Vatican,AVEPRO inapanua dhamira yake duniani kote kwa semina katika mabara yote!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kufuatia agizo lililotolewa na Papa Francisko, Shirika la Vatican la Tathmini na Uendelezaji wa Ubora katika Vyuo Vikuu na Vitivo vya Kanisa(AVEPRO,) limeandaa semina nne za kikanda katika miezi ya hivi karibuni katika mabara haya. Ni kutoka kupanua shughuli zake hadi Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Afrika, na Asia-Oceania, bila kupuuza Ulaya, hasa vyuo vikuu vya Kirumi na vituo vya kipapa. Chombo hiki AVEPRO kilichoanzishwa na Papa Benedikto XVI mnamo mnamo 2007, kinalenga kuhamasisha na kukuza utamaduni wa ubora ndani ya taasisi za kitaaluma za kikanisa, zile zinazotegemea moja kwa moja Vatican, na kuhakikisha vigezo vyao vya ubora vilivyothibitishwa kimataifa, kuongoza tathmini zinazolingana za kitaaluma na mipango ya kimkakati inayofuata.
Semina Nne Duniani kote
Kazi zilizotolewa na Papa, ambazo Shirika hilo hufanya kwa ushirikiano wa karibu na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, linaloongozwa na Kardinali José Tolentino de Mendonça, pia zinajumuisha, kuanzia mwaka 2023, utekelezaji wa utume wa AVEPRO katika mabara yote. Kiukweli, katika sehemu ya kwanza ya historia yake (2007-2023), Shirika hilo lilikuwa likifanya kazi hasa barani Ulaya, likianzisha michakato ya tathmini ya ubora wa kitaaluma kwa takriban taasisi 150 kati ya 200 zilizopo katika bara hilo. Hata hivyo, kama ilivyotajwa, utume wa AVEPRO unahusisha Ulimwengu mzima. Kwa sababu hiyo, Papa Francisko aliomba kupanua wigo wake wa utekelezaji zaidi ya Ulaya. Kwa lengo hilo, Shirika hilo limeandaa semina nne hadi sasa. Tatu zimefanyika mwaka 2024: Ya kwanza, iliyofanyika mnamo Mei 14 na 15, akililenga bara la Amerika Kaskazini (Marekani na Canada) na iliandaliwa Washington, D.C., na Chuo Kikuu Katoliki cha Amerika (CUA); ya pili, iliyolenga Amerika Kusini, ilifanyika huko Bogotá mnamo Septemba 10 na 11, iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Javeriana (PUJ); na ya tatu, kwa ajili ya Afrika, ilifanyika huko Kinshasa mnamo Novemba 12 na 13, iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Congo (UCC). Mnamo 2025, semina hiyo ilifanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thomas huko Manila (UST) nchini Ufilipino na ilikusudiwa kwa taasisi za kitaaluma Asia na Oceania.
Malengo ya semina hizi yalikuwa mengi. Kwanza kabisa, ilikuwa ni kuongeza uelewa wa kazi ambayo tayari imefanywa ndani ya taasisi za kitaaluma katika maeneo mbalimbali ili kukuza ubora wa kitaaluma, ikiwa ni pamoja na nguvu, udhaifu, fursa, na vitisho (SWOT). Pia ilikuwa muhimu kuelewa moja kwa moja hali ya taasisi hizo katika suala la muundo, utawala, mifumo ya vyuo vikuu vya kitaifa, idadi ya wanafunzi, na uhusiano wowote na mashirika ya ubora ya kitaifa au ya kimataifa. Zaidi ya hayo, mawasiliano ya kibinafsi na mamlaka za kitaaluma (kama vile Wakuu wa Shule, na wengine) na maprofesa yalikuwa muhimu. Kipengele hiki cha mwisho ni muhimu kwa kuanzisha uhusiano wa kuaminiana na kuheshimiana.
"Tafsiri" ya Veritatis Gaudium
Mahali pa kuanzia semina hizo ilikuwa "tafsiri" halisi ya utangulizi wa Katiba ya Kitume ya Veritatis Gaudium, pamoja na hati zingine za zinazohusiana na vyuo vikuu. Hizi zina mapendekezo yanayolenga kufikia kiwango cha juu cha ubora kinachoungwa mkono na utafiti, wazi kwa miktadha mingine ya kitaaluma na kijamii, iliyojengwa kupitia mitandao, na kuzingatia utambuzi na maendeleo ya kimifumo na mifumo mipya. Ahadi hii inakuza uundaji wa mtandao kati ya taasisi zenyewe, na kuziwezesha kushiriki masuala na wasiwasi unaojirudia katika Vituo mbalimbali na kuanzisha mipango ya pamoja kuhusu utafiti na ubadilishanaji wa maprofesa na wanafunzi. Mbali na Utangulizi wa Katiba ya Kitume Veritatis Gaudium, juhudi zilifanywa kurudia miongozo ya Papa Francisko inayopatikana katika "Mkataba wa Kimataifa wa Elimu," pamoja na nyongeza zilizofanywa na Papa Leo XIV.
Kutazama wakati Ujao
Hatimaye, semina hizi ziliwasilisha shirika la AVEPRO na mbinu zake za kufanya kazi, pamoja na huduma zinazotolewa katika uwanja wa ukuzaji ubora, zikisisitiza kigezo cha ufikiaji wazi wa mchakato wa tathmini na mwelekeo wa kimataifa, kitaaluma, na sinodi ya kanisa ya taasisi za kikanisa za elimu ya juu. Kazi iliyokamilishwa ilijumuisha kanuni tatu zinazowakilisha vyema mbinu ya AVEPRO: ukarimu, ushawishi, na roho ya kukosoa na chanya. Katika miaka ijayo, Shirika litaendelea kujenga juu ya maendeleo haya kwa kuandaa mikutano zaidi, ana kwa ana na mtandaoni. Ni muhimu kukuza utamaduni wa ubora utakaosababisha michakato ya tathmini ya kitaaluma ambayo itafaidi kweli vituo vya kikanisa vya elimu ya juu vya Kanisa Katoliki.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here