Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani 2026: Sifa za Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Lengo ni kuhamasisha utoaji wa haki msingi kwa wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi zaidi sanjari na kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi wengi. Katika maadhimisho haya, Jumuiya ya Kimataifa inapenda kutambua na kuenzi mchango wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mei Mosi: Umoja!

Na Padre Octavian O. Hinju, CP. JUCo, Morogoro Tanzania.

Leo tuna mtazama Yosefu Mtakatifu kama kipimo na kielelezo cha wote wanao wajibika katika kufanya kazi kama mojawapo ya njia na nafasi ya kushirikiana na Mungu mwenyewe ambaye utendaji wake unajidhihirisha na kujifunua wazi kwetu sisi kupitia viumbe alivyoviumba Yeye mwenyewe. Sikukuu ya Mei Mosi ni ukumbusho kuwa kazi ni kipimo cha utu na wale wote wanaofanya kazi wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, kuanzia tarehe 8 Desemba 2020 hadi tarehe 8 Desemba 2022 Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi katika maisha. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika katika ndoto.

Mei Mosi Ni Kumbukumbu ya Mauaji ya Halaiki, Chicago Marekani
Mei Mosi Ni Kumbukumbu ya Mauaji ya Halaiki, Chicago Marekani

Lengo la maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu anasema Baba Mtakatifu Francisko, lilikuwa ni kuwasaidia waamini kumfahamu na kumpenda Mtakatifu Yosefu aliyekuwa na mang’amuzi ya kibinadamu kama walivyo waamini wengi duniani. Ni Mtakatifu ambaye hakushtushwa sana na mambo, hakuwa na karama maalum wala kati ya watu wa nyakati zake, hakuwa mtu mashuhuri. Na wala Maandiko Matakatifu hayaoneshi maneno yaliyotoka kinywani mwake hata kidogo, lakini machoni pa Mwenyezi Mungu, aliweza kutenda matendo makuu katika maisha na utume wake. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Redemptoris custos”, yaani “Mlinzi wa Mkombozi” uliochapishwa kunako tarehe 15 Agosti 1989 anamtaja Mtakatifu Yosefu kuwa ni Mlinzi wa Mkombozi na Familia Takatifu. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti, aliyejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu anapomweka Mungu pembeni mwa mipango na vipaumbele vya maisha yake, matokeo ni kutumbukia katika majanga yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Lengo ni kuhamasisha utoaji wa haki msingi kwa wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi zaidi sanjari na kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi wengi. Katika maadhimisho haya, Jumuiya ya Kimataifa inapenda kutambua na kuenzi mchango wa wafanyakazi katika sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mei Mosi, ni siku maalum ya kuonesha umoja na mshikamano kati ya wafanyakazi, sanjari na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi, sehemu mbalimbali za dunia. Mei Mosi ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea kunako mwaka 1886 katika viwanja vya Haymarket Chicago, nchini Marekani. Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi wakati wa mgomo wa kupinga masaa nane ya kazi ambapo mtu asiyejulikana aliwarushia askari bomu. Polisi waliwalirushia risasi wafanyakazi hao na hivyo kupelekea vifo vya wafanyakazi wanne.

Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani: Utu, heshima na haki msingi
Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani: Utu, heshima na haki msingi   (AFP or licensors)

Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo muhimu sana katika sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Binadamu wanapaswa kuangaliana na kuchukuliana kama ndugu wamoja na kwamba, kazi nzima ya uumbaji ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inashangaza sana machoni pa binadamu! Kazi inamtambulisha mwanadamu na kumwezesha kutekeleza karama na mapaji mbalimbali aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Kwa njia ya kazi, mwanadamu anashiriki pia katika mpango wa kazi ya uumbaji ulioanzishwa na Mwenyezi Mungu na hivyo kushiriki pia katika mchakato wa mshikamano na jirani zake. Licha ya shida na magumu yanayojitokeza katika kazi, lakini kazi inamwezesha mtu kukua na kukomaa, pamoja na kutekeleza ndoto za maisha yake. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa vile Sikukuu hii iligubikwa sana na kilio cha wafanyakazi, machafuko, kinzani na misigano, hasa kwenye Karne ya Kumi na tisa, Mama Kanisa akataka Mtakatifu Yosefu kuwa ni kielelezo makini cha mapambano ya kudai haki msingi za wafanyakazi, utu na heshima yao pamoja na kutoa hadhi kwa kazi kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa kazi ya uumbaji na ukombozi ambayo hata Kristo Yesu mwenyewe aliishiriki kiasi hata cha watu kumsema: “Huyu si yule seremala…” Mk. 6:3. Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; kwa kutambua na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mei Mosi, Utu, Heshima na Haki Msingi za wafanyakazi duniani
Mei Mosi, Utu, Heshima na Haki Msingi za wafanyakazi duniani   (AFP or licensors)

