Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Dominika tarehe 2 Agosti 2026 limezindua rasmi Kongamano la Pili la Wanaliturujia Barani Afrika : Utamadunisho! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Dominika tarehe 2 Agosti 2026 limezindua rasmi Kongamano la Pili la Wanaliturujia Barani Afrika : Utamadunisho!  (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika: Utamadunisho!

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia.

Na Fredy William, Kijichi, - Dar es Salaam

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia. Hii ni changamoto kwa wanataalimungu kuzama zaidi katika Fumbo la Mungu, kwa kuangalia maelekeo mbalimbali ya imani ya kikristo sanjari na kutafuta lugha mpya zitakazosaidia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa na hivyo kuzamisha mizizi yake katika historia ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Taalimungu ni kwa ajili ya huduma ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa wanataalimungu kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kuendeleza maisha na utume wa Kanisa Ulimwenguni. Malezi na majiundo ya kitaalimungu si kwa ajili ya wateule wachache, bali ni kwa ajili ya watu wote wa Mungu, kwa kuwawezesha waamini kupata nyenzo za kutangaza na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Dominika tarehe 2 Agosti 2026 limezindua rasmi Kongamano la Pili la Wanaliturujia Barani Afrika kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa katika Parokia ya Epifania, Kijichi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, huku Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi, OFMCap, akiwa Mwadhimishaji mkuu. Akihubiri katika Misa hiyo iliyowakutanisha washiriki kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika, Askofu mkuu Ruwa'ichi alisisitiza kuwa chini ya Kristo, Kanisa Katoliki Barani Afrika ni moja, hivyo lina wajibu wa kuthamini na kukuza tamaduni njema zilizopo ili kuendelea kuimarisha mizizi ya imani ya Kikristo Barani Afrika. Alieleza kuwa dhana ya utumadunisho wa Liturujia haipaswi kueleweka kwa kuhusishwa tu na uimbaji wa nyimbo za asili au matumizi ya ngoma, bali ni mchakato mpana unaolenga kuyatakasa na kuyainua yale yote yaliyo mema katika tamaduni za Kiafrika ili yawe njia ya kumwabudu na kumtukuza Mungu. "Bila utamadunisho, imani yetu ni bure. Hivyo tusiache nyuma utamaduni wetu, bali tuutumie vizuri kwa ajili ya kumtukuza Mungu," amesema Askofu mkuu Ruwa'ichi.

Watoto ni baraka kutoka kwa Mungu.
Watoto ni baraka kutoka kwa Mungu.   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Aidha, amewataka wataalamu wa Liturujia kutoka Mataifa mbalimbali kushirikiana katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna ambavyo Kanisa linaweza kuendelea kuhubiri Injili kwa kutumia hazina na amana ya tamaduni za Kiafrika bila kupoteza utakatifu, umoja na utambulisho wa Liturujia ya Kanisa Katoliki. Kongamano hilo linaendelea nchini Tanzania chini ya uratibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na linawakutanisha wanaliturujia kutoka Pwani ya Pembe, Cameroon, Togo, Nigeria, Msumbiji, Angola, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na mwenyeji Tanzania. Kilele cha kongamano hilo kitakuwa Agosti 8, 2026, kwa Misa Takatifu ya Hitimisho itakayoadhimishwa katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kwa kuwakutanisha wataalamu wa Liturujia kutoka sehemu mbalimbali za Afrika, kongamano hili linatarajiwa kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa Barani Afrika na kuendeleza tafakari kuhusu nafasi ya utamaduni katika kuadhimisha Liturujia kwa uaminifu kwa Mapokeo ya Kanisa na kwa manufaa ya uinjilishaji wa kizazi cha sasa. Askofu Mkuu Ruwa'ichi Awakaribisha Washiriki: Kabla ya Baraka ya mwisho, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi, OFMCap, aliwakaribisha rasmi washiriki wote wa Kongamano la Pili la Wanaliturujia Afrika kwa niaba ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Pia aliwashukuru waamini wa Parokia ya Epifania, Kijichi kwa maandalizi mazuri ya kuwapokea wageni kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika, akiwatakia washiriki wote heri na baraka za Mungu katika kipindi chote cha kongamano. "Kwa niaba ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ninawakaribisha wote katika Kongamano hili la Pili la Wanaliturujia Barani Afrika. Mwenyezi Mungu awabariki na awaongoze katika siku zote za tafakari na majadiliano yenu," alisema Askofu Mkuu Ruwa'ichi. Kongamano la Pili la Wanaliturujia Afrika linaendelea nchini Tanzania chini ya uratibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na linawakutanisha wataalamu wa Liturujia kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kwa lengo la kuimarisha tafakari kuhusu nafasi ya Liturujia katika uinjilishaji, utamadunisho na maisha ya Kanisa.

