Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa UN:Kanisa ni mshirika muhimu katika kuwasaidia wakimbizi

Barham Salih,Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa,alizungumza na Vatican News kuhusu mkutano wake na Papa Leo XIV,Januari 26 na changamoto zinazokabili Shirika hilo katika kuwasaidia wakimbizi Ulimwenguni kote.

Na Isabella H. de Carvalho – Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi(UNHCR,(reported), liliripoti kwamba kufikia katikati ya mwaka 2025, watu milioni 117.3 duniani kote walikuwa wamelazimika kukimbia makwao kutokana na migogoro, vurugu, mateso, au matukio mengine, na miongoni mwao walikuwa karibu wakimbizi milioni 42.5. Baba Mtakatifu  Leo XIV, kama watangulizi wake kabla yake, alielezea mara kwa mara wasiwasi wa Kanisa kwa wahamiaji na wakimbizi na alihimiza ulimwengu usiwe mtulivu mbele ya suala hili. Siku ya Jumatatu, tarehe 26 Januari 2026, Papa alikutana mjini Vatican na Barham Salih, Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa (, United Nations High Commissioner for Refugees) na Rais wa zamani wa Iraq kuanzia 2018 hadi 2022.

Papa akizungumza na Kamishna Mkuu  wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa
Papa akizungumza na Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa   (@Vatican Media)

Bwana Salih alipitia maisha haya kama mkimbizi mwenyewe, na sasa ameanza jukumu hili jipya katika Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, kuanzia tarehe 1 Januari 2026. Katika mahojiano na Vatican News, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa alizungumzia mkutano wake na Papa Leo XIV na alielezea changamoto tofauti ambazo UNHCR inakabiliwa nazo katika kazi yake leo, huku wakimbizi wengi wakijitahidi kutoka katika hali za kuhamishwa na mashirika ya kibinadamu yakihitaji rasilimali nyingi.

Mkutano wako ulikuwaje asubuhi ya leo na Papa Leo XIV?

Ilikuwa heshima kubwa kwangu kukutana na Baba Mtakatifu. Nilikuwa na hamu ya kuwa na Mkutano huu mapema katika kipindi changu. Nimekuwa katika nafasi hii kama Kamishna Mkuu wa Wakimbizi kwa chini ya majuma manne tu, kwa hivyo ilikuwa fursa nzuri kwangu kuzungumza na Baba Mtakatifu kuhusu hali ya wakimbizi. Nimefurahishwa na msaada wake usiokoma kwa wakimbizi duniani kote, na mamlaka yake ya kimaadili ni muhimu sana. Usaidizi wake kwa kile tunachofanya katika UNHCR ni muhimu sana. Tunasisitiza hitaji la ushirikiano wetu na Kanisa na mashirika yanayotegemea imani tunapojaribu kutekeleza agizo letu la kuwasaidia wakimbizi duniani kote. Sauti ya Papa na mamlaka yake ya kimaadili ni muhimu. Tunaona huu kama ushirikiano muhimu na mali tunayotegemea, tunapoendelea kutekeleza agizo letu la kuwasaidia wakimbizi duniani kote.

Ulichukua madaraka Januari 1. Je, ni vipaumbele gani vya mamlaka yako?

Ninachukua jukumu hili wakati wa changamoto kubwa: viwango visivyo vya kawaida vya uhamisho, wakati wa kupungua kwa nafasi ya kibinadamu, na rasilimali chache zinazopatikana kushughulikia ukubwa wa tatizo tulilonalo. Kipaumbele changu kitakuwa ni kuzingatia utetezi ili kutoa rasilimali zaidi kwa mahitaji ya idadi ya wakimbizi kote ulimwenguni, lakini wakati huo huo ili kutekeleza agizo letu. Hii ina maana ya ulinzi kwa wakimbizi, kutoa msaada wa dharura wa kuokoa maisha kwa watu wanaohitaji sana, lakini pia kufanya kazi kwa bidii katika suluhisho za kudumu. Si vizuri kuona wakimbizi wengi wakihukumiwa hali ya uhamisho wa muda mrefu kwa miaka mitano au zaidi, wakati mwingine muongo mmoja au hata miwili.

Watu hawa wamekwama katika kambi zinazotegemea misaada ya kibinadamu ya kimataifa. Hilo halikubaliki. Tunahitaji kusonga mbele zaidi ya hapo, kuelekea suluhisho jumuishi zaidi na la kudumu. Nilikuwa Chad na Kenya Juma lilopita ambapo nilikutana na wakimbizi ambao wamekuwa katika baadhi ya jamii hizi kwa miaka 25 hivi iliyopita, tangu 2003, na wengi zaidi walikuwa wakiwasili siku moja kabla. Hii inaniambia kwamba tunahitaji kufanya zaidi kuhusu watu ambao wamehukumiwa kuhama makazi yao kwa muda mrefu.

Hilo ni jambo ambalo UNHCR haiwezi kufanya peke yake. Inahitaji juhudi za pamoja zaidi na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, lakini pia mataifa mwenyeji na jumuiya ya kimataifa na benki za maendeleo. Kwa njia hiyo tunaweza kuunda mazingira kwa mataifa haya mwenyeji kuwahudumia wakimbizi na kuwajumuisha katika maisha yao ya kitaifa kama wachangiaji badala ya kutegemea misaada ya kibinadamu tu. Nchi kama Kenya, Ethiopia, Uganda na Chad zinapitisha sera jumuishi zaidi na malazi kwa wakimbizi, zikiwaruhusu kuingia katika mfumo wao wa kitaifa, huduma za afya, mfumo wa elimu, masoko ya kazi, upatikanaji wa huduma za kisheria na huduma za kifedha. Hili linahitaji kuhimizwa kupitia misaada ya maendeleo ili hii iwe na manufaa kwa mataifa mwenyeji na pia inaruhusu kuingizwa kwa wakimbizi zaidi ya maisha kambini kwa sababu mwisho wa siku, wakimbizi si idadi tu. Ni watu wenye mamlaka. Wanastahili heshima. Wanastahili kulindwa.

