Mwishoni mwa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, imetoa wito mzito kwa: Familia, Kanisa, serikali, viongozi wa kisiasa na wadau wote wa maendeleo . Mwishoni mwa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, imetoa wito mzito kwa: Familia, Kanisa, serikali, viongozi wa kisiasa na wadau wote wa maendeleo .  (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Mkutano Mkuu wa 21 wa Maaskofu wa AMECEA: Tamko la Maaskofu!

Mwishoni mwa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, Dominika tarehe 26 Julai 2026 AMECEA imetoa wito mzito kwa: Familia, Kanisa, serikali, viongozi wa kisiasa na wadau wote wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kushirikiana kwa dhati katika kuandamana, kuwawezesha na kuwajengea mazingira yanayowawezesha vijana kutimiza wito wao katika Kanisa na jamii kwa ujumla.

Na Fredy William, - Nairobi, Kenya

Kaulimbiu iliyonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe Dominika tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu umeadhimishwa kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA imeadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961 na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan Kongwe, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zilialikwa kushiriki kama nchi watazamaji.

Tamko la Maaskofu wa AMECEA: Vijana wapewe Kipaumbele cha pekee
Tamko la Maaskofu wa AMECEA: Vijana wapewe Kipaumbele cha pekee

Mwishoni mwa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, imetoa wito mzito kwa: Familia, Kanisa, serikali, viongozi wa kisiasa na wadau wote wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kushirikiana kwa dhati katika kuandamana, kuwawezesha na kuwajengea mazingira yanayowawezesha vijana kutimiza wito wao katika Kanisa na jamii. Tamko hilo lilitolewa Julai 26, wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ya kilele cha Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, na kusomwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Karonga nchini Malawi, Mhashamu Martin Mtumbuka, kwa niaba ya Maaskofu wa AMECEA.

Vijana ni Kanisa la Leo na Kesho yenye matumaini
Vijana ni Kanisa la Leo na Kesho yenye matumaini

Katika tamko hilo, Maaskofu wa AMECEA wanasisitiza kwamba, mustakabali wa Afrika Mashariki hauwezi kujengwa bila kuwapa vijana nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na maendeleo ya jamii. Walieleza kuwa vijana wanapaswa kuonekana si kama walengwa wa huduma pekee, bali kama washirika wa kweli katika maisha na utume wa Kanisa na katika mchakato wa ujenzi wa ustawi wa jamii. Maaskofu wanawahimiza waamini Wakatoliki kote katika nchi wanachama wa AMECEA kuwakaribisha vijana kwa moyo wa upendo na kuwapa nafasi za kushiriki katika maamuzi na uongozi wa shughuli za kitume na kichungaji. Walitoa rai kwa Parokia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo (JNNK) na miundo yote ya kijimbo kujenga mazingira yanayothamini sauti ya vijana, huku wakiendelea kuwapatia makuzi na malezi ya kina ya imani yanayojengwa juu ya Kristo Yesu na Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki.

AMECEA: Vijana ni washirika wa kweli katika maisha na utume wa Kanisa
AMECEA: Vijana ni washirika wa kweli katika maisha na utume wa Kanisa

Aidha, Maaskofu walielekeza ujumbe wao kwa Serikali na mamlaka za umma, wakizitaka kuendelea kuweka sera na mifumo inayolinda utu wa kila binadamu na kupanua fursa za elimu kwa vijana. Pia walisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira yanayowezesha ujasiriamali, ajira zenye staha, uhamaji salama na ushiriki wa vijana katika shughuli za kiraia, huku wakihimiza viongozi kuimarisha utamaduni wa mazungumzo na maridhiano kama njia ya kudumisha misingi ya haki, amani na kutatua migogoro. Kwa namna ya pekee, tamko hili liliwakumbusha viongozi wa kisiasa wajibu wao wa kuheshimu hadhi ya vijana. Maaskofu wanaeleza kwamba vijana wamekuwa wakilalamikia kutumiwa wakati wa kampeni za uchaguzi na kuachwa mara baada ya uchaguzi kukamilika. Walisisitiza kuwa mwenendo huo unapaswa kukomeshwa, wakieleza kuwa vijana hawapaswi kuwa nyenzo za kufanikisha maslahi ya kisiasa bali washirika wenye mchango wa kudumu katika ustawi na maendeleo ya taifa. Zaidi ya hayo, viongozi wa Kanisa wanawaalika wadau mbalimbali wa maendeleo, Makanisa na Madhehebu mbalimbali, viongozi wa dini, sekta binafsi pamoja na mashirika ya maendeleo kushirikiana katika kujenga mifumo madhubuti ya kichungaji, elimu, msaada wa kisaikolojia na kijamii pamoja na miundombinu ya kidijitali itakayowawezesha vijana kukua katika utu, heshima, maarifa na imani.

Vijana washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa
Vijana washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa

"Vijana ni Kanisa la leo": Katika ujumbe wao, Maaskofu wametoa msisitizo kuwa vijana si Kanisa la kesho pekee bali tayari ni Kanisa la leo. Wakirejea mafundisho ya Mtume Paulo kwa Timotheo (1 Tim. 4:12), aliyewahimiza vijana kutoruhusu mtu yeyote kuwadharau kwa sababu ya umri wao, bali wawe vielelezo katika maneno, mwenendo, upendo, imani na usafi wa maisha. Katika mwanga wa safari ya Kisinodi na Ujenzi wa Kanisa la Kimisionari, Maaskofu wa AMECEA wanawahamasisha vijana kuendelea kutembea pamoja na Kristo Yesu kama wanafunzi waliokuwa njiani kuelekea Emau; kusikiliza Neno la Mungu kwa mioyo inayowaka shauku ya Injili, kumtambua Kristo Yesu katika Ekaristi Takatifu na kisha kurejea katika jamii zao kama mashuhuda wa matumaini na Injili ya Kristo, wakitembea kwa umoja pamoja na Maaskofu na Kanisa zima. "Vijana siyo tu mustakabali wa Kanisa na jamii; tayari ni sehemu hai ya Kanisa la leo. Wanapaswa kupewa nafasi ya kushiriki, kuongoza na kujenga dunia yenye matumaini, haki na amani."

Umoja na mshikamano wa Kanisa ni muhimu sana katika utume wake.
Umoja na mshikamano wa Kanisa ni muhimu sana katika utume wake.

Wito wa kujenga kizazi cha matumaini: Wakihitimisha Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuliombea Kanisa na kushirikiana katika kuwalea na kuwawezesha vijana wa Afrika Mashariki. Walieleza kwamba kupitia ushirikiano huo, Kanisa na jamii vitaendelea kujenga madaraja ya umoja, matumaini, haki, maridhiano na utawala bora kwa ustawi, maendeleo na manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Ujumbe huo unaakisi dhamira ya AMECEA ya kuifanya huduma kwa vijana kuwa kipaumbele cha kichungaji kwa sasa na miaka ijayo, ukiwaalika vijana wenyewe kuwa wahusika wakuu katika maisha na utume wa Kanisa na katika kujenga Afrika Mashariki yenye haki, amani, mshikamano na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.

Tamko la AMECEA
27 Julai 2026, 16:00