Mafanikio ya Chuo Cha Katekesi Cha Mtakatifu Francisko Ksaveri, UDOM, Tanzania
Na Padre Wenceslaus Bamugasheki, C.PP.S., Jimbo kuu la Dodoma, - Dodoma.
Makatekista wameteuliwa kwa ajili ya huduma ya Katekesi, muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Kumbe, Makatekista ni sehemu muhimu sana ya wahudumu wa Kanisa wanaochangamotishwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Mama Kanisa anawashukuru Makatekista kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana hii kwa ari na moyo mkuu, daima wakiwa karibu na Familia ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, ili kukuza na kuboresha imani. Hata pale dhamana hii inapoonekana kuwa ni nzito kutokana na upungufu wa rasilimali na vitendea kazi; wanakapokabiliana na vikwazo pamoja na kinzani za maisha, watambue kwamba, kazi yao ni takatifu na kwamba Roho Mtakatifu yuko na anatenda kazi pamoja nao wakati wote wanapomtangaza Kristo Yesu na kwamba, Roho Mtakatifu anawakirimia mwanga na nguvu wanazohitaji katika utekelezaji wa utume wao! Katekesi kwa vijana na watoto ni muhimu sana katika mchakato wa kurithisha imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Makatekista wanapaswa kuwa kweli ni walimu na mashuhuda wa imani tendaji! Mama Kanisa anawaomba Mashahidi wa Uganda, wasimamizi na waombezi wa Makatekista ili kweli Makatekista waweze kuwa walimu wenye hekima, wanaoshuhudia kwa maneno na matendo ukweli angavu wa Mwenyezi Mungu na furaha ya Injili. Wawe ni mashuhuda wa utakatifu wa maisha, kwa kutoka kimasomaso kutangaza na kueneza mbegu ya Neno la Mungu; wawe na imani kwa ahadi ambazo Kristo ametoa kwa wafuasi wake, kwani watarejea kutoka katika utume wao wakiwa na kicheko cha furaha midomoni mwao na mavuno mengi.
Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Ubinadamu wa ajabu" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” Papa Leo XIV anawaasa wanadamu kuchagua kati ya kujenga mnara wa Babeli na kujenga mji wa Mungu. Mnara wa Babeli ni kielelezo cha mwanadamu aliyetawaliwa na kilema cha kiburi na kujenga ufalme wa Mungu (Yerusalemu) ni ishara ya mtu anayejitahidi kuishi fadhila ya unyenyekevu kama Kristo Yesu aliye mpole na mnyenyekevu wa moyo (Mt. 11:29). Katika Ibada ya Misa Takatifu ya mahafali iliyoadhimishwa katika Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri UDOM, Padre Felix Mushobozi C.PP.S., Katibu mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania, amewaasa hayo Makatekista waliohitimu kozi ya Katekesi kwa muda wa miaka miwili. Kwa mwaka 2026 katika Chuo cha Katekesi cha Makatifu Francisko Ksaveri UDOM wamehitimu makatekista 64 ambapo kati yao wamehitimu wanawake 28 na wanaume 36. Padre Felix Mushobozi, C.PP.S., akitafakari Injili ya Dominika ya 14 Mwaka A wa Kanisa yaani Mt. 11:25-30 amewaasa na kuwahimiza Makatekista wahitimu mafunzo ya Katekesi wawe tayari kumwiga Kristo Yesu aliye mpole na mnyenyekevu wa moyo. Wahitimu hao ni vijana wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma, UDOM ambao wanatenga muda wao wa ziada kusoma masomo hayo ya Katekesi. Kwa hakika Mungu ndiye anayeita, anaowataka na kuwatuma waende kufanya kazi katika shamba lake. Vijana hawa wa Chuo kikuu ni mwanga mpya katika Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na hasa katika matumizi ya teknolojia ya akili unde.
