2025.10.17 Askofu Mkuu Pena Parra huko Lateran na Maaskofu wa Venezuela. 2025.10.17 Askofu Mkuu Pena Parra huko Lateran na Maaskofu wa Venezuela. 

Peña Parra:José Hernández Cisneros Mtakatifu wa daraja na upatanisho!

Katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran,Katibu Msaidizi wa Vatican alipendekeza kutafakari utangazwaji wa Daktari wa Venezuela kama ishara ya amani na diplomasia ya kukutana kwa ajili ya nchi.

Na Sebastián Sansón Ferrari – Vatican.

Safari ya kiroho, ya kikanisa na kibinadamu kuhusu jinsi utakatifu unavyoweza kutenda kama upatanisho wa umoja kati ya watu. Hii ndiyo hotuba iliyotolewa alasiri ya tarehe 18 Oktoba 2025 na Askofu Mkuu Edgar Peña Parra, Katibu Msaidizi wa Vatican wa Masuala Makuu ya Sekretarieti ya Vatican kwenye Kongamano lenye mada: “Ushuhuda kwa Mchakato wa Amani: Changamoto ya Watakatifu Wapya wa Venezuela," lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran. Katika mada yake, yenye kichwa: "Utangazaji: Fursa ya Kuunganishwa tena na Amani, Diplomasia ya Kukutana," Askofu Mkuu alizungumza kwa hisia za mtoto wa kiume kurudi katika nchi yake, na kuamsha kumbukumbu ya mmoja wa watani wake mashuhuri:  José Gregorio Hernández, ambaye alitangazwa   kuwa Mtakatifu na kuwa tukio la kitaifa mnamo tarehe 19 Oktoba 2025.

Muda wa Upatanisho

"Kumzungumzia José Gregorio kunamaanisha kuzungumza juu ya ardhi yetu, watu wetu, mizizi yetu ya kina," Peña Parra alisema. "Tamaa yangu kuu ni kwamba kutawazwa kwa Dk. José Gregorio Hernández kuwa mtakatifu kupatikane kama wakati wa upatanisho kwa watu wa Venezuela, kama fursa nzuri ya kutazama siku zijazo pamoja, sio kutoka kwa upinzani, lakini kutoka kwa huduma ya unyenyekevu aliyoijumuisha." Kila kutangazwa kuwa mtakatifu, kwa yenyewe, ni kitendo cha amani, alisisitiza naibu huyo. Kanisa halipendekezi tu kielelezo cha maisha ya Kikristo, bali inatoa jamii "ushahidi wa ubinadamu waliopatanishwa." Hivyo, watakatifu wanakuwa “madaraja ya ushirika ambapo siasa au mazungumzo yanashindwa,” kwa sababu wana uwezo wa kuunganisha mioyo iliyogawanyika chini ya bendera ya imani na mapendo.

Watakatifu ambao wameweka Alama ya Maisha ya Watu

Katika hotuba yake, Askofu Mkuu Peña Parra pia alikumbuka mifano ya watakatifu ambao wameweka alama katika historia ya watu wao: Mtakatifu Oscar Romero, Mtakatifu Teresa wa Calcutta, Mtakatifu Martin de Porres, na Mtakatifu Thomas More, takwimu zinazoonesha jinsi utakatifu unavyoweza kuhamasisha mabadiliko ya kijamii. Alitