Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa Teule na ni muhtasari wa Habari Njema ya Wokovu. Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa Teule na ni muhtasari wa Habari Njema ya Wokovu.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 4 ya Mwaka A: Heri za Mlimani Muhtasari wa Injili ya Kristo Yesu

Heri hizi ni kiini cha Injili, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa Teule kuanzia Ibrahimu, nazo zatimiliza ahadi hizo si kwa kuzipanga tena kwa ajili ya kupata nchi, bali kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Heri hizi zachora uso wa Kristo na kufafanua mapendo, zaonesha wito wa mwamini anayeshiriki Fumbo la Pasaka; zinaangaza matendo na maisha ya kikristo, zinatoa ahadi za matumaini katika taabu, zikitangaza baraka na tuzo ya wokovu, yaani maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4, mwaka A wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Kiini cha ujumbe ni Heri za kiinjili, mwongozo wa maisha ya kikristo katika kuuelekea uzima wa milele mbinguni. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa; Heri hizi ni kiini cha mahubiri ya Kristo Yesu, muhtasari wa ahadi za Mungu kwa Taifa Teule kuanzia Ibrahimu, nazo zatimiliza ahadi hizo si kwa kuzipanga tena kwa ajili ya kupata nchi, bali kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Heri hizi zachora uso wa Yesu Kristo na kufafanua mapendo yake, zaonyesha wito wa mwamini anayeshiriki: Utukufu wa Mateso na Ufufuko wake, zinaangaza matendo na hali zilizo za maisha ya kikristo, zinatoa ahadi za matumaini katika taabu, zikitangaza baraka na tuzo ya wokovu, yaani, maisha ya uzima wa milele mbinguni (rej. KKK 1716-1717). Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema; “Ee Bwana Mungu wetu, utuokoe, utukusanye kwa kututoa katika mataifa, tulishukuru jina lako takatifu, tuzifanyie shangwe sifa zako” (Zab. 106:47). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Bwana Mungu wetu, utujalie kukuheshimu kwa moyo wetu, na kuwapenda watu wote kwa mapendo ya kweli.”

Heri za Mlimani ni Muhtasari wa Injili ya Kristo Yesu
Heri za Mlimani ni Muhtasari wa Injili ya Kristo Yesu   (@VATICAN MEDIA)

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Sefania (Sef. 2: 3, 3: 12-13). Sefania ni mmoja wa manabii wadogo, aliyeishi muda mfupi kabla ya kuharibiwa kwa Hekalu la Yerusalemi, na alihubiri miaka michache kabla ya Nabii Yeremia. Hivyo aliishi wakati wa machafuko ya kidini, kijamii na kisiasa yako juu sana; watu waliabudu sanamu, viongozi wa kisiasa waliishi katika ndimbwi la uovu, na viongozi wa kidini waliadhimishi ibada kwa Mungu ovyo ovyo. Katika hali hii, Nabii Sefania anatabiri kuwa siku ya hukumu na adhabu kwa watenda maovu, imekaribia (1:8-12). Hivyo anawaasa watu wanaomcha Bwana waendelee kumtafuta wasije nao wakakengeuka na kuadhibiwa. Na kwa maskini na walioonewa wasikate tamaa bali walitumainie jina la Bwana. Hata nyakati zetu wapo viongozi wanaotumia vibaya mamlaka waliyopewa, wakijilimbikizia mali kwa jasho na damu za maskini. Ujumbe kwetu ni huu; tukikumbwa na hali kama hiyo, tusikate tamaa na kujiingiza katika uovu kama wao, bali tuweke tumaini letu kwa Mungu, Yeye ni mwaminifu kwa ahadi zake, atatuokoa katika maovu yote. Ni katika tumaini hili wimbo wa katikati unasema hivi; “Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Bwana huishika kweli milele, huwafanyia hukumu walioonewa. Huwapa wenye njaa chakula, hufungua waliofungwa. Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane. Bwana huwapenda wenye haki; bali njia ya wasio haki huipotosha. Bwana atamiliki milele. Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Aleluya” (Mt. 5, 3; Zab. 145:7-10.)

Angalieni wito wenu mlioitiwa!
Angalieni wito wenu mlioitiwa!   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1kor 1:26-31). Ujumbe ni huu; Mungu amewachagua wanyonge wanaodharauliwa ili awaibishe wenye nguvu na vyeo vya kidunia, wasiomtumainia Yeye. Tunasoma hivi; “Angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, ili mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele zake”. Kumbe maskini na wanyonge wanainuliwa kwa hekima na uwezo wa kimungu. Na mateso wanayopata sasa si kitu yakilinganishwa na utukufu na fahari watakayoipa mbinguni. Nao watu waovu watapata hukumu ya Mungu kutokana na ufidhuli wao wa kutegemea mali na vyeo, wakidhani wamezipata kwa uwezo wao. Mzaburi anaonya kuwa hawatadumu katika fahari hizo, watakufa tuu kama mnyama, mali na vyote walivyojikusanyia, hawatachukua hata kimoja (rej. Zab 49). Ni katika tumaini hili tusiogope wala kukata tamaa tunapodhulumiwa, bali tuendelee kuweka tumaini letu kwa Mungu hakimu mwenye haki.

