Juma la kuhamasisha Umoja wa Kikristo. Juma la kuhamasisha Umoja wa Kikristo. 

Kard.Koch na Bartholomew I:Jitihada za pamoja zinahitajika kwa ajili ya Uekumeni

Ulisomwa Ujumbe wa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo na Patriaki wa Kiekumeni Bartholomew I,tarehe 18 Januari 2026 katika hitimisho la Mkutano wa Kiekumeni huko Bari nchini Italia,wenye mada:“Uongofu kati ya Wakatoliki na Waorthodox katika Roho Mtakatifu,”uliohamasishwa na Jumuiya ya Yesu,Chama cha Kimataifa cha Waamini katika Kanisa Katoliki.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

"Ushirika na ushuhuda wa pamoja si tu miongoni mwa malengo yatakayofikiwa mwishoni mwa safari, bali pia ni ukweli ambao tayari unaweza kupatikana leo hii.” Haya yamo katika Ujumbe wa Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, uliotumwa kwa Askofu Mkuu Giuseppe Satriano, wa Jimbo Kuu la  Bari-Bitonto, nchini Italia,  wakati wa hatua ya pili ya mkutano uliohitimishwa Dominika tarehe 18 Januari 2026 kwa kuhamasishwa  na Jumuiya ya Yesu, Chama cha Kimataifa cha Waamini wa Kanisa Katoliki, ukiongozwa na mada: “Mazungumzo kati ya Wakatoliki na Waorthodox katika Roho Mtakatifu.”

Kutokana na mada hiyo, Kardinali Koch alisisitiza kuwa ni wazi kwamba hili si tukio la kitaaluma tu, bali ni uzoefu wa kukutana na kushiriki uzoefu wa maisha ya kiroho. Chaguo hili linafaa sana, kwa kuwa mhusika mkuu wa kweli wa safari ya umoja ni Roho Mtakatifu, na roho ya juhudi zote za kuanzisha tena ushirika kamili kati ya waliobatizwa katika Kristo ni umoja wa kiroho, ambao unahitaji, kwanza kabisa, sala na urejesho wa ndani."

Kufanya Kazi Pamoja

Kwa upande wa Kardinali, Koch alisisitiza kuwa kuna "maeneo mengi ya kichungaji, kiutamaduni, na upendo ambapo waamini wa Makanisa tofauti wanaweza kufanya kazi pamoja, wakitoa ushuhuda wa imani yao katika Yesu Kristo."

Patriaki Bartholomew:Ushirikiano unahitaji utambuzi wa mazungumzo ya kitaalimungu

Na katika tukio hilo, Patriaki wa Umoja wa Kiekumeni,  Bartholomew I alishiriki mtazamo huu, akisisitiza, katika ujumbe wake kwa ajili ya tukio hilo, kwamba "ushirikiano na ushirika kati ya Makanisa na kujitolea binafsi kwa kila mwamini hakuwezi kupunguzwa kuwa mtazamo wa uhisani au ushirikiano wa kimaadili-kijamii. Badala yake, zinahitaji utambuzi wa kweli, mazungumzo ya kitaalimungu, na harakati ya sala, tafakari, na liturujia ya kubadilika."

Mwanadamu na Ulimwengu

Kulingana na Patriaki Bartholomew, "Ushirika na ushuhuda katika mwanga wa Roho Mtakatifu humaanisha kuhuisha kila tendo, kuanzia sayansi hadi siasa, ili kutambua uhusiano wa karibu kati ya anthropolojia na ulimwengu, kati ya ubinadamu na ulimwengu. Kwa hivyo tunaweza kupata ushirika, na uhusiano wa Utatu, na kwa hivyo kutoa ushuhuda wa pamoja, ikiwa tutafanikiwa  tukuunda ndani yetu ubinadamu mpya, chumvi ya dunia, kupitia kazi ya Roho Mtakatifu, katika Kristo, akitubadilisha kama mbingu mpya na dunia mpya katika mtazamo wa eskatolojia, kama picha  zinazofunua Utatu Mtakatifu Zaidi katika ushirika wa milele wa upendo."

Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Wakristo

Uzoefu wa aina hii na mikutano ya kiprogramu unaongezeka wakati wa Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Wakristo, ambapo mada ya mwaka huu 2026 ikiwa: "Mmoja ni mwili, mmoja ni Roho, kama vile Mungu alivyowaita tumaini moja." Juma hili lilifunguliwa Dominika tarehe 18 Januari,  ambapo litafungwa Dominika tarehe 25 Januari 2026  katika  Siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo, Mtume wa Watu, ambapo Baba Mtakatifu Leo XIV anatarajia kuhitimisha tukio hili kwa kusherehekea Masifu ya Jioni katika Basilika ya Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta mjini Roma saa 11:30  jioni masaa ya Ulaya.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

21 Januari 2026, 10:46