Siku ya XXX ya Watawa Ulimwenguni,Februari 2:Watawa,mbegu za amani penye jeraha ya hadhi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Vyama vya Maisha ya Kitume limetuma barua yenye kichwa: "Unabii wa uwepo: maisha yaliyowekwa wakfu ambapo heshima hujeruhiwa na imani imejaribiwa.” Barua hiyo inakuja siku chache tu kabla ya Siku ya XXX ya Watawa Ulimwenguni kwa 2026, sanjari na Siku kuu ya Kutolewa kwa Bwana Hekaluni, itakayoadhimishwa Jumatatu tarehe 2 Februari, kwa Ibada ya misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV katika Basilika ya Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Barua imetiwa saini na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maisha ya wakfu na vyama vya Kitume Sr. Simona Brambilla, M.C.,Kardinali Ángel F. Artime, S.D.B. Makamu na Sr. Tiziana Merletti, S.F.P., Katibu Mkuu.
Ifuatayo ni barua kamili:
Wapendwa wanawake na wanaume waliowekwa wakfu, kwa barua hii, tunataka kuwafikia katika kila sehemu ya Dunia, katika maeneo mnayoishi na kutekeleza utume wenu, ili kutoa shukrani zetu kwa uaminifu wenu kwa Injili na kwa zawadi ya maisha ambayo huwa mbegu iliyotawanyika katika mikunjo ya historia. Maisha ambayo wakati mwingine yalioneshwa na majaribu, lakini yaliishi kila mara kama ishara ya matumaini. Katika mwaka uliopita(2025), wakati wa Ziara za Baraza la Kipapa na ziara za kichungaji, tumekuwa na kipaji cha kugusa na kuguswa na maisha haya, tukikutana na nyuso za watu wengi waliowekwa wakfu walioitwa kushiriki hali ngumu: mazingira yaliyooneshwa na migogoro, ukosefu wa utulivu wa kijamii na kisiasa, umaskini, kutengwa, uhamiaji wa kulazimishwa, hadhi ya wachache wa kidini, vurugu, na mivutano inayojaribu utu wa watu, uhuru, na wakati mwingine hata imani yao.
Uzoefu wa maisha ya wakfu
Uzoefu huu unaonesha jinsi kipimo cha kinabii cha maisha yaliyowekwa wakfu kilivyo na nguvu kama "uwepo unaobaki:" pamoja na watu waliojeruhiwa na watu binafsi, katika sehemu ambazo Injili mara nyingi huishi katika hali ya udhaifu na majaribu. "Kubaki" huku kunachukua aina na changamoto tofauti, kwa sababu ugumu wa jamii zetu ni tofauti: ambapo maisha ya kila siku yanaoneshwa na udhaifu wa kitaasisi na ukosefu wa usalama; ambapo watu walio wachache wa kidini hupata shinikizo na vikwazo; ambapo ustawi unaambatana na upweke, mgawanyiko, aina mpya za umaskini, na kutojali; ambapo uhamiaji, ukosefu wa usawa, na vurugu zilizoenea hupinga kuishi pamoja kwa raia. Katika sehemu nyingi za dunia, hali ya kisiasa na kijamii hujaribu uaminifu na huondoa matumaini: na hasa kwa sababu hiyo, uwepo wenu mwaminifu, mnyenyekevu, mbunifu, na wenye busara unakuwa ishara kwamba Mungu hawaachi watu wake.
