Askofu Mkuu Gallagher Anatembelea Urusi 24-28 Agosti 2026: Diplomasia ya Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu.
Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948.
Ni katika muktadha huu wa Diplomasia ya Vatican Kimataifa, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kuanzia Jumatatu tarehe 24 hadi Ijumaa tarehe 28 Agosti 2026 anafanya ziara ya kikazi nchini Urusi kwa kukutana na viongozi wakuu wa Serikali ya Urusi, baadhi ya viongozi wa Kanisa la Kiorthodox la Urusi pamoja na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Urusi. Ziara hii ya kikazi itakamilishwa kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Alhamisi tarehe 27 Agosti 2026. Lengo la ziara hii ya kikazi ni kuendelea kuragibisha majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari na diplomasia mintarafu vita kati ya Urusi na Ukraine iliyoanza kutimua vumbi mwezi Februari mwaka 2022. Kwa mara ya mwisho Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa alifanya ziara ya kikazi nchini Urusi kunako Mwezi Novemba 2021.