Sala ya Kuombea Umoja wa Wakristo Ni Mchakato Endelevu
Sr. Roselyne Wambani Wafula, FSP, - Roma.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujipambanua kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kujikita katika kutafuta na kudumisha haki na amani, sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia pamoja na mambo mengine: Kuhusu umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, 2033, huko mjini Yerusalemu, mahali ambapo Kristo Yesu aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, Siku ile ya Pentekoste, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo huku akirejea kwenye kauli mbiu yake: "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja.” Familia ya Mtakatifu Paulo, yaani Wanapaolini, Jumuiya ya Kimataifa ya Mapadre, Watawa wa kike, na Waamini walei, jioni ya kuamkia Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa walikusanyika kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, wakirudia ombi la Mtakatifu Paulo mwenyewe la 'Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja' (Waefeso 4:5). Ikumbukwe pia kwamba, Januari 15, 2026 Familia hii ya Wapaolini, iliadhimisha kumbukizi ya Karne Moja ya ujio wao katika Jiji la Milele yaani Roma. Masomo tuliyoyasikia yote yanatuongoza kwenye taswira moja kubwa: mwanga ambao Mungu huwasha pale ambapo panaonekana kuwa na mipaka, migawanyiko, na giza.
Hayo yamesemwa na Mheshimiwa Padre Roberto Ponti, Mkuu wa Shirika la Wapaulini, Kanda ya Roma katika mkesha wa Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, tarehe 24 Januari 2026. Nabii Isaya anazungumzia Galilaya ya Mataifa, nchi ya kupita, pembezoni, iliyokumbwa na mgongano wa watu na tamaduni tofauti. Kulingana na Injili ya Mathayo, ambapo Yesu anaanza huduma yake ya hadharani: Yesu haanzii katikati au mijini, bali kutoka pembezoni; si kutoka sehemu ambazo tayari zipo salama, bali kutoka kwa zile zilizo wazi na zilizojaa watu wengi. Nuru hii haifuti tofauti, hailainishi hadithi, bali hupita ndani yake, na kuzibadilisha. Ni nuru inayotuelekeza kwenye wongofu: "Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia." Mt 3:2. Katika Injili, wongofu haumaanishi tu kurekebisha kitu kibaya, na mienendo isiyo ya Kimungu, bali kubadilisha mwelekeo, kuelekeza maisha kwenye kitovu kipya. Na hii haitumiki tu kwa waamini binafsi, bali pia kwa jamii, na kwa Kanisa kwa ujumla. Katika maadhimisho ya Juma la Sala kwa ajili ya Kuombea Umoja wa Wakristo, wito huu wa toba na wongofu wa ndani unachukua maana ya kina zaidi. Wongofu unamaanisha kujiruhusu kuongozwa na kile kinachounganisha, badala ya kile kinachotofautisha au kinachogawanya; inamaanisha kumweka Kristo Yesu katikati, kuacha mitazamo hiyo, hata ya kikanisa, hata ya kiroho, ambayo wakati mwingine huwa chanzo cha umbali au upinzani. Kumbe, mchakato wa umoja wa Wakristo ni zoezi endelevu miongoni mwa wote wanaothamini tunu na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo kuwa nuru na mwanga wa kila hatua katika safari ya Imani na Maisha ya kawaida.
Padre Roberto Ponti, anasema, tunafahamu ni kiasi gani Padre Alberione alitafuta umoja na kuomba kwa ajili ya jumuiya zake na kwa Kanisa zima. Mtakatifu Paulo, katika Nyaraka zake kwa Waefeso, na hasa katika nukuu iliyotumika kama msingi wa sala ya kwa ajili ya kuombea Umoja wa wakristo kwa Mwaka 2026 anatumia maneno rahisi lakini yenye maana kubwa: mwili mmoja, Roho mmoja, tumaini moja, Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Ni kama pumzi nzito kutoka Kanisani, akijikumbusha kile kinachomfanya kuwa kiini chake. Umoja haupatikani kutokana na makubaliano ya Shirika au mkakati wa kidiplomasia ambao labda tunaweza kuufikia kwa juhudi fulani, bali kutokana na zawadi iliyopokelewa: umoja wa Roho, ambao lazima uhifadhiwe "kwa kifungo cha amani." Wakati huo huo, Mtakatifu Paulo haoneshi umoja kama umoja. Kwa kila mmoja, anasema, neema tofauti imetolewa. Karama ni nyingi, huduma ni tofauti, lakini mmoja ni mwili unaokua wakati kila karama inapomwilishwa kama huduma na si kama kujionesha. Umoja wa Wakristo hauondoi wingi, bali unauelekeza kwenye ujenzi wa ushirika. Migawanyiko ya Korintho si tofauti sana na yetu: "Mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo, mimi ni wa Kefa..." Wakati wa kumiliki, ambayo mara nyingi hutokana na ubinafsi, wakati kila mtu anajifikiria sana na kuchukua nafasi ya Kristo Yesu, kwa kurejea: mtu, busara, mila inapopewa kipaumbele, basi hata Injili ina hatari ya kuondolewa nguvu zake. Mtakatifu Paulo yuko wazi: Kristo Yesu hajagawanyika. Na hakuna hata mmoja wetu aliyebatizwa kwa jina la mwingine, isipokuwa kwa jina, la Baba, la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