Leo ni furaha kote ulimwenguni, tunapo alikwa na Mama Kanisa kumtazama Mtakatifu Yosefu kama kipimo na kielelezo cha wote wanao wajibika katika kufanya kazi kama moja ya njia mojawapo ya kushirikiana na Mungu mwenyewe ambaye utendaji wake unaendelea kujidhihirisha kwa nyakati zote katika viumbe alivyoviumba. Mei Mosi ni ukumbusho kuwa kazi ni kipimo cha utu na thamani ya ubinadamu unaojali na kuwajibika ipasavyo; nao wale wote wanaofanya kazi wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa. kumbe katika Mawazo ya namna hiyo, kazi inakuwa kwetu ni kipimo cha utu cha heshima ya mwanadamu. Kama mfano na kielelezo chetu, kupitia Mtakatifu Yosefu utu wa binadamu unahimizwa kutambua kwamba kazi ni njia ya kushiriki moja kwa moja katika kazi ya kimungu ya uumbaji; nayo kazi hutusaidia kuzitegemeza familia za kikristu na ni nyenzo ya kujipatia mahitaji ya msingi. Sikukuu hii inatukumbusha waamini kote duniani kuthamini kazi bila kujali kada zetu ili kudumisha haki msingi za jamii na wajibu katika kazi hizo. Leo tumtazame Mtakatifu Yosefu sio tu kama: Fundi Seremala na Baba Mlishi wa Yesu, bali kama mtu mwenye haki na Hekima aliyependa kufanya kazi zake katika hali ya ukimya na utulivu mkubwa. Hakuwa mlalamishi bali mwenye utayari wa daima kupokea mpango na maongozi ya kimungu.

Kuna wafanyakazi wanaofariki dunia kutokana na ukosefu wa usalama kazini
Kuna wafanyakazi wanaofariki dunia kutokana na ukosefu wa usalama kazini

Kama ilivyo kwa akina baba wengi, Mtakatifu Yosefu alimlea na kumfundisha Yesu ili aweze kufuata kazi yake mwenyewe kama fundi. Katika Injili, Yesu anaitwa “Mwana wa Seremala” (Mt. 13:55). Maisha ya Mtakatifu Yosefu yanatuonyesha hadhi ya kazi ya mwanadamu, ambayo ni wajibu na ukamilifu wa wanadamu, ambao kwa njia hii mwanadamu anatawala juu ya kazi yote ya uumbaji, na kushiriki katika kazi ya Muumba. Vilevile hushiriki katika kutoa huduma yake kwa jamii, na kushiriki katika mpango wa Mungu wa wokovu. Mt. Yosefu alipenda kazi yake. Hakulalamika kamwe juu ya uchovu, lakini kama mtu wa imani aliiinua juu kwake Mungu ili iwe kwa manufaa na matumizi ya wema na ukarimu wa Mungu kwa watu wote. Aliridhika na kazi yake, kwa sababu moyoni mwake hakutamani mali na hakuwaonea wivu matajiri; kwa Mt. Yosefu, kazi haikuwa njia ya kutosheleza uchoyo wake mwenyewe, bali chombo cha kutegemeza familia yake. Na, kwa kufuata amri na maagizo ya Mungu, siku ya Bwana, Mtakatifu Yosefu aliadhimisha mapumziko ya kila juma na kushiriki katika sherehe sawasawa na tamaduni za kiyahudi kama ilivyokuwa desturi kwa watu wengine. Ifahamike kwamba, pamoja na kuwa ni Mume wa Bikira Maria, na Baba Mlishi wa Yesu, Mtakatifu Yosefu alikuwa Seremala. Kupitia kazi ya mikono yake, Yosefu aliipatia Familia Takatifu mahitaji yote ya kibinadamu, na kushiriki katika mpango mtakatifu wa wokovu. Injili ya Mathayo inamtaja Yosefu kama “mtu mwenye haki”, ambapo katika lugha ya Biblia inamaanisha mtu anayependa na kuheshimu sheria kama kielelezo cha mapenzi ya Mungu. Kama Bikira Maria, Yosefu pia alitembelewa na Malaika, ambaye alimtokea katika ndoto. Na, tena kama Bikira Maria mchumba wake, Mt. Yosefu alitamka “Ndiyo yenye nguvu na Imani kwa nyakati zote”, ambapo wakati Malaika alipofunua kwamba Mtoto aliyemzaa alikuwa ametungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Sikuu ya Wafanyakazi Duniani: Utu, Heshima na Haki Msingi
Sikuu ya Wafanyakazi Duniani: Utu, Heshima na Haki Msingi   (ANSA)

Sifa ya pekee ya Mtakatifu Yosefu ni ukimya, mtu asiyetajwa sana katika Maandiko Matakatifu. Hakuna neno lake lililoandikwa katika Injili. Hatajwi baada ya kupatikana kwa Kristo Hekaluni. Labda mpaka kufikia wakati Yesu apolianza utume na maisha yake ya hadhara, hata kwenye harusi ya huko Kana, Mtakatifu Yosefu alikuwa tayari amepita na kujizamisha kwenye maisha ya ukimya na utulivu mkuu, ingawa hatujui ni lini au wapi alikufa hata mahali alipozikwa bado ni fumbo. Kumbe hata sisi leo hii, hatupaswi kushangazwa na tendo hili zuri la kupenda kufanya kazi. Tutambue kuwa hakuna kazi duni ya kazi ya mikono: ndio maana tayari katika Agano la Kale, Mungu alionekana kwa njia ya mfano kama mkulima wa zabibu, mpanzi, au mchungaji. Basi tumwombe Mungu kupitia maombezi ya Mt. Yosefu ili kuhakikisha kwamba wafanyakazi hawapotezi ufahamu wa Kikristo kuhusu kazi. Tumwombe yeye aliye Mlezi wa Kanisa la Ulimwengu ili tuweze kuzitazama kazi kama njia ya wokovu wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Sikukuu ya Wafanyakazi
30 Aprili 2026, 15:34