Mkutano mkuu wa 47 wa WAWATA Taifa, Viongozi wapya na vipaumbele kati ya Mwaka 2026 hadi 2029 Mkutano mkuu wa 47 wa WAWATA Taifa, Viongozi wapya na vipaumbele kati ya Mwaka 2026 hadi 2029 

Mkutano Mkuu wa 47 wa WAWATA: Viongozi Wapya Na Vipaumbele 2026-2029

Papa Leo XIV anataja sifa muhimu katika uongozi: Kusikiliza na uwajibikaji wa pamoja; ukweli na uwazi; Ukaribu wa kindugu; na utambuzi wa Jumuiya. Uongozi bora ni ule unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa ushiriki na uwajibikaji wa wanajumuiya wake; mambo msingi yanayopaswa kuzamishwa akilini kila wakati kiongozi anapotaka kutumia mamlaka yake. Ikumbukwe kwamba, watu wanaasili na historia tofauti; utambulisho wao sanjari na kanuni maadili na utu wema.

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Singida, Tanzania.

Tumsifu Yesu Kristo, Miele Amina! Kwa niaba ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka, neema zake nyingi na kwa kutuwezesha kukamilisha kwa amani na mafanikio Mkutano Mkuu wa Taifa wa Uchaguzi uliofanyika Jimbo Katoliki Singida kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 8 Juni 2026. Uchaguzi huu umefanyika chini ya usimamizi wa Padre Alister Makubi, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC; Padre Delphinus Ngaiza, Mkurugenzi wa Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC pamoja na Godfrey Leonard, Katibu Msaidizi Halmashauri Walei Taifa. Viongozi wafuatao wamechaguliwa kuiongoza WAWATA katika Kipindi cha Miaka Mitatu yaani kuanzia Mwaka 2026-2029. Nao ni: Mama Evaline Malisa Ntenga, kutoka Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala, Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Mwenyekiti; Esther Andrew Bundala, Mwenyekiti Msaidizi, kutoka Parokia ya Yesu Kristo Kuhani Mkuu, Bwiru, Jimbo kuu la Mwanza; Stella Kahwa, Katibu mkuu kutoka Parokia ya Mtakatifu Theresia, Jimbo kuu la Dar es Salaam; Flora Maro Mgalla Katibu mkuu Msaidizi kutoka Parokia ya Mtakatifu Maria Magdalena, Kimara Mtoni, Jimbo kuu la Dar es Salaam na hatimaye ni Dora Chuma Chikongoye, Mtunza hazina kutoka Parokia ya Mtakatifu Petero Clever, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Papa Leo XIV akiwa na Mahujaji wa WAWATA kutoka Tanzania
Papa Leo XIV akiwa na Mahujaji wa WAWATA kutoka Tanzania

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: "Kuhudumia, Kuandamana, Kuongoza ni misingi na mienendo ya uongozi katika mashirika na vyama vya kitume.” Haya ni mambo makuu yanayopaswa kumwilishwa mintarafu mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Ikumbukwe kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayopaswa kusimikwa katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; kwa kulinda na kudumisha karama na malengo makuu ya vyama na mashirika ya Kikanisa, sanjari na kujikita katika mchakato wa malezi na makuzi wa wanachama wao. Kanisa lilianzishwa na Kristo Yesu kama ishara ya daima ya mapenzi yake ya wokovu kwa ulimwengu wote na ni mahali palipopendelewa na Mwenyezi Mungu, ambapo watu wote, katika kila zama, wanaweza kupokea matunda ya ukombozi na kupata maisha mapya ambayo Kristo Yesu anawakirimia waja wake. Kwa maana hii, asili ya Kanisa ni kisakramenti: hakika ina mwelekeo wa nje na wa kitaasisi pamoja na miundo yake, na wakati huo huo, ni ishara ya ufanisi ya ushirika ambayo kwayo waamini wanashiriki katika maisha yenyewe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa vyama vya kitume, mashirika ya kikanisa na jumuiya mpya, uongozi katika mifumo hii umekabidhiwa kwa waamini walei na unaonesha ushiriki wao katika ofisi ya Kifalme ya Kristo Yesu, inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo.

