2026.01.26 Kardinali Pietro Parolin- Denmark. 2026.01.26 Kardinali Pietro Parolin- Denmark. 

Kard.Parolin:Kanisa linabaki kuwa la kuaminika si kupitia nguvu,hesabu au mikakati!

Katibu Mkuu wa Vatican,aliongoza Misa katika Kanisa Kuu la Copenhagen kama Mwakilishi wa Papa katika sherehe za Jubilei ya miaka 1200 ya kuanza utume wa Mtakatifu Ansgar nchini Denmark.Katika mahubiri,Kardinali Parolin alifafanua Mmisionari huyo katika muktadha wa Ulimwengu wetu uliojeruhiwa na aina mpya za utumwa,kiuchumi,kiutamaduni na kiroho na kuonesha kutengwa na kutojali.Alisisitiza kuwa Uaminifu hautokani na mamlaka bali ushuhuda.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

"Mtakatifu Ansgar alisikia Injili hii na alionyesha ujasiri na uaminifu kwa kuacha sehemu na watu aliowajua ili kumfuata Yesu." Haya yalisema na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, wakati wa kuongoza  ibada ya Misa Takatifu akiwa mwakilishi wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Jubilei ya miaka 1200 ya kuanza kwa utume wa Mtakatifu Ansgar, iliyofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Ansgar, huko Copenhagen, nchini Denmark, Dominika tarehe 25 Januari 2026. Kwa kuongozwa masomo ya  Isaya 52,7-10, Kor. 1,18-25, Mk 1,14-20,  Kardinali alionesha furaha kusherehekea pamoja  Siku hiyo ya kila mwaka ya  Mtakatifu Mlinzi wa Jimbo hilo  na Kanisa Kuu hilo. Siku kuu hii ni muhimu sana mwaka huu, kwa sababu ya  hatua muhimu katika maisha ya Kanisa hili: miaka 1200 ya utume wa Mtakatifu Ansgar nchini Denmark.

Katika tukio hilo  la heshima, Kardinali Parolin aliwapatia salamu za dhati za Papa Leo XIV, ambaye "alinituma kuwa kati yenu kama Mwakilishi wake kama ishara ya ukaribu wake wa kiroho na upendo kwa watu wa Denmark, ambao Mtakatifu Ansgar aliwapenda sana na kuwahudumia kwa uaminifu mkubwa. Ishara hii haikumbuki uhusiano ulioanzishwa hapo awali tu, bali inaweka sasa, katika wakati wetu, wasiwasi uleule wa kichungaji na msukumo wa kiinjili ambao uliamsha utume wa Ansgar. Kwa sababu hiyo, hatukumbuki kitu kilichotokea miaka hiyo yote iliyopita tu." Kardibali Parolin aliendelea kusema kuwa "Tukichukua imani yetu ya Kikristo kwa uzito, kuwasili kwa mjumbe huyu wa Habari Njema kunastahili kusherehekewa leo, kwa sababu kunatutaka Kanisa, kutoka kwetu,  hapa na sasa, likituita kupokea Injili upya na kuishuhudia kwa uaminifu na ujasiri ule ule."

Kardinali Parolin wakati wa mahubiri huko Denmark
Kardinali Parolin wakati wa mahubiri huko Denmark

Kardinali Parolin akidadavua masomo yaliyosomwa alisema, kwa kusikia kutoka kwa nabii Isaya anatupa taswira inayoweka mwelekeo wa sherehe ya leo: “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima,  miguu ya mtu aletaye habari njema, atangazaye amani, aletaye habari njema, atangazaye wokovu” (Isaya 52,7). Nabii haakisi ujumbe kama vile mjumbe, ambaye miguu yake ni mizuri si kwa sababu ya mawazo au maelezo yoyote ambayo mjumbe huleta, bali kwa sababu huleta habari njema, habari ambazo zinaweza kuwaokoa watu kwa kubadilisha mioyo ya wale wanaosikia ujumbe na kuwaweka huru. Utume wa  Mtakatifu Ansgar ulitokana na uzoefu wa ajabu wa ukombozi katika maisha yake mwenyewe. Akiwa kijana, alipata maono ya Kristo ambapo alisikia maneno, «Msiogope; mimi ndiye ninayefuta dhambi zenu.” Mwandishi wa wasifu wake na mshirika wake Rimbert aliandika ndoto hiyo  baada ya Ansgar kufariki na kuongeza, “akiwa ameimarishwa na kujiamini katika msamaha wa dhambi zake, alifurahi kwa furaha kubwa» (RIMBERT, Vita Anskarii, 4.25). Ansgar alikuwa amekutana na furaha ya kusamehewa na Mungu, na alitamani kushiriki furaha hiyo na wengine. Hiyo ndiyo habari njema aliyoleta.

