Kristo anafuta dhambi kwa upendo.Watumiao vibaya mamlaka watajibu kwa Mungu!
Tiziana Campisi na Angella Rwezaula – Vatican.
Huko Yerusalemu ni kuingia kati ya barabara ndogo yenye mambo mengi katika ì Njia ya Uchungu na mateso, iliyopitiwa na Yesu, baada ya kuhukumiwa kifo, hadi Golgota, mahali pa kusulibiwa. Ilikuwa hivyo miaka elfu mbili iliyopita na ni sawa sawa na leo hii: katika mazingira ya kelele, katikati ya watu ambao wanashirikishana imani katika Kristo, lakini hata wengine wanaocheka na kutukana. Ndivyo ilivyo maisha ya kila siku. Na ni njia ya Msalaba katika Ulimwengu mamboleo, ambao kwa bahati mbaya, unatumiwa na mamlaka binafsi na mara nyingi kukosa heshima ya hadhi ya binadamu. Haya yanaibuka katika tafakari iliyoandikwa na Padre Francesco Patton(OFM), kwa ajili ya tukio la kiutamaduni la usiku wa Ijumaa Kuu tarehe 3 Aprili 2026 katika Uwanja wa Kale wa mateso ya wakristo wa Flavio ujulikanao Colosseum, katika Kilima cha Palatino, Roma itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye anatabeba Msalaba kwa vituo vyote 14.
Nguvu ya Wanadamu na Nguvu ya Yesu
Ndugu Mdogo aliyekuwa Msimamizi wa Nchi Takatifu, analinganisha Injili za Mateso na maandishi ya Mtakatifu Francis wa Assisi, katika ukumbusho wa miaka mia nane ya kifo chake, ambayo inaadhimishwa mwaka huu. Anaendeleza tafakari zake kwa kutafsiri upya uzoefu wa Kristo katika uhalisia wa leo hii, akileta mafundisho yake katika wakati uliopo, akilinganisha nguvu inayotumiwa na wanadamu na nguvu ya upendo wa Yesu. Kwanza kabisa, katika Kituo cha Kwanza, ambapo Yesu, katika mazungumzo na Pilato, anafichua "kila dhana ya kibinadamu ya nguvu." "Hata leo hii, kuna wale wanaoamini wamepokea mamlaka isiyo na kikomo na wanafikiri wanaweza kuitumia na kuitumia vibaya wapendavyo," Padre Patton anasisitiza, lakini "kila mamlaka italazimika kujibu mbele ya Mungu kwa njia yake ya kutumia nguvu iliyopokelewa, " "kuhukumu," "kuanzisha vita au kuimaliza," "kuelimisha vurugu au amani," "kuchochea hamu ya kulipiza kisasi" au "upatanisho," na tena "kutumia uchumi kuwakandamiza watu au kuwakomboa kutoka katika umaskini," "kukanyaga hadhi ya binadamu au kuilinda," "kukuza na kutetea maisha au kuyakataa na kuyakandamiza."
Kutoheshimu hadhi ya binadamu
Matumizi mabaya ya madaraka ni mada inayojirudia katika Kituo cha Kumi, "Yesu amevuliwa nguo zake." Jaribio hilo la Askari la kumdhalilisha na kumvua Kristo hadhi yake ya kibinadamu, kwa Mfransikani huyo,alibainisha kuwa "linarudiwa kila mara hata katika siku zetu": wakati "serikali za kimabavu" zinapowalazimisha "wafungwa kubaki nusu uchi” mateso hufanywa, au kuna wale wanaoidhinisha na kutumia "aina za utafutaji na udhibiti ambao hauheshimu" ubinadamu. Na "wabakaji na wanyanyasaji wanaifanya," "tasnia ya burudani, inapoonesha uchi ili kupata watazamaji wengi zaidi" na pia "ulimwengu wa habari, unapowafichua watu mbele ya maoni ya umma." Lakini mtu yeyote anaweza pia kukiuka utu wa mtu anaposhindwa "kuheshimu unyenyekevu wake, ukaribu wake, au faragha yake." Na kwa hivyo lazima tujiruhusu kuvikwa na Yesu kwa "unyenyekevu," "huruma," na "hisia mpya ya unyenyekevu."
