Kard.Parolin nchini Denmark:Tutafute kile kinachotuunganisha!
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican akiwa, Denmark kwa siku mbili kama mjumbe wa Baba Mtakatifu, kwa ajili ya Maadhimisho ya miaka 1200 ya kuanza kwa utume wa Mtakatifu Ansgar, aliwatia moyo Wakristo kufanya mazoezi. Ni katika mahiburi yake katika Masifu ya jioni ya Kiekumeni yalioongozwa tarehe 24 Januari 2026, katika Kanisa Kuu la Kilutheri la Mama Yetu huko Copenhagen. Kardinali Parolin akianza alisema kuwa, muunganiko huo wa maombi ulizindua kukaa kwake katika nchi ya Kaskazini katika kumkumbuka mtawa na Askofu Mkuu Mbenedikito ambaye ni Mtakatifu na mlinzi wa Scandinavia, ambaye alijitolea maisha yake kuinjilisha Denmark na Sweden katika karne ya 9. “Mpango huo wa pamoja wa Makanisa Katoliki na Kilutheri unatoa fursa zaidi ya "kuimarisha ushirikiano na udugu kati ya Makanisa yetu, alisitiza “katika utume wa Kikristo na ushuhuda."
Tushukuru fursa ya kukutana kama wanafunzi wa Bwana
Kardinali aliendelea kwamba walikusnyika hapo jioni hiyo katika roho ya kusikiliza na kuomba, “tukishukuru kwa fursa ya kukutana kama wanafunzi wa Bwana, tukiitwa kutafuta kinachotuunganisha na kushuhudia pamoja Injili. Katika mazingira haya ya heshima na ushirika wa kidugu, tunamkabidhi Bwana safari yetu na tumaini letu. Ziara na sherehe ya Jubilei ya kuadhimisha mwanzo wa Utume wa Mtakatifu Ansgar nchini Denmark ziko katika mwisho wa Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Kikristo, wakati ambapo Bwana anatuita "tutembee pamoja katika Roho mmoja, "alisisitiza. Kardinali kwa hiyo alipenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Askofu wa Copenhagen, Peter Skov-Jakobsen, na kwa wote walioshiriki katika mkutano huo wa maombi ya kiekumeni katika Kanisa Kuu la Kilutheri. Alishukuru sana kwa mpango wa pamoja wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kilutheri kukusanyika pamoja jioni hiyo, kusali na kutoa ushuhuda, katika nyayo za Mtume wa Kaskazini, Mtakatifu Ansgar, kwa Neno la Mungu lililotangazwa "kwa uwazi na upendo" kwa watu wa Denmark. Wakati huu wa ushirika, aliongeza kardinal kwa unaoishi kupitia kusikiliza kwa makini Neno na sala ya pamoja, uimarishe ushirikiano na udugu kati ya Makanisa yetu katika utume na ushuhuda wa Kikristo.
Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Kikristo
Mada ya Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Kikristo yanatokana na Barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso: “Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa kwa tumaini moja la wito wenu” (Efe 4:4). Neno hili linatukumbusha kwamba Kanisa limeitwa kuishi umoja si kama umoja tu, bali kama ushirika hai katika utofauti. Umoja hautokani na kile tunachozalisha; ni zawadi ya Roho: “Kanisa si shirika lililobuniwa nasi, bali ni ukweli hai unaokua kupitia utendaji wa Roho Mtakatifu” (J. Ratzinger, Ushirika katika Kanisa, 2004, uk. 44). Kwa mtazamo huu, Wakatoliki na Walutheri wanaweza tayari kutambuana kama washiriki wa Mwili mmoja wa Kristo, licha ya tofauti za kihistoria na za kiliturujia. Mada ya siku inatualika kutafakari: “Kila mmoja wetu amepewa neema kulingana na kipimo cha kipaji cha Kristo” (Efe 4:7). Hapo pia, neema ni zawadi ya kibinafsi inayotangulia sifa zote za kibinadamu na kumwezesha kila mtu kuchangia umoja wa Mwili.