Katibu Mkuu wa Vatican kwa upande wa  Injili alibainisha hiyo inatwambia  jinsi Yesu alivyoanza utume wake. Alitoka wakati wake jangwani si kwenda Yerusalemu, bali Galilaya, mahali pa kawaida na pa chini sana. Maneno yake ya kwanza yanashangaza: "Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia" (Mk 1,15). Wakati wa kuamua kwa yeyote anayemsikia si wakati mwingine au mahali pengine, bali hapa na sasa. Yohane Mbatizaji alikuwa amekamatwa tu; lakini Yesu alichagua wakati huo wa majaribu na dhahiri "Tubuni, na kuamini Injili" (Mk, 1,15). Alichotaka haikuwa tu kutuambia jambo fulani, bali kutuomba tubadilike, tuongoke. Sio sana kuhusu juhudi zozote za kimaadili tunazoweza kufanya bali kutuomba tuone mambo kwa njia mpya, kutambua kwamba Mungu tayari anafanya kazi katika maisha yetu, pamoja na mipaka na mapungufu yetu yote. Karibu mara moja, Yesu aliwaita wanafunzi wake wa kwanza: “Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu” (Mk 1:17).

Jubilei ya Mtakatifu Ansgar
Jubilei ya Mtakatifu Ansgar   (Marco Chwalek / Erzbistum Hamburg)

Mtakatifu Ansgar alisikia Injili hii hii na alionesha ujasiri na uaminifu kwa kuacha sehemu na watu aliowajua ili kumfuata Yesu. Alipokuwa mtoto, aliingia katika monasteri huko Corbie nchini Ufaransa. Alipokuwa na umri wa miaka 21, alihamia katika monasteri mpya ya Corvey, Ujerumani  leo. Kisha, mfalme alipowaomba mapadre wamsindikize  Mfalme wa Denmark aliyekuwa abatizwa punde, Harald Klak, Ansgar alikuwa jasiri wa kutosha kuhama tena, wakati huu kama mmisionari kwenda Denmark, kutangaza Injili katika nchi yao.

Mwandishi wa wasifu wake aliandika tena: “Wengi walianza kushangazwa na mazungumzo aliyokuwa tayari kufanya, akiacha nchi yake na jamaa zake, na hata mapendo  matamu ya ndugu aliolelewa nao, badala yake anapaswa kuchagua kutafuta watu wa kigeni na kuishi miongoni mwa wageni na wapagani" (Vita Anskarii). Ansgar aliitikia wito wa kwenda hapo  kwa utii na uaminifu. Dhamira yake haikujengwa juu ya mikakati au mafanikio, bali juu ya uaminifu kwa Bwana wake Yesu. Moja ya matendo yake ya kwanza huko Denmark ilikuwa kununua uhuru wa baadhi ya watumwa, kwa hivyo pia alileta ukombozi kwa njia halisi, zoezi la vitendo la Ukristo lilisikika katika maneno ya Kierkegaard: “uthibitisho wa Ukristo ni maisha ya Mkristo” (Fanya Ukristo).

Maadhimisho ya Jubilei ya Mtakatifu Ansgar
Maadhimisho ya Jubilei ya Mtakatifu Ansgar   (Marco Chwalek / Erzbistum Hamburg)

Injili haitoi suluhishi dhahania bali maono ya mwanadamu

Katika ulimwengu ambao bado umejeruhiwa na aina mpya za utumwa - kiuchumi, kiutamaduni, kiroho, na ulio na alama ya kutengwa na kutojali - ishara ya Ansgar inazungumza kwa umuhimu mpya. Injili haitoi suluhisho za dhahania, bali ni maono ya mwanadamu ambaye heshima yake inayotangulia kila hesabu. Kanisa linabaki kuwa la kuaminika si kupitia nguvu, hesabu, au mikakati, bali imani inapogeuka kuwa ushuhuda ulio hai, unaotafsiriwa kuwa matendo halisi ya ukombozi, haki, na huruma ambayo hurejesha heshima na njia wazi za uhuru wa kweli.

Kardinali Parolin aliendelea kudadavua kutoka Somo la Pili kwamba “Maneno tuliyosikia katika somo la pili la leo, kutoka Barua ya Kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho, ni kukabiliana na kitendawili, kile ambacho Paulo anakiita "upumbavu wa msalaba". Katika ulimwengu ambapo watu wanafundishwa kuthamini nguvu, ushawishi na mafanikio, Kristo aliyesulubiwa anaonekana mjinga, mshindwa. Lakini upumbavu huu ni hekima ya Mungu (taz. 1 Kor 1, 18-25), kwa sababu unatuonesha upendo unaoweza kujitoa kikamilifu.