Parokia ya Epifania Mwenyeji waa Kongamano la Pili la Liturujia Afrika
Parokia ya Epifania Mwenyeji waa Kongamano la Pili la Liturujia Afrika   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu Masondole awakaribisha wanakongamano; aomba Roho Mtakatifu aongoze Kongamano la Pili la Wanaliturujia Afrika: Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki Bunda, ambaye pia Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amewakaribisha washiriki wa Kongamano la Pili la Wanaliturujia Afrika na kuwaomba waendelee kushirikiana kwa moyo wa sala, wakiongozwa na Roho Mtakatifu katika tafakari na majadiliano ya kongamano hilo. Akizungumza katika Misa Takatifu ya Ufunguzi wa Kongamano hilo iliyofanyika Agosti 2, 2026 katika Parokia ya Epifania, Kijichi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Askofu Masondole alisema moyo wake umejaa furaha kwa kuona wito wa Kanisa Barani Afrika ukiwakutanisha wataalamu wa Liturujia kutoka Mataifa mbalimbali kwa ajili ya kutafakari maisha ya Liturujia na utume wa Kanisa. Alitoa shukrani za pekee kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi, OFMCap, kwa kulipokea kongamano hilo katika Jimbo lake, huku akiwashukuru pia Maaskofu wote, viongozi wa Kanisa na washiriki kwa kujitoa kwao katika kuendeleza huduma ya Liturujia Barani Afrika. "Ujio wenu pekee ni ishara ya kujitoa katika huduma ya Liturujia na katika kulijenga Kanisa la Afrika. Namwomba Roho Mtakatifu atuongoze katika kongamano hili ili liwe na mafanikio makubwa kwa ajili ya Kanisa," alisema Askofu Masondole. Ujumbe wa Kardinali Arthur Roche: Katika tukio hilo, Askofu Masondole pia alisoma ujumbe wa Kardinali Arthur Roche, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa ambaye alieleza kuwa kongamano hilo lina umuhimu mkubwa kwa kuwa linagusa maisha ya kila Mkristo na nafasi ya utamaduni wa Afrika katika maisha ya Liturujia ya Kanisa. Katika ujumbe huo, Kardinali Roche alisisitiza kuwa Kanisa linathamini tamaduni za watu bila kupoteza uhalisia wa imani ya Kikristo, huku akieleza kuwa Liturujia hutumia lugha na alama zinazoeleweka na watu wa eneo husika ili kuwaongoza kwa Kristo. Aidha, alifafanua kuwa matumizi ya alama za Liturujia kama maji, mkate na divai yanaendelea kuwa ishara kuu zinazowaunganisha waamini wote katika fumbo la wokovu kupitia Kristo Yesu. “Ninasali kwamba kazi yenu iweze kuyasaidia zaidi na zaidi Makanisa ya Afrika kuadhimisha fumbo la Kristo kwa uaminifu kwa Mapokeo ya Kanisa na katika utajiri halisi wa tamaduni za watu wenu. Nawaombea liturujia iwe kweli mahali ambapo Neno anaendelea kukaa kati ya wanadamu na ambapo watu bado wanaweza kuona utukufu Wake.”