Padre Mushobozi akiwakumbusha wajibu wao amesema, Makatekista ni washiriki wa huduma ya kufundisha, kuongoza na kutakatifuza. Kazi hii wanaifanya pamoja na Mapadre na Maaskofu. Daima wanapaswa kujua kuwa wao wanatumwa kwa maskini na wahitaji kama Kristo Yesu alivyojishusha na kuishi kati ya maskini na pamoja nao. Wanapaswa kuwa na kipaumbele cha pekee au upendeleo wa pekee kwa maskini. Hii ni kanuni msingi ya mafundisho ya taalimungu maadili na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kumbukeni kwamba neno Katekista linatokana na neno la Kiyunani (Katechein) lenye maana ya mwangwi. Hivyo, Makatekista ni mwangwi wa mafundisho ya Kristo Yesu na daima wanapaswa kuufanya mwangwi huo usikike tena na tena maskioni mwa maskini ili waonje huruma na upendo wa Mungu. Mungu alipomuumba mwanadamu alikuwa na lengo mahsusi. Alituumba ili tumjue, tumpende na kumtumikia na mwisho tukaishi naye milele mbinguni. Kwa hiyo Makatekista wanao wajibu wa kufundisha jamii ya watu waweze kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia.
Naye Padre Wenceslaus Bamugasheki, C.PP.S., Mkurugenzi wa Katekesi Jimbo Kuu Katoliki Dodoma na Mkuu wa Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri UDOM, aliwakumbusha wahitimu kuitafakari kauli mbiu ya Chuo isemayo, “Fundisheni kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”, Mt. 28:20. Makatekista wanapaswa kufundisha mafundisho ya Kristo na Kanisa lake. Katekista daima akumbuke kwamba kama alivyo mwangwi anawajibika daima kuzingatia misingi miwili katika maisha yake ya utume yaani: “Kerygma.” Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia ni katekesi ya jinsi ambavyo Wakristo wanavyopaswa kuishi kikamilifu imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Utume wa Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Huu ni mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; kuishi upendo wa kidugu kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, ili kuleta wokovu na hivyo kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano. “Tunzeni heshima ya Kanisa kwa kufundisha ukweli uliofunuliwa na Mwenyezi Mungu. Mafundisho ya Kanisa yamejengwa katika nguzo ya: Ufunuo, Mapokeo na Mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium.” Huu ni uwezo na wajibu wa Mama Kanisa kupitia kwa Maaskofu na Baba Mtakatifu kufafanua, kulinda, na kuhifadhi ukweli wa Neno la Mungu. Mamlaka hii haiko juu ya Neno la Mungu, bali ni mtumishi wake, na hutumika kulinda waamini wasipotee katika mafundisho potofu. Katekista daima awe mlinzi wa mtoto akionesha maadili mema mbele ya jamii anayoiongoza.
Aidha, Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile ambaye naye ni mmojawapo wa wahitimu wa kozi ya Katekesi amesema, “wito huu wa kumtumikia Mungu kama Katekista hasa kwa vijana wa Chuo kikuu, vijana wauone ni wa thamani sana mbele za Mungu na jamii ya sasa. Watu wengi wanatamani wasomi wote wawe na hofu ya Mungu. Waajiri wengi wanapenda wamwajiri mtu mwaminifu. Hivyo, vijana elimu hii adhimu mliyoipata daima iwafanye muwe Mabalozi wema wa kuleta chachu nzuri kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mheshimiwa Dr. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, TMA, ambaye alikuwa mgeni maalum siku ya mahafali aliwaambia vijana kuwa elimu waliyoipata imewapa wajibu mkubwa katika jamii na Kanisa kwani sasa wanashiriki kazi ya Mungu mwenyewe. Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri kilianza mwaka 2016 kama darasa lisilo rasmi. Katika kipindi hicho vijana waliotaka kuwasaidia vijana wenzao katika kujiandaa kwa Sakramenti za Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi walifundishwa kwa muda wa majuma mawili tu ndani ya kipindi cha Pasaka wakisomea katika kigango cha Mtakatifu Yohane Mvuvi, Ndaki ya Sanaa na Sayansi Jamii. Wanachuo walikuwa wachache sana na walifundishwa na watawa na mafrateri waliokuja kwa utume katika parokia yetu. Mwaka 2020 darasa lilihamishiwa katika kigango cha Mtakatifu Maria Immakulata ndaki ya Elimu.
