Mtakatifu Don Bosco: Mwalimu, Baba na Mlezi wa Vijana wa Kizazi Kipya!
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB, - Iringa, Tanzania.
Mtakatifu Yohane Bosco, Padre, Baba na Mwalimu wa vijana wa kizazi kipya, anakumbukwa na kuadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari. Ni Padre aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa vijana waliokimbilia mjini Torino, Kaskazini mwa Italia kutafuta fursa za ajira baada ya kutokea kwa Mapinduzi ya Viwanda wakati huo. Kwa kusoma alama za nyakati, akaanzisha mahali pa kuwakutanisha vijana, akawapatia malezi, makuzi na majiundo makini ya kitaaluma na huo ukawa ni mwanzo wa Vituo vya michezo na malezi ya vijana Parokiani “Oratorio.” Mtindo wake wa elimu na makuzi kwa vijana ukawa ni dira na mwongozo wa Mtakatifu Francisko wa Sale, Muasisi wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco. Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco, “Societas Sancti Francisci Salesii, SDB” lilianzishwa na Mtakatifu Yohane Bosco kunako mwaka 1859 na kukita utume wake miongoni mwa vijana maskini, huko Torino, Kaskazini mwa Italia. Wasalesiani wa Don Bosco wanaendelea kujisadaka hasa kwa ajili ya malezi, makuzi na elimu kwa vijana kwa kuwekeza hasa katika sekta ya elimu, vituo vya mafunzo, kilimo na utume katika vyombo vya mawasiliano ya jamii. Wasalesiani wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwani matunda yake ndani ya mti mkubwa ambao ni Familia ya Kisalesiani, Familia ya Don Bosco, ambapo leo hii wapo katika Mataifa 134 duniani ikiwemo Tanzania, Kenya, Sudani na Sudani Kusini, ishara ya imani, matumaini na mapendo. “Kwa ajili yenu nasoma, kwa ajili yenu nafanya kazi, kwa ajili yenu naishi, kwa ajili yenu nipo tayari hata kutoa maisha yangu” Haya ni maneno ya Mtakatifu Yohane Bosco, anayeonesha kwamba maisha yake yote akili yake, nguvu zake, muda wake, kazi yake, na hata uhai wake aliyatoa kama sadaka kwa ajili ya malezi, wokovu na ustawi wa vijana.
Mtakatifu huyu alizaliwa mwaka 1815 katika karne ya 19 huko Torino nchini Italia ambapo kila tarehe 31 Januari Kanisa linafanya kumbukumbu ya kumuenzi Mtakatifu huyu. Anakumbukwa kama Mwanzilishi wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco, Masista au Mabinti wa Mama yetu Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Wasalesiani Washiriki, na kama baba wa Familia ya Kisalesiani ya leo. Vilevile, anakumbukwa katika Kanisa kama mlezi na mchungaji Mtakatifu wa vijana, aliyefungua njia ya utakatifu kwa vijana, aliyetoa mbinu ya malezi inayoambatana na hali ya kiroho, na aliyepokea kutoka kwa Roho Mtakatifu karama maalum inayoendana na nyakati za sasa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana (Angelus) ya Dominika tarehe 31 Januari 2022, alimkumbuka Mtakatifu Yohane Bosco katika sikukuu yake kwa maneno ambayo bado yana umuhimu mkubwa hadi leo. “Tumfikirie mtakatifu huyu mkubwa, baba na mwalimu wa vijana. Hakujifungia ndani ya sakristia, wala hakujitenga na mambo yake binafsi. Alitoka kwenda mitaani kuwatafuta vijana, kwa ubunifu uliokuwa alama yake ya pekee.” Don Bosco alikuwa mtu aliyewapenda sana vijana na kujitoa kikamilifu kwa wokovu wao. Maisha yake yalikuwa ushuhuda hai wa Yesu Kristo na Injili yake, akiishi katika umoja wa karibu na Kanisa na Baba Mtakatifu. Alijitambulisha kwa maisha ya sala ya kudumu, uhusiano wa ndani na Mungu, na ibada ya dhati kwa Bikira Maria, Msaada wa Wakristo. Kwa neema ya Roho Mtakatifu, alipokea karama za kiroho na hata miujiza, yote kwa lengo la kuwalea, kuwalinda na kuwaongoza vijana katika njia ya imani na utakatifu.