Utamadunisho wa Liturujia msingi wake ni Fumbo la Umwilisho
Utamadunisho wa Liturujia msingi wake ni Fumbo la Umwilisho   (@Vatican Media)

Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa Katika Maadhimisho ya Kongamano la Pili la Kimataifa la Wanaliturujia Wa Afrika Agosti 2-9, 2026: Waheshimiwa, Wapendwa Wanaliturujia wa Makanisa Barani Afrika, Wapendwa Marafiki, nina furaha kwamba mmeamua kuendelea na mikutano yenu katika mfumo wa Kongamano la Kimataifa la Wanaliturujia wa Afrika, ambalo lilianza zaidi ya miaka miwili iliyopita nchini Senegal. Tafakari yenu ya sasa juu ya utamadunisho wa liturujia itakuwa huduma muhimu kwa Kanisa, kwa kuwa inagusa kiini cha maisha ya Kikristo: kukutana na Mungu katika fumbo linaloadhimishwa ndani ya muktadha wa utajiri wa tamaduni mbalimbali za Afrika. Kujitolea kwenu ni muhimu hasa leo, wakati ambapo Kanisa linaitwa kuelewa kwa kina zaidi jinsi Injili inavyoweza kupata mwili ndani ya tamaduni za watu bila kupoteza chochote cha ukweli wake au nguvu yake ya ukombozi. Utamadunisho wa liturujia si suala la pili au la urembo tu, kwa kuwa linahusu namna halisi ambavyo Fumbo la Kristo linawafikia wanaume na wanawake wa kila taifa, lugha na utamaduni.

Liturujia kwa njia ya Sakramenti inaendelea kuwa ni kazi ya Yesu
Liturujia kwa njia ya Sakramenti inaendelea kuwa ni kazi ya Yesu   (@Vatican Media)

1. "Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu" (Yn 1:14): Utamadunisho wa liturujia unapata msingi wake hasa katika fumbo la Umwilisho. Kama vile Neno wa milele wa Baba alivyotwaa hali halisi ya kihistoria, kitamaduni na kibinadamu, vivyo hivyo Liturujia inaitwa kudhihirisha fumbo la Kristo kupitia lugha, ishara na mitindo inayoeleweka na yenye maana kwa kila taifa. Mwana wa Mungu hakujifunua kwa namna ya kinadharia; badala yake, alichukua lugha, ishara, alama, utamaduni na hisia halisi za kibinadamu (taz. Gaudium et spes, 22). Kwa sababu hii, Liturujia, ambayo kwa njia ya sakramenti inaendeleza kazi ya Kristo katika historia yote, haiwezi kubaki kuwa ngeni kwa maisha na tamaduni za watu. Inatumia uhalisia wa kimwili na wa kibinadamu ili kuleta uwepo wa Mungu siku hadi siku: vitu vya asili kama maji, mafuta, divai na mkate vinaunganishwa na ishara kama vile kuweka mikono na ishara ya msalaba na maneno yaliyoongozwa na Maandiko au yaliyotamkwa na Yesu Mwenyewe. Hivyo, kupitia "Ninakubatiza", "Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu", au "Ninakondolea dhambi zako", tunashiriki katika kazi ya wokovu ya Kristo. Kwa kweli, katika Liturujia «utakaso wa mwanadamu unaashiriwa na ishara zinazotambulika kwa hisia» (Sacrosanctum Concilium, 7.)

