Radio Maria Tanzania imekuwa chombo cha uinjilishaji, upendo na faraja kwa miaka 30 kwa watu wa Mungu nchini Tanzania Radio Maria Tanzania imekuwa chombo cha uinjilishaji, upendo na faraja kwa miaka 30 kwa watu wa Mungu nchini Tanzania 

Kumbukizi ya Miaka 30 ya Radio Maria: Uinjilishaji, Upendo na Faraja

Radio Maria ni ushuhuda wa muujiza wa Mungu unaoonekana kupitia miaka 30 ya utume wake; msingi uliojengwa na walei. Askofu Kilaini amesema chombo hicho kilianzishwa na walei ambao walibeba jukumu la kukiendeleza kupitia michango na majitoleo yao huku wakipata mwongozo na ushirikiano kutoka kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki. Amesema mchango huo umeiwezesha Radio Maria Tanzania kuwa ni chombo cha: Uinjilishaji, upendo na faraja kwa watu wote.

Na Fredy William - DAR ES SALAAM.

Miaka 30 ya Radio Maria Tanzania imeelezwa kuwa ni ushuhuda wa uaminifu wa Mungu na nguvu ya utume unaotekelezwa kwa imani, kujitolea na mshikamano wa waamini, huku safari ya chombo hicho cha uinjilishaji ikifananishwa na punje ya haradali iliyopandwa miaka 30 iliyopita na sasa kukua na kutoa kivuli cha faraja kwa maelfu ya watu nchini. Akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha miaka 30 ya Radio Maria Tanzania, yaliyofanyika sambamba na Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni kwa Bikira Maria, Askofu Msaidizi mstaafu Method Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba, amesema safari hiyo ni alama ya namna Mungu anavyoweza kutumia jambo linaloonekana dogo kuzaa matunda makubwa katika utume na maisha ya Kanisa. Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, kaulimbiu ya maadhimisho hayo, “Uinjilishaji, Upendo na Faraja,” inaakisi kwa kina utume ambao Radio Maria Tanzania imekuwa ikiutekeleza kwa miongo mitatu, kwa kuwafikia watu katika mazingira mbalimbali ya maisha kupitia sala, Neno la Mungu, Misa Takatifu, Rozari na vipindi vinavyolenga kujenga na kuimarisha imani. Kutoka punje ya haradali hadi chombo cha uinjilishaji Askofu Kilaini ameihusisha safari ya Radio Maria Tanzania na mfano wa punje ya haradali unaopatikana katika Mafundisho ya Yesu Kristo, akieleza kuwa ingawa mbegu hiyo ni ndogo, inapoota hukua na kuwa kubwa. Amesema vivyo hivyo, Radio Maria Tanzania ilianza ikiwa na hatua ndogo, lakini kwa neema ya Mungu, uaminifu wa waamini na kujitolea kwa watu mbalimbali, imeendelea kukua na kufikia maeneo mengi ya Tanzania.

Viongozi wa Kanisa waliohudhuria Kumbukizi ya Miaka 30 ya Radio Maria
Viongozi wa Kanisa waliohudhuria Kumbukizi ya Miaka 30 ya Radio Maria

“Naitazama Radio Maria Tanzania kama punje ya haradali; punje ndogo iliyopandwa, lakini ikishaota inakuwa kubwa,” amesema Askofu Kilaini. Amesema ukuaji huo si jambo la kujisifu kwa nguvu za kibinadamu pekee, bali ni ushuhuda wa muujiza wa Mungu unaoonekana kupitia miaka 30 ya utume wa Radio Maria Tanzania. Msingi wa utume uliojengwa na Waamini walei: Akirejea historia ya Radio Maria Tanzania, Askofu Kilaini amesema chombo hicho kilianzishwa na Walei ambao walibeba jukumu la kukiendeleza kupitia michango na majitoleo yao huku wakipata mwongozo na ushirikiano kutoka kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki. Amesema mchango huo wa Walei, pamoja na ushirikiano wa viongozi wa Kanisa na watu wenye mapenzi mema, umewezesha Radio Maria Tanzania kuwa miongoni mwa vyombo muhimu vya uinjilishaji kupitia vyombo vya habari katika Bara la Afrika. Katika historia hiyo, amemtaja kwa namna ya pekee Askofu mkuu mstaafu Norbert Wendelin Mtega kama mmoja wa viongozi muhimu katika hatua za mwanzo za ujio na uanzishwaji wa Radio Maria nchini Tanzania. Askofu Kilaini amesema katika Mkutano Mkuu wa AMECEA, Askofu mkuu Mtega aliona umuhimu wa Radio Maria kuja Tanzania na kuendeleza utume wake wa uinjilishaji, hatua iliyowezesha kuanzishwa kwa utume huo nchini mwaka 1996, katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea.