Yosefu wa Arimathaya na Nikodemo katika (Kituo cha 13)ni mifano ya hili, wanapoomba mwili wa Yesu kwa ajili ya mazishi ya heshima. Hata hivyo, leo hii kuna "maiti ambazo hazijarudishwa na ambazo hazijazikwa" na "mama," "ndugu, jaama," na "marafiki wa waliohukumiwa" ambao "wanalazimishwa kujinyenyekeza mbele ya mamlaka ili mabaki ya jamaa zao walioteswa warudishwe kwao." Lakini "hata mwili wa mtu aliyekufa unadumisha utu wa mtu huyo na hauwezi kudharauliwa, au kufichwa, au kuharibiwa, au kutorudishwa, au kunyimwa mazishi stahiki," anasisitiza mwandishi wa tafakari hiyo kwamba, na si tu ule wa "mtu mwema," lakini pia "mwili wa mhalifu unastahili heshima." Hii ndiyo sababu lazima kuwe na nafasi ya hisia ya "huruma," "kuhisi mateso ya wafungwa," "kuonesha mshikamano na wafungwa wa kisiasa," "kuelewa familia za mateka," "kuomboleza wafu walio chini ya vifusi," na "kuwaheshimu marehemu wote."
Nguvu Halisi
Hata hivyo, nguvu halisi inaoneshwa kwetu na Yesu aliyesulubiwa msalabani, Kituo cha 11. Ni "ya mtu anayeweza kushinda kifo kwa kutoa uzima" na kufuta uovu kwa "upendo" kupitia msamaha, "si ya mtu anayeamini anaweza kuondoa uhai wa mwingine kwa kusababisha kifo" au "anatumia nguvu na vurugu kujilazimisha." Kristo ni Mfalme na anatawala kutoka msalabani, Padre Patton anasisitiza, lakini hatumii "nguvu dhahiri ya majeshi," bali "udhaifu dhahiri wa upendo, ambao unaruhusu kupigiliwa chini." "Si upendo kupitia nguvu unaoshinda, bali nguvu ya upendo."
Njia ya Unyenyekevu
Katika safari ya kwenda Golgotha, Yesu, ambaye "anakumbatia msalaba na kuubeba mabegani mwake" (Kituo cha 2), "anajichukulia ubinadamu wetu," akijichukulia "utumwa wetu" na "makosa yetu," anatufundisha tusiogope msalaba. "Tupe neema ya kukufuata katika njia hiyo hiyo," Padre Patton anaomba, akimgeukia Mungu, ili awaweke huru wanadamu "kutoka kwa tamaa ya utukufu wa kibinadamu," "kutoka kwa kishawishi cha kuwapuuza wale wanaoteseka" na kutoka kwa ubinafsi. Na hivyo anguko lingine la Kristo linakuwa mwaliko "wa kujifunza njia ya unyenyekevu," hata kutokana na uzoefu wa makwazo na "udhalilishaji ambapo ni kuanzia chini"(Kituo cha tatu.)
Kwa hivyo, kujishusha, kuinama(Kituo cha saba), kama Yesu alivyofanya alipowaosha "miguu ya wanafunzi wake kwenye Karamu Kuu ya Mwisho" na kutoa "mfano wa huduma, mafundisho ya upendo wa kidugu, na unabii wa kutoa uhai wake." Shauku hii ya kutuongoza "katika uzima wa Mungu" inamwongoza Kristo kuwafikia wanadamu, na hivyo anapoanguka, anafanya hivyo "kuwainua wale waliokandamizwa na dhuluma, kwa uongo, kwa kila aina ya unyonyaji na kila aina ya vurugu," na pia "kwa taabu inayotokana na uchumi unaolenga faida ya mtu binafsi, badala ya manufaa ya wote." Anguko lake la tatu, basi,(Kituo cha IX ) ni mbinu yake ya kukabiliana na udhaifu wa kibinadamu, kutia moyo kuendelea na "safari" katika "nyayo" zake, kwa sababu "haijalishi ni mara ngapi tunaanguka, upendo wake, msamaha" wake, na huruma" yake ni zawadi kubwa zaidi.