Naye Neno Alifanyika Mwili, akakaa kwetu, Yn 1:14
Naye Neno Alifanyika Mwili, akakaa kwetu, Yn 1:14   (ANSA)

2. "Nasi tukauona utukufu wake" (Yn 1:14): Katika utangulizi wa Injili yake, Mtume Yohane anashuhudia kwa shukrani na mshangao jinsi fumbo kuu la Umwilisho lilivyomwezesha yeye na watu wa nyakati zake kuona kwa macho yao wenyewe utukufu wa Mungu uliofunuliwa katika Yesu Kristo. Yesu Mwenyewe baadaye angesema: "Heri macho yanayoona mnayoyaona ninyi. Kwa maana ninawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie" (Lk 10:23-24). Hata hivyo, kwetu sisi tunaokuja baada ya matukio haya, baraka nyingine imetolewa: "Heri wale ambao hawajaona, lakini wameamini" (Yoh 20:29). Hatuoni Mungu kwa macho yetu wenyewe, wala hatusikii neno lake moja kwa moja kutoka kwenye midomo yake; lakini wakati huo wa pekee katika historia ya wokovu unaletwa kwetu per ritus et preces [kwa njia ya ibada na sala] (Sacrosanctum Concilium, 48). Taratibu hizi na sala zinatokana na uzoefu halisi wa wanafunzi waliomfuata Bwana, kushuhudia matendo yake, kusikia maneno yake na kushiriki katika Pasaka yake. Kwa njia hii Kanisa lilijifunza kuweka hai kumbukumbu yake, likiendelea kufuata nyayo zake hadi nyakati zetu.

Kuna Umuhimu wa Kutamadunisha Liturujia
Kuna Umuhimu wa Kutamadunisha Liturujia   (@VATICAN MEDIA)

Liturujia inahifadhi kile wanafunzi na jumuiya ya kwanza ya kikanisa walichokiona, kusikia na kupokea kutoka kwa Bwana (taz. 1 Yoh 1:1-3). Kila utamadunisho halisi lazima uanzie kwenye uzoefu huu wa kimsingi: si suala la kuunda liturujia mpya, bali ni kuruhusu fumbo lililopokelewa kutoka kwa Mitume lipate udhihirisho wa kweli katika maisha ya watu. Kwa kuzingatia tafakari hizi, inakuwa wazi kwamba utamadunisho ni mabadiliko ya kina yanayotokea karibu kwa mtindo wa "kunyonyana" (osmosis) wakati fumbo linaloadhimishwa linapokutana na utamaduni ambao hadi wakati huo ulikuwa haujalizoea. Hivyo basi, utamadunisho halisi si nyongeza tu ya nje ya vipengele vya kitamaduni na asili kwenye liturujia, wala hauhusishi kuanzisha vipengele vipya vya sherehe au kutafsiri tu matini za kiliturujia katika lugha ya asili. Ni jambo la kina zaidi: mkutano kati ya Mungu, aliyepo kikasramenti, na historia, utamaduni na "roho" hasa ya watu.

Umuhimu wa Utamadunisho na Liturujia ya Kanisa
Umuhimu wa Utamadunisho na Liturujia ya Kanisa   (@Vatican Media)

