Balozi Mahmoud Thabit Kombo Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, amekutana na kuzungumza kwa faragha na Baba Mtakatifu Leo XVI mjini Vatican. Balozi Mahmoud Thabit Kombo Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, amekutana na kuzungumza kwa faragha na Baba Mtakatifu Leo XVI mjini Vatican.  (@VATICAN MEDIA)

Waziri Kombo Akutana na Papa Leo XIV: Nyaraka za Maaskofu Tanzania

Balozi Mahmoud Thabit Kombo Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Jumatano tarehe 28 Januari 2026 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican na baadaye kuhudhuria Katekesi ya Papa Leo XVI kuhusu Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Nyaraka na Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania unachota amana na utajiri wake katika Biblia na Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Jumatano tarehe 28 Januari 2026 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican na baadaye kuhudhuria Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuhusu: Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Balozi Mahmoud Thabit Kombo katika ziara hii ya kikazi alikuwa ameambatana na Professa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Waziri wa kazi maalum Ikulu; Balozi wa Tanzania mjini Vatican Mhe. Balozi Hassan Mwameta.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na Papa Leo XIV Vatican
Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na Papa Leo XIV Vatican   (@VATICAN MEDIA)

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Matamko na Ujumbe wa Kwaresima
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Matamko na Ujumbe wa Kwaresima

Ni kawaida ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, yaani “Tanzania Episcopal Conference” (TEC) kutoa Ujumbe wa Kwaresima kwa Wakatoliki wote kila Mwaka kabla ya kuanza rasmi Kipindi cha Kwaresima. TEC inatoa Ujumbe huo ambao Wakatoliki wote wanapaswa kuufuata ukiwa ni Mwongozo wa Tafakari yao ya kuwaongoza katika kipindi chote cha Kwaresima. Kwa mfano, Mwaka 2025 Ujumbe wa Kwaresima ulikuwa "𝑺𝑰𝑴𝑨𝑴𝑬𝑵𝑰 𝑰𝑴𝑨𝑹𝑨 𝑲𝑨𝑻𝑰𝑲𝑨 𝑰𝑴𝑨𝑵𝑰" (1 Korintho 16:13). Na Mwaka huu wa 2026 pia watautoa Ujumbe wa Kwaresima kama ilivyo kawaida ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki. Naomba kutoa Tahadhari kwa wale wote watakaovurugwa na Ujumbe huo ujao wa Kwaresima kwa mwaka 2026; na kuuhusianisha na Masuala na au Hali ilivyo kwa sasa katika Taifa letu. Ujumbe wa Kwaresima huwa unagusa Maisha ya Kiroho na Kimwili ya Mkristo Mkatoliki. Pamoja na Ujumbe kusisitiza katika Kusali, Kufunga, Kutubu, Kutenda Matendo Mema na ya Huruma; Ujumbe huu pia hugusia Maisha ya Kimwili ya Wakatoliki katika Nyanja zote za Maisha ya Mwanadamu, yaani Kisiasa, Kiuchumi, Kijamii na kiroho. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, linawahimiza waamini wote kujiepusha na dhambi pamoja na mizizi yote ya dhambi kama vile: Uasherati, Ulafi, Tamaa, Uchoyo, Uvivu, Hasira, Wivu, Kiburi. Katika Ujumbe huo Wakatoliki pia hukumbushwa kuishi Maisha ya Fadhila za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo.

Papa Leo XIV amekutana na kuzungumza na Waziri Kombo mjini Vatican
Papa Leo XIV amekutana na kuzungumza na Waziri Kombo mjini Vatican   (ANSA)

