Kongamano la Tatu  la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika kufanyika Luanda, Angola 2028. Kongamano la Tatu la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika kufanyika Luanda, Angola 2028. 

Kongamano la Tatu la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika Kufanyika Luanda, Angola 2028

Utamadunisho wa Liturujia unapata msingi wake katika Fumbo la Umwilisho. Kama vile Neno wa milele wa Baba alivyotwaa hali halisi ya kihistoria, kitamaduni na kibinadamu, vivyo hivyo Liturujia inaitwa kudhihirisha fumbo la Kristo kupitia lugha, ishara na mitindo inayoeleweka na yenye maana kwa kila taifa. Kristo Yesu hakujifunua kwa namna ya kinadharia; badala yake, alichukua lugha, ishara, alama, utamaduni na hisia halisi za kibinadamu. Gaudium et Spes, 22.

Na Dalphina Rubyema, - Dar es Salaam na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican

Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa Katika Maadhimisho ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia Wa Afrika kuanzia tarehe 2 hadi 9 Agosti 2026 uliotolewa na Kardinali Arthur Roche Mwenyekiti wa Baraza alisema kwamba, Utamadunisho wa Liturujia unapata msingi wake hasa katika Fumbo la Umwilisho. Kama vile Neno wa milele wa Baba alivyotwaa hali halisi ya kihistoria, kitamaduni na kibinadamu, vivyo hivyo Liturujia inaitwa kudhihirisha fumbo la Kristo kupitia lugha, ishara na mitindo inayoeleweka na yenye maana kwa kila taifa. Mwana wa Mungu hakujifunua kwa namna ya kinadharia; badala yake, alichukua lugha, ishara, alama, utamaduni na hisia halisi za kibinadamu (taz. Gaudium et spes, 22). Kwa sababu hii, Liturujia, ambayo kwa njia ya Sakramenti inaendeleza kazi ya Kristo katika historia yote, haiwezi kubaki kuwa ngeni kwa maisha na tamaduni za watu. Inatumia uhalisia wa kimwili na wa kibinadamu ili kuleta uwepo wa Mungu siku hadi siku: vitu vya asili kama maji, mafuta, divai na mkate vinaunganishwa na ishara kama vile kuweka mikono na ishara ya msalaba na maneno yaliyoongozwa na Maandiko au yaliyotamkwa na Yesu Mwenyewe. Hivyo, kupitia "Ninakubatiza", "Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu", au "Ninakondolea dhambi zako", tunashiriki katika kazi ya wokovu ya Kristo. Kwa kweli, katika Liturujia “utakaso wa mwanadamu unaashiriwa na ishara zinazotambulika kwa hisia” (Sacrosanctum Concilium, 7.)

 Ibada ya Misa Takatifu Kufunga Kongamano la Pili la Kimataifa la Liturujia
Ibada ya Misa Takatifu Kufunga Kongamano la Pili la Kimataifa la Liturujia

Liturujia inahifadhi kile wanafunzi na jumuiya ya kwanza ya Wakristo walichokiona, kusikia na kupokea kutoka kwa Bwana (taz. 1 Yoh 1:1-3). Kila utamadunisho halisi lazima uanzie kwenye uzoefu huu wa kimsingi: si suala la kuunda liturujia mpya, bali ni kuruhusu fumbo lililopokelewa kutoka kwa Mitume lipate udhihirisho wa kweli katika maisha ya watu. Kwa kuzingatia tafakari hizi, inakuwa wazi kwamba utamadunisho ni mabadiliko ya kina yanayotokea karibu kwa mtindo wa "kunyonyana" (osmosis) wakati fumbo linaloadhimishwa linapokutana na utamaduni ambao hadi wakati huo ulikuwa haujalizoea. Hivyo basi, utamadunisho halisi si nyongeza tu ya nje ya vipengele vya kitamaduni na asili kwenye Liturujia, wala hauhusishi kuanzisha vipengele vipya vya sherehe au kutafsiri tu matini za kiliturujia katika lugha ya asili. Ni jambo la kina zaidi: mkutano kati ya Mungu, aliyepo kisakramenti na historia, utamaduni na "roho" hasa ya watu.

Utamadunisho wa Liturujia unapata msingi wake katika Fumbo la Umwilisho
Utamadunisho wa Liturujia unapata msingi wake katika Fumbo la Umwilisho   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV alivyokumbusha: “ni lazima kufafanua kwamba utamadunisho haulingani na kufanya tamaduni kuwa takatifu au kuzipitisha kama mfumo mkuu wa kufasiri ujumbe wa Injili, wala hauwezi kupunguzwa kuwa mlingano unaokwenda na wakati au urekebishaji wa kijuujuu tu wa ujumbe wa Kikristo, kwani hakuna utamaduni, hata uwe na thamani kiasi gani, unaoweza kulinganishwa tu na Ufunuo au kuwa kigezo cha mwisho cha imani. Kuhalalisha kila kitu kilichopo kitamaduni au kutetea vitendo, mitazamo ya ulimwengu au miundo inayopingana na Injili na utu wa mtu itakuwa ni kupuuza kwamba kila utamaduni kama ukweli wowote wa kibinadamu lazima uangazwe na kubadilishwa na neema inayotiririka kutoka katika fumbo la Pasaka la Kristo. Badala yake, utamadunisho ni mchakato unaodai na kutakasa, ambapo kwayo Injili, huku ikibaki bila kubadilika katika ukweli wake, inatambua, kupambanua na kuchukua semina Verbi [mbegu za Neno] zilizopo katika tamaduni, na wakati huohuo inatakasa na kuinua maadili yake ya kweli, ikiziweka huru kutoka kwa kile kinachofifisha au kuharibu taswira yake. Mbegu hizi za Neno, kama alama za utendaji wa awali wa Roho, zinapata katika Yesu Kristo kigezo cha ukweli na utimilifu wake.” (Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Washiriki wa "Kongamano la Kichungaji-Kitaalimungu" katika Tukio la Guadalupe, Februari 5, 2026).

