Ni kwa njia ya Ubatizo tunazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu, na hivyo tunakuwa ni watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ni kwa njia ya Ubatizo tunazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu, na hivyo tunakuwa ni watoto wa Mungu na wa Kanisa.  

Kardinali Rugambwa: Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Alama Muhimu!

Kardinali Rugambwa katika mahubiri yake, ametumia fursa hii kufafanua alama muhimu zilizojionesha wakati Kristo Yesu alipobatizwa Mtoni Yordani: Alama ya kwanza ni Maji: Alama ya kifo na uhai; Mbingu zikamfunukia, Roho Mtakatifu akashuka juu yake kama hua; alama ya mabadiliko ya ndani ya mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu; alama ya tatu ni Roho Mtakatifu aliyemshukia Kristo Yesu na sauti ya Baba wa milele ikasikika: Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika Ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya Ubatizo tunazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu, na hivyo tunakuwa ni watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa Ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao maisha na uzima wa milele; Fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa Hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika Sakramenti hii. Kwa maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Mama Kanisa anahitimisha Kipindi cha Noeli, kilichowapatia waamini nafasi ya kulitafakari Fumbo la Umwilisho. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Sherehe za Noeli ni chemchemi ya Injili ya matumaini na furaha ya kweli; ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu na utume unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo. Tafakari ya Fumbo la Umwilisho, Neno aliyefanyika mwili inatia moyo neno jipya na la kweli katika Kanisa zima na hivyo kuwataka waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Fumbo la Umwilisho, ambayo ni adhimisho la Fumbo la imani, mapendo na matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Ni sherehe ya matumaini, kwa sababu Mtoto Yesu anawasha tena moto wa matumaini ndani ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa ni: mashuhuda, vyombo na wajumbe wa Injili ya amani. Wakiwa wamesheheni fadhila hizi nyoyoni mwao, kamwe hawawezi kuogopa usiku na kwamba, wanaweza kukabiliana kikamilifu na changamoto ya mapambazuko ya siku mpya.

Papa Leo XIV: Noeli ni Sherehe ya Imani, Matumaini na Mapendo
Papa Leo XIV: Noeli ni Sherehe ya Imani, Matumaini na Mapendo   (@Vatican Media)

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania, katika maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 11 Januari 2026, ameadhimisha sikukuu hii kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria In Montesano Chiesa Degli Artisti.” Hili ni Kanisa kuu kwa ajili ya wasanii wa Italia. Katika ibada hii ya Misa Takatifu alishirikiana na Askofu Antonio Staglianò, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Taalimungu, na kuhudhuriwa na watanzania pamoja na wasanii kutoka sehemu mbalimbali za Italia. Kadiri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao ulikuwa ni ubatizo wa toba, ni mwanzo wa mafumbo ya maisha yake ya hadhara, baada ya mafumbo ya maisha yake ya utotoni (KKK 528), na yale yaliyofichika ambayo Injili haziyasimulii, yaani maisha yake kuanzia miaka 12 hadi 30 hivi (KKK 534, 535) Lakini Ubatizo tunaobatizwa sisi waamini ni Sakramenti inayotufanya tuzaliwe upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na kufanywa watoto wa Mungu na wana wa Kanisa, washiriki wa ufalme, ukuhani na unabii wa Kristo Yesu. Hii ni Sakramenti kati ya zile Sakramenti Saba zilizoanzishwa na Kristo Yesu. Sakramenti katika mapokeo na imani ya Ukristo ni ishara na chombo cha neema ya Mungu. Kardinali Protase Rugambwa anasema, Ubatizo wa Yohane Mbatizaji ulikuwa ni Ubatizo wa toba kwa maondoleo ya dhambi. Hili lilikuwa ni ni tukio la kuwandaa watu wateule wa Mungu kumpokea Kristo Yesu aliyekuwa anakuja kati yao, ambaye bado alikuwa hajajifunua; Huyu ndiye Kristo Yesu aliyezaliwa katika hali ya unyenyekevu na upole, mwaliko kwa waamini kushirikishana zawadi na amana katika uhalisia wa maisha; kwa kukutana na wengine na kuanza kutembea kwa pamoja. Kristo Yesu hakuwa na umuhimu wa kubatizwa, kwani hakuwa na dhambi, lakini alibatizwa, kama kielelezo cha mshikamano na binadamu mdhambi, ili kukaa pamoja na wadhambi.