UNHCR inajibu vipi dharura za sasa  ulimwenguni kote, ikizingatiwa kupunguzwa kwa ufadhili kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni, hasa kutokana na kupungua kwa misaada kutoka Marekani? Hii itakuwa na athari gani katika miezi ijayo?

Hivi majuzi Marekani imetenga dola bilioni 2 za usaidizi kwa mfuko uliounganishwa katika Umoja wa Mataifa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA). Hili linakaribishwa na tunatumaini msaada zaidi utakuja kwa njia hiyo. Lakini, bila shaka, kutokana na ukubwa wa tatizo, rasilimali zinazopatikana ni chache sana. Tunahitaji kuanzisha kampeni ya utetezi yenye nguvu zaidi ili kuleta rasilimali zaidi. Mwishowe, kusaidia katika hali ngumu ya wakimbizi ni jukumu la pamoja la kimataifa.

Ukiangalia idadi, ni ya kushangaza sana na mahitaji ni halisi, kwa hivyo tunahitaji rasilimali zaidi, bila shaka kuhusu hilo. Kwa mantiki hiyo hiyo, tunapaswa kuzoea zaidi. Tunapaswa kuboresha ajenda yetu ya mageuzi na kuunda ufanisi zaidi katika mfumo ili msaada unaopatikana uwafikie watu unaokusudiwa. Tayari, pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, tunashiriki katika baadhi ya harakati hizi za mageuzi na ufanisi ili kuhakikisha kwamba mfumo wa misaada ya kimataifa unaitikia vyema zaidi na una gharama nafuu zaidi. Idadi ya wakimbizi na wale waliokimbia makazi yao inaongezeka kila mara, na kufikia idadi kubwa ya watu wanaokimbia migogoro, ukiukwaji wa haki za binadamu, na migogoro ya hali ya hewa.

Ni mwenendo unaokua na hakuna kinachoonekana kuweza kuuzuia... Ni masuala gani muhimu zaidi kwa UNHCR kwa sasa, na mahitaji ya dharura zaidi yako wapi?

Ukienda katika nchi zinazozunguka Sudan na kuangalia wimbi la wakimbizi kutoka nchi hiyo, hakika kuna hitaji la dharura. Ukizungumzia hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ni hitaji la dharura. Ukizungumzia kuhusu Venezuela na mienendo ya huko, ni hitaji la dharura. Au ukiangalia Warohingya, ambapo watu wengi wamekwama kambini na katika hali hii kwa miongo miwili iliyopita. Mtu hawezi kujizuia kubainisha  na kuainisha kama hitaji la dharura. Ni hali ngumu sana kusema uharaka uko wapi. Huku tukizingatia mahitaji ya kila siku ya watu, msaada wa kibinadamu pia ni muhimu ili kutafuta njia za suluhisho la kudumu. Tunapaswa kufanya kazi kwa bidii katika kutafuta suluhisho endelevu zinazoruhusu jamii hizi za wakimbizi kujumuishwa katika maisha ya kitaifa na kujitegemea. Suluhisho hizi pia zinahitaji kuendana na haki zao za msingi za binadamu za ulinzi na utu, lakini pia ziwe msaada kwa mataifa yenye hifadhi ambayo wako nayo leo.

Ni nini kinachokusumbua zaidi katika nafasi yako ya sasa

Ukosefu wa rasilimali ni msingi, na kila mgogoro unaokuja unahitaji rasilimali zetu zaidi, na kuna migogoro mingi kote ulimwenguni. Katika muktadha huo, nataka kusema kwamba dunia inaitwa kufanya zaidi ili kuzuia migogoro isiongezeke na kudhibiti na kutatua. Mgogoro wa uhamiaji una suluhisho moja la msingi na hilo ni amani na kuwa na watu wenye chaguo la kurudi majumbani mwao kwa usalama na heshima.

Ni wito gani ungependa kutoa kwa jumuiya ya kimataifa?

Ni jukumu letu la kisheria kama jumuiya ya kimataifa kulinda na kutoa msaada kwa watu wanaohitaji. Pia tunahitaji kusaidia kutoa suluhisho za kudumu kwa wale waliohamishwa. Huu ni wajibu wa kisheria, ni wajibu wa kimaadili na unazungumzia ubinadamu wetu wa pamoja. Hili ni jambo la kimaadili kufanya na pia ni jambo sahihi kufanya.

Ulizungumza mapema kuhusu umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na Kanisa na mashirika yanayotegemea imani. Mashirika ya kidini yanawezaje kusaidia UNHCR?

Mashirika yanayotegemea imani na mashirika ya Kanisa yamekuwa yakisaidia. Ninaweza kushuhudia kutokana na uzoefu wangu binafsi kazi muhimu waliyoifanya na ushirikiano muhimu walio nao na Umoja wa Mataifa. Matumaini yangu ni kwamba tunaweza pia kufanya kazi zaidi na mashirika mengine ya imani na kufanya kazi katika uhisani huu wa kidini ambao unaweza kuungana ili kuzungumza kuhusu maadili ya msingi ya imani yetu kwa upande wa ubinadamu, na katika kuwasaidia wanadamu wenzetu wanaohitaji.

KAMISHINA WA WAKIMBIZI WA UN

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

27 Januari 2026, 11:05