Bara la Afrika Ni Eneo Muafaka la Utamadunisho
Bara la Afrika Ni Eneo Muafaka la Utamadunisho   (@Vatican Media)

Bara la Afrika Ni Eneo Muafaka la Utamadunisho: Makanisa mahalia Barani Afrika leo yanawakilisha moja wapo ya mazingira yenye matunda zaidi kwa maendeleo ya utamadunisho wa liturujia. Utajiri wa ishara wa tamaduni za Kiafrika, umuhimu wa mwili, thamani ya jamii, na hisia za matakatifu na sherehe hufanya ardhi hii kuwa muafaka kwa liturujia iliyo hai na shirikishi. Katika jumuiya nyingi za Kiafrika, maadhimisho ya kiliturujia hayaonekani kama tendo rasmi tu, bali kama tukio kamilifu linalohusisha mtu mzima: mwili, hisia, uhusiano, kumbukumbu na matumaini. Wimbo, ngoma, mdundo, ukimya na ishara za ibada ni lugha asilia ambazo kupitia hizo fumbo la Kikristo linapata udhihirisho wa kweli. Hisia hii ni zawadi ya ajabu kwa Kanisa zima, inatukumbusha kwamba ushiriki wa kimwili si jambo la pembeni: mwanadamu humwabudu Mungu kwa nafsi yake yote. Uzoefu katika nchi mbalimbali za Afrika unaonyesha kwamba utamadunisho, unapoongozwa ipasavyo, si tu unafanya liturujia kueleweka zaidi bali pia unachangia katika uinjilishaji wa kina zaidi. Unawawezesha waamini kutambua kwamba Injili sio ngeni kwa utambulisho wao bali ni utimilifu wake. Michakato ya utamadunisho inahitaji muda, kujifunza, sala, majaribio na tathmini. Haziwezi kubuniwa haraka haraka au kulazimishwa. Jumuiya zinazosali lazima zisindikizwe kwa busara na hekima ya kichungaji katika ukuaji wao wa kiroho, maendeleo ya kikanisa na kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa fumbo linaloadhimishwa.

Utamadunisho unachangia katika mchakato wa uinjilishaji
Utamadunisho unachangia katika mchakato wa uinjilishaji   (@Vatican Media)

Wanaliturujia wametakiwa kuwaandaa wataalam wa Liturujia katika ngazi na maeneo mbalimbali mijini na vijijini, ambao watawajengea waamini uelewa juu ya kile wanachotakiwa kuzingatia wakati wa adhimisho la Misa Takatifu, tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo baadhi ya maeneo wanaliturujia wamekuwa wakiwinda makosa badala ya kujenga uelewa. Rai hiyo imetolewa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, OFM.Cap wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Kufunga Maadhimisho ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia Wa Afrika liliyofanyika tarehe 9 Agosti 2026 kwenye Kanisa la Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam. Amesema, lengo la Liturujia iwe ni kuwatafutiwa waamini utakatifu badala ya kuwinda makosa ya Kiliturujia, jambo ambalo amesema, litafanikiwa endapo Wanalitujia katika nchi na majimbo husika, watandaa wataalam katika ngazi mbalimbali ili kuwa karibu na waamini na kuwaeleza wanayotakiwa kufanya wakati wa adhimisho la kiliturujia. “Daima Utakatifu wa Liturujia ubaki na paleple na mwisho wa siku, maadhimiso yake yatufikishe mbinguni... Wanaliturujia msiwinde makosa kwani lengo si kutafuta makosa... hata hivyo kuweni makini kwani kwa sasa kuna usasa mwingi ambapo vitu vinabadilishwa kila siku, hivyo ni wajibu wenu nyie waataalam kuhakikisha Kanisa linabaki kwenye utakatifu wake,” amesisitiza.