3. Ee mabadilishano ya ajabu! (O admirabile commercium!) Mabadilishano ya kimaajabu yaliyoanzishwa katika Fumbo la Umwilisho yanaendelea kuzaa matunda katika maisha ya Kanisa. Kama vile Neno wa milele wa Baba alivyochukua mwili wa kibinadamu na hivyo utamaduni halisi bila kupoteza utambulisho Wake wa kiungu, vivyo hivyo liturujia inaingia katika tamaduni za watu bila kupoteza utambulisho wake wa kikanisa na kisakramenti. Hata hivyo, mambo fulani lazima yazingatiwe. Kama Baba Mtakatifu Leo XIV alivyokumbusha: «ni lazima kufafanua kwamba utamadunisho haulingani na kufanya tamaduni kuwa takatifu au kuzipitisha kama mfumo mkuu wa kufasiri ujumbe wa Injili, wala hauwezi kupunguzwa kuwa mlingano unaokwenda na wakati au urekebishaji wa kijuujuu tu wa ujumbe wa Kikristo, kwani hakuna utamaduni, hata uwe na thamani kiasi gani, unaoweza kulinganishwa tu na Ufunuo au kuwa kigezo cha mwisho cha imani. Kuhalalisha kila kitu kilichopo kitamaduni au kutetea vitendo, mitazamo ya ulimwengu au miundo inayopingana na Injili na utu wa mtu itakuwa ni kupuuza kwamba kila utamaduni kama ukweli wowote wa kibinadamu lazima uangazwe na kubadilishwa na neema inayotiririka kutoka katika fumbo la Pasaka la Kristo. Badala yake, utamadunisho ni mchakato unaodai na kutakasa, ambapo kwayo Injili, huku ikibaki bila kubadilika katika ukweli wake, inatambua, kupambanua na kuchukua semina Verbi [mbegu za Neno] zilizopo katika tamaduni, na wakati huohuo inatakasa na kuinua maadili yake ya kweli, ikiziweka huru kutoka kwa kile kinachofifisha au kuharibu taswira yake. Mbegu hizi za Neno, kama alama za utendaji wa awali wa Roho, zinapata katika Yesu Kristo kigezo cha ukweli na utimilifu wake.» (Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Washiriki wa "Kongamano la Kichungaji-Kitaalimungu" katika Tukio la Guadalupe, Februari 5, 2026).

Utamadunisho uwasaidie waamini kuelewa Fumbo linaloadhimishwa
Utamadunisho uwasaidie waamini kuelewa Fumbo linaloadhimishwa   (@Vatican Media)

4. Kwa Ajili ya Utamadunisho wa Liturujia: Kwa kuzingatia tafakari ya kitaalimungu na uzoefu uliopatikana na Kanisa zima katika uwanja wa uinjilishaji, inawezekana kutambua baadhi ya vigezo muhimu vinavyopaswa kuongoza mchakato wa utamadunisho wa liturujia. a) Lengo la Utamadunisho: Maelekezo Varietates legitimae na. 35 yanasema kwamba, kwanza kabisa, lengo la utamadunisho lazima lieleweke wazi «ambalo ni lile lililowekwa na Mtaguso wa Pili wa Vatican kama msingi wa urejesho wa jumla wa liturujia: "Matini na ibada vinapaswa kuandaliwa kwa namna ambayo zinaeleza kwa uwazi zaidi mambo matakatifu zinayoashiria na ili watu wa Kikristo, kwa kadiri inavyowezekana, waweze kuelewa kwa urahisi na kushiriki katika ibada hizo kikamilifu, kwa utendaji na inavyostahili jumuiya." Pia, ibada zinahitaji "kurekebishwa kulingana na uwezo wa waamini na kwamba kusiwe na haja ya maelezo mengi ili zieleweke." Hata hivyo, asili ya liturujia lazima ikumbukwe daima, kama ilivyo kwa tabia ya kibiblia na mapokeo ya muundo wake na namna ya pekee inavyodhihirishwa». Hivyo basi, lengo la utamadunisho sio upekee au hamu ya kufanya liturujia ivutie zaidi tu. Lengo lake ni kwamba fumbo linaloadhimishwa liweze kuelezwa kwa uwazi zaidi na kwamba watu wa Kikristo waweze kushiriki kikamilifu, kwa utendaji na kwa pamoja kama jumuiya katika mafumbo matakatifu.

Umuhimu wa uaminifu kwa Fumbo linaloadhimishwa
Umuhimu wa uaminifu kwa Fumbo linaloadhimishwa   (@Vatican Media)

b) Uaminifu kwa Fumbo Linaloadhimishwa: Fumbo la Kristo lazima libaki kuwa kitovu na kigezo cha kila marekebisho. Njia za kitamaduni zinazopitishwa katika maadhimisho hazipaswi kuchukua nafasi au kufifisha Fumbo hili. Badala yake, zinapaswa kuwezesha kukutana na Mungu bila kubadilisha Ufunuo Wake wa mwisho, ambao umefikia utimilifu wake katika nafsi ya Yesu Kristo. Kwa sababu hii, Varietates legitimae inasema: «Mchakato wa utamadunisho unapaswa kudumisha umoja muhimu wa ibada ya Kirumi. Umoja huu kwa sasa unadhihirishwa katika matoleo ya kawaida ya vitabu vya liturujia, vilivyochapishwa kwa mamlaka ya Mapapa na katika vitabu vya liturujia vilivyoidhinishwa na mabaraza ya maaskofu kwa maeneo yao na kuthibitishwa na Kiti cha Kitume. Kazi ya utamadunisho haitabirii uundaji wa familia mpya za mapokeo ya ibada; utamadunisho unajibu mahitaji ya utamaduni fulani na kusababisha mabadiliko ambayo bado yanabaki kuwa sehemu ya mapokeo ya Kirumi» (Varietates legitimae, 36). Ni muhimu sana kukumbuka haya leo, wakati ambapo wakati mwingine kuna hatari ya kuchanganya utamadunisho na majaribio ya kiholela au ubunifu wa kufikirika—ambao wakati mwingine ni mbaya sana—bila sheria (taz. Desiderio desideravi, 48). Liturujia si mali ya kiongozi mmoja anayeadhimisha, kikundi fulani, au hisia za kitamaduni zilizotengwa. Matendo ya kiliturujia si matendo ya binafsi bali ni maadhimisho ya Kanisa lenyewe ambalo ni Sakramenti ya umoja, yaani, taifa takatifu lililokusanyika na kupangwa chini ya Maaskofu katika umoja na Papa. Kwa hivyo, matendo ya kiliturujia ni ya mwili mzima wa Kanisa na yanajidhihirisha na kuliathiri (taz. Kan. 837 §1 CIC).

Fumbo linaloadhimishwa liwe ni kigezo cha kila marekebisho
Fumbo linaloadhimishwa liwe ni kigezo cha kila marekebisho   (@Vatican Media)

c) Mwelekeo wa Kikanisa: Utamadunisho sio juhudi za kibinafsi au za mahali pekee, bali ni tendo la upendo ambalo Kanisa linalifanya kwa ajili ya Injili na tamaduni, kwa kutii amri: "Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu" (Mt 28:19). Utamadunisho unafanikishwa katika ushirika na Kanisa, katika mazungumzo na wachungaji, na mapokeo yote ya kikanisa, na waamini na pia na wataalamu wa utamaduni. «Marekebisho ya ibada ya Kirumi, hata katika uwanja wa utamadunisho, yanategemea kabisa mamlaka ya Kanisa. Mamlaka haya ni ya Kiti cha Kitume, kinachotumia haya kupitia Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa; pia ni ya, ndani ya mipaka iliyowekwa na sheria, mabaraza ya maaskofu na askofu wa jimbo. "Hakuna mtu mwingine, hata kama yeye ni kuhani, anayeweza kwa hiari yake kuongeza, kuondoa au kubadilisha chochote katika liturujia." Utamadunisho hauachwi kwa uamuzi wa kibinafsi wa waadhimishaji au kwa uamuzi wa pamoja wa kusanyiko» (Varietates legitimae, 37). Katika Hija yake ya Kitume Barani Afrika, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Leo XIV pia aliwakumbusha waamini: «lazima tuwe macho daima kuhusu aina hizo za dini za kiasili ambazo hakika ni sehemu ya mizizi ya utamaduni wenu, lakini wakati huo huo zinahatarisha kuchanganya na kuingiza mambo ya kishirikina na ya kichawi ambayo hayasaidii safari yenu ya kiroho. Bakini waaminifu kwa kile Kanisa linachofundisha, waaminini wachungaji wenu, na mwelekeze macho yenu kwa Yesu, anayejifunua katika Neno na Ekaristi» (Homilia ya Mtakatifu, Kilamba/Angola, 19 Aprili 2026). Utamadunisho wa kweli huzaliwa ndani ya Kanisa kupitia tendo la upambanuzi wa pande nyingi.

