Fadhila ya matumaini ni muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia katika Ulimwengu mamboleo Fadhila ya matumaini ni muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia katika Ulimwengu mamboleo  (@VATICAN MEDIA)

Sikukuu ya Familia Takatifu: Mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia

Mama Kanisa anapenda kuwahimiza waamini kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii inayotaka kugeuzia kisogo utakatifu wa maisha ya ndoa. Mama Kanisa anatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani. Padre Denis A. Wigira kutoka Dar-es-Salaam ametia Neno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, wakati huu Mama Kanisa anapoelekea kufunga Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Fadhila ya matumaini ni muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia katika Ulimwengu mamboleo. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii inayotaka kugeuzia kisogo utakatifu wa maisha ya ndoa. Mama Kanisa anatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbalimbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Kwa hakika kuna haja ya kuwa na mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ili waweze kulielewa na hatimaye, kulipokea pendo la Mungu katika uhalisia wa maisha yao: Hii ni nguvu inayounganisha, kupatanisha na kuimarisha umoja na mshikamano. Ndoa ya Kikristo inasimikwa katika upendo kati ya Bwana na Bibi, tayari kupokea na kuendeleza zawadi ya maisha; malezi na makuzi ya watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Papa Leo XIV anasema, ndoa sio bora, lakini ni kanuni ya upendo wa kweli kati ya mwanaume na mwanamke: huu ni upendo kamili unaosimikwa kwenye uaminifu na wenye kuzaa matunda. Kumbe, wazazi wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa watoto wao, ili wawe wamoja, kama Fumbo la Utatu Mtakatifu, tayari kutoa zawadi ya maisha. Wazazi wawalee watoto wao katika: uhuru wa kweli na utii. Baba Mtakatifu Leo XIV anawasihi watoto kuwa na moyo wa shukrani kwa wazazi na walezi wao kwa zawadi ya maisha. Watoto wawapende, wawaheshimu na kuwatii wazazi na walezi wao. Rej. Kut 20:12.

Ndoa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu
Ndoa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu   (@Vatican Media)

Ndoa ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya upendo wa kweli wa wanandoa na wito mahususi wa kuishi kama bwana na bibi. Ndoa ni Sakramenti na zawadi inayowawezesha wanandoa kujikita katika mchakato wa utakatifu na wokovu wa wanandoa wenyewe. Kwa mwelekeo huu tendo la ndoa ndani ya familia, lililotakatifuzwa kwa Sakramenti na ni njia ya kukua na kukomaa katika neema na Fumbo la maisha ya ndoa, mwaliko kwa wanandoa ni kumwomba Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili aweze kuibariki Ndoa yao. Kanisa halina budi kuwasaidia wanandoa wanaoishi “uchumba sugu” wale waliofunga ndoa ya Serikali; wanandoa wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha ya ndoa, baada ya kuoa au kuolewa na kuachika na baadaye kuamua kuoa au kuolewa tena. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwashughulikia watu hawa kwa kuongozwa na ukweli wa upendo; wawafafanulie kwa kina na mapana mafundisho ya Kanisa na kwamba, hakuna majibu ya mkato, bali kila kesi inapaswa kushughulikiwa kikamilifu. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia.” Waamini wanakumbushwa kwamba, Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi, kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mpango wa Mungu kwa mwanadamu sanjari na Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia. Katika kuuenzi umuhimu wa familia katika maisha mazima ya mwanadamu, kuna umuhimu pia wa kuilinda familia dhidi ya maadui wake. Ndiyo maana nawaalika katika tafakari hii tuwaaangalie maadui wanaoishambulia familia leo.

Waamini wawe ni mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia
Waamini wawe ni mashuhuda wa Injili ya ndoa na familia   (@Vatican Media)

Adui wa kwanza tunaweza kumwita siasa mamboleo na adui wa pili ni utamaduni wa kuabudu uhuru usiokuwa na mipaka, hatari sana kwa tunu msingi za kifamilia. Katika maisha ya ndoa na familia, kuna matatizo, raha na karaha zake! Huko ni patashika nguo kuchanika, lakini yote haya ni mambo mpito, jambo la msingi ni kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwani Ndoa ni Sakramenti ya Kanisa kwa ajili pamoja na Kanisa na kwamba, upendo wa dhati kabisa unawezekana hata katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto kwa wanandoa na familia kuhakikisha kwamba, wanadumu katika nia njema, upendo wa dhati na uaminifu endelevu katika taabu na raha; katika magonjwa na afya; wapendane na kuheshimiana siku zote za maisha yao!Changamoto hizo ni kama vile: Talaka, Ndoa za utotoni, Uchumba sugu, Ndoa za mitaala, Kukosa uaminifu ndani ya ndoa, Ndoa za kurithi wajane, Mahusiano ya Jinsia moja, Ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali, Ndoa zisizo na watoto, Kubadili maumbile. Matatizo mengine ni pamoja na: Familia za mzazi moja, Familia zenye mchanganyiko wa Imani, Familia zinayoishi katika mazingira magumu ya uchumi, Familia zenye watoto walemavu, Familia zisizo na mzazi hata mmoja, Familia zisizoishi imani, Familia zisizo na maadili, Familia zilizopoteza uwezo wa kulea, Familia zisizo na kipato. Asili ya matatizo katika ndoa na familia ni pamoja na: Utamaduni na Mazingira: Tunaishi katika historia yenye mazoea, mila, desturi na mapokeo ya wazee wetu.  Iko sehemu ya utamaduni wetu isiyokubaliana na ukweli wa kimungu ambao ni wa lazima katika kuishi ndoa safi na familia bora. Mpaka sasa katika mazingira yetu zipo tamaduni zinazoruhusu talaka, ndoa za utotoni, uchumba sugu, ndoa za mitaala, “nyumba ndogo”, ndoa za kurithi wajane, ndoa za jinsia moja na ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali. Ni jukumu la kila mkristu, ndani ya familia, kuchekecha utamaduni wake, kwani kumekuwa na chenga zisizopita katika chujio la Kristo aliye Mwanga wa maisha yetu.