Pamoja na hayo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pia katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa Waamini Wakatoliki, huwasisitiza sana Wakatoliki kuishi Maisha ya Kikristo na kueneza Utume wa Kristo Yesu kwa watu wote wakati wote, popote na kwa yeyote. Utume wa Mkristo Mkatoliki hauna mipaka. Mkatoliki awe kazini, awe na cheo, wadhifa au mamlaka ya uongozi na kiutawala, bado anaendelea kubaki kuwa ni Mkristo mkatoliki anayepaswa kuutumikia ukristo wake huku akitambua kuwa cheo chochote alichonacho sio kikubwa kuliko cheo cha ukristo wake alichokipata kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kwa Mkatoliki, Ukristo ni zawadi ya Mungu kwa waja wake. Mkristo Mkatoliki anafundishwa, kuhimizwa na kusisitizwa kuwa Mkweli na kuushuhudia Ukweli siku zote; maana Yesu Kristo Mwenyewe ndiye Njia na Ukweli na Uzima (Yohane 14:6). Tena anaamriwa kutenda HAKI, kudumisha Upendo, Kulinda Amani, kutoa msamaha, kuwa mwema, mkarimu na kuwatendea Matendo mengine ya Huruma. Kwa mantiki hiyo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linapotoa Ujumbe wa Kwaresima ambao unawagusa moja kwa moja Wanasiasa, Watawala au Viongozi wenye Nyadhifa Serikalini au kwenye Vyama vyao vya Siasa, Wanataaluma, Wafanyabiashara, Wakulima, Bodaboda, nk; anayelengwa huko ni Mkristo Mkatoliki. Na anapokemewa kuacha uovu, hafanywi hivyo kwa sababu ya cheo chake Serikalini au kwenye taaluma yake au popote pale, bali anakemewa kwa sababu ya “Ukristo” wake. Maana yeye ni Mkristo Mkatoliki kwa Sakramenti ya Ubatizo anayepaswa kuacha uovu na kutenda mema. Na kama ametenda uovu, anakumbushwa na kusisitizwa kutubu, kuongoka na kuacha kutenda maovu.

Askofu mkuu Ruwaichi, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani TEC.
Askofu mkuu Ruwaichi, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani TEC.

Na endapo Ujumbe wa Kwaresima wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, kwa Wakatoliki utaonekana unawagusa moja moja na watu wengine pia ambao sio Wakatoliki, basi ijulikane mapema kuwa ni kwa sababu maovu wanayoyatenda watu hao, yana uhalisia wa moja kwa moja na yale ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki linawakemea waamini wake Wakatoliki wasiyafanye. Sio kusudio la moja kwa moja la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwalenga waamini au waamini wasiokuwa Wakatoliki. Ikitokea hivyo, basi hiyo itakuwa ni “coincidence” tu. Lakini ikumbukwe pia kuwa hili ndilo jukumu la viongozi wa kiroho au kidini kukemea maovu kwa mtu mmoja mmoja, katika familia, jamii, Taifa na Dunia katika ujumla wake. Kwa kuyatambua hayo, wewe ambaye sio mwamini mkatoliki, utakapoguswa moja kwa moja na Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki, TEC kwa Wakatoliki, ukae kwa kutulia ili Ujumbe ukuingie, ukubadilishe na ukurudishe kwenye njia inayompendeza Mungu na wanadamu badala ya kutumia muda mwingi kutengeneza “Propaganda,” kuleta maigizo ya kutaka kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa Viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Ukweli wa Ujumbe wa Neno la Mungu unaokemea Maovu: Mauaji na Dhambi nyingine hauwezi kupingwa kwa kuwachukia viongozi wa dini. Dawa ya dhambi ni toba ya kweli na kusudio la dhati ya kuacha dhambi. Ili Mwenyezi Mungu amsamehe mtu dhambi zake, ni lazima mkosefu huyo akiri dhambi zake, ajutie, na akusudie kutokutenda dhambi tena. Kumchukia anayewakemea watu wasitende uovu, hakuwezi kuwatakasa watenda maovu hayo. Viongozi wa Kiroho ni sawa na Manabii ambao wanaleta Ujumbe wa Mungu kwa njia ya vinywa vyao. Ujumbe wa Mungu huwa hauletwi kwa lugha ya kubembelezana. Mungu anapowatuma Manabii wake kuuleta ujumbe wa kuwataka waache uovu na kujikita katika kutenda mema na haki.

Maaskofu Tanzania
28 Januari 2026, 14:30