunako tarehe 26 Juni 2026 kwa lengo la "kuleta utulivu katika mipaka ya Kusini ya Jamhuri ya Lebanon na kufikia amani ya haki na ya kudumu." Vatican inaonesha kuridhishwa kwa hatua hiyo, kwa kuelezea pia wasi wasi kuhusu changamoto zinazoendelea kujitokeza katika utekelezaji wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 20 Agosti 2026 amekutana na kuzungumza na Rais Joseph Aoun wa Lebanon ambaye baadaye, amebahatika kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo yao wamejikita zaidi katika kujadili “Mkataba wa Mfumo wa Pande Tatu” “Trilateral Framework Agreement” uliotiwa saini mjini Washington na Marekani, Israel, na Lebanon kunako tarehe 26 Juni 2026 kwa lengo la "kuleta utulivu katika mipaka ya Kusini ya Jamhuri ya Lebanon na kufikia amani ya haki na ya kudumu." Vatican inaonesha kuridhishwa kwa hatua hiyo, kwa kuelezea pia wasi wasi mkubwa kuhusu changamoto zinazoendelea kujitokeza katika utekelezaji wake na kwamba, Vatican itaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kufikia amani ya haki na ya kudumu.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa na Ujumbe wa Rais wa Lebanon
Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa na Ujumbe wa Rais wa Lebanon   (@Vatican Media)

Ofisi ya Rais wa Lebanon imetoa shukrani kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuunga mkono juhudi hizi za kuisaidia Lebanon. Hasa, imetoa wito wa kuendelea kuungwa mkono kwa madai ya Beirut ambayo yanakazia zaidi wito kwa Israel kutekeleza masharti ya huo wa Mkataba wa Mfumo wa Pande Tatu” “Trilateral Framework Agreement”  uliotiwa saini chini ya usimamizi wa Marekani tarehe 26 Juni 2026. Rais Joseph Aoun aliitaka Israel kusitisha mashambulizi ya kila siku yanayolenga raia, miundombinu, na vijiji Kusini mwa nchi hiyo, na kuondoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ili kuruhusu ujenzi mpya wa maeneo yaliyoharibiwa na hatimaye kurejea kwa watu waliokimbia makazi yao kwa hofu ya mashambulizi.

Lebanon 2026
21 Agosti 2026, 15:36