Maaskofu wa Vietnam wakutana na Papa Leo XIV:Kanisa ni familia
Vatican News
Akirudi Vatican baada ya Ziara yake ya Kitume ya siku 11 kwa mataifa manne barani Afrika, kuanzia Algeria, Cameroon, Angola na hatimaye Guinea ya Ikweta, ratiba ya Papa Leo XIV, mjini Vatican ilianza mara moja kama kawaida tarehe 24 Aprili 2026 kwa kukutana na Maaskofu wa Vietnam wakiwa katika ziara yao ya kichungaji iitwayo:“La visita ad limina Apostolorum.” Ziara iliyofanywa na Maaskofu kwa ushirikiano na Vatican, inalenga kuimarisha wajibu wao kama warithi wa Mitume na ushirika wao wa kihierarkia na Mrithi wa Petro. Ikizingatia sala katika makaburi ya Mtakatifu Petro na Paulo, pia hutumika kama wakati muhimu katika huduma ya kichungaji ya Papa, ambapo hukutana na Maaskofu kujadili mambo yanayohusiana na utume wao wa Kikanisa.
Baada ya Mkutano na Papa, Askofu Dominic Nguyen Tuan Anh, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Xuân Lộc alielezea mkutano huo kama wa kidugu, akisema kwamba hata "baada ya safari ndefu ya Afrika, Papa alichukua muda asubuhi ya leo kukutana nasi kwa moyo wake wote." Vietnam ina takriban Wakatoliki milioni saba na ni Jumuiya ya tano kubwa ya Wakatoliki kwa ukubwa barani Asia. Askofu Nguyen Tuan Anh alielezea jinsi Papa alivyofurahi kusikia kuhusu Kanisa mahalia nchini, ambalo Askofu alilielezea kuwa na "imani imara." Aliongeza kuwa katika ulimwengu unaoendelea kukua unaoendeshwa na teknolojia, Kanisa la Vietnam linafanya kazi kujibu maswali kuhusu imani na Akili Unde (AI) na vyombo vya habari. Kwa hivyo, Askofu alisisitiza umuhimu wa "kuungana" ili kukabiliana na changamoto hizo za kisasa.
Yafuatayo ni maswali na majibu ya mahojiano
Maaskofu wa Vietnam walikutana na Papa Leo XIV tarehe 24 Aprili asubuhi kama sehemu ya ziara yao ya ad limina. Mkutano huo ulikuwaje?
Kwanza, baada ya safari ndefu kwenda Afrika, alichukua muda asubuhi tarehe 24 Aprili kukutana nasi kwa moyo wake wote. Tulihisi hivyo, naye alisema hivyo. Ingawa alikuwa amechoka kidogo, alikuwa na furaha sana na mwenye tabasamu kusikia kuhusu Kanisa la Kivietinamu. Pili, jinsi alivyoungana nasi ilikuwa ya kidugu sana. Yeye kweli ndiye Mrithi wa Mtakatifu Petro, na sisi ni warithi wa mitume. Mazingira ya yalikuwa ya familia ya Kanisa. Sote tuna jukumu la kuchangia katika kuunda umoja na ushirika katika Kanisa. Tunahisi kweli kwamba tuko katika ushirika na Papa, Vatican na Kanisa la Ulimwengu. Kanisa la Kivietinamu ni familia, na katika utamaduni wetu, familia ni kitu cha muhimu na imara. Kanisa pia limebarikiwa kwa neema ya Mungu na kwa damu ya mashahidi wetu.
Hali ikoje katika Kanisa la Kivietinamu sasa?
Nadhani katika Kanisa tunahitaji mchango na umoja wa kila mtu: maaskofu, mapadre, waamini na watawa. Tunathaminiwa kwa imani yetu imara. Lakini pia tunakabiliwa na changamoto zote kama kila mtu mwingine, haswa sasa na Akili Unde (AI) na vyombo vya habari. Kwa hivyo tunahitaji kuungana; tunahitaji kuwa wamoja, na kwa neema ya Mungu, tunaweza kukabiliana na changamoto hii katika njia ya imani na matumaini
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here