Kardinali Rugambwa amefafanua alama za Ubatizo wa Kristo Yesu
Kardinali Rugambwa amefafanua alama za Ubatizo wa Kristo Yesu

Kardinali Rugambwa katika mahubiri yake, ametumia fursa hii kufafanua alama muhimu zilizojionesha wakati Kristo Yesu alipobatizwa Mtoni Yordani: Alama ya kwanza ni Maji ambayo ni alama ya maangamizi kama inavyojionesha kwenye Agano la Kale kwa gharika wakati wa Nuhu; mafuriko yaliyosababisha maafa makubwa na hivyo kuangamiza ulimwengu wa dhambi. Maji pia ni alama ya uhai, kwani bila maji, hakuna maisha na kwamba, Maji kwa dini kubwa ni alama ya uhai! Mababa wa Kanisa wanakiona Kisima cha Ubatizo kuwa ni “Tumbo la Mama Kanisa” ambalo waamini wanazaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu” na hivyo kushiriki: Ufalme, Ukuhani na Unabii wa Kristo Yesu. Waamini kwa “kuzamishwa” katika maji ya Ubatizo, wanaondolewa ile dhambi ya asili na kuwawezesha kuwa watu wapya, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kardinali Rugambwa amesema, Kristo Yesu alipokwisha kubatizwa, Mbingu zikamfunukia, Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa hua na kukaa juu yake. Kufunga kwa mbingu ni alama ya mabadiliko ya ndani ya mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu anafungua Agano Jipya na Mbingu mpya na kwamba, mbingu imefunguka kwa ajili ya watu wote na wala si kwa ajili ya watu wachache, bali kwa binadamu wote. Mbingu kufunguka ni alama ya pili ambayo ni muhimu sana katika Ubatizo wa Kristo Yesu. Alama ya tatu ni Roho Mtakatifu aliyeshuka na kukaa juu ya Kristo Yesu mfano wa hua na sauti ya Baba wa Milele ikasikika ikisema: “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” Mt 3:17. Huu ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kwa Ubatizo waamini wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu
Kwa Ubatizo waamini wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu

Kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, baada ya gharika kuu, Njiwa alitumwa na kurejesha ujumbe “akiwa na jani bichi la Mzeituni kinywani mwake.” Mwa 8:11. Huu ukawa ni mwanzo mpya! Ubatizo unawakirimia waamini neema ya kuwa ni wana “wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.” Kol 3:12-14. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, waamini wawe tayari kuomba msaada kutoka kwa Baba yao wa mbinguni; daima wakijitahidi kuwa watu wema na watakatifu. Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, amehitimisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini kuonesha moyo wa shukrani kwa neema na baraka nyingi ambazo Mwenyezi Mungu anawakirimia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, changamoto na mwaliko kwa waamini kuishi mintarafu Sakramenti ya Ubatizo kwa kutambua ile heshima kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia: “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.” 1Yn 3:1.

Kanisa kuu la "Santa Maria In MOntesano" Kanisa la Wasanii nchini Italia
Kanisa kuu la "Santa Maria In MOntesano" Kanisa la Wasanii nchini Italia

Wakati huo, Askofu Antonio Staglianò, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Taalimungu amemshukuru na kumpongeza Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora kwa kuonesha moyo wa shukrani, urafiki, udugu wa kibinadamu, umoja na upendo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba Roho Mtakatifu ni nguvu ya upendo inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwani Mungu ni upendo; ni Mwenye haki na ni mwingi wa huruma. Kwa kuwa Kanisa hili kuu limetengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya wasanii, kumbe lugha inayotumika pia ni kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya! Yaani Vijana wa Gen-Z! Askofu Antonio Staglianò, amemkabidhi Kardinali Rugambwa Kitabu alichokiandika kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya kinachojulikana kama “Pop Christology, Uno Zibaldone, Un Sapere Del Senso Della Vita in Dio-Amore” Yaani: "Pop Christology, Hodgepodge, Maarifa ya Maana ya Maisha katika Mungu ni upendo."

Kardinali Rugambwa Ubatizo
13 Januari 2026, 14:58