Miaka 60 ya Maisha na Utume wa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Tanzania 1966-2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 18 Septemba 2025 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., uliongozwa na kauli mbiu: “Damu ya Kristo, Tumaini la Ulimwengu” na kuwapongeza waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, waliokuwa wazi kwa utendaji wa Roho Mtakatifu, wakaweza kusoma na kufasiri alama za nyakati na hatimaye kujibu kwa njia yenye mwanga wa kiinjili kwa mahitaji ambayo yalijitokeza hatua kwa hatua. Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na mambo mengine alikazia kuhusu: wito wa maisha ya kitawa yanayosimikwa katika ujenzi wa jumuiya, kama mahali patakatifu na chemchemi ya maongozi; ushuhuda na nguvu katika utume; ili katika ushirika, wema uweze kuongezeka na kukua. Pili ni Utii kama kielelezo cha upendo, ili hatimaye, kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Utii, katika maana yake ya ndani kabisa inakita mizizi yake katika dhana ya kuwasikiliza wengine kwa bidii na ukarimu; Utii ni tendo kuu la upendo linalosimikwa katika imani, sadaka na ujenzi wa mahusiano ya kudumu; maisha ya pamoja na hivyo kuimarishwa katika uaminifu. Utii ni shule ya uhuru katika upendo. Mtakatifu Gaspari Del Bufalo alisoma alama za nyakati. Alikuwa na uwezo wa: kutazama, kutathmini, kupenda na kisha kuyamwilisha yote haya katika matendo, tayari kuwahudumia watu katika mahitaji yao msingi, huku wakiitambua sauti ya Mungu katika umaskini wa jirani zake. Hii ni changamoto kwa wanashirika katika ulimwengu mamboleo kujikita katika maadili, ili kusonga mbele! Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 12 Januari 2025 alimtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini, kuwa ni Mwenyeheri. Yeye alizaliwa tarehe 28 Agosti 1795 huko Spoleto, Perugia nchini Italia. Akapewa daraja Takatifu ya Upadre tarehe 19 Desemba 1818.
Tarehe 15 Agosti 1820 akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, lililokuwa limeanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo tarehe 15 Agosti 1815. Alijiunga na Shirika baada ya kuvutiwa sana na mahubiri yaliyotolewa na Mtakatifu Gaspari, kuhusu Fumbo la Ukombozi chemchemi ya upendo wa kimisionari. Kumbe, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo ni msingi wa ukombozi wa mwanadamu na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote. Tasaufi hii ina msingi wake katika Neno la Mungu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo ndilo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa na maisha ya Mkristo kwa jumla. Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa imani ya Kikristo na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. Rej KKK 1324 na 1327. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu walipotua nanga ya matumaini kwa watu wa Mungu nchini Tanzania, tarehe 19 Mei 1966, chini ya usimamizi na uongozi wa Mwenyeheri Giovanni Merlini, ambaye kwa sasa masalia yake yanatembezwa kwenye nyumba za Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, kama sehemu ya kumbukizi ya tukio hili la kihistoria. Maadhimisho haya yamezinduliwa na Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Tanzania kwa kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi watatu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu nao ni: Padre Revocatus Bernard, C.PP.S.; Padre Yohanes Mfilinge, C.PP.S., pamoja na Padre Laurent Kabila, C.PP.S. Waamini walei wanaoshiriki maisha, utume na karama ya Shirika walipewa mishumaa, ili wawe ni nuru na mwanga wa imani, matumaini na mapendo, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa sanjari na kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa mifano bora ya maisha yao.
Kumbukizi ya Miaka 60 ya Maisha na Utume wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ni ushuhuda wa safari ndefu ya imani, matumaini na mapendo, iliyowagusa watu wengi katika maisha na utume wao na kwamba, hii ni fursa ya kuendelea kuimarisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika wongofu wa kimisionari na shughuli za kitume na kichungaji zinazotekelezwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., ndani na nje ya Tanzania, sanjari na kuyatakatifuza malimwengu. Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, nchini Tanzania katika wosia wake kwa Mapadre wapya amewataka wasiogope katika maisha na wito wao kwani Mwenyezi Mungu: atawalinda, atawategemeza, atawapatia nguvu na kuwaongoza kwani wao ni vyombo na wajumbe wa Neno la Mungu wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu; wawatakase kwa ile kweli “Neno lako ndiyo kweli.” Yn 17:17. Neno la Mungu ndilo msingi wa ukweli halisi na msingi wa utakatifu. Watambue kwamba, katika maisha na utume wao, Mapadre wanashirikiana na Mwenyezi Mungu anayefanya kazi ndani mwao kwa ajili ya wokovu kwa watu wake: Kiroho na kimwili; Kifikra, kielimu sanjari na kulea pamoja na kukuza dhamiri nyofu, ili kutakatifuza nyoyo za waamini wao, ili wapendane kama Mwenyezi Mungu anavyowapenda.
Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA., amekazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Thamani ya wito, uhai, maisha na utume wao kwamba, watambue kuwa wao ni watoto wateule wa Mungu na kwamba, Mwenyezi Mungu ana mpango na malengo nao, ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi utume wao, huku wakitenda kazi ya Kristo Yesu; Mapadre anasema Askofu Musomba ni wawakilishi wa Kristo, kichwa cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, wanaotekeleza utume wao kwa: kufundisha, kutakatifuza na kuongoza. Mapadre ni Kristo wa pili “Alter Christus” wanapotekeleza utume wao katika Kanisa. Utume huu unafumbatwa katika maisha ya Kristo mfufuka, anaendelea kufundisha, kutakatifuza na kuliongoza Kanisa lake. Hivyo Mapadre wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa uaminifu na ukamilifu; kwa unyenyekevu wa moyo ambao kimsingi ni chimbuko la utii wa kweli. Majiundo yao sasa yawawezeshe kutekeleza vyema utume wao wa: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Waamini walei wanachangia kwa kiasi kikubwa katika: Maisha, malezi, miito na majiundo ya Mapadre wao, lakini Mwenyezi Mungu anayewaita anaangalia undani wa maisha yao! Mapadre wanahimizwa kuwa ni vyombo vya huruma ya Mungu na msamaha; wawe ni mifano bora ya kuigwa; wakite maisha yao katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo huruma: kiroho na kimwili. Wawe ni mifano bora ya maisha ya kiroho, maadili na utu wema. Maneno yao yawe ni ya hekima na busara ili wawavute waamini katika safari ya kwenda mbinguni, huku wakiwatangulia kwa kuwaonesha njia. Waoneshe huduma ya upendo kwa wote, hata ikiwabidi kuyamimina maisha yao! Wasiogope kukemea pale waamini wao wanapotangatanga katika imani na utu wema; wanapodanganywa na kutopea katika upotevu wa imani. Wawafundishe kweli za imani ya Kanisa Katoliki.
Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Ili kweli Mapadre waweze kuwa ni wahudumu wa kweli wa Sakramenti za Kanisa wanapaswa kusimika maisha yao katika: Sala, tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; wawe ni mashuhuda wa usafi wa moyo na kwamba, kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu wataweza kukwepa vishawishi na mitego katika maisha na wito wao, daima Kristo Yesu awe ni dira na kiongozi wa maisha yao. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, daima alitoka na kuwaendea watu ili kuwafundisha, kuwaganga na kuwaponya magonjwa na madhaifu wao; kuwasamehe dhambi zao na hivyo kuwarudishia tena hadhi yao kama wana wa Mungu kwa kuwahubiria furaha ya Injili inayopata chimbuko lake katika Kristo Yesu.
Injili anasema Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Waamini wajibidiishe kulifahamu Neno la Mungu, kulitafakari, kulisali na kulimwilisha katika vipengele mbalimbali vya maisha yao. Mapadre wahakikishe kwamba, wanawafundisha waamini wao kuhusu Neno la Mungu; Mafundisho Tanzu ya Kanisa, pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili waamini wao waweze kuwa makini na kamwe wasimezwe na malimwengu na hatimaye, wakakengeuka na hivyo kugeuka kuwa ni vibaraka. Mapadri wanaitwa na kutumwa: Kufundisha, Kuhubiri na kuishi kile wanacho hubiri. Kwa upande wao, waamini wanapaswa kuwa tayari kufundishwa, kuongozwa na kutakatifuzwa. Waachane na kiburi kwani kiburi kinafunga neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre wajitahidi kuponya hofu, makovu na madonda ya ndani. Amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kiutu kumbe hakuna sababu ya kutangatanga, bali waamini watulie tu kama “maji mtungini.” Waamini wanapojikuta wakihangaika katika imani, utu wema na maadili wachunguze mambo msingi yanayopungua katika maisha yao. Ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, Wakristo wanapaswa kujikita katika malezi na majiundo makini ya watoto wao; watambue na hatimaye, waweze kuitika vyema miito yao mbalimbali ndani ya Kanisa.
