Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri wa Kenya afungua Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, awahimiza vijana kutumia teknolojia na vipaji kujenga mustakabali wa Bara la Afrika Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri wa Kenya afungua Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, awahimiza vijana kutumia teknolojia na vipaji kujenga mustakabali wa Bara la Afrika 

Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: Hotuba ya Ufunguzi: Haki na Amani

Vijana wa Afrika Mashariki wametakiwa kuwa mabalozi wa amani, umoja na maendeleo kwa kutumia: karama na vipaji vyao; elimu na teknolojia kwa manufaa ya jamii badala ya kuruhusu migawanyiko ya kisiasa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kuwanyima mustakabali wao. Vijana wametakiwa kuwa ni vyombo na wajumbe wa Habari Njema ya Wokovu kwa kueneza ujumbe wa:haki, amani, matumaini, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu!

Na Fredy William - Nairobi, Kenya.

Vijana wa Afrika Mashariki wametakiwa kuwa mabalozi wa amani, umoja na maendeleo kwa kutumia: karama na vipaji vyao; elimu na teknolojia kwa manufaa ya jamii badala ya kuruhusu migawanyiko ya kisiasa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kuwanyima mustakabali wao. Wito huo umetolewa Jumatatu tarehe 20 Julai 2026 na Waziri Mkuu wa Mawaziri wa Jamhuri ya Kenya, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora, Mheshimiwa Wycliffe Musalia Mudavadi, alipomwakilisha Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto, katika ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA. Mkutano huu unafanyika kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Akizungumza mbele ya Maaskofu, mapadri, watawa, waamini na wajumbe kutoka nchi mbalimbali za AMECEA, Mudavadi aliwashukuru Maaskofu kwa kuandaa mkutano huo, akieleza kuwa ni heshima kubwa kwa Kenya kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu unaolenga kuimarisha umoja, amani, maisha na utume wa Kanisa katika Afrika Mashariki. Alisema Serikali ya Kenya inaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki katika kuwainua vijana kupitia elimu, mafunzo ya ujuzi na fursa mbalimbali za ajira, akibainisha kuwa uwekezaji kwa vijana ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya taifa. "Rais William Ruto anaendelea kuwekeza katika elimu, maarifa na fursa za ajira kwa vijana. Tunaamini vijana ndiyo nguvu ya sasa na ya baadaye ya taifa letu," alisema.

Maaskofu wa AMECEA wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 21
Maaskofu wa AMECEA wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa 21

Mudavadi pia aliwataka vijana wanaoshiriki mkutano huo kuwa mabalozi wa Habari Njema ya Wokovu katika nchi zao kwa kueneza ujumbe wa: Imani, matumaini, upendo, haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaojengwa juu ya kanuni maadili ya Kikristo. Aliwasihi vijana kujiepusha na siasa za chuki na vurugu, akisisitiza kuwa uchaguzi ni tukio la muda mfupi lakini amani ni msingi wa maisha ya kila siku ya wananchi. "Mnalo jukumu la kulinda demokrasia, kupinga rushwa na kujenga jamii yenye haki. Msiache tofauti za kisiasa ziwagawanye, bali wekeni mbele maslahi ya watu na nchi zenu," alisisitiza. Katika zama za maendeleo makubwa ya teknolojia, Mudavadi aliwahimiza vijana kutumia kwa busara mitandao ya kijamii na Akili Unde (Artificial Intelligence - AI), akisema vifaa hivyo vinaweza kuwa daraja la kupata elimu, ufadhili wa masomo, visa na fursa mbalimbali za maendeleo iwapo vitatumika kwa uwajibikaji. Alionya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya majukwaa ya kidijitali yanaweza kuwanyima vijana nafasi muhimu za maendeleo, hivyo akawahimiza kuyatumia kwa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na kuwajibika."Tumia mitandao ya kijamii kujijenga, kujifunza na kutafuta fursa. Usiruhusu matumizi mabaya ya teknolojia yakaharibu mustakabali wako," alisema. Aidha, alitambua mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki nchini Kenya katika sekta za elimu, afya na huduma za kijamii, akisema taasisi hizo zimeendelea kuwa nguzo muhimu katika kujenga amani, utu na maendeleo ya wananchi. Kwa namna ya pekee, aliwaomba washiriki wa mkutano kuendelea kuiombea Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili zipate amani ya kudumu, akirejea wito ambao ulitolewa mara kwa mara na Hayati Baba Mtakatifu Francisko na sasa Papa Leo XIV kuhusu Mataifa hayo.

Vijana wa kizazi kipya wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema
Vijana wa kizazi kipya wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema

Mudavadi pia aliwakumbusha vijana historia ya machafuko ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2007 yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja, wengi wao wakiwa vijana, akisema tukio hilo linaendelea kuwa fundisho kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila amani. "Hata miundombinu mizuri na uchumi imara haviwezi kuwa na thamani kama taifa halina amani. Tunawategemea vijana kuwa walinzi wa haki na amani na wajenzi wa leo na kesho iliyo bora," alisema. Akitoa ushuhuda wa maisha yake, Mudavadi alisema aliingia Bungeni akiwa na umri wa miaka 28 na kuwa Waziri wa Fedha akiwa na miaka 32, akiwahimiza vijana kuwa na maono, nidhamu na kujituma kwa sababu hakuna jambo lisilowezekana kwa mtu mwenye malengo. "Kuwa na mwelekeo, kuwa na nidhamu na usikate tamaa. Vijana wana uwezo mkubwa wa kubadili historia ya taifa na Bara letu," aliwaambia. Akihitimisha hotuba yake, Waziri Musalia Mudavadi alitangaza rasmi kufunguliwa kwa Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, huku akitoa wito kwa washiriki wote kuendelea kushirikiana katika kujenga Kanisa linalokuza: Haki, amani, mshikamano wa udugu wa kibinadamu na matumaini kwa watu wa Afrika Mashariki.

Mh. Wycliffe Musalia Mudavadi akifungua Mkutano wa 21 wa AMECEA.
Mh. Wycliffe Musalia Mudavadi akifungua Mkutano wa 21 wa AMECEA.

Vijana wa Kanisa Katoliki wametakiwa kutambua kuwa wao ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii, kwa kujenga madaraja ya upendo, haki na umoja badala ya kuta za mgawanyiko, huku wakiongozwa na nguvu ya Roho Mtakatifu katika kutangaza na kushuhudia Injili. Wito huo umetolewa na Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Dominika tarehe 19 Julai 2026. Hitimisho la mahubiri ya Kardinali Czerny yameweka msingi wa safari ya Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA kwa kuwakumbusha waamini, na hasa vijana, kuwa Mungu anaendelea kufanya mambo mapya kupitia watu wake. Wakiwa na subira, imani na uongozi wa Roho Mtakatifu, wanaalikwa kuwa chachu ya mabadiliko, wajenzi wa umoja na mashuhuda wa Injili katika Afrika ya Mashariki na duniani. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961 na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Tanzania, ikiwa na Majimbo 34, Kenya Majimbo 27; Uganda Majimbo 19, Ethiopia Majimbo 13, Zambia Majimbo 12; Malawi Majimbo 8; Sudan ya Kusini Majimbo 7, Sudan Kongwe Majimbo 9 na Eritrea Majimbo 8. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.

AMECEA 21 Hotuba ya Ufunguzi
21 Julai 2026, 09:07