Kubaki Kiinjili kamwe si kujiuzulu
Barua ya Baraza La Kipapa la Maisha ya wakfu inaendele: "Kubaki" Kiinjili kamwe si kutoweza kusonga au kujiuzulu: ni matumaini hai yanayozalisha mitazamo na ishara za amani: maneno yanayo ondoa silaha pale ambapo majeraha ya migogoro yanaonekana kufuta udugu, mahusiano yanayoshuhudia hamu ya mazungumzo kati ya tamaduni na dini, chaguzi zinazowalinda wadogo hata wanaposimama kando yao huja kwa gharama, uvumilivu katika michakato hata ndani ya Jumuiya ya Kanisa, uvumilivu katika kutafuta njia za upatanisho ili kujengwa kupitia kusikiliza na kuomba, ujasiri katika kukemea hali na miundo inayokataa utu na haki ya watu. Kwa sababu, hasa hiyo ni kweli, kubaki huku si chaguo la kibinafsi au la kijumuiya tu, bali kunakuwa neno la kinabii kwa Kanisa zima na kwa ulimwengu. Katika tendo hilo la kubaki kama mbegu inayokubali kifo ili maisha yaweze kustawi, katika aina mbalimbali na zinazokamilishana, unabii wa maisha yote yaliyowekwa wakfu unaoneshwa. Maisha ya kitume huonesha ukaribu unaofanya kazi unaounga mkono hadhi iliyojeruhiwa; ulinzi wa maisha ya kutafakari, kupitia maombezi na uaminifu, tumaini wakati imani inapojaribiwa; Taasisi za kidunia hushuhudia Injili kama chachu ya fumbo katika hali halisi za kijumuiya na kitaaluma; Ordo virginum yaani Shirika la Mabikira, huonesha nguvu ya kujinyima na uaminifu unaofungua wakati ujao; maisha ya kibinafsi ya Waerimiti, hukumbusha ukuu wa Mungu na muhimu ambao huondoa silaha moyoni.
Amani haizaliwi kutokana na upinzaji, bali kukutana
Katika utofauti wa aina hizi, unabii mmoja huchukua umbo: kubaki na upendo, bila kuacha, bila kukaa kimya, na kufanya maisha ya mtu kuwa Neno la wakati huu katika historia. Ni ndani ya unabii huu wa kubaki ndipo ushuhuda wa amani unapokomaa. Papa Leo XIV amekumbusha hili kwa kuendelea katika hotuba zake, akionesha amani si kama utopia wa kufikirika, bali kama safari yenye kuhitaji usikivu na ya kila siku inayohitaji kusikiliza, mazungumzo, uvumilivu, ubadilishaji wa akili na moyo, na kukataa mantiki ya wenye nguvu wanaowashinda wanyonge. Amani haizaliwi kutokana na upinzani, bali kutokana na kukutana, kutokana na uwajibikaji wa pamoja, kutokana na uwezo wa kusikiliza na kusafiri kisinodi, kutokana na upendo kwa wote katika namna ya Injili, ambayo kulingana nayo wote ni kaka na dada. Kwa sababu hiyo, maisha yaliyowekwa wakfu, yanapobaki karibu na majeraha ya ubinadamu bila kujisalimisha kwa mantiki ya migogoro, lakini bila kukataa kusema ukweli wa Mungu kuhusu ubinadamu na historia, huwa, mara nyingi bila shangwe, fundi wa amani.
Mtindo wa Kiinjili unaoendelea kutafuta kila siku
Wapendwa wanawake na wanaume waliowekwa wakfu, tunawashukuru kwa uvumilivu wenu wakati matunda yanaonekana kuwa mbali, kwa amani mnayopanda hata wakati haitambuliwi. Tunaendelea kuthamini uzoefu wa Jubilei ya Maisha Yaliyowekwa Wakfu, ambayo ilituita kuwa mahujaji wa matumaini katika njia ya amani. Hii si kauli mbiu au mtindo. Tulipitia kwa uhalisia hata katika safari iliyoandaa mkutano wetu jijini Roma. Badala yake, ni mtindo wa kiinjili unaoendelea kutafuta kila siku, popote ambapo heshima inajeruhiwa na imani inajaribiwa. Tunamkabidhi kila mmoja wenu kwa Bwana, ili awafanye imara katika tumaini na upole moyoni, muweze kubaki, kufariji, na kuanza upya: na hivyo kuwa, katika Kanisa na katika ulimwengu, unabii wa uwepo na mbegu ya amani.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here