Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: Kardinali Rugambwa: Mikakati ya Kichungaji: Maisha
Na Fredy William - Nairobi, Kenya
Kardinali Protase Rugambwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Katoliki Tabora, Tanzania amewataka watu wateule wa Mungu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kujenga uchungaji unaogusa maisha halisi ya watu kwa kuwa madaraja ya tumaini, upendo na uinjilishaji, wakifuata mfano wa Mtakatifu Maria Magdalena, aliyekuwa shuhuda wa kwanza wa Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Akiongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kuhitimisha Majadiliano wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) iliyoadhimishwa tarehe 22 Julai 2026 Jijini Nairobi, Kardinali Rugambwa alisema simulizi ya Mtakatifu Maria Magdalena inawakumbusha Wakristo wote kuwa kukutana na Kristo si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. "Maria Magdalena hakubaki mahali pale baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Alitumwa kwenda kuwashuhudia wengine Habari Njema. Huo ndio mwaliko ambao sisi sote tunaupokea leo tunapohitimisha majadiliano katika Mkutano Mkuu wa 21wa AMECEA," alisema Kardinali Rugambwa. Alifafanua kuwa upendo kati ya Kristo na Kanisa unaodhihirishwa katika ushuhuda wa Mtakatifu Maria Magdalena ni mfano wa upendo wa kweli unaopaswa kuwa msingi wa maisha na utume wa Kanisa, huku akisisitiza kuwa kila Mkristo aliyebatizwa amepewa wajibu wa kushiriki kikamilifu katika kazi ya uinjilishaji kama: Nabii, Mfalme na Kuhani.
Katika mahubiri yake, Kardinali Rugambwa alikumbusha kuwa Kanisa la Afrika Mashariki haliwezi kutenganisha uinjilishaji na hali halisi ya maisha ya waamini wake na kwamba, Bara la Afrika linaendelea kukabiliwa na changamoto za umaskini, ujinga, baa la njaa, maradhi; ukosefu wa maji safi na salama, ukosefu wa ajira na uhamaji wa vijana wanaolazimika kuvuka mipaka kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kwa sababu hiyo, aliwataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha uchungaji wao unakuwa karibu na watu, ukisikiliza mahitaji yao na kuwapatia tumaini linalotoka kwa Kristo Yesu. "Tunapoalikwa kujenga madaraja ya umoja na matumaini, tusisahau mateso ambayo watu wetu wanapitia kila siku. Kanisa linapaswa kuwa karibu nao kwa kuwatia moyo na kuwaongoza katika safari yao ya matumaini, imani na maisha," alisisitiza.
Akigusia nafasi ya vijana, Kardinali Rugambwa alisema changamoto wanazokutana nazo leo zinahitaji Kanisa linalowasikiliza, kuwalea na kuwaongoza kwa upendo. Alibainisha kuwa vijana wengi wanahangaika kutafuta ajira, elimu na fursa za maisha, huku wengine wakihama kutoka nchi zao kwenda mataifa mengine wakitafuta fursa na matumaini ya maisha bora. Alisisitiza kuwa jukumu la Kanisa si kutangaza Habari Njema kwa maneno pekee, bali pia kuandamana na vijana katika safari yao ya kila siku. "Leo siwezi kuzungumza kuhusu Kristo pekee bila kugusa maisha halisi ya vijana wetu. Tunapaswa kuwa karibu nao na kuwasaidia kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi" alisema. Akirejea ushuhuda wa Maria Magdalena, Kardinali Rugambwa alisema Kanisa linapaswa kuendelea kuwa daraja linalowaunganisha watu na Kristo Yesu kupitia ushuhuda wa maisha, huduma na upendo. Aliwataka Wachungaji wa AMECEA kujiuliza kwa dhati kama wanaendelea kujenga madaraja ya umoja na matumaini kwa watu waliokabidhiwa kuwahudumia. "Je, sisi kama wachungaji tunajenga madaraja kama alivyofanya Maria Magdalena? Hili ndilo swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza," alisema.