Waamini walei, wafadhili na marafiki wa Radio Maria Tanzania
Waamini walei, wafadhili na marafiki wa Radio Maria Tanzania

Kwa msingi huo, amesema jina la Askofu mkuu Norbert Wendelin Mtega haliwezi kutenganishwa na historia ya Radio Maria Tanzania. “Miguu ya Mama Maria” inayofika kwa wenye maumivuAkizungumzia nafasi ya Radio Maria katika maisha ya waamini, Askofu Kilaini amesema chombo hicho kimekuwa kama miguu ya Mama Maria, inayofikisha sala, upendo na faraja kwa watu ambao wakati mwingine hawawezi kufika katika maeneo ya ibada. Amesema kupitia vipindi vyake, Radio Maria imeendelea kuwafikia wazee, wagonjwa, watu walioko majumbani, hospitalini na hata katika mazingira magumu ya maisha, ikiwapatia nafasi ya kushiriki katika Misa Takatifu, kusali Rozari, kusikiliza Neno la Mungu na kupata mafundisho mbalimbali ya imani. Kwa mtazamo wake, utume huo unaendana kwa namna ya pekee na Sherehe ya Kupalizwa Mbinguni kwa Bikira Maria, ambayo inaashiria utukufu na ushindi wa Mama wa Mungu. Amehusisha pia utume wa Radio Maria na tukio la Kana, ambako Bikira Maria aliwaelekeza watumishi kumtii Yesu, akisisitiza kwamba Radio Maria inapaswa kuendelea kuwa chombo kinachowaelekeza watu kwa Kristo. Kwa lugha ya mfano, amesema watu wenye “mitungi ya huzuni” wanaweza kupata faraja, waliokumbwa na migogoro katika familia wanaweza kupata mwanga wa upatanisho, na wale wanaobeba maumivu mbalimbali wanaweza kutiwa moyo kupitia ujumbe wa Injili unaofikishwa na Radio Maria Tanzania.

Waamini wakishangilia kumbukizi ya miaka 30 ya Radio Maria Tanzania
Waamini wakishangilia kumbukizi ya miaka 30 ya Radio Maria Tanzania

Utume unaobebwa na sadaka na majitoleo: Askofu Kilaini amesisitiza kuwa Radio Maria Tanzania imeweza kufikisha miaka 30 bila kutegemea mfumo wa matangazo ya kibiashara, bali kwa kiasi kikubwa ikiendeshwa kupitia michango na sadaka za watu wanaoamini katika utume wake. Amesema kila mchango, hata kama ni mdogo, una nafasi katika kuendeleza kazi ya uinjilishaji. Aidha, amewapongeza maelfu ya watu wanaojitolea muda, ujuzi, fedha na rasilimali mbalimbali kuhakikisha Radio Maria inaendelea kutoa vipindi kwa siku zote za juma. Amewapongeza pia Maaskofu, na Mapadre walioweka masanduku ya michango katika Parokia zao, vijana wanaoshiriki katika kuandaa vipindi pamoja na wale wote wanaotumia vipaji, karama na utaalamu wao kuendeleza utume wa Radio Maria. Kwa namna ya pekee, amewapongeza wafanyakazi wa Radio Maria Tanzania wakiongozwa na Rais wa Radio Maria Tanzania, Humphrey Kira, pamoja na viongozi na watendaji wengine waliobeba jukumu la kuhakikisha utume huo unaendelea. Pia amemtaja Padri Camilius Nikata, Mkurugenzi wa kwanza wa Radio Maria Tanzania, pamoja na Padri Dominic Mavula, C.PP.S., na wengine walioendelea kushiriki katika kuijenga taasisi hiyo.