Wasimamizi na Viongozi wapya wa WAWATA kwa Mwaka 2026 hadi mwaka 2029
Wasimamizi na Viongozi wapya wa WAWATA kwa Mwaka 2026 hadi mwaka 2029

Hii ni huduma kwa ajili ya waamini wengine na ujenzi wa maisha ya ushirika na huduma hii ni tunda la uchaguzi huru, ambao lazima ueleweke kuwa ni kielelezo cha utambuzi wa pamoja unaoruhusu sauti ya kila mtu kuoneshwa kwa uhuru zaidi. Kumbe, uongozi ni karama ya Roho Mtakatifu inayotambulikana kuwa ni zao la imani kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi; ni kwa ajili ya kuendeleza mema ya jumuiya, ushirika na Kanisa katika ujumla wake. Kumbe, uongozi kamwe hauwezi kutumika kwa ajili ya masilahi ya mtu binafsi, ufahari pamoja na hali ya mtu kutaka kujimwambafai na kwamba, uongozi hauwezi kamwe kulazimishwa kutoka juu, lazime uwe ni zawadi inayotambulika na kukubalika katika jamii na kwamba, zawadi hii inatokana na uchaguzi huru, ili kuleta ufanisi. Uongozi lazima utambuliwe na wachungaji wa Kanisa ambao husimamia uhalisi na matumizi sahihi ya karama za waamini. Baba Mtakatifu Leo XIV anataja sifa muhimu katika uongozi: Kusikiliza na uwajibikaji wa pamoja; ukweli na uwazi; Ukaribu wa kindugu; na utambuzi wa Jumuiya. Uongozi bora ni ule unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa ushiriki na uwajibikaji wa wanajumuiya wake; mambo msingi yanayopaswa kuzamishwa akilini kila wakati kiongozi anapotaka kutumia mamlaka yake. Ikumbukwe kwamba, watu wanaasili na historia tofauti; utambulisho wao sanjari na kanuni maadili na utu wema. Kumbe, viongozi wanaitwa kujivika jukumu la Kinabii, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza mahitaji ya sasa ya shughuli za kichungaji, ili kufahamu jinsi ya kukabiliana na changamoto mpya sanjari na hisia za kitamaduni, kijamii na za kiroho katika Ulimwengu mamboleo. Ni kwa njia hii, kiongozi anaweza kuwa ni Mkristo, mwanafunzi na mmisionari katika ulimwengu mamboleo na ndani ya Kanisa. Dhamana ya Unabii ndani ya Kanisa ni kukuza: Ukweli na Uwazi; Kusoma alama za nyakati; kujitamadunisha pamoja na kuangalia maisha na utume wa Kanisa, mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.

Askofu  Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida
Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida

Mkutano huu ulikuwa wa kihistoria kwa WAWATA. Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa WAWATA, Mkutano Mkuu wa 47 wa Taifa umefanyika nje ya Dar es Salaam yalipo Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Hatua hii ilitokana na maombi na matarajio ya muda mrefu ya wanachama wa WAWATA kwamba, shughuli za Taifa zianze kuzunguka katika majimbo mbalimbali nchini ili kuimarisha: Umoja, ushiriki na uzoefu wa Kanisa katika Tanzania nzima. Singida ilichaguliwa kuwa mwanzo wa safari hii kwa kuwa iko katikati ya Tanzania na hivyo kurahisisha ushiriki wa wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Aidha, Jimbo Katoliki Singida linaongozwa na Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Mwenyekiti wa Idara ya Walei ya TEC na Mlezi wa vyama vya kitume nchini. Kwa namna hiyo, mkutano huu haukuwa mkutano wa uchaguzi pekee, bali pia ulikuwa ni hija ya kiroho, nafasi ya kujifunza, kujenga udugu wa kibinadamu na kushuhudia utakatifu na uzuri wa Kanisa letu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Padre Delphinus Ngaiza akiteta na Papa Leo XIV alipokutana nao hivi karibuni
Padre Delphinus Ngaiza akiteta na Papa Leo XIV alipokutana nao hivi karibuni