Tafakari ya Kitaalimungu na Malezi Endelevu ni muhimu
Tafakari ya Kitaalimungu na Malezi Endelevu ni muhimu

d) Tafakari ya Kitaalimungu na Malezi Endelevu: Zaidi ya yote utamadunisho unahitaji tafakari nzito na ya kina ya kitaalimungu. «Katika uchambuzi wa tendo la kiliturujia kwa minajili ya utamadunisho wake, ni muhimu kuzingatia thamani ya kimapokeo ya vipengele vya tendo na hasa asili yake ya kibiblia au ya mababa wa kanisa (patristic), kwa sababu haitoshi kutofautisha kati ya kile kinachoweza kubadilishwa na kile ambacho hakibadiliki» (Varietates legitimae, 38). Ishara za kiliturujia zina maana ya kina ya kitaalimungu ambayo haiwezi kupuuzwa. Kabla ya kujumuisha kipengele kipya, ni lazima kuelewa kikamilifu thamani ya vipengele vya ibada vilivyopo tayari katika Mapokeo ya Kirumi, tukikumbuka kwamba si kila kipengele cha kitamaduni kinaendana na imani ya Kikristo, na asili ya Fumbo linaloadhimishwa, au na miundo ya awali ya ibada. Ni lazima pia ikumbukwe kwamba marekebisho ya kiliturujia si tu tunda la uchunguzi wa kiakili. Ni zoezi la kiroho na la kikanisa la kupambanua ambalo kwa lazima linahitaji malezi endelevu kwa wale wote waliokabidhiwa jukumu la kutekeleza utamadunisho na kwa wale walioitwa kufyonza na kupokea vipengele hivi vipya katika ibada inayotolewa kwa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko, akimnukuu Romano Guardini, alisema wazi kwamba «bila malezi ya kiliturujia "basi marekebisho ya ibada na matini hayatawezesha mambo mengi"» (Desiderio desideravi, 34). Utamadunisho usiokuwa na tafakari ya kutosha ya kitaalimungu na malezi ya kiliturujia unahatarisha kupunguzwa kuwa mfululizo wa marekebisho ya kiutendaji ambayo yanaendana tu na mielekeo ya kijamii ya kisasa, ilhali unapaswa kuwa nguvu ya wokovu inayoweza kuhamasisha na kubadilisha jamii.

Bara la Afrika ni Eneo Muafaka wa Utamadunisho
Bara la Afrika ni Eneo Muafaka wa Utamadunisho   (@Vatican Media)

5. Afrika: Eneo Muafaka la Utamadunisho: Makanisa mahalia Barani Afrika leo yanawakilisha moja wapo ya mazingira yenye matunda zaidi kwa maendeleo ya utamadunisho wa liturujia. Utajiri wa ishara wa tamaduni za Kiafrika, umuhimu wa mwili, thamani ya jamii, na hisia za matakatifu na sherehe hufanya ardhi hii kuwa muafaka kwa liturujia iliyo hai na shirikishi. Katika jumuiya nyingi za Kiafrika, maadhimisho ya kiliturujia hayaonekani kama tendo rasmi tu, bali kama tukio kamilifu linalohusisha mtu mzima: mwili, hisia, uhusiano, kumbukumbu na matumaini. Wimbo, ngoma, mdundo, ukimya na ishara za ibada ni lugha asilia ambazo kupitia hizo fumbo la Kikristo linapata udhihirisho wa kweli. Hisia hii ni zawadi ya ajabu kwa Kanisa zima, inatukumbusha kwamba ushiriki wa kimwili si jambo la pembeni: mwanadamu humwabudu Mungu kwa nafsi yake yote. Uzoefu katika nchi mbalimbali za Afrika unaonyesha kwamba utamadunisho, unapoongozwa ipasavyo, si tu unafanya liturujia kueleweka zaidi bali pia unachangia katika uinjilishaji wa kina zaidi. Unawawezesha waamini kutambua kwamba Injili sio ngeni kwa utambulisho wao bali ni utimilifu wake. Michakato ya utamadunisho inahitaji muda, kujifunza, sala, majaribio na tathmini. Haziwezi kubuniwa haraka haraka au kulazimishwa. Jumuiya zinazosali lazima zisindikizwe kwa busara na hekima ya kichungaji katika ukuaji wao wa kiroho, maendeleo ya kikanisa na kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa fumbo linaloadhimishwa.