Makatekista wasiozidi 16 walianza masomo kwa kila siku za Jumamosi saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana wakifundishwa na Paroko na frateri aliyekuwepo kwa utume baadaye Mapadre wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu kutoka Jumuiya za mjini Dodoma walianza kuja kufundisha wakimsaidia frateri. Kwa lengo la kutaka kupanua mafunzo ya Katekesi wanafunzi walikubaliana kuendelea na mafunzo wakati wa likizo fupi ya muhula wa kwanza wa masomo. Walioshiriki mafunzo kwa muda huo walitunukiwa vyeti vilivyoonesha ushiriki wa mafunzo na mada walizosoma. Katika Programu hiyo mwitiko wa washiriki wa mafunzo ulikuwa duni kutokana na utofauti wa ratiba za mihula ya masomo hasa kwa ndaki ya Tiba, na wanachuo wengi kutamani kwenda kwao likizo.Mwaka wa masomo 2021/2022 mafunzo yaliongezeka baada ya frateri aliyekuwepo kwa muda wake wa uchungaji kuwa na bidii ya kufundisha katekesi, alitumia muda mwingi kwa siku za Jumamosi saa 3:00 hadi saa 7:00 mchana na Jumapili saa 12:00 jioni hadi saa 2:00 usiku. Hali hiyo iliwavuta waamini wengi kujiunga na mafunzo na kuongeza idadi hadi kufikia makatekista 43. Hadi wakati huo chuo chetu kilikuwa hakitambuliki rasmi nje ya Jimbo Kuu la Dodoma.
Mwaka 2022 uongozi wa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania na Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya OFM Cap wa Jimbo kuu Katoliki la Dodoma, walifanya utaratibu wa kukisajili chuo hiki. Hatimaye mnamo 31 Agosti, 2022 kilisajiriwa kama Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri –UDOM kwa namba K/036, kikiwa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Padre Wencenslaus Bamugasheki. Kwa mara ya kwanza walihitimu Makatekista 37, wanawake 10 na wanaume 27 ambao walifanya mitihani ya katekesi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Mwaka uliofuata walihitimu Makatekista 44 na mwaka 2025 walihitimu makatekista 46. Mwaka huu 2026 tunamshukuru Mungu kwa kuhitimu makatekista 64 [ke 28 na me36] ambao ndio hawa walioko hapa wakimeremeta. Mpaka sasa chuo kina jumla ya Makatekista 114[ke48 na me 66] ambao wanafundishwa na wakufunzi Mapadre 12 wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wanaohudumu katika Jimbo kuu Katoliki la Dodoma. Tunatarajia idadi ya wanaojiunga kuongezeka kwani bado tunaendelea kuhamasisha katika vigango vyetu hasa kwa mwaka wa kwanza wa masomo na wanaoendelea na masomo ambapo tunaamini kwa tukio hili la leo la kutunukiwa vyeti watahamasika zaidi kujiunga na Chuo.
Wakisoma risala kwa Mgeni Rasmi wana chuo wameelezea mafanikio walioyapata kwa kusoma kozi ya Katekesi kuwa ni pamoja na: Kuongezeka kwa wasomi ambao wamekomaa kiimani, kimaadili na kiutu na kwa sasa kufaa kutumika katika nafasi mbalimbali katika jamii na Kanisa hasa ulimwengu huu wa utandawazi. Kuongezeka kwa walimu weledi wa mafundisho ya dini kwa wanafunzi hasa wa Sakramenti kama Ubatizo, Komunio, Kipaimara na Ndoa pia Mafundisho ya wakatukumeni na waamini wote. Kufundisha dini katika shule za msingi na sekondari zilizomo ndani ya parokia yetu. Kupata wahudumu na wasimamizi wa shughuli za Kiliturujia katika vigango vya parokia yetu ya Mtakatifu Francisko Ksaveri na katika vigango vya parokia zetu tunazotoka na tunazokwenda kuishi baada ya kuhitimu Chuo kikuu. Uenezaji wa tunu msingi za Kiinjili kupitia mafunzo ya vitendo kwa makatekista wakati wa likizo ndefu, jambo ambalo limeleta mshangao na limekitangaza chuo chetu kwa watu wengi.Chuo kimezalisha walimu mahiri wa mafundisho ya dini ambao wanaweza kufundisha katika vyuo vingine vya katekesi vilivyopo au vinavyofunguliwa katika vyuo vikuu na maeneo mengine katika majimbo yetu na kupanua uwanda wa ajira. Uwepo wa Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri umewezesha kupata watu mahiri wa kuitetea imani ya Kanisa Katoliki dhidi ya mafundisho: Potofu, uongo na uzushi; si kwa malumbano ya midahalo bali kwa kutoa mafundisho sahihi hasa katika ulimwengu huu wenye mkururo mkubwa wa Kanisa. Kozi hii ya Katekesi imesaidia kuchochea miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa baadhi ya makatekista wenzetu kujiunga malezi ya seminari (kwa sasa ni Mafrateri) na wengine kufunga ndoa takatifu.