Tunamshukuru kwa namna ya pekee Mhashamu Askofu Edward Mapunda kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu, kwa kutuongoza katika sala, kutushauri na kututia moyo. Tunawashukuru pia viongozi wa Jimbo Katoliki Singida, Mapadre, watawa, waamini na wananchi wa Singida kwa mapokezi yao ya kipekee yaliyofanya wajumbe wote wajisikie wapo Singida. Tunatoa pongezi kwa VIONGOZI wote wa WAWATA Tanzania kwa kupokea mabadiliko haya kwa moyo wa wazi na mtazamo chanya, jambo lililochangia mafanikio makubwa ya mkutano huu. Tunamshukuru Mungu pia kwa kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi wapya wa WAWATA Taifa katika hali ya amani, umoja na mshikamano. Tunaamini uchaguzi huu umefanyika chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu na tunawaombea viongozi wote waliochaguliwa ili watimize wajibu wao kwa hekima, uadilifu na moyo wa huduma huku wakiendelea kujikita katika ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi. Tunatoa shukrani za dhati kwa Kanisa letu Mama; kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Maaskofu wote, Idara ya Walei, Idara ya Kichungaji, walezi wetu wa kiroho na viongozi wote wa Kanisa wanaoendelea kutuongoza na kutusindikiza katika maisha na utume wetu wa kila siku.

Mama Evaline malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa
Mama Evaline malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa

Tunatoa shukrani za pekee kwa waume zetu na familia zetu. Baba Askofu Mapunda alitukumbusha kwamba tusiwasahau wale wanaotupa nafasi ya kushiriki utume huu wa Kanisa, wanaotusimamia katika familia zetu na mara nyingi hata kuchangia rasilimali zinazowezesha shughuli zetu kufanyika. Tunawatambua na kuwashukuru kwa upendo, uvumilivu na ushirikiano wao. Tunawashukuru wanawake wakatoliki wote katika majimbo yote nchini kwa kujitolea kwao katika huduma za Kanisa, malezi ya familia, uinjilishaji na maendeleo ya jamii. Baba Askofu Mapunda alisisitiza kwamba Kanisa linaendelea kung'ara, kukua na kushamiri kutokana na mchango mkubwa wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa.Katika mafunzo na wosia wake, Baba Askofu Mapunda alitukumbusha kwanza umuhimu wa Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Alituhimiza kumkimbilia Yesu wa Ekaristi katika sala na ibada, kwa kuwa humo ndimo tunapopata nguvu za maisha na utume wetu. Aidha, alitukumbusha kuendelea kumtegemea Mama yetu Bikira Maria na kumwomba daima atuombee kwa Mwanae Yesu Kristo. Pia alisisitiza umuhimu wa umoja, uwazi, uwajibikaji na mshikamano kati ya viongozi na wale wanaowaongoza. Alitukumbusha kwamba uongozi wa Kikristo ni huduma inayojengwa juu ya ukweli na uwazi; ushirikishwaji, uwajibikaji na kutafuta mema ya jumuiya badala ya maslahi binafsi. Alituhimiza kufanya tathmini za mara kwa mara ili kujirekebisha na kuimarisha utume wetu.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi akizungumza na ujumbe wa WAWATA
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi akizungumza na ujumbe wa WAWATA

Zaidi ya yote, Baba Askofu alisisitiza juu ya upendo. Alitukumbusha kuwa lengo la maisha ya Kikristo si kutafuta nafasi au madaraka, bali ni kumtukuza Mungu na kufika mbinguni. Kila huduma tunayotoa inapaswa kuelekezwa katika wokovu wa roho za watu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Katika semina maalumu iliyotolewa wakati wa mkutano, wajumbe walikumbushwa umuhimu wa malezi ya familia. Ilisisitizwa kwamba, katika mpango wa Mungu, mume na mke ni zawadi kwa kila mmoja. Kwa lugha rahisi ilielezwa kwamba mtoto wa kwanza wa mwanamke aliyeolewa ni mume wake, na mtoto wa kwanza wa mwanaume aliyeoa ni mke wake. Watoto wanaozaliwa baadaye huwa watoto wa familia nzima. Mafundisho haya yalisisitiza umuhimu wa wanandoa kupeana muda, upendo, malezi na ushirikiano ili kujenga familia imara, kwa kuwa familia ndiyo shule ya kwanza ya imani, maadili na utu wa mwanadamu. Kimsingi Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

