Tafakari Dominika ya 13 Mwaka A wa kanisa: Ukarimu ni amana na tunu: Tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, Maandiko Matakatifu yamesheheni ujumbe unao akisi ukarimu wa Mungu. Tafakari Dominika ya 13 Mwaka A wa kanisa: Ukarimu ni amana na tunu: Tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, Maandiko Matakatifu yamesheheni ujumbe unao akisi ukarimu wa Mungu.   (@VATICAN MEDIA)

Tafakari Dominika 13 Mwaka A: Ukarimu Ni Hazina na Amana ya Maisha ya Kiroho

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa, inatupatia nafasi ya pekee kutafakari juu ya ukarimu kama hazina na amana ya maisha ya kiroho na kiutu, ndiyo moja ya fadhila za kikristu. Kama ilivyo kwa wema na huruma zilizo sifa za Mungu, ukarimu pia humtambulisha Mungu kwa watu wake. Kwa asili, ukarimu ni tabia njema ya kupokea, kuheshimu, na kuwahudumia wageni kwa moyo mkunjufu, bila uchoyo na ubinafsi.

Na Padre Octavian O. Hinju, CP. Jordan University College, Morogoro Tz.

Damu Azizi ya Yesu ni Ishara na kielelezo cha ukarimu wa kimungu unao fumbatwa katika Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristu Msulubiwa. Damu Azizi ya Yesu inatusaidia kuishi kiini cha Ekaristi Takatifu iliyo halisi ya uwepo wa Mungu miongoni mwa watu wake akiendelea kutuonesha ukarimu wake wa ajabu. Ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kuonesha ukarimu wa kimungu hasa kwa watu maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Ukarimu ni tunu! Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka A wa Kanisa, inatupatia nafasi ya pekee kutafakari juu ya ukarimu kama hazina na amana ya maisha ya kiroho na kiutu, ndiyo moja ya fadhila za kikristu. Kama ilivyo kwa wema na huruma zilizo sifa za Mungu, ukarimu pia humtambulisha Mungu kwa watu wake. Kwa asili, ukarimu ni tabia njema ya kupokea, kuheshimu, na kuwahudumia wageni au watu wengine kwa moyo mkunjufu na bila ubinafsi. Huambatana na kutoa msaada kama vile chakula, malazi, au muda kwa wahitaji na kuwajali majirani. Tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, Maandiko Matakatifu yamesheheni ujumbe unao akisi ukarimu wa Mungu.

Ukarimu wa Mwenyezi mungu unajionesha kwenye kazi ya uumbaji
Ukarimu wa Mwenyezi mungu unajionesha kwenye kazi ya uumbaji   (© Vatican News)

Katika tendo la ajabu la uumbaji, Mwenyezi Mungu kwa ukarimu mkubwa alikubali kujifananisha nasi kwa jinsi iliyo ya ajabu na ya kupendeza, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo (Mwz. 1:26). Katika shida kwa ukarimu mkubwa Mungu aliendelea kuwa bega kwa bega na watu wake, “Katika shida yangu nalimwita BWANA; BWANA akanijibu akaniweka panapo nafasi. BWANA yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? BWANA yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. Ni heri kumkimbilia BWANA Kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia BWANA. Kuliko kuwatumainia wakuu” (Zab. 118:5-9). Palipo na changamoto, Mungu alisimama na watu wake ili kuwaokoa, “Musa akawajibu Waisraeli, Msiogope. Simameni imara, nanyi mtauona wokovu Bwana atakaowapatia leo. Hao Wamisri mnaowaona leo kamwe hamtawaona tena. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mnatakiwa kutulia tu” (Kut. 14:13-14). Katika njaa Mungu aliendelea kuwalisha watu wake na manabii wake, Katika 1 Wafalme 19:7, tunaona Malaika wa Mwenyezi-Mungu akimtokea Nabii Eliya kwa mara ya pili alipokuwa amechoka sana na kukata tamaa jangwani. Malaika akamgusa na kumwambia: ‘Inuka ule, kwa kuwa safari hii ni ndefu mno kwako.’