Kila mwaka, katika Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco kupitia Mkuu wa Shirika ulimwenguni, hutolewa Kauli Mbiu inayobeba ujumbe fulani kama nafasi kwa Familia ya Kisalesiani kuungana pamoja kwa sala na tafakari, kusikiliza na kushirikishana pamoja. Kwa namna hiyo, kila kikundi kupitia wito na karama yake kinapata chakula cha safari ya kiroho, ya karama na ya kichungaji. Tukikumbuka kauli Mbiu ya mwaka 2025, Tukiwa tumejikita katika matumaini, tu mahujaji na vijana, kauli mbiu ilitupatia fursa ya kuunganika na kutembea na Kanisa katika kutafakari fumbo la Kristo, ambaye ni chanzo na msaada wa tumaini letu. Kupitia mada ya Tumaini halitahayarishi, tuliweza kutafakari ni kwa jinsi gani fumbo la Mungu muumbaji anayetutembelea kupitia Mwanawe wa pekee linavyoendelea kututegemeza hadi sasa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Tafakari hiyo imetusaidia kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku na kutambua ukweli halisi unaoakisi fumbo la upendo wa Mungu kwetu sisi. Tumaini ni nguvu na uthibitisho ambao “tayari” tunauishi na kuutafakari. Tumaini pia ni chanzo cha nguvu na furaha kwa ambao bado hawajavipokea.
Kauli Mbiu ya Mwaka 2026 iliyotolewa na Mkuu wetu wa Shirika, Padre Fabio Attard, SDB inasema “Lolote atakalowaambia fanyeni” (Yn 2,5), inatualika kuwa na imani thabiti na kutambua changamoto na mahitaji ya wakati wetu na kuamini katika Neno linaloleta mabadiliko, linalobadilisha changamoto kuwa fursa, uchovu wa malezi kuwa tumaini. Ni mwaliko unaowagusa wote vijana, walezi, familia, jumuia – na inayotafsiriwa katika chaguzi za kila siku za Haki, Usawa na Utumishi. Kauli mbiu hii ni kama dira ya kiroho na ya kielimu-inatukumbusha kuwa kuelimisha maana yake kujiweka karibu, kusikiliza, kuleta uhuru wa talanta na vipaji kwa kila kijana. Ishara ya kwanza huko Kana inatuonyesha ujumbe wa msingi wa Yesu: anatualika kuyaweka maisha yetu mikononi mwa neno lake na kuliamini. Leo, Kana ni mahali tunapoishi: nyumbani, kazini, katika utume wetu, na miongoni mwa vijana, walimu na wazazi tunaokutana nao kila siku. Kama ilivyokuwa Kana, hata leo Maria ana nafasi muhimu sana. Anatembea pamoja nasi na anatualika tuamini, tuchukue hatua ya imani kwa hiari, ili tuwe watumishi wa kweli. Kana ni mahali pa kawaida na pa kimya, lakini ndipo mpango wa upendo wa Mungu kwa wanadamu unatimia. Kana ni kila mahali tunapotumwa, mahali ambapo Mungu anaendelea kuwa karibu nasi kupitia watu wanaolisikiliza Neno lake, kuliamini na kuliishi. Ikiwa Kana ya Galilaya ni kila mahali tunapoishi, basi sisi ndio tunaalikwa na Bwana kuwa ishara na waleta upendo wake kwa vijana na kwa watu wote.
Bikira Maria angeweza kuchagua kukaa pembeni na kusema, “Si jukumu langu”, hata kama aliona wazi aibu na huzuni iliyokuwa inakuja kwa kuishiwa na divai. Lakini hakufanya hivyo. Hakubaki kimya wala hajitengi. Anachagua kujali na kuchukua hatua. Hapo ndipo changamoto kubwa kwa sisi vijana inapoanzia: ni kwa kiwango gani tunaruhusu yale yanayotokea katika jamii yetu—shuleni, mitandaoni, majumbani, kazini au miongoni mwa marafiki zetu—yatuguse kweli? Tunachukua msimamo gani tunapoona ukosefu wa haki, maumivu, upweke au kukata tamaa, ilhali ni rahisi kusema, “Sio tatizo langu” au “Sina cha kufanya”? Chaguo la Bikira Maria linatukumbusha kwa upole lakini kwa nguvu kwamba kutojali siyo suluhisho. Kutojali kunaonekana kuwa salama, lakini kiukweli kunaruhusu mambo mabaya kuendelea. Kimya chetu kinaweza kuumiza kama maneno mabaya au vitendo vibaya. Bikira Maria anatualika sisi vijana kuwa macho, wenye moyo unaosikia, na wenye ujasiri wa kuchukua hatua—hata kama ni ndogo kwa ajili ya wengine. Kwa kumfuata Yesu, tunaitwa tusibaki watazamaji wa maisha, bali kuwa washiriki wanaoleta mabadiliko chanya. Kama Bikira Maria, tunaweza kuwa sauti na mashuhuda wa matumaini, ishara ya upendo, na mwanzo wa mabadiliko chanya katika ulimwengu mamboleo. Nawatakia Sherehe njema ya Mtakatifu Yohane Bosco.