Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: Umuhimu wa Vijana Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Fredy William, - Nairobi, Kenya.
Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) Jumatano tarehe 22 Julai 2026 umehitimisha majadiliano yaliyolenga kupembua nafasi ya vijana katika maisha na utume wa Kanisa, huku Maaskofu wakitoa wito wa kuimarisha usindikizaji wa kichungaji, uwezeshaji na uwekezaji kwa vijana katika eneo lote la AMECEA. Baada ya vipindi vya kusikiliza sauti za vijana na mawasilisho mbalimbali yaliyotolewa wakati wa Mkutano, Maaskofu walitafakari kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na kukubaliana juu ya hatua mbalimbali zitakazosaidia kuimarisha huduma kwa vijana katika Kanisa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuanzisha na kuimarisha miundo ya huduma kwa vijana katika ngazi mbalimbali za Kanisa, ili kuhakikisha vijana wanaandamana na Kanisa katika safari yao ya imani na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Aidha, Mkutano umesistizia umuhimu wa kuandaa programu za kichungaji zinazowawezesha vijana kukua kiroho, kiutu, kimaadili; kijamii na kitume.
Vilevile, Mkutano ulipendekeza kuimarishwa kwa malezi ya katekesi na ya kisakramenti kwa vijana, pamoja na kuendeleza mbinu za malezi ya rika kwa rika (peer formation) na matumizi ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo kupitia majukwaa ya kidijitali, ili kuwafikia vijana kwa njia zinazokidhi mazingira ya ulimwengu mamboleo.Maaskofu pia walmekazia umuhimu wa kuimarisha nafasi ya familia kama Kanisa dogo la nyumbani; shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha na kuvumiliana. Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu. Maaskofu wanasema familia ni shule ya kwanza ya imani na kwamba kuna haja ya kukuza na kuimarisha katekesi ya familia sanjari na kuhimiza ushiriki wa wazazi na watoto katika maisha ya kiliturujia na ya kisakramenti ya Kanisa.
Katika kutambua changamoto zinazowakabili vijana wa kizazi kipya, Mkutano ulitoa wito wa kuimarisha huduma za kichungaji zinazolenga afya ya akili, ustahimilivu na ustawi wa vijana, ili waweze kukabiliana vyema na changamoto za maisha kwa mwanga na tunu za Kiinjili. Aidha, Maaskofu walisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutambuliwa na kuaminiwa kama washiriki muhimu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na kimisionari na jamii katika ujumla wake Hivyo, walipendekeza kuendelea kuwajengea uwezo wa kiuongozi, kuwashirikisha katika michakato ya kufanya maamuzi na kuunga mkono taratibu na sera zinazokuza utawala bora, ushiriki wa vijana na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.
Sanjari na hilo, Mkutano umekazia umuhimu wa kuwajengea vijana uwezo wa kutumia vyema maendeleo makubwa ya teknolojia za mawasiliano kwa kuwaandaa kuwa wamisionari wa kidijitali (Digital Missionaries), watakaotumia majukwaa ya kidijitali kushuhudia na kuitangaza Injili kwa ubunifu, uadilifu na ufanisi. Kwa kupitia maazimio hayo, Kanisa katika ukanda wa AMECEA linaonesha dhamira ya kuendelea kuwasindikiza vijana, kuwasikiliza na kuwapa nafasi ya kuwa washiriki hai katika maisha na utume wa Kanisa na katika ujenzi wa jamii yenye matumaini, haki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Itakumbukwa kwamba, kaulimbiu inayonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961 na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan Kongwe, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.