Ukarimu kwa wageni ni ndoana ya rehema na neema ya Mungu
Ukarimu kwa wageni ni ndoana ya rehema na neema ya Mungu   (ANSA)

Na katika Agano Jipya Mungu alidhihisha tendo la ukarimu kwa njia ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo, ‘Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele (Yoh. 3:16). Kumbe ukarimu ni tendo la moyo lenye kumsukuma mtu kutojifikiria yeye mwenyewe bali mahitaji ya watu wengine. Katika Ekaristi Takatifu, Kristu Yesu anaendeleza tendo hili akituita na kutuagiza sisi nasi Kutenda vivyo hivyo, kwani Ekaristi Takatifu ni ndiyo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa na maisha ya Mkristo kwa jumla. (Rej. KKK, 1324). Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa imani yetu na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. (Rej. Rej KKK, 1327).Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Pili cha Wafalme (2 Fal. 4:8-11, 14-16a). Somo hili linatuonesha ukarimu ambao alitendewa Nabii Elisha kwa sababu tu ni mtumishi wa Mungu. Elisha alikuwa akipita mara kwa mara katika mji wa Shunemu, akitokea kwake kuelekea kule ambako Mungu alimtuma kwenda kufanya unabii. Katika moyo wa ukarimu, mama mmoja wa mji huo anamkaribisha awe anapitia katika nyumba yao ili kumpunguzia mwendo na adha za safari kulingana na mazingira ya wakati huo. Itakumbukwa kuwa nyakati hizi safari za kinabii zilifanyika kwa miguu tena katika mazingira magumu na hatarishi sana. Pasi na kujua mipango ya Mungu kwake na familia yake, Kwa mama yule tendo hilo liligeuka kuwa chanzo na neema na baraka.  Yeye na mumewe hawakuwa na mtoto, Elisha alimtabiria kupata mtoto na kweli mwaka uliofuata akajaliwa baraka hiyo aliyokuwa anaingoja kwa miaka mingi.

Familia ni shule ya upendo, ukarimu na mshikamano
Familia ni shule ya upendo, ukarimu na mshikamano   (@Vatican Media)

Tendo hili lina shabihiana na ukarimu wa Abrahamu kwa wageni ambao katika kuondoka walimtakia baraka ya Mungu kuwa mkewe atapata mtoto (Mwz. 18). Kumbe, somo hili linatoa fundisho kuwa ukarimu ni hazina inayogusa moyo wa Mungu. tukishirikiana na mtu wa Mungu tunapata baraka, mfano wa yule mwanamke Mshumeni aliyemlisha Nabii Elisha. Baada ya kuonja ukarimu, ni mwaliko wa kushukuru kama alivyofanya Nabii Elisha ambaye kama tone la shukrani alimwagulia mama yule kuwa atapata mtoto ingawa yeye na bwana wake walikuwa wazee. Sisi nasi kama waamini wabatizwa tusiache kutenda kwa ukaribu kwani Mungu hutujia kwa njia na namna tusizo zijua na ambazo ni ngeni machoni petu. Pia tunaalikwa kuruka viunzi vya desturi zetu za kupenda kuwatendea ukarimu wale tu tunao wafahamu tukitarajia pengine nasi tutatendewa vivyo hivyo. Ukarimu wa kimungu ni kugusa maisha ya watu wengine bila kujali tutapata nini kama malipo ya ukarimu wetu. Kumbe tukiuishi ukarimu basi tutafurahia wema nafadhili za Mungu katika maiha yetu ya kila siku kama anavyo Sali mzaburi akisema hivi, “Fadhili za BWANA nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako, (Zab. 89:1-2).