WAWATA wakati wa Hija yao nchini Italia, Ufaransa na Ureno
WAWATA wakati wa Hija yao nchini Italia, Ufaransa na Ureno

Aidha, mkutano ulisisitiza umuhimu wa malezi ya vijana wa kike na wa kiume, ambao ndio viongozi, wazazi na waamini wa leo na kesho. Katika kutekeleza wajibu huu, WAWATA imeazimia kuimarisha zaidi ushirikiano wake na UWAKA ili kujenga mwendelezo wa malezi kutoka ujana hadi utu uzima. Ushirikiano huu unalenga kuwajenga vijana katika imani, maadili, uongozi, uwajibikaji na maandalizi ya maisha ya familia na huduma kwa Kanisa. Tunapoadhimisha mafanikio ya mkutano huu, tunaendelea kuongozwa na maono ya Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye ameweka mkazo mkubwa katika ustawi wa familia. Baba Mtakatifu ametukumbusha umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, heshima ya ubaba na umama, pamoja na wajibu wa wazazi katika malezi na makuzi ya watoto. Ameonesha wasiwasi wake juu ya changamoto zinazoikabili familia katika ulimwengu mamboleo na kwa sababu hiyo ametoa wito kwa kila mmoja kutafakari kwa kina mustakabali wa familia katika Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Vipaumbele vya WAWATA katika Kipindi cha Mwaka 2026-2029: Utu
Vipaumbele vya WAWATA katika Kipindi cha Mwaka 2026-2029: Utu

Kwa kuzingatia maelekezo ya Kanisa na changamoto za nyakati hizi, WAWATA imepitisha vipaumbele vya miaka 2026 hadi 2029 vinavyojikita katika kuimarisha familia kama shule ya imani, upendo na utakatifu; kuimarisha malezi ya vijana na WAWATA/UWAKA Chipukizi; kukuza: uelewa na matumizi ya TEHAMA, mitandao ya kijamii na Teknolojia ya Akili Unde katika uinjilishaji; Waraka wa kwanza wa Kitume wa Papa Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Ubinadamu wa ajabu" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” uwe ni dira na mwongozo wetu;  kuendeleza utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; kuimarisha uongozi wa wanawake kwa roho ya kimisionari na kisinodi; kutetea heshima ya uhai na utu wa mwanadamu; pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kuimarisha utume wa Kanisa na maendeleo ya jamii. Kwa namna ya pekee, mkutano huu umehimiza matumizi sahihi ya TEHAMA na teknolojia ya Akili Unde kama nyenzo za uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo.

Mama Evaline malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa
Mama Evaline malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa

 

WAWATA imejipanga kuwajengea wanawake uwezo wa kutumia teknolojia hizi kwa hekima na busara; kwa maadili na uwajibikaji ili kueneza Habari Njema, kuimarisha malezi ya familia, kuwafikia vijana na kujenga jamii inayosimikwa katika: utu, ukweli, haki na amani; matumaini na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mwisho, tunawaomba waamini wote, viongozi wa Kanisa, familia zetu na watu wote wenye mapenzi mema waendelee kutuombea. Tuombeane ili kazi ya Kristo iendelee kusonga mbele, familia zetu ziwe imara, vijana wetu wakue katika maadili mema, na WAWATA iendelee kuwa chombo cha uinjilishaji, matumaini na huduma kwa Kanisa na Taifa. Mama Maria, Malkia wa Mitume, utuombee. Tumsifu Yesu Kristo, Miele Amina.

Mkutano Mkuu WAWATA 2026

 

14 Juni 2026, 15:05