Mkutano utafanyika mjini Vatican katika kumbukizi ya miaka 10 ya kuchapishwa kwa Wosia wa Amoris Laettia. Mkutano utafanyika mjini Vatican katika kumbukizi ya miaka 10 ya kuchapishwa kwa Wosia wa Amoris Laettia.  (ANSA)

Amoris laetitia:Hati ya maandalizi ya Mkutano wa Oktoba 2026 imechapishwa!

Baraza la Kipapa la Walei,Familia na Maisha na Sekretarieti Kuu ya Sinodi kwa pamoja wamechapisha hati ya maandalizi.Ni chombo cha kuandaa na kuhuisha Mkutano ambao Papa Leo XIV aliuitisha mjini Vatican kuanzia tarehe 7 hadi 14 Oktoba 2026 pamoja na wakuu wa Makanisa Katoliki ya Mashariki na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu katika hafla ya maadhimisho ya miaka kumi ya Wosia wa Kitume wa Papa Francisko.

Vatican News

Hati ya maandalizi na mchakato wake wa kazi ya Mkutano uliotangazwa na Baba Mtakatifu Leo XIV utakaofanyika mjini Vatican kuanzia Oktoba 7 hadi 14, 2026 imetumwa kwa wakuu wa Makanisa Katoliki ya Mashariki ya Kisheria na kwa  Marais wa Mabaraza ya Maaskofu na kutangazwa Jumatatu tarehe 6 Julai 2026. Mkutano huo ulitangazwa katika Ujumbe wake wa tarehe 19 Machi 2026, wakati wa maadhimisho ya miaka kumi ya Wosia wa Kitume wa Amoris Laetitia, baada ya sinodi, uliochapishwa mnamo tarehe 19 Machi 2016, na Baba Mtakatifu Francisko, ni matunda ya safari ya miaka mitatu ya utambuzi wa kisinodi iliyojikita katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa Maalum wa Sinodi ya Maaskofu(2014) na Mkutano Mkuu wa Kawaida wa XIV wa Sinodi ya Maaskofu (2015).

Kusikilizana na Utambuzi wa Sinodi

Kwa kutambua mabadiliko yanayoendelea kuathiri familia, Papa Leo XIV alielezea nia yake ya "kuendelea, kupitia kusikilizana, na utambuzi wa sinodi kuhusu hatua za kuchukua ili kutangaza Injili kwa familia leo hii, kwa kuzingatia Amoris Laetitia na kuzingatia kile kinachotimizwa katika Makanisa mahalia." Katika kuhitimisha Mkutano Mkuu Maalum wa hivi karibuni, mnamo tarehe 27 Juni 2026, Papa Leo XIV alirudi kwenye mada ya familia: "Pale ambapo familia inaungwa mkono na kusindikizwa, shule ya mahusiano, mshikamano, na matumaini hukua; pale inapojeruhiwa au kutengwa, jamii nzima hubeba matokeo." Katika tukio hilo hilo, alitangaza kwamba familia kadhaa pia zitashiriki katika Mkutano huo, walioalikwa kushirikisha uzoefu wao: "Uwepo wao ni muhimu, lakini ninatumaini kwamba wote watakaokuja watajiandaa kwa kusikiliza kwa makini na kuleta uzoefu wa familia za Makanisa yao."

Nafasi Halisi ya Kukutana

Jijini Roma, Maaskofu kutoka ulimwenguni kote wataalikwa kujadili mada zilizoainishwa katika Safari ya Kimaadili na kusikilizana. Kisha watazindua upya, ndani ya Makanisa yao ya ndani na pamoja na familia, uhamasishaji wa pamoja wa kichungaji kwa familia, maisha ya kibinadamu, na wito wa ndoa. Kwa hivyo, ni safari ya kichungaji yenye hadhi kubwa, ambayo huweka familia katikati, si tu kama wapokeaji wa hatua ya Kanisa, bali kama watu wa utume wake, ambapo Injili hupata umbo katika mahusiano ya kila siku, chaguzi, udhaifu, na matumaini. Mkutano huo, ingawa si Mkutano wa Sinodi ya Maaskofu, utafanyika kwa mtindo wa kisinodi kwa sababu, kama Papa Leo XIV alivyoonesha mwishoni mwa  kutano Mkuu Maalum wa Makardinali, unashiriki roho ya mchakato wa utekelezaji wa Sinodi, unaojumuisha kusikiliza, kusali, na utambuzi..

Mada

Kuna mada tano muhimu zilipendekezwa kwa ajili ya tafakari ya washiriki, kabla na wakati wa mkutano:

1. Familia leo: ukweli, uzuri, na changamoto — kutambua ishara za nyakati kuanzia uzoefu wa familia na ahadi ya Kanisa leo hii.

2. Vijana na ugunduzi wa wito wa ndoa — Kuwasikiliza vijana na kuwasindikiza katika kugundua thamani ya ndoa.

3. Maisha ya Ndoa. Miaka ya Kwanza ya Ndoa: Wakati wa Kuamua — Kuwasikiliza na kuwasindikiza wanandoa katika miaka ya kwanza ya maisha ya ndoa na katika kila hatua ya maisha yao.

4. Katika magumu ya maisha: kuwasindikiza na kusaidia — Kutembea na familia katika hali ngumu.

5. Familia za Kikristo, watu wa utume wa Kanisa — Kukumbatia upendo wa wanandoa na familia kama nguvu inayosukuma utume.

Ratiba ya mada inapatikana katika tovuti ya familia:

https://www.laityfamilylife.va/ na https://www.synod.va katika lugha mbalimbali.

AMORIS LAETITIA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

06 Julai 2026, 13:00