Ratiba ya Papa na Makardinali. Ratiba ya Papa na Makardinali.  (ANSA)

Vatican yatoa ratiba ya Mkutano Mkuu wa Papa na Makardinali

Papa Leo XIV atakutana na wajumbe wa Baraza la Makardinali mnamo Juni 26-27 kwa ajili ya Mkutano Mkuu maalum unaozingatia hali ya sasa ya Kanisa na ulimwengu, kutafuta amani na utekelezaji wa Sinodi.

Vatican News

Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu ilitoa ratiba ya Mkutano maalum wa Baraza la Makardinali uliopangwa  kufanyika kuanzia Juni 26-27, kabla  ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo. Papa Leo XIV atapokutana na Makardinali, watajadili masuala muhimu kama vile migogoro inayoikumba dunia na jinsi gani Kanisa linavyopaswa kuwasiliana kupitia lugha na mitazamo ili kujenga amani na upatanisho. Huu utakuwa mkutano wa pili wa Baraza la Makardinali na Papa Leo XIV, kufuatia mkutano uliofanyika mnamo mwezi Januari 2026, ambao uliwakutanisha Makardinali wapiga kura 170 na wasio wapiga kura kutoka ulimwenguni kote.

Mwishoni mwa Mutano huo, Papa alitangaza mkutano wa  mwezi Juni, akiwaambia Makardinali kwamba: "Ninahisi na ninapata hitaji la kuweza kuwategemea." Kulingana na Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu, kazi hiyo itafuata njia ya "sinodi", pamoja na sala, ukimya, tafakari ya kibinafsi, majadiliano ya kikundi, na vikao vya jumla. Makardinali wameombwa kudumisha "siri" kuhusu kinachoendelea ukumbini na kutotoa taarifa kwa vyombo vya habari wakati wa Mkutano  ili kuhifadhi mazingira ya kubadilishana kidugu.

Vipindi vinne vya kutafakari

Washiriki watagawanywa katika vikundi 20. Makundi tisa yataundwa na Makardinali wapiga kura ambao ni Maaskofu, wakiwemo Mbalozi wa Kitume na Makardinali wapiga kura ambao wamekamilisha huduma yao kama Maaskofu. Makundi mengine kumi na moja yatajumuisha Makardinali wapiga kura wa Curia  Romana na Makardinali wasio wapiga kura. Kila kundi litakuwa na rais, ambaye atasimamia majadiliano na kuweka muda, pamoja na katibu, ambaye atakusanya michango ya maoni  na kuandika ripoti ya mwisho ya kikundi.

Mkutano utaanza Ijumaa, Juni 26, huku Misa ikifanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ikiongozwa na Papa Leo XIV. Kisha Makardinali watahamia katika Ukumbi wa Paulo VI kwa ajili ya kikao cha ufunguzi, ambacho kitaanza wimbo wa kumkaribisha Roho Mtakatifu “Veni Creator Spiritus,” hotuba ya Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la  Makardinali, na utangulizi wa Papa. Kipindi cha kwanza kitaakisi swali: “Tunaitwa kutangaza Injili katika ulimwengu wa aina gani?” Kardinali Grzegorz Ryś, Askofu Mkuu wa Krakow, atatoa tafakari ya kibiblia, ikifuatiwa na ukimya, sala, kushirikishana kwa vikundi, na ripoti katika kikao cha jumla.

Siku ya Ijumaa alasiri, kikao cha pili kitaakisi mada "Utamaduni wa nguvu na ustaarabu wa upendo." Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa  Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ataakisi mada hiyo, akitoa Sura ya V ya Magnifica humanitas, waraka wa Baba Mtakatifu uliochapishwa hivi karibuni.

Kujenga manufaa ya wote

Jumamosi 27 Juni  asubuhi, baada ya Misa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro itakayoongozwa  na Kardinali Re, Makardinali wataanza tena kazi yao katika Ukumbi wa Paulo VI. Kikao cha tatu, chenye mada "Kujenga katika Mema: maeneo ya kazi ya wakati wetu," kitatambulishwa na Kardinali Stephen Brislin, Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Johannesburg na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Kusini. Majadiliano yatazingatia mipasuko inayofanya iwe vigumu kujenga manufaa ya wote, maswali yanayoibuka kutoka kwa watu na jumuiya, na msaada ambao Makanisa mahalia pamoja na Kanisa la Ulimwengu wote wanaweza kutoa.

Kikao cha nne na cha mwisho kitafanyika Jumamosi alasiri katika Ukumbi Mpya wa Sinodi na kitajikita na "Njia ya kutekeleza Sinodi." Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sinodi, ya Maaskofu atatambulisha mada, kuanzia waraka Kuelekea Mikutano ya Sinodi 2027-2028: Hatua, Vigezo, na Vyombo vya Maandalizi. Kikao hicho kitajumuisha maswali ya ufafanuzi, mazungumzo na Papa Leo XIV, na uingiliaji kati utaruhusiwa usiozidi dakika tatu.

Hotuba ya kuhitimisha ya Papa itamaliza Mkutano huo wa Makardinali, ikifuatiwa na uimbaji wa Shukrani kwa Mungu uitwao Te Deum na chakula cha jioni na Papa Leo XIV katika Ukumbi wa Paulo VI. Siku ya Jumatatu, tarehe 29 Juni, Papa Leo XIV ataongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa Maadhimisho ya Sherehe ya Mitume Mtakatifu Petro na Paulo.

Papa na Makardinali mjini Vatican

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here.

23 Juni 2026, 15:51