Siku ya hukumu na adhabu kwa watenda maovu imekaribia
Siku ya hukumu na adhabu kwa watenda maovu imekaribia   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo (Mt 5:1-12). Ni mwongozo na wasifu wa wale watakaoingia katika Ufalme wa Mungu kwa kuziishi Heri za Kiinjili. Ni wale wamtegemeao Mungu katika yote, yaani maskini wa roho, wenye huzuni, wenye upole, wenye njaa na kiu ya haki, wenye rehema, wenye moyo safi, wapatanishi, wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, wanaoshutumiwa na kuudhiwa na kunenewa kila neno baya kwa uongo, kwa ajili ya Kristo. Hawa wote wanaahidiwa furaha kubwa mbinguni. Hivyo heri hizi zinajibu tamaa asilia ya mwanadamu ya kutafuta furaha kila siku, furaha inayotimilika kwa Mungu pekee. Maana Mungu peke yake atosheleza (rej. KKK 1718). Ni katika muktadha huu, heri hizi zafunua sababu za uwepo wa mwanadamu, na lengo la mwisho la matendo ya mtu yaani kuingia katika furaha ya Bwana, kumwona Mungu, ndiye Heri halisi. Kwa maana Mungu alituweka duniani tupate kumjua, kumpenda, kumtumikia, na mwisho kufika kwake mbinguni, kushiriki naye uzima wa milele, kuingia katika utukufu wa Kristo na katika uzima wa Utatu Mtakatifu (rej. KKK 1719-1721). Heri hizi zapita ufahamu wa akili na nguvu za kibinadamu (rej. KKK 1722).

Heri za Mlimani Ni Kiini cha Ahadi za Mungu
Heri za Mlimani Ni Kiini cha Ahadi za Mungu   (@VATICAN MEDIA)

Ndiyo maana tunaalikwa kuwa maskini wa roho, kutambua kuwa maisha yetu na yote tuliyo nayo bila Mungu hayana maana yoyote. Ni umaskini wa roho ndio unaotuelekeza tuwe na upole na unyenyekevu, Kristo akiwa kielelezo chetu. Naye anatuambia; “Jifunzeni kwangu kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt. 11:29). Tukikosa upole na unyenyekevu wa moyo, tunaingia katika kilema cha kiburi na majivuno, vizingiti vya kuwa karibu na Mungu asili ya mema yote. Na ili tuwe karibu na Mungu tunapaswa kuwa na moyo safi, kwa kutokujihusisha na matendo machafu ya kimwili kwa ujumla wake, na kuwa na mwenendo safi na sahihi kwa maneno na matendo, kulingana na mapenzi ya Mungu. Moyo unatajwa kama kielelezo kwa kuwa ni kiini cha utu wa mtu (Mithali 4:23) na ndani yake hutoka mawazo mema au mabaya (Mk 7:20 – 23.) Kumbe, tunaona kuwa heri ya kweli haipatikani katika utajiri, wala katika utukufu, au mamlaka, au umaarufu wa kibinadamu, bali katika Mungu, aliye asili ya vitu vyote. Ndiyo maana ili tuweze kuingia katika ufalme wake kunatudai kuwa na kiu ya kutenda haki, kujiepusha na usujudu wa sanamu ya utajiri, mamlaka, au umaarufu kwa kupiga kelele katika ulimwenguni wa mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii (rej. KKK 1723). Kuepukana na mambo haya kwa nguvu zetu wenyewe tu, hatuwezi, isipokuwa kwa neema zake Mungu. Mama Kanisa akilitambua hili katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisali; “Ee Bwana, tunaleta dhabihu za ibada yetu kwenye madhabahu yako; uwe radhi kuzipokea na kuzifanya ziwe sakramenti ya ukombozi wetu”. Na hili ndilo tumaini letu kama sala baada ya Komunyo inayohitimisha maadhimisho ya dominika hii inavyosema; “Ee Bwana, sisi tuliokula sadaka ya ukombozi wetu, tunakuomba utuzidishie daima imani ya kweli kwa chakula hicho kiletacho uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo!

D4 Mwaka A Kanisa
29 Januari 2026, 15:15