Ask.Mkuu Ettore:Afya ya akili,Vijana watambue kuwa wao ni sura na mfano wa Mungu
Sr Ernestina Patrick Lasway – Vatican.
Katika ulimwengu wa usasa, vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi za afya ya akili, ambazo zinaweza kusababisha kukata tamaa na hatimaye kujiua. Haya yalizungumzwa katika hotuba ya Askofu Mkuu Ettore Balestrero, Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa huko Geneva, Uswiss, katika Kikao cha 158 cha Bodi ya Utendaji cha Shirika la Afya Duniani(WHO),kilichohusu Agenda ya 7 ya Afya ya Akili, tarehe 3 Februari 2026.. Akianza hotuba hiyo Askofu Mkuu Balestrero alisema kwamba ujumbe wake unazingatia Ripoti ya Mkurugenzi Mkuu kuhusu Afya ya Akili. Askofu Mkuu alisema, “jambo linalotia hofu kubwa ni hali ya vijana na takwimu zinazohusiana na kujiua, ambacho ni chanzo cha tatu kikuu cha vifo katika kizazi cha leo hii. Afya ya akili ni mojawapo ya maeneo ya afya yaliyoachwa bila kupewa kipaumbele. Mara nyingi huambatana na dhana potofu, ukosefu wa maarifa kuhusu masuala mahususi, pamoja na upotoshaji wa taarifa. Duniani kote, watu wenye changamoto za afya ya akili mara nyingi hukumbwa na unyanyapaa na ubaguzi, hali inayoweza kusababisha kutengwa na kutoshirikishwa katika jamii.”
Thamani ya Maisha ya Mwanadamu
Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa aliendelea kubainisha kuwa katika ulimwengu wa usasa, vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi za afya ya akili, ambazo zinaweza kusababisha kukata tamaa na hatimaye kujiua. Kuathirika huku mara nyingi kunaweza kuhusishwa na migogoro ya iliyopo inayotokana na kupotea kwa maana ya kina na thamani ya maisha ya mwanadamu. Kwa hiyo, kuna haja ya kutambua na kukiri kwa kiwango kikubwa zaidi mwelekeo wa mahitaji ya kiroho na kimwili ya mwanadamu.
Vijana watambue kuwa wao ni sura na mfano wa Mungu
Mwakilishi wa Vatican alisisitiza kwamba sambamba na huduma na msaada wa kitaalamu wa afya ya akili, msaada wa kiroho una mchango mkubwa wa kutoa hisia ya kina ya kuhusishwa na wengine, dhamira muhimu ya maisha, pamoja na simulizi lenye nguvu ya matumaini katikati ya changamoto za maisha.” Kwa namna hiyo aliongeza “ Vijana wanapotambua kwamba wao si matokeo ya bahati nasibu ya ulimwengu, bali wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na wanapendwa na Mungu ana mpango nao, maisha hupata maana, hata katikati ya maumivu na mateso.”
Kwa kuhihitimisha Askofu Mkuu Ettore alisema kuwa “katika utamaduni wa pilikapilika za hapa na pale, uharaka na kutojali unaotuzuia kutambua mahitaji na mateso ya wengine,msaada wa kiroho unakuza utambuzi wa zawadi ya uhai na hadhi ya kila binadamu aliyopewa na Mungu. Pia hurahisisha utafutaji wa maana ya maisha na kuchangia ujenzi wa jamii yenye mahusiano ya kweli, ambapo kujali wote kunajumuisha kubeba maumivu ya wengine.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here