Kard.Semeraro:Matendo ya upendo ya Mtakatifu Longo yanazungumzia imani yake
Vatican News
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mchakato wa kuwatangaza Watakatifu Kardinali Marcello Semeraro, Dominika tarehe 26 Oktoba 2025 aliongoza Misa Takatifu katika uwanja mbele ya Basilika ya Bikira Maria Mwenyeheri wa Rozari Takatifu, katika fursa ya kutoa Shukrani kwa Mungu kwa ajili ya kutangazwa mwanzilishi wa Madhabahu hiyo, Bartolo Longo na wenzake iliyofanyika mnamo tarehe 19 Oktoba 2025, katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambayo iliongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV.
Mtakatifu Bartolo Longo aliifanya mbegu ya ubatizo wake izae matunda katika utakatifu, akitoa mfano wa kile, ambacho Kardinali Semeraro alielezea kuwa, Papa Francisko aliandika katika Waraka wake wa Gaudete et exsultate, yaani 'Furahi na Shangilia' kwamba "Neema ya ubatizo wenu izae matunda katika njia ya utakatifu." Kwa njia hiyo, Kardinali Semeraro alisema kwamba, "katika mahubiri yake katika Misa ya kutangazwa kuwa Mtakatifu, Papa Leo XIV alisema "watakatifu, kwa neema ya Mungu, waliweka taa ya imani ikiwaka; kiukweli, wao wenyewe wakawa taa zenye uwezo wa kueneza nuru ya Kristo."
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza Watakatifu kisha alimtaja Mtakatifu Teresa wa Avila kusisitiza kwamba "ishara ya uhakika ya kujua kama tunatenda upendo wa Mungu ni kuona jinsi tunavyompenda jirani yetu. Matendo mengi ya upendo ya Mtakatifu Longo yanazungumzia imani yake na uhusiano wake halisi na Mungu: hayo ni matunda ya ubatizo wake. Alifikiria kituo cha watoto yatima cha wanawake kilichoanzishwa mwaka 1887, kituo cha watoto wa wafungwa kilichoanzishwa mwaka 1892, na Taasisi ya mabinti za wafungwa iliyoanzishwa mwaka 1922. Mwaka 1897, alianzisha Watawa wa Dominika, waitwao, Binti wa Rozari Takatifu wa Pompei. Yote haya sasa yanapitia maisha mapya na pia kukabiliana na dharura mpya," alisisitiza.
Hii ndiyo hali ya Taasisi ya Bartolo Longo, "ambayo sasa inawakaribisha na kuwaelimisha watoto na vijana kutoka katika hali ngumu za kifamilia, chini ya mwongozo wa Shirika la Ndugu wa Shule za Kikristo," "Kituo cha Elimu cha Bikira Mwenyeheri wa Rozari kinachoendeshwa na Masista wa Dominika wa Pompeii," ambamo "Nyumba ya Emmanuel huwakaribisha watoto na akina mama walio katika shida," "Kituo cha Yohane Paul II cha Watoto na Familia, chenye nyumba tano za kifamilia zilizokabidhiwa kwa vyombo mbalimbali vya kikanisa," na "Jiko la Supu liitwalo Papa Francisko kwa ajili ya Maskini," linalosimamiwa na Shirika la Kijeshi la Malta.
Kardinali Semeraro alisisitiza kwamba kazi nyingi za upendo zinashuhudia, kwamba Mtakatifu Bartolo Longo "alikuwa jicho na mkono wa Mungu; uwepo wake duniani na kazi alizoanzisha ni mwongozo kwa Mungu katika siku zetu za sasa." Ni kwa matunda haya yote ya utakatifu wa Mtakatifu Longo”, ambapo Kardinali alihitimisha huku akimshukuru Mungu na wakati huo huo "hayati Papa Francisko, aliyeamua kutangazwa Mtakatifu, na Papa Leo XIV" aliyemtangaza Mtakatifu.
Mwanzoni mwa Misa, utangulizi uliotolewa na Askofu Mkuu Tommaso Caputo,Msimamizi wa Madhahahu hiyo ya Kipapa akimshukuru Kardinali Semeraro.
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida letu kwa kubofya hapa: Just click here