Sr. Alessandra Smerilli Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu “Dicasterium ad Integrale Humanum Progressum Curandum” ni chombo cha Vatican kilichoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuratibu na kuendeleza huduma za Kanisa Katoliki katika masuala ya haki, amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne tarehe 30 Juni 2026 amefanya uteuzi wa viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kumteuwa Mheshimiwa Sr. Alessandra Smerilli, kutoka Shirika la Masista Wasalesian wa Mtakatifu Yohane Bosco: “Salesian Sisters; au Daughters of Mary Help of Christians, F.M.A” kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Na kabla ya uteuzi huu, Mheshimiwa Sr. Alessandra Smerilli alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza hili na ataanza utume wake mpya tarehe1 Septemba 2026. Itakumbukwa kwamba, Mheshimiwa Sr. Alessandra Smerilli alizaliwa tarehe 14 Septemba 1974 huko Vasto, CH., Italia. Kunako Mwaka 1997 alijiunga na Shirika la Masista Wasalesian wa Mtakatifu Yohane Bosco. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu wa Kipindi cha Mpito kuanzia 26 Agosti 2021 hadi 23 Aprili 2022 alipoteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Na tarehe 30 Juni 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Leo XIV amemteuwa Kardinali Fabio Baggio, wa Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Charles Borromeo, SC., kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Mendeleo Fungamani ya Binadamu na kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani akiwa amekabidhiwa kazi maalum kama Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Juu cha “Laudato si,” mahali ambapo pametengwa maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo na elimu juu ya ikolojia fungamani ya binadamu. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Fabio Baggio, C.S., alizaliwa tarehe 15 Januari 1965 huko Bassano del Grappa, Jimbo la Vicenza, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa tarehe 11 Julai 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre katika Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Charles Borromeo. Tarehe Mosi, Januari 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Tarehe 31 Oktoba 2024 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali na kusimikwa rasmi tarehe 7 Desemba 2024. Tarehe 11 Januari 2025 akawekwa wakfu kuwa Askofu, akiwa na dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Na hatimaye, tarehe 30 Juni 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa Kardinali Fabio Baggio, C.S., kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Leo XIV amemthibitisha Monsinyo Jozef Barlaš kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Itakumbukwa kwamba, Monsinyo Jozef Barlaš alizaliwa tarehe 7 Mei 1985 huko Snina, nchini Slovakia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 19 Juni 2010 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo la Košice nchini Slovakia na kuteuliwa kuwa Afisa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 24 Novemba 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, utume anaouanza rasmi tarehe Mosi Septemba 2026.