Neema hotolewa kulingana na kipimo
Paulo anaonesha kwamba neema hutolewa "kulingana na kipimo:" kipimo hiki hakimaanishi ukosefu wa usawa, bali ni aina mbalimbali za vipaji kwa ajili ya kujenga uzima. Roho Mtakatifu haondoi tofauti, bali anazipatanisha, kwa sababu “hafuti utofauti, bali anazipatanisha katika upendo”(R. Cantamessa, Roho Mtakatifu katika Maisha ya Yesu na Kanisa, 2001, uk. 263). Hivyo, karama, huduma, na hisia tofauti huwa vyombo vya kutumikia pamoja, katika tumaini moja ambalo Mungu anawaita Wakristo wote. Katika mtazamo huo wa huduma halisi na uwajibikaji wa pamoja, ushuhuda wa Kikristo hauwezi kubaki wa kufikirika au kuzuiliwa kwa maneno pekee, lakini lazima uonekane na kuonekana katika historia. Tukikabiliwa na mateso ya watu binafsi na watu, hatuwezi kutazama mbali, wala kutojali hakuwezi kuwa chaguo. Uaminifu kwa Injili unatuita kwa ushuhuda ulio wazi katika ukweli, wenye huruma katika upendo, na ujasiri katika vitendo, ili nuru ya Kristo iwafikie wale wanaoishi katika giza, hofu, na kutengwa.
Tumaini la Kikristo halitegemei tunachokiona au kuelewa bali ni uwazi wa kuamini Mungu
Tumeitwa kutambua upendo kwa maneno halisi, bila kupuuza mazungumzo ya kiekumene: "uekumene wa upendo huendeleza ushirika miongoni mwa Wakristo na pia huangazia mazungumzo katika ukweli, kuimarisha azimio la kuheshimiana na mwendelezo wa mazungumzo ya kidugu”(Benedikto XVI, kwa washiriki katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo, 17 Novemba 2006). Tumaini la Kikristo halitegemei kile tunachokiona au kuelewa kikamilifu, bali ni uwazi wa kuamini uaminifu wa Mungu na utimilifu wa ahadi zake. Linatuita kutazama wakati ujao kwa ujasiri na kuishi kwa matumaini ya uhakika, tukiwa na uhakika kwamba Mungu anatimiza kile alichoahidi. Katika mwanga huu, umoja wa kiekumene hautuombi kukataa zawadi tulizopokea, bali kuzitoa katika ushirika: «umoja wa Kanisa hukua wakati zawadi maalum zinapowekwa kwa ajili ya huduma ya Mwili mmoja wa Kristo”(W. Kasper, Ili wote wawe kitu kimoja,2004). Kwa hivyo, neema pia ni jukumu: neema si fursa kamwe, bali ni wito wa kutumikia.
Wakristo tumeitwa kusali na kufanya kazi kwa ajili ya kufikia lengo la umoja
Na kama Papa Leo XIV alivyotukumbusha katika mkutano wake wa kwanza na wawakilishi wa Makanisa mengine na Jumuiya za kikanisa, na wa dini zingine, kuwa: “umoja wetu unafikiwa kwa kiwango tunachokutana nacho katika Bwana Yesu. Kadiri tunavyokuwa waaminifu na watiifu zaidi kwake, ndivyo tunavyozidi kuwa na umoja miongoni mwetu. Basi, sisi Wakristo sote tumeitwa kuomba na kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo hili, hatua kwa hatua, lengo ambalo ni, na linabaki kuwa kazi ya Roho Mtakatifu”(Papa Leo XIV, Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa wawakilishi wa Makanisa mengine na Jumuiya za kikanisa, na wa dini zingine, 19 Mei 2025).” Kwa kuhitimisha Kardinali Parolin alisema, “Agizo hili litutie moyo kuendelea kwa uvumilivu na uaminifu katika njia ya kuelekea umoja, tukiwa na uhakika kwamba kila kukutana kwa dhati katika Kristo kunatuleta karibu na ushirika ambao Bwana anauita Kanisa lake. Amina.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here