Waamini wasimame kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya kifo
Waamini wasimame kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya kifo   (@VATICAN MEDIA)

Harakati za kila mmoja ambazo zinalenga moja kwa moja kuibomoa familia: Harakati hizi zinatangaza na kupigia upatu uhuru usio wa kweli kwa mwanadamu.  Zinapotosha ukweli kwa kutenganisha ukweli wa maisha na ukweli wa asili katika viumbe na maumbile yao.  Maisha ya kiroho, maisha ya ndoa na familia, yanakuwa ni jambo binafsi na la faragha bila kuhusisha jamii na wala kumhusisha Mungu.  Uhusiano wa mtu na jamii unahuishwa katika sheria tu ambazo jamii inazitunga na kuzibadili mara kwa mara. Matokeo mabaya ya harakati hizi ni kukithiri kwa ubinafsi, kuenea na kuzagaa kwa matukio yenye kuchochea waziwazi tamaa za ngono kati ya watu wa rika zote. Wimbi kubwa la maisha huria, bila malengo wala kanuni na nidhamu ya kukataa malengo mema. Kuongezeka kwa mifarakano ya ndani ya nafsi na hivyo mifarakano kati ya mtu na mtu ndani na nje ya familia kunakoshuhudiwa na matatizo ya msongo wa mawazo, hali ya kukata tamaa. Harakati hizi zimejaa kwa wengi, na pia mtazamo potofu kuhusiana na maadili katika ndoa na familia. Na hivi mtu kufikia mahali kujiaminisha kwamba maisha yanawezekana bila Mungu na bila utu. Msimamo huu haumwezeshi mtu kupokea na kudumisha tunu njema za maisha ya ndoa na familia, ambazo kuasisi tunu hizo huzifanya ndoa na familia zifanyike katika kweli na zidumu na kusitawi na kuzaa matunda. Changamoto za ndoa na familia kimsingi ni changamoto za kukubali na kupokea tunu za maisha ya ndoa na familia. Tunahitaji kujihoji mbele ya Kristo juu ya wito wa kuwa wavumilivu, wasamehevu, wenye kiasi na wenye subira Rej. 1Kor.13:1-8). Tunahitaji kujipima tena kama tunazithamini na kuvutiwa nazo zile heri nane alizozitangaza Bwana wetu Yesu Kristo ambazo ni usafi wa moyo, upole, unyenyekevu, upatanisho, kuudhiwa kwa ajili ya haki, kukubali kushindwa/kudhulumiwa kwa sifa na utukufu wa Mungu (Mt.5:3-12).

Familia ni mahali pa kujifunza fadhila mbalimbali za Kikristo
Familia ni mahali pa kujifunza fadhila mbalimbali za Kikristo   (@Vatican Media)

Tunahitaji kujithamini mbele ya Mungu, kuona thamani ya upendo wa Kristo kwetu na wa yule aliyetupatia Kristo.  Maana “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye” (Rum.8:32). Hakuna anayeweza kututenga na upendo wa Kristo (Rum.8:35-39). Utatuzi wa matatizo mengi katika ndoa unajikita kimsingi katika changamoto ya kurudisha sura njema ya maagano kati ya Mungu na katika utakatifu kati ya Kristo na Kanisa lake (Rej.Waefeso 5:21-25). Wakristo wenye ndoa na ni wazazi kwa njia ya ubatizo wao, wanawajibika kutoa mchango wao wa pekee kwa ajili ya kufafanua mafundisho na tunu za kiinijli katika mazingira na tamaduni mbalimbali ambamo kwazo wanafamilia huishi maisha ya familia. Wanandoa kwa namna ya pekee, wamestahilishwa jukumu hilo kwa sababu ya karama yao na ni jukumu lao la kisakramenti hasa Sakramenti ya ndoa. Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika maisha na utume wa familia, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima; ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika: Uhai, huruma na mapendo. Familia za Kikristo hazina budi kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya vikwazo na kinzani zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo. Huu ndio uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni ushuhuda wa Injili ya familia unaotangazwa katika ukimya.

Kuna changamoto nyingi katika maisha ya ndoa na familia
Kuna changamoto nyingi katika maisha ya ndoa na familia   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi katika maisha. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika katika ndoto. Mtakatifu Yosefu aendelee kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya ndo ana familia. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii inayotaka kugeuzia kisogo utakatifu wa maisha ya ndoa. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbalimbali za Kikristo, kiutu na kijamii!

Wazazi wanawajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao
Wazazi wanawajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao   (@Vatican Media)

Kwa sasa tunajiunga na Padre Denis Agnes Wigira, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam anayechambua kuhusu changamoto ya utasa katika familia, baadhi ya sababu zake na umuhimu wa kudumu katika uaminifu wa maisha ya ndoa.

Familia Takatifu
27 Desemba 2025, 17:03