Akihitimisha mahubiri yake, Kardinali Protase Rugambwa amemwomba Roho Mtakatifu ayaimarishe Majimbo yote ya AMECEA, ili yaendelee kuwa chemchemi ya ushuhuda wa Injili kwa kujenga Kanisa linalosikiliza, linaloandamana na watu na linaloendelea kuokoa roho za watu kwa njia ya upendo na huduma. Alisisitiza kuwa mfano wa Mtakatifu Maria Magdalena ubaki kuwa chachu ya uinjilishaji mpya na wa kina katika Kanisa la Afrika Mashariki, hasa katika kipindi hiki ambacho Kanisa linaendelea kutembea katika Safari ya Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimsionari likijenga madaraja ya umoja, tumaini, haki na utawala bora. Ibada hii ya Misa Takatifu imehamasishwa na watu wa Mungu kutoka Tanzania.
Maria Magdalena ni Mtakatifu aliyesikia na kupewa dhamana ya kuwapasha ndugu zake Kristo Yesu kwamba: kweli Yesu amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena ni shuhuda na mtangazaji wa Ufufuko wa Kristo Yesu kama walivyokuwa Mitume wengine ndiyo maana Mtakatifu Thoma wa Akwino anamwita kuwa ni “Mtume wa Mitume” kwani alitangaza kile ambacho Mitume watapaswa kukitangaza na kukishuhudia hadi miisho ya dunia. Maria Magdalena ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaoganga, na kuponya; upendo unaomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ndiyo maana Kumbukumbu ya Mtakatifu Maria Magdalena imepandishwa hadhi sasa na kuwa ni Sikukuu kwa Kanisa zima. Tarehe 22 Julai ya kila mwaka sasa Kanisa linasali na kuwaombea wanawake wote walioonesha ujasiri wa pekee katika kumwamini, kumpenda na kumtangaza Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu kwa watu wa nyakati mbalimbali duniani. Kweli ni vyema na haki kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na utukufu wake ulioshuhudiwa na Kristo Yesu na kutangazwa na Mtakatifu Maria Magdalena. Akabahatika kuwa Mtume kwa Mitume wa Yesu waliokimbia mbio kwenda kushuhudia kaburi wazi, Kristo Yesu akiwa amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena alibahatika kumwona Kristo Yesu, “mubashara” yule aliyekuwa amempenda wakati wa uhai wake, akashuhudia akiteswa, kufa na kuzikwa. Akabahatika kumwabudu akiwa amefufuka kwa wafu kama anavyosimulia Mwinjili Yohane 20:1-18. Mtakatifu Maria Magdalena akawa ni shuhuda wa Injili hai, yaani Kristo Yesu, Bustani iliyokuwa chanzo cha kifo wakati wa Eva na Adamu, sasa inakuwa ni chemchemi ya maisha mapya na furaha ya Injili.
Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu ndiye kiini cha historia ya wokovu na ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Yesu. Pasaka ni siku ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni siku ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti ambao sisi nasi kwa ubatizo tunakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Pasaka ni siku ya upatanisho, ni mwanzo wa maisha mapya katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Hii ndiyo Siku iliyofanywa na Bwana, tuifurahie na kuishangilia kwani Yesu amefufuka kweli kweli! Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, Mtakatifu Maria Madgalena alipata heshima ya kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia kufufuka kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, "testis divinae misericordiae", kama Papa Gregory Mkuu anavyofafanua. Yesu Mfufuka akamwonjesha huruma na upendo wake; chemchemi ya maisha mapya, dhidi ya Eva aliyesababisha kifo. Yesu akamwambia Maria Magdalena “Non me tangere”, yaani “Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” Yn 20:17. Huu ni wito pia kwa Kanisa kuambata imani na kuendelea kuamini ubinadamu unaojionesha katika Fumbo la Mungu.
Mama Kanisa kuanzia tarehe 22 Julai 2016 anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Maria Magdalena, yaani wa Magdala (Kwa lugha ya Kigiriki Μαρία ἡ Μαγδαληνή) ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi maarufu zaidi wa Yesu wa Nazareti, hasa kutokana na sifa ya kuwa wa kwanza kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka. Rej. Mk 16:9 na Yn 20:16. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la kuipandisha kumbukumbu ya Mtakatifu Maria Magdalena kuwa ni Sikukuu ya lazima kwenye Kalenda ya Kanisa Katoliki ni kuendelea kutafakari kuhusu: wito, utu, heshima, hadhi na haki msingi za wanawake sanjari na mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo. Itakumbukwa kwamba, kaulimbiu inayonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961 na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan Kongwe, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.