Mtakatifu Ansgar alikabiliwa na changamoto kubwa upinzani, na alionekana kushindwa, lakini mafanikio hayakuwa yale aliyolenga. Alipoulizwa ni neema gani angemwomba Mungu, alijibu, "Kama ningekuwa ninastahili mbele za Bwana wangu, ningemwomba anipe ishara moja: yaani, kwamba kwa neema yake angenifanya mtu mwema" (Vita Anskarii, 39,74). Alitaka zaidi ya kitu kingine chochote kuwa zaidi na zaidi kama Kristo. Historia ya maisha ya Ansgar inatukumbusha kwamba Kanisa hukua si hasa kwa idadi, bali kwa wanaume na wanawake wanaoishi maisha ya uaminifu, uvumilivu na upendo. Utume huanza na mioyo inayobadilika. Kwa maana hiyo, Jubilei si mtazamo wa zamani, bali ni wakati wa sasa wa uwajibikaji. Inatuita tupyaishe ujasiri wa kiinjili, kuwa uwepo unaosindikiza na kutumikia, na kulinda tumaini ambapo historia inaonekana kuchoka. Tukiwa tumeungana katika tumaini, katika historia yote, tunaitwa hata leo kushuhudia kwamba kuzaa matunda hutokana na upendo unaounganisha na uaminifu katika hatua inayoendelea ya Mungu, hata katika hali dhaifu zaidi.

Nembo ya Mtakatifu Ansgar huko Denmark
Nembo ya Mtakatifu Ansgar huko Denmark   (Marco Chwalek / Erzbistum Hamburg)

Historia ya Denmark

Haya yote yanamaanisha nini leo Denmark? Denmark si nchi ya kipagani ambayo Ansgar aliikutana nayo alipofika hapa. Historia ya Denmark imeainishwa bila kufutika na urithi wake wa Kikristo, siku hizi jumuiya ya Wakatoliki, pamoja na Walutheri na watu wote wenye mapenzi mema, wanataka kuchangia maisha ya jamii hii kupitia huduma, mshikamano, na heshima kwa utu wa binadamu. Wakristo wanapofanya kazi pamoja, hasa katika kazi za upendo na huduma kwa wale wanaohitaji zaidi, wanawapa jamii nzima ushuhuda wenye nguvu kwa Injili na kwa Kristo mwenyewe. Wanapeleka habari njema, ambazo watu wanatamani kusikia. Kama Papa Benedikto XVI alivyoandika: “Upendo wa Kristo unatuhimiza kufanya kazi pamoja, ili ulimwengu uweze kuamini” (Tomos Agapis, 27 Mei 2006). Mtakatifu Ansgar alijua kwamba utume wetu kama wafuasi wa Yesu Kristo huanza na moyo uliobadilishwa; anatukumbusha kwamba ukuaji na afya ya Kanisa hupimwa si sana kwa idadi au mipango iliyofanikiwa, bali zaidi kwa uwezo wetu wa kutembea na Kristo na kubaki karibu naye katika kila hali.

Papa Leo XIV, katika siku za kwanza za huduma yake, akikutana na wawakilishi wa Makanisa mengine na jumuiya za Kikristo, alikumbuka maana ya kauli mbiu yake ya kiaskofu: “In  Illo uno unum, ni “usemi wa Mtakatifu Agostino wa Hippo unaotukumbusha jinsi sisi pia, ingawa tuko wengi, “katika Mmoja - yaani Kristo - sisi tu mmoja” (Enarr. katika Zab., 127, 3). Zaidi ya hayo, ushirika wetu unafikiwa kwa kiwango tunachokutana katika Bwana Yesu. […] Sisi Wakristo, basi, sote tumeitwa kuomba na kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo hili, hatua kwa hatua, ambalo ni na linabaki kuwa kazi ya Roho Mtakatifu” (19 Mei 2025).

Kwa kuhitimisha, Kardinali Parolin alisema kwamba “Sherehe yetu ya jubilei hii na ipyaishe ndani yetu imani iliyo hai, ujasiri unaotokana na tumaini na upendo halisi na wenye ufanisi kwa Mungu na kwa wanaume na wanawake wenzetu. Bwana, aliyemwita Mtakatifu Ansgar kuwatumikia watu wake huko Denmark, aendelee kuliongoza Kanisa katika nchi hii na  ulimwenguni kote , ili wote waweze kusikia na kuitikia habari njema ya wokovu. Amina.”

Kardinali Parolin akiwa huko Denmark
Kardinali Parolin akiwa huko Denmark   (Marco Chwalek / Erzbistum Hamburg)
26 Januari 2026, 12:06