Utamadunisho unachangia katika Uinjilishaji wa kina: mtu mzima
Utamadunisho unachangia katika Uinjilishaji wa kina: mtu mzima   (Vatican Media)

Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa, katika mahubiri yake ya Noeli juu ya "mabadilishano ya ajabu," anataja pia fumbo la Kugeuka Sura: «Ili kuwasilisha kwa wanadamu yeye ambaye angeweza kuonekana na wanadamu na ambaye wanadamu wangeweza kumfuata ipasavyo, Mungu alifanyika mwanadamu. Na kisha alipokuwa akiishi kati ya wanadamu, na akiwa amesimama pamoja na mitume watatu aliowapeleka pembeni mahali pa siri, ghafla aling'aa mbele yao, akiwa na utukufu wa kiungu, ambao mitume waliokuwepo walishindwa hata kumtazama vizuri, kwa sababu ya udhaifu wa hisia zao za kibinadamu» (Sermon 371, 2). Utamadunisho halisi hufuata mwelekeo huu huo: huingia kwa unyenyekevu katika maisha ya watu na, baada ya muda, huruhusu utukufu wa Kristo kung'aa kwa uwazi zaidi. Kazi na tafakari yenu katika siku hizi zijazo ina umuhimu mkubwa. Ninawahimiza mwendelee kujifunza Maelekezo ya Varietates legitimae kwa uvumilivu na kwa kina, maana yanasalia kuwa andiko la msingi kwa kuelewa maana halisi ya utamadunisho wa liturujia. Pia ninawaalika mjifunze mifano mikuu ya kihistoria ya utamadunisho katika maisha ya Kanisa: kupita kwa Ukristo katika ulimwengu wa Kigiriki na baadaye katika ulimwengu wa Kilatini; mkutano wake na tamaduni za Amerika; na kazi ya kimisionari ya Matteo Ricci na Roberto de Nobili. Walijitahidi kuelewa kwa kina tamaduni walizokutana nazo bila kuisaliti Injili au kudhoofisha imani ya Kanisa. Mfano wao na kazi yao inaweza kuangaza njia yenu wenyewe ya utamadunisho. Ninasali kwamba kazi yenu iweze kuyasaidia zaidi na zaidi Makanisa ya Afrika kuadhimisha fumbo la Kristo kwa uaminifu kwa mapokeo ya Kanisa na katika utajiri halisi wa tamaduni za watu wenu. Nawaombea liturujia iwe kweli mahali ambapo Neno anaendelea kukaa kati ya wanadamu na ambapo watu bado wanaweza kuona utukufu Wake. Tukiwa na shukrani kwa mpango huu, tunawakabidhi ninyi nyote, washiriki wa Kongamano la Pili la Wanaliturujia wa Afrika huko Kurasini, Tanzania, kwa Bikira Maria Mbarikiwa, Malkia wa Kawekamo.

Kanisa Barani Afrika Liadhimishe Mafumbo ya Kanisa kwa uaminifu na Mapokeo
Kanisa Barani Afrika Liadhimishe Mafumbo ya Kanisa kwa uaminifu na Mapokeo

Kutoka Vatican, 29 Juni 2026

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo

Kardinali Arthur Roche

Mwenyekiti wa Baraza.

Liturujia Barani Afrika

03 Agosti 2026, 14:49