Wakirene wa leo hii
Bado akitazama wakati uliopo barabarani kuelekea Kalvari, Padre Patton anawatambua katika Simon wa Kirene, Kituo cha V, wengi ambao "huchagua kufanya jambo jema kwa wengine katika kila sehemu ya dunia," "maelfu ya watu wa kujitolea" wanaowasaidia "wale wanaohitaji chakula, elimu, huduma ya matibabu, haki," wakihatarisha maisha yao wenyewe. Wengi pia ni wasioamini, ambao bila kujua wanamsaidia Kristo "bado wanabeba msalaba" kwa kuwajali watu wengine, anabainisha Padre Patton, ambapo wanamwomba Mungu kwamba kila mtu ajifunze kuwa na huruma naupendo "wa ukweli na dhati," kwa kuzingatia "watesekao na waliokataliwa na wale walioachwa peke yao na wasiojali."
Wanawake Katika Njia ya Msalaba
Hata wanawake waliopo katika saa za Mateso wana jambo la kumwambia mwanadamu wa sasa. Veronica, ambaye "anajua jinsi ya kumtambua" Yesu katika "uzuri wake ulioharibika," Kituo cha VI, anatuhimiza kumwona Kristo "katika kila mtu aliyehukumiwa na ubaguzi," "katika maskini walionyimwa heshima yao," "katika wanawake wahanga wa biashara haramu na utumwa," "katika watoto ambao utoto wao umeibiwa." Na wanawake wa Yerusalemu(Kituo cha VIII) wanakumbuka uwepo wote wa wanawake "popote pale kuna mateso au hitaji": "katika hospitali na nyumba za wazee, katika jumuiya za matibabu na ukarimu, katika nyumba za familia kwa watoto walio katika mazingira magumu zaidi, katika vituo vya misheni vya mbali zaidi vinavyofungua shule na zahanati, katika vita na maeneo ya migogoro kuwasaidia waliojeruhiwa na kuwafariji manusura." Lakini pia tunaweza kuwatambua ndani yao wale wanaowalilia watoto wao, "waliochukuliwa na kufungwa wakati wa maandamano, waliofukuzwa kwa sera zisizo na huruma, walioharibikiwa na meli katika safari za matumaini, walioangamizwa katika maeneo ya vita, na walioangamizwa katika kambi za mauaji."
Machozi wanayotoa lazima yamwagike leo "ili kulia juu ya majanga ya vita," "juu ya mauaji ya halaiki na mauaji ya halaiki," "juu ya ubaguzi wa kunyanyasa." Na kisha kuna mama, Maria, (Kituo cha Nne,) yule ambaye, chini ya Msalaba, Yesu anamwomba "aendelee kumzaa na kuendelea kuwa mama" kwa wote. Na Ndugu Mdogo alimwomba Mama Maria ageuze macho yake kuelekea "mama wengi sana" ambao "huwaona watoto wao wakikamatwa, wakiteswa, wakihukumiwa, wakiuawa," wale "waliozinduliwa usingizini katikati ya usiku kwa habari za kuhuzunisha," na wale "wanaokesha hospitalini kwa ajili ya watoto wanaokufa." Na anaomba faraja kwa "yatima, hasa wale ambao ni yatima kutokana na vita," "wahamiaji, watu waliokimbia makazi yao, na wakimbizi," wale wanaoteseka na kuadhibiwa isivyo haki, wale ambao "wamepoteza maana ya maisha," na wale wanaokufa peke yao.
Kufuata njia ya Yesu katika ulimwengu halisi
Kwa tafakari zake, kwa kifupi, Padre Patton anatualika "kufuata nyayo za Yesu," si "mila au kiakili tu," bali ile ambayo "inahusisha utu wetu wote na maisha yetu yote," kama Mtakatifu Francis wa Assisi anavyoonesha katika Sala ya Mateso ya Bwana kwa: "Leteni miili yenu kama sadaka mkachukue msalaba wake mtakatifu, na kufuata amri zake takatifu zaidi hadi mwisho." Kwa sababu "Njia ya Msalaba si njia ya wale wanaoishi katika ulimwengu wa ibada isiyo na maji na kumbukumbu ya kufikirika, lakini badala yake "mazoezi ya wale wanaojua kwamba imani, tumaini, na upendo lazima viwe katika ulimwengu halisi." Ni hapa ambapo mwamini, ambaye anaendelea kupingwa, "lazima afanye njia ya Yesu ya kuendelea kuwa yake."