Mwishoni mwa mahubiri yake Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA alisema: sasa ndio wakati wa kumwilisha: Tasaufi, maisha ya jumuiya na utume wao unahamasishwa na viongozi waliozama katika karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Anawapongeza Mapadre wapya kwa kutikia na kuvumilia malezi na majiundo yao sasa wako tayari kuishi wito na karama ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, kwa kujitahidi kumwilisha yote waliojifunza wakati wa malezi na makuzi yao ya Kipadre na kwamba, Utii unasimikwa katika unyenyekevu wa moyo! Waendelee kujisikia nyumbani wakiwa ndani ya Shirika, wakite maisha yao katika Usafi wa moyo na kwamba, maisha ya Jumuiya ni mlinzi mkuu wa maisha na wito wa Kipadre; Maisha ya kijumuiya yanalinda na kudumisha viapo vya maisha na utume wa Kipadre.
HISTORIA YA MIAKA 60 YA SHIRIKA LA WAMISIONARI WA DAMU AZIZI YA YESU: 1966 HADI MWAKA 2026: Mwanzo wa Shirika: Shirika la Wamisonari wa Damu Azizi ya Yesu (Missionaries of the Precious Blood, C.PP.S., na hapa Tanzania limesajiliwa kama (The Society of The Precious Blood), ni Shirika la kazi za kitume la mapadre na mabruda lililoanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo tarehe 15 Agosti 1815 huko Giano, Italia, katika Abasia ya Mtakatifu Felix na kuwekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mama Bikira Maria na usimamizi wa Mtakatifu Francisko Xsaveri. Lengo la Mtakatifu Gaspari katika kuanzisha Shirika lilikuwa ni kueneza upendo wa Kristo Yesu aliouonesha alipomwaga Damu yake Azizi pale Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ndiyo maana Gaspari alisema, “natamani niwe na ndimi elfu ili upendo huu uwafikie watu wote.” Kuenea kwa Shirika: Tangu mwanzo huo, maelfu ya wamisionari wamevutwa na moyo wa Mtakatifu Gaspari na wameendeleza utume huo. Licha ya changamoto nyingi za mwanzoni, Shirika liliendelea kukua na kuenea hata nje ya Italia. Hadi sasa kuna Wanashirika takriban 500 na wameenea katika Mabara yote duniani katika nchi zaidi ya 20 zilizogawanyika katika: Kanda 8, Vikarieti 2 na Misheni 2. Karama ya Shirika.
Wamisionari wa C.PP.S., wanaongozwa na mihimili mikuu mitatu yaani: Utume, Maisha ya Jumuiya na Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu. Kwa Mtakatifu Gaspari na hata kwa wanashirika wote, Kristo Yesu kumwaga Damu yakeAzizi ni alama ya upendo mkuu wa Mungu kwa watu wa kila kabila, lugha, jamaa na Taifa (Ufu.5:9; 2kor.5:14). Tasaufi hii ya Damu Azizi ndiyo inayowahamasisha na kuwasukuma wamisionari waishi pamoja katika Jumuiya wakiunganishwa kwa kifungo cha upendo bila kuweka nadhiri, wanapata fursa ya kusali na kutafakari Neno la Mungu ili waende kuhudumia na kuleta upatanisho kati ya watu. Ujio wa Shirika la Wamisonari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania ulikuwa ni tunda la maadhimisho ya Jubilei ya miaka 150 toka kuanzishwa kwake: Makao makuu ya Shirika hapa Tanzania yalianzia Manyoni, kisha Morogoro na sasa yapo kisasa, Dodoma (2002). Wanashirika walifika mara ya kwanza Tanzania tarehe 19 Mei, 1966 wakati Shirika lilipokuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 150. Wanashirika watatu: Padre Josefu Montenegro, C.PP.S., Padre Dino Gioia, C.PP.S., na Bruda Franco Palumbo, C.PP.S., walifika Dodoma na kupokelewa na Mapadre wa Shirika la Mateso “Wapassionisti” chini ya Askofu wa kwanza wa Jimbo la Dodoma, Mhashamu Askofu Jeremiah Pesce, C.P., Wakati huo, Hayati Askofu Mattias Isuja Joseph alikuwa Katibu wa Jimbo Katoliki Dodoma.
Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, waliwasili Manyoni tarehe 11 Februari 1967 na kuanza rasmi kuwahudumia watu wa Manyoni na vitongoji vyake; wakati huo ikiwa katika Jimbo Katoliki la Dodoma. Kwa kipindi cha miezi kadhaa kabla ya kukabidhiwa shughuli za kitume wilayani Manyoni, wamisionari hao waliishi Jimboni Dodoma. Padre Kandido mwanashirika wa Shirika la Mateso Jimboni Dodoma alikuwa kiongozi wao katika kipindi cha kujiandaa kufanya kazi za kimisionari hapa nchini Tanzania. Wenyeji waliowapokea wamisionari wa kwanza Manyoni ni pamoja na Mzee Lazaro Kayombo aliyekuwa mfanyakazi wa reli, Katekista Roman Mwinyipanduka, Hilary Msahala – aliyekuwa Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Manyoni, Thadei Mhagama aliyekuwa msaidizi wa mkuu wa magereza, gereza la Manyoni; Julitha Mtonyi na mume wake hawa walikuwa ni wakulima, Moses Chambago, Maria – ambaye baadaye alikuwa mpishi wa Mapadre, Mzee Paulo Mwimbwa – baadaye akawa Katekista na mwalimu Florian. Wamisionari wengine waliofika baadaye kufanya kazi nchini Tanzania kutoka Italia ni pamoja na: Pd. Mario Dariozzi, Br. Umberto Reale, Pd. Domenico Altieri, Pd. Vincent Boselli, Pd. Francis Bartoloni, Pd. Ernesto Gizzi, Pd. John Piepoli, Pd Sebastian Benedettini, Pd. Antonio calabrese, Pd. Enzo Zoino, Pd. Gennaro Cespites, Pd. Mario Brotini na hatimaye, ni Pd Cosimo Turi. Kutoka nchini Canada ni pamoja na Br. Antony Canterucci, Pd. Brendan Dohertry na kutoka nchini Marekani ni pamoja na Pd. Timothy Coday, Br. Alan na Pd. James Froelich. Mwaka 1969, masista wanne wa Shirika la Waabuduo Damu Azizi ya Kristo Yesu kutoka nchini Italia waliwasili. Hawa ni (Sr. Delphina Gnere, Sr. Angelina Palmigiani, Sr. Nicolina Scataglia na Sr. Romana Sacchetti). Hawa walifika Tanzania na kuanza kushirikiana na wamisionari hawa katika kueneza Neno la Mungu na huduma za kijamii kama vile elimu, afya na katekesi kwa njia ya ufufnuo wao makini.
Utume: tangu mwanzoni, Wamisionari waliweka mkazo kwenye utume wa utangazaji na ushuhuda wa Injili kwa watu wa Mataifa (Mission ad gentes), wakihubiri Neno la Mungu kwa watu wote na kubatiza wanaoamini. Wanaeneza Neno la Mungu kwa njia mbalimbali, huduma za kichungaji na kimisionari maparokiani, mafungo ya kiroho, utume kwa vijana, huduma za jamii kama hospitali, shule, maji na maendeleo mbalimbali ya jamii. Baada ya kufungua nyumba ya Manyoni na kwa kusoma alama za nyakati, kutokana na ongezeko la waaamini na wahitaji, Wamisionari kwa kushirikiana na Askofu Bernad Mabula, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida na kufungua Parokia ya Itigi (1973) na baadaye Chibumagwa (1978) katika Jimbo la Singida. Kwa vile wamisionari hawa walihitaji vitu mbalimbali kutoka Dar es Salaam iliwalazimu kufungua nyumba ya “Procura” na hatimaye, Mwadhama Kardinali Laureano Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam aliwaomba wafungue Parokia ya Tegeta (1979) Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Ongezeko la waamini lililazimu kufungua Parokia nyingine ikiwemo Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi Mtongani (1999) na baadaye Kituo cha Hija na Parokia ya Mtakatifu Gaspari del Bufalo Mbezi Beach (2007). Hata hivyo leo kuna Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja, Boko (2003) na Parokia ya mt. Andrea Mtume - Bahari Beach (26 Agosti 2012) katika Jimbo kuu la Dar-es-Salaam. Katika Jimbo Katoliki la Morogoro Shirika linahudumia Parokia ya Mwili na Damu – Kola-B (2002); Jimbo Katoliki la Ifakara wanashirika wapo katika Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, Mkula (Oktoba 2007); Jimbo kuu la Dodoma Parokia ya Bikira Maria Mama wa Damu Azizi, Kisasa (2 Januari 2011) pamoja na Parokia ya Mtakatifu Francisko Ksaveri ya Chuo