Sakramenti ya Ubatizo: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu
Sakramenti ya Ubatizo: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 6:3-4, 8-11). Somo letu la pili siku hii ya leo, linaeleza kinaganaga maana ya msingi kabisa ya Sakramenti ya Ubatizo. Tunafahamu kuwa ubatizo ni Sakramenti ya mwanzo wa maisha ya kiroho kwa mkristu. Ni Sakramenti inayomwondolea mbatizwa dhambi ya asili na kumrudishia utukufu wa kuwa mwana wa Mungu, utukufu ambao ulipotezwa kwa dhambi ya asili yaani dhambi ya Adamu na Eva. Katika somo la leo, mtume Paulo anaongeza kuwa anayebatizwa anazamishwa katika kifo cha Kristo na anainuliwa pamoja naye katika ufufuko wake. Kwa lugha na maana nyingine, Paulo anasema kuwa kwa sakramenti ya ubatizo, yule anayebatizwa anaunganishwa na fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Mkristu anapozamishwa katika maji au anapomwagiwa maji ya ubatizo anakufa, si katika mwili bali katika dhambi. Ili kama vile ambavyo kifo cha Kristo kiliishinda dhambi basi na yeye kwa nguvu ya sakramenti ya ubatizo anatangaziwa ushindi dhidi ya dhambi. Muumini anapozamishwa au anapomwagiwa maji anafufuka. Ili kama Kristo alipofufuka katika mwili, mbatizwa afufuke katika maisha mapya. Katika ubatizo tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo kwa sababu tunahakikishiwa ushindi dhidi ya dhambi na tunazaliwa katika maisha mapya. Na hii ndiyo inayotangaza hadhi mpya tunayoipata kwa njia ya ubatizo. Ni kwa tendo la ubatizo mbatizwa anapewa dhima tatu za msingi yaani ukuhani, ufalme na unabii (Rej. CIC, 204-208) ili kwa kuishi vema nyajibu hizo muumini aweze kuurithi uzima wa milele.

Ufuasi wa Kristo: Mungu apewe kipaumbele cha kwanza
Ufuasi wa Kristo: Mungu apewe kipaumbele cha kwanza   (@Vatican Media)

Somo la Injili linalo beba tafakari ya siku hii ya leo ni kutoka katika Injili ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 10:37-42). Katika somo hili la Injili Yesu anasema ampendaye baba au mama kuliko mimi hanistahili, apendaye mwana au binti kuliko mimi hanistahili wala yule asiyechukua msalaba wake kunifuata hanistahili. Kumbe ni lazima kuelewa jambo hapa ya kuwa Kristu hatutumi twende tukawachukie wazazi, ndugu jamaa na marafiki bali anatuonya juu ya ni wapi tumeelekeza hasa upendo wetu. Sharti ifahamike kwamba upendo wa kibinadamu hugawanyika kiasi cha kuchochea hata upendeleo hata kumsahau Yesu. Kumbe, Kristu anataka kwanza tumpende yeye aliye asili ya upendo wote. Kibinadamu Baba na mama wanawakilisha chimbuko, historia na asili ya kule tulikotokea. Tunaweza kusema pia kuwa wanawakilisha asili ya utu wetu. Sasa leo Yesu anasema mtu anayejishikamanisha na hayo kiasi cha kuona kuwa Yesu hana nafasi katika asili yake, hafai kuwa mfuasi wake. Kama binadamu tuna asili yetu, tuna chimbuko letu lakini kabla ya hayo yote sisi asili na chimbuko letu ni Mungu mwenyewe. Historia yetu haiwezi kukamilika kama haitatambua uwepo wa Mungu. Watoto wanawakilisha matumaini yajayo, wanawakilisha kesho yetu. Kumbe tusali leo kuomba kushikamana na Yesu, tupange mipango na mikakati yetu Pamoja naye ili aweze kutuongoza mpaka mwisho. Tunapo shrehekea Dominika hii ya 13 tumwombe Kristu atupe neema siku zote ya kuiandaa kesho yetu na huu ni wajibu wetu wa msingi lakini kuiandaa kesho yetu bila kutambua kuwa kuna kesho ya maisha ambayo Kristo anatualika kuiangalia tutakuwa tunakosa kipengele muhimu sana katika maisha yetu. Basi na tusali kama alivyo Sali Mt. Ignatius wa Loyola akisema “Chukua, Bwana, pokea uhuru wangu wote, kumbukumbu yangu, ufahamu wangu, na mapenzi yangu yote. Yote niliyo nayo na yote nilivyo navyo Umenipa: Yote nakurudishia Bwana; fanya nayo upendavyo, sawasawa na mapenzi yako. Unipe upendo wako na neema yako, maana hayo yanitosha. Kwa njia ya Kristu Bwana wetu.” Amina.

Liturujia D13 Mwaka A
26 Juni 2026, 15:08