Mchakato wa utamadunisho unahitaji muda, sala, majaribio na tathmini
Mchakato wa utamadunisho unahitaji muda, sala, majaribio na tathmini   (@Vatican Media)

Mhashamu Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi amesema, Liturujia iwe kwa ajili ya kuwatafuta na kuwarudisha waliopotea, kuwafariji waliojeruhiwa na wenye mahitaji mbalimbali, lakini pia kuwafanya waamini kuwa huru kuzungumza kiroho na Mungu wao, na hasa kuwezesha waamini kurudi kwenye utamadunisho kwa kuingiza tamaduni nzuri kwenye Liturujia, bila kuingiza usasa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia. Hii ni changamoto kwa wanataalimungu kuzama zaidi katika Fumbo la Mungu, kwa kuangalia maelekeo mbalimbali ya imani ya kikristo sanjari na kutafuta lugha mpya zitakazosaidia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa na hivyo kuzamisha mizizi yake katika historia ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Taalimungu ni kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa wanataalimungu kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Ulimwenguni. Malezi na majiundo ya kitaalimungu si kwa ajili ya wateule wachache, bali ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu, kwa kuwawezesha waamini kupata nyenzo za kutangaza na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha.

Liturujia inahifadhi Mapokeo ya Kanisa
Liturujia inahifadhi Mapokeo ya Kanisa

“Yesu anajitambulisha kama Mfalme anayetumikia si kama watawala wa mataifa ambao hutawala kwa mabavu... (Mt. 20:25-26), lakini pia Mfalme anayewatafuta waliopotea na kuwarudisha kundini wale waliojeruhiwa pamoja na anawaponya wenye mahangaiko mbalimbali (Ezekieli 34:16)… Mfalme kipimo anachotudai ni upendo wa Mungu, upendo kwa jirani zetu na tutahukumiwa kulingana na vile tulivyowatendea wengine,” amesisitiza. Ameongeza “Liturujia ituwezeshe kutoka kwenye kundi la mbuzi na kuingizwa kwenye kundi la kondoo...ituweke tuwe kitu kimoja tukizingatia zetu za mahangaiko huku kila mtu akijiuliza kwamba, je, anapokuja kuabudu anastahili kuja kama alivyo kuanzia mavazi, matoleo yake. mahali upoabudia na vifaa unavyotumia?” Pia akaisistiza liturujia kupewa nafasi yake na hasa kuepuka maelezo mengi na marefu wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ambapo amesema “Liturujia haitakiwi kuwa na matangazo mengi, bali maneno machache na hata ikibidi ni iwe ya kimya kimya,” amesema. Akizungumza wakati wa Kufunga Maadhimisho ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia Wa Afrika, Mratibu wa ‘Consociation’ya Liturujia Afrika (CLA), Abate Profesa Olivier Marie Sarr, amesema suala la utamadunisho katika Liturujia kwa sasa siyo hiari bali ni suala linalotakiwa kuwekewa msisitizo na ushuhuda unatakiwa kuhusisha sala na matendo, hivyo akatoa rai kwa washiriki wa Kongamano hilo, kuwa mbegu yenye tija lakini akiweka msisitizo kwamba utamadunisho unaolengwa ni ule unalinda tunu za Kanisa Katoliki Afrika na duniani katika ujumla wake. Lakini pia akatumia nafasi hiyo kulitangaza jiji la Luanda, nchini Angola kuwa mwenyeji wa Kongamano la Tatu la Utamadunisho wa Liturujia Afrika kwa mwaka 2028 huku akiwatakia washiriki hao safari njema na maandalizi ya Kongamano lijalo na kwamba daima, Liturujia ihakisi maisha halisi kwa kuleta furaha na amani katika Kanisa na jamii kwa ujumla.

Kongamano la Tatu la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika Kuadhimishwa Angola
Kongamano la Tatu la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika Kuadhimishwa Angola

Upande wake Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, kwa niaba ya Idara ya Liturujia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, amesema Maadhimisho ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia Wa Afrika, limewapatia washiriki fursa ya kushirikishana utajiri wa mazuri yaliyomo ndani ya tamaduni mbalimbali Afrika wakisindikizwa na mada kutoka kwa wataalam wabobezi. Pia aliwashukuru wote waliochangia kwa ari na mali kufanikisha Kongamano hili, ikiwemo michango kutoka kwa Maaskofu wa majimbo mbalimbali, washiriki wenyewe lakini pia mchango mkubwa wa ukarimu na mapokezi kutoka Parokia za Kijichi na Tabata ambazo zimekuwa mwenyeji waIbada ya Misa ya Ufunguzi na Kufunga Kongamano hilo lililoratibiwa na Idara ya Liturujia TEC. Maadhimisho ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia Wa Afrika yalianza tarehe 2-8 Agosti 2026, liliwakutanisha Wanaliturujia kutoka nchi Pwani ya Pembe, Cameroon, Senegal, Togo, Nigeria, Msumbiji, Kenya, DRC, Angola, Uganda na mwenyeji Tanzania. Kongamano hilo lilifunguliwa rasmi na Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM na ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Kinshasa nchini DRC, Kardinali Fridoline Ambongo huku Askofu mkuu Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Yudda Thadeaus Ruwa’ichi OFM.Cap akiongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi iliyoadhimishwa Dominika tarehe 2 Agosti 2026 katika Kanisa la Parokia ya Epifania, Kijichi Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kongamano la Liturujia Barani Afrika

 

13 Agosti 2026, 10:17