Kikundi cha Saba na cha Tisa kwa pamoja vimewasilisha kuhusu sifa na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa wakati wa mchakato wa kuteuwa Askofu mahalia. Kikundi cha Saba na cha Tisa kwa pamoja vimewasilisha kuhusu sifa na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa wakati wa mchakato wa kuteuwa Askofu mahalia.   (@Vatican Media)

Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Uteuzi wa Maaskofu, Maadili na Utu Wema

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kikundi cha Saba na cha Tisa kwa pamoja vimewasilisha kuhusu sifa na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa wakati wa mchakato wa kuteuwa Askofu mahalia. Pili ni jinsi ya kuratibu masuala mtambuka mintarafu mafundisho ya Kanisa, shughuli za kichungaji; kanuni maadili na utu wema; Dhamana na wajibu wa Askofu mahalia; Asili na muundo wake.. Mambo mengine ni pamoja na hija za kitume za Maaskofu Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia Mwaka 2021-2024 yalinogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya, yalizinduliwa kwa mkesha wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho mambo msingi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari linalosimikwa katika utamaduni wa kujadiliana, kusikilizana na kutenda kwa pamoja! Hakuna ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pasi na toba, wongofu wa ndani na upatanisho. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kikundi cha Saba na cha Tisa kwa pamoja vimewasilisha kuhusu sifa na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa wakati wa mchakato wa kuteuwa Askofu mahalia. Pili ni jinsi ya kuratibu masuala mtambuka mintarafu mafundisho ya Kanisa, shughuli za kichungaji; kanuni maadili na utu wema; Dhamana na wajibu wa Askofu mahalia; Asili na muundo wake.

Uteuzi wa Maaskofu wapya uzingatie mchakato wa Kisinodi
Uteuzi wa Maaskofu wapya uzingatie mchakato wa Kisinodi   (@Vatican Media)

Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Vikundi vyote viwili vimegusa kiini cha maisha na utume wa Kanisa mintarafu uteuzi wa Askofu mahalia, kwani huu ni utambuzi wa kweli unaopaswa kufanywa na Jumuiya ya Kikristo kwani hakuna mchungaji bila kundi na wala hakuna kundi bila mchungaji, changamoto ni kuwasikiliza wahusika, kusoma alama za nyakati na ukweli na hivyo kuleta pamoja aina tofauti za maarifa na kwamba, hapa njia inayofaa ni ile ya Kisinodi.

Uteuzi wa Maaskofu Mahalia uzingatie mchakato wa Kisinodi
Uteuzi wa Maaskofu Mahalia uzingatie mchakato wa Kisinodi   (@Vatican Media)

Sehemu ya Kwanza ya Ripoti ya Mwisho ya Kikundi cha 7 inatoa mapendekezo kuhusu uteuzi wa watahiniwa wa uaskofu kama wakati wa utambuzi wa kweli wa kikanisa, unaoongozwa na Roho Mtakatifu katika mazingira ya sala na kusikiliza. Wahusika wakuu ni pamoja na Kanisa mahalia na Askofu wake, Maaskofu wa Jimbo kuu au Baraza la Maaskofu pamoja na Balozi wa Vatican katika nchi husika, ili kupata wasifu wa Kisinodi na Kimisionari, kwa ajili ya uteuzi wa Askofu, kwa kuzingatia hali na mahitaji ya Kanisa husika.  Pale ambapo kiti cha Askofu mahalia kinapokaribia kuwa wazi, Askofu Jimbo anapaswa kuitisha Mkutano wa Baraza la Mapadre na Baraza la Kichungaji la Jimbo, ili kupata maoni juu ya mahitaji ya jimbo na kuwasilisha maoni yao kwa Askofu mahalia. Pale inapowezekana, mchakato huu wahusishwe wajumbe wa Halmashauri ya Walei, wawakilishi wa watawa, vijana na maskini na kwamba, sifa kuu ya Askofu mtarajiwa iwe ni umahiri wake katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; Utamaduni wa kusikiliza, majadiliano ya kitamaduni, mambo msingi katika ujenzi wa Kanisa. Mabaraza ya Kipapa yatakuwa na dhamana ya kupitia na kukagua taarifa hii mintarafu mwanga wa Sinodi. Kikundi hiki kinaendelea kujadili kuhusu kazi na wajibu wa Kiaskofu, ziara za kitume mjini Vatican sanjari na malezi na makuzi ya Maaskofu mahalia.

Hija za Kitume za Maaskofu mjini Vatican
Hija za Kitume za Maaskofu mjini Vatican

Ripoti ya Mwisho ya Kikundi cha 9 inapendekeza mabadiliko ya dhana katika njia ambayo Kanisa linashughulikia maswali magumu zaidi ya: Mafundisho tanzu ya Kanisa, shughuli za kichungaji, kanuni maadili na utu wema mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume sura ya 10 hadi 15 ambazo zinashuhudia tofauti za kitamaduni bila kuathiri upya wa Injili. Chaguo la kwanza muhimu linahusu istilahi: Kikundi kimependelea kuzungumza juu ya maswali "yanayoibuka" badala ya "ya kutatanisha" lengo likiwa ni kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kupitia toba na wongofu wa ndani; ujenzi wa uhusiano kwa kuzingatia umoja, ukweli na uwazi pamoja na kukazia “Kanuni ya shughuli za kichungaji” kwa kuwa na Mpatanishi ambaye Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani mwake. Katika kushughulikia masuala mtambuka Kikundi hiki kinapendekeza hatua tatu kama sehemu ya mbinu mkakati yaani: kujisikiliza, kuzingatia hali halisi sanjari na kuwakusanya watu wenye taaluma mbalimbali ili kutoa ushauri. Majadiliano katika roho yanasalia kuwa chombo cha upendeleo cha kuendeleza utamaduni wa kikanisa wa Sinodi. Katika sehemu ya tatu ya Taarifa, Kikundi kinatumia njia hii kikamilifu kwa maswali mawili ambayo kwa sasa yanajitokeza katika maisha ya Makanisa mahalia, yaliyochaguliwa kwa usahihi kwa utofauti wao: uzoefu wa watu wa jinsia moja ambao ni waamini, na uzoefu wa kutofanya vurugu - inayoshuhudiwa na harakati ya vijana wa Kiserbia ambayo ilichangia anguko la amani la Miloševic kutoka kwa Wakristo wa awali. Katika hali zote mbili, Kundi halitoi maoni ya uhakika lakini linakazia umuhimu wa kusikiliza moja kwa moja kwa njia ya shuhuda thabiti - linapendekeza njia za utambuzi wa kimaadili na kitaalimungu na maswali ya wazi, ili kila jumuiya iweze kuchukua "jukumu la kutambua na kuendeleza mema ambayo kwayo Mungu hutenda katika historia na katika uzoefu wa watu." Taarifa za Mwisho, pamoja na muhtasari katika lugha tano, zinapatikana kwenye tovuti ya Sekretarieti Kuu ya Sinodi kwa anuani ifuatayo: www.synod.va: www.synod.va

Taarifa ya Sinodi
05 Mei 2026, 15:23