Kikuu cha Dodoma-UDOM (19 Desemba 2015). Katika Jimbo Katoliki la Bariadi, Wamisionari wa DamuAazizi wanahudumu katika Parokia ya Old Maswa tangu 25 Novemba 2018, na mwaka 2019 kule Shanwe Jimbo Katoliki la Mpanda. (Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara – Parokia ya Benako tarehe 25 septemba 2021; Jimboni Mbulu wapo katika Parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Gunyoda toka tarehe 8 Oktoba 2021; katika Jimbo Katoliki la Singida wapo pia katika parokia ya Mtakatifu Ursula, Mkiwa toka mwezi Novemba 2021 na katika Parokia ya Manyoni zimezaliwa Parokia tano, nazo ni: Mtakatifu Gaspari Mwembeni; Mtakatifu Benedikto Majengo; Mtakatifu Francisko wa Assisi Mwanzi; Mtakatifu Anna Msemembo na Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Idodyandole. Hizi mbili za mwisho bado ni Parokia teule. Katika Jimbo Katoliki la Musoma wapo katika Parokia teule ya Nata).
Taasisi nyingine zilizoanzishwa kama sehemu ya utume wa Shirika ni pamoja na: Manyoni Chuo cha Ufundi, VTC (1973/74), Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. wakisukumwa na kauli mbiu ya: Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya Itigi, Manyoni, Singida tarehe 15 Septemba 1987; Mradi wa Uchimbaji Visima vya Maji (C.PP.S., Water Project”) ulioanzishwa na Kanda ya Atlantic, Canada (1975), Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspar, VTC – Kunduchi Mtongani (1988), Radio Mwangaza (24 Desemba 2002), “St. Gaspar Hotel and Conference Centre (2010), “St. Gaspar Nursing School” (1989), “Mission Development Foundation – MDF [2014] na Gaspar del Bufalo House – GDB house, Tegeta (6 Julai 2016). Licha ya utume wa kawaida wa Neno la Mungu na Huduma za kijamii, Shirika limekuwa mstari wa mbele kuwashirikisha watu mmoja mmoja na katika vikundi karama yake. Vipo vikundi vyenye majina mbalimbali karibu mahala pote wanapofanya kazi wamisionari, lakini kwa pamoja vinajulikana kama “Utume wa Damu Azizi ya Yesu” wakishirikiana na wale waliowahi kupata malezi ya kishirika (Ex-seminarians) wakijulikana kwa jina la “C.PP.S., Amici Tanzania.” Mahusiano ya vikundi hivi na Shirika yanawasaidia watu waendelee kukua kiroho na kupata fursa ya kushiriki maisha na utume wa Shirika kila mmoja kadiri ya karama, wito na nafasi yake.
Malezi na Waseminari: Wamisionari walitamani utume wa Shirika hapa Tanzania uwe endelevu na angavu. Baada ya miaka kadhaa ya uzoefu wa mazingira, mila, desturi na tamaduni za kitanzania, walianzisha kazi ya malezi kwa vijana walioonesha nia ya kujiunga na Shirika. Walijenga nyumba ya kwanza ya malezi ya Mtakatifu Francisko Ksaveri Itigi (1982), baadaye ilijengwa nyumba ya Mtumishi wa Mungu Yohane Merlini Miyuji – Dodoma (1987) na hatimaye, St. Gaspar College Morogoro (1983). Kwa sasa Shirika lina waseminari zaidi 50 walio katika ngazi mbali mbali za malezi. Wamisionari wa kwanza wazalendo, Pd. Felix Mushobozi na Pd. Onesphory Kayombo ambao walisherehekea Jubilei ya Fedha ya Upadre mwaka 2016, waliingia Shirikani rasmi na kwa daima mwaka 1990. Tangu wakati huo idadi ya wamisionari iliongezeka hadi kufikia 115 mwaka huu 2026. Ushirikiano na Kanda nyingine za Shirika: Kanda ya Tanzania ni sehemu ya Shirika zima duniani na hivyo maisha na utume wake ni sehemu ya utume wa shirika zima. Tanzania imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wanashirika wengine mahali pengine duniani, mfano, Kanda za Italia, Atlantic (Kanada), Iberia (Hispania, Ureno na Guinea Bissau), “Cansas city na Cincinnati (Amerika Kaskazini na Kusini), Teutonic (Ujerumani na Austria), Poland na Vikarieti ya India. Kanda ya Tanzania imekuwa tayari kuwatuma wamisionari wake mahali pengine na kupokea wamisionari kutoka Kanda nyingine za Shirika ili kushiriki maisha na utume wake.
