Lango la Jubilei ya Matumaini Kanisa Kuu la B. Maria Mkuu Lafungwa Rasmi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yameanza kufunga Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani.
Ni katika muktadha wa kufunga Malango ya Makanisa ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kardinali Rolandas Makrickas, Mhudumu mkuu wa Kanisa la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma, tarehe 25 Desemba 2025 amefunga rasmi Lango la Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma kwa Ibada ya Misa takatifu, hili ni Lango ambalo limetengwa kwa heshima ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yalizinduliwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko na yanafungwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, mashuhuda na viongozi wa Kanisa. Katika mahubiri yake, amekazia ujumbe wa Nabii Isaya unaowakumbusha waamini kwamba, wameitwa na kutumwa kuwa ni wajumbe wa haki na amani; watu makini wanaosikiliza Mwana wa Mungu na hatimaye, wanageuka kuwa ni mashuhuda wa mwanga unaong’ara gizani. Lango la Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu limefungwa rasmi, lakini neema na baraka kutoka kwa Mungu bado ziko wazi, katika Moyo wa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Mahujaji wengi wamevuka Lango la Jubilei, alama ya kukimbilia na kuambata huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Nyoyo za waamini zitaendelea kuwa wazi, ili kupokea neema, baraka na msamaha wa Mungu, anayetawala, anayefariji na kukomboa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ametangaza na kushuhudia uwepo angavu na endelevu wa Mungu katika maisha ya waja wake. Huu ni uwepo wa Mungu anayeokoa na kusamehe dhambi za watoto wake. Mwaka huu wa matumaini umewarejeshea tena, utu na heshima wale waliokuwa wamevunjika na kupondeka nyoyo na kwamba, Injili ya matumaini ni alama ya upendo wa Mungu usiokuwa na kifani; huyu ni Mungu anayewajali na kuwapenda waja wake upeo; Mungu anayesamehe na kusahau, Mungu anayesadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Huyu ni Mungu anayezungumza kwa njia ya Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu, anayefariji na kuwaongoza waja wake kwa upendo. Maadhimisho ya Jubilei ni mwaliko na changamoto ya kuendelea kusikiliza Neno la Mungu, ili kupyaisha matumaini; kushiriki Sakramenti za Kanisa, chemchemi za neema na baraka katika maisha, tayari kutangaza na kushuhudia makuu ya Mungu katika maisha yao. Haya ni matumaini yanayowashirikisha maisha na uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa waamini kukuza na kudumisha fadhila ya ukarimu, kwa kumpokea Mungu katika maisha yao; wawe tayari kumpokea Mungu, zawadi ya maisha dhidi ya Utamaduni wa kifo. Kardinali Rolandas Makrickas, Mhudumu mkuu wa Kanisa la Bikira Maria mkuu, Jimbo kuu la Roma anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanaacha Malango ya: Huruma ya Mungu, Upatanisho na Udugu wa Kibinadamu, yakiwa wazi. Hii ni fursa ya kuendelea kukumbuka Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” ya Baba Mtakatifu Francisko; maisha yake pasi na makuu kutoka kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliyezikwa Kanisani hapo. Huu ni mwaliko wa kujenga Kanisa la Kisinodi, Kanisa linalosikiliza na kujibu kilio cha Maskini na Dunia Mama; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, bila kusahau kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; huruma ya Mungu ikipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa bila kusahau dhamana ya upatanisho unaopata chimbuko katika maisha ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake.
Maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini yaendelee kuwasha Injili ya matumaini inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, ile mbegu ya matumaini iendelee kuzaa matunda katika maisha ya kila siku. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa mwanga usiozimika, huruma isiyokuwa na kikomo na matumaini yasiyo danganya, na kwamba, kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Kanisa liwe na ujasiri wa kubeba mikononi mwa waamini Injili na ndugu kuwakumbatia katika sakafu ya nyoyo zao!