Miaka 30 ya Radio Maria: Upyaishaji na ushiriki mkubwa zaidi
Miaka 30 ya Radio Maria: Upyaishaji na ushiriki mkubwa zaidi

Kutoka Songea hadi kufikia masafa 60. Akizungumza kuhusu matunda ya safari hiyo, Askofu Kilaini amesema Radio Maria Tanzania imeendelea kupanua wigo wake na sasa imefikia masafa takribani 60 katika Majimbo 37 ya Kanisa Katoliki nchini. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya ushuhuda wa uaminifu wa wasikilizaji, marafiki na wafadhili wa Radio Maria ambao wameendelea kuunga mkono utume wake kwa miaka yote 30. Ameeleza kuwa matarajio ya kupata leseni ya kitaifa na kuifikisha Radio Maria katika maeneo mengi zaidi ya Tanzania yanapaswa kuwa changamoto kwa waamini kuendelea kushiriki katika utume huo. Kwa kuwa Radio Maria haina mipaka ya jengo la Kanisa, amesema ujumbe wake unaweza kumfikia mtu mahali popote mgonjwa aliye hospitalini, mzee aliye nyumbani, mtu aliyeko gerezani au mtu anayepitia changamoto mbalimbali za maisha.

Fundi Mitambo wa radio Maria akiwa mitamboni
Fundi Mitambo wa radio Maria akiwa mitamboni

Miaka 30 ijayo: Wito wa kupyaisha Radio Maria Tanzania: Akigeukia miaka 30 ijayo, Askofu Kilaini amesema maadhimisho hayo hayapaswi kuishia katika kusherehekea historia iliyopita, bali yawe mwanzo wa hatua mpya ya utume. Ameweka mbele wito wa “kufanywa upya” ili Radio Maria Tanzania iendelee kuwa mbegu ya huruma, matumaini na Injili katika jamii. Amesema wale ambao wamekuwa waaminifu kwa miaka 30 kupitia sala, sadaka na misaada wanapaswa kuendelea kuwa sehemu ya safari hiyo, huku wengine wapya wakialikwa kuwa marafiki wa Radio Maria na washiriki wa utume wa kueneza Habari Njema ya Wokovu. “Tunapotazama miaka 30 ijayo, tunaitwa kufanywa upya, ili Radio Maria iendelee kuwa mbegu ya huruma, mbegu ya matumaini,” amesema. Ameongeza kuwa wito huo ni kuwawezesha watu wengi zaidi kuwa marafiki wa Radio Maria na kuwa mashuhuda wa matumaini katika maeneo yao.

Ibada ya Misa Takatifu, Kumbuzi ya Miaka 30 ya Radio Maria Tanzania
Ibada ya Misa Takatifu, Kumbuzi ya Miaka 30 ya Radio Maria Tanzania

Shukrani kwa miaka 30 na mwaliko wa kuendelea na safari: Akihitimisha ujumbe wake, Askofu Kilaini amewashukuru wote waliohusika katika safari ya miaka 30 ya Radio Maria Tanzania, akiwemo kila aliyetoa muda, maarifa, fedha, vifaa, sala na nguvu kazi katika hatua mbalimbali za utume huo. Amesema mafanikio yaliyofikiwa ni matokeo ya ushirikiano mpana wa Kanisa, Walei, Mapadre, wataalamu, vijana, wafanyakazi na marafiki wa Radio Maria. Ametoa wito kwa waamini kuendelea kuiwezesha Radio Maria Tanzania ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi na kuendeleza utume wa uinjilishaji, upendo na faraja. Akiwaunganisha waamini na maadhimisho ya Bikira Maria, Askofu Kilaini amewakabidhi wote kwa maombezi ya Mama wa Mungu, akiomba Mungu awabariki, azibariki familia zao na kazi zao, na awajalie kuendelea kuwa sehemu ya utume wa Radio Maria Tanzania. Miaka 30 ya Radio Maria Tanzania, kwa hiyo, si tu kumbukumbu ya muda uliopita; ni ushuhuda wa mbegu iliyopandwa kwa imani, ikalelewa kwa sadaka na kujitolea, na sasa inaitwa kuzaa matunda mapya kwa miaka 30 ijayo.

Radio Maria Miaka 30
17 Agosti 2026, 15:33