Kuadhimisha Ekaristi hii hapa, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma, usiku wa kuamkia sikukuu ya kuongoka kwa Mtume Paulo, huyapa maneno haya uzito maalum. Mtume Paulo hakukutana na wazo la kidini lenye kushawishi zaidi, bali Mtu aliyebadilisha mtazamo wake kwa kiasi kikubwa. Wongofu wake ni mabadiliko kutoka kwa ukweli uliomilikiwa hadi ukweli uliopo; kutoka kwa utambulisho unaotengana hadi utume unaounganisha; kutoka kwa Mungu aliyelindwa kwa silaha hadi Mungu aliyetangazwa na kushuhudiwa; na uzima, mkutano unaoweka huru Mataifa yote bila kuzingatia utofauti wowote ule, maana umoja ni nguvu na utengano, ni udhaifu.Katika mahali hapa, hatuwezi kushindwa kukumbuka miaka mia moja tangu kuwasili kwa Familia ya Mtakatifu Paulo hapa Roma, iliyoadhimishwa hivi karibuni. Tukio dogo katika historia ya dunia, lakini lililopewa umuhimu kwa safari ya familia ya Wanapaolini, ya kidini iliyoitwa kutumikia Injili kwa kutumia vyombo vyote vya Upashanaji Habari au Mawasiliano ya Kijamii. Kuja Roma, kwa Mapadre wa Mtakatifu Paulo na Mabinti Wa Mtakatifu Paulo, na hatimaye familia nzima ya Mtakatifu Paulo, kama ilivyo sasa, kulimaanisha kuchagua kitovu cha kutochukua nafasi, bali kujiweka katika huduma ya ulimwengu wa Kanisa; kukubali changamoto ya kukutana, majadiliano ya kiekumene, pamoja na kuamini kwamba inawezekana kutangazwa kwa Injili kwa kutumia lugha, tamaduni, na hisia tofauti. Ni hadithi iliyounganishwa sana na hamu ya umoja ambayo tunaikabidhi kwa njia ya sala zetu leo.
Umoja wa Wakristo si wazo la kufikirika wala anasa kwa nyakati bora. Ni hitaji la Kiinjili, ili ulimwengu uweze kuamini. Katika wakati uliojaa mgawanyiko mkubwa, ushirika hata usio kamili, hata wa kuchosha tayari ni ushuhuda. Hatujaitwa kujenga umoja kwa juhudi zetu pekee, bali kulinda kile ambacho tumepewa, tukiruhusu kuongoka daima na Injili. Basi, katika sherehe hii, tuombe neema ya wongofu wa kibinafsi na wa kikanisa unaoturudisha kwenye yale yaliyo ya msingi, yale mambo muhimu. Mwishoni na tujifunze, kama Mtume Paulo, kupoteza kitu chetu wenyewe, ili kuwa wa Kristo Yesu kikamilifu zaidi. Na nuru iliyozuka Galilaya ya Mataifa iendelee kuangaza njia ya Kanisa, hadi sote kwa pamoja tutakapofikia umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu, katika utimilifu wa Kristo Yesu. Ndivyo alivyohitimisha mahubiri yake Mheshimiwa Padre Roberto Ponti, Mkuu wa Shirika la Wapaulini, Kanda ya Roma katika mkesha wa Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, tarehe 24 Januari 2026.
Wakati huo huo, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam anasema kuna njia mbalimbali za kuweza kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yako. Kwa Ubatizo, kwa kusoma na kusikiliza Neno la Mungu na kwa kupokea Sakramenti za Kanisa katika hali ya neema na uchaji. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, Rej. Gal 1:15, akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Mtume Paulo anasema, “Nilipokuwa nimekaribia kufika Dameski, mnamo muda wa kama saa sita mchana, kulitokea mwanga mkali kutoka mbinguni ukaangaza pande zote kuni zunguka. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli! Sauli! Mbona unanitesa?’ Nikajibu, ‘Wewe ni nani Bwana?’ Naye akajibu, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti unayemtesa.” Mdo 22:6-8. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi anasema, mtu yeyote anamtesa na kumdhulumu Mkristo atambue kwamba, anamtesa na kumdhulumu Kristo Yesu. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina wito wa Sauli, jinsi alivyoitwa na Kristo Yesu, akamwongokea Mungu, toka katika upofu mwili, akabahatika kuuona Mwanga wa kweli, Kristo Yesu Mfufuka, akawa kweli ni chombo kiteule cha Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Jina la Mungu kwa watu wa Mataifa. Rej. Mdo 9:15.