Ukuaji wa Shirika: Idadi ya Wamisionari iliongezeka, utume wa Shirika ulipanuka, Shirika hapa Tanzania limeendelea kukua hadi kufikia ngazi ya “Vikarieti” mwaka 1998 na hatimaye, ngazi ya Kanda tarehe 8 Agosti 2015 kama tunda na zawadi ya Jubilei ya Miaka 200 ya Uhai wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni Mapadre waliowahi kuongoza Shirika hapa Tanzania kwa nyakati tofauti ni: Padre Dino Gioia, Pd. Francis Bartoloni, Padre Antonio Calabrese, Pd. Vincent Boselli, Pd. Joachim Ndelianaruwa, Pd. Reginald Mrosso, Pd. Chesco Msaga na Pd. Vedasto Ngowi. Uongozi wa Shirika, Kanda ya Tanzania huchaguliwa kwa kura kila baada ya miaka minne kadiri ya Katiba ya Shirika. Viongozi wa sasa ambao watamaliza muda wao wa uongozi Julai 2027 ni Pd. Vedasto Ngowi, Mkuu wa Kanda, Pd. Achileus Mutalemwa (Mshauri wa kwanza na Makamu mkuu wa Kanda), Pd. Felix Mushobozi (Mshauri wa pili na Katibu wa Kanda), Pd. Richard Kungi (Mshauri wa tatu) na Pd. Dominic Mwaluko (Mshauri wa nne na Mhasibu wa Kanda.) Mwaka huu tarehe 24 Januari 2026 Shirika linafanya kumbukizi ya miaka 60 toka Shirika liingie nchini Tanzania, hata hivyo Shirika hapa limekuwa na changamoto nyingi pamoja na kuwapoteza wapendwa wake kumi na moja kwa nyakati tofauti hawa ni; Pd. Basil Ndeshingio (2004), Pd. Antonio Calabrese (2009), Pd. Joachim Ndelianaruwa (2013), Pd. Ansovinus Makwanda (2014), Pd. Fabian Ruganyiza (2016), Pd. Ernesto Gizzi (2016), Pd. Onesphory Kayombo (2018), Pd. Joseph Mabala (2019), Pd. Richard Orota (2023), Pd. Nicholaus Ngowi (2024) na Pd. Emmanuel Kimoruru aliyefariki mwaka 2025.
Hitimisho: Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 60 ya uwepo, maisha na utume wa Shirika nchini Tanzania ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema ya kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama shuhuda na vyombo vya: haki, matumaini na huruma ya Mungu. Maadhimisho haya ni muda muafaka kwa Wanashirika kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa: matumaini, huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ukarimu na wema wake wa daima, kwa maana kupitia wanashirika: mapadre na mabruda; masista na waamini walei ambao wameshirikiana nasi katika maisha na utume wetu kwa miaka sitini hapa Tanzania. Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima mzima: kiroho na kimwili, makuzi ya maisha ya kiroho, Tasaufi ya Damu Azizi, huduma nyingi za kijamii zimewanufaisha watu wengi katika nchi yetu ya Tanzania. Aidha, tunapomshukuru Mungu kwa ufanisi tuliofikia tunatambua pia changamoto mbalimbali tulizopitia. Tunajiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Gaspari mwanzilishi wetu, Bikira Maria Mama wa Damu Azizi na Mtakatifu Francisko Ksaveri msimamizi wetu. Tunawashukuru wamisionari wote wa Shirika, Maaskofu, Mapadre, Watawa, Wafadhili, watu wote tunaofanya nao kazi na wote wenye mapenzi mema. “ndoto ya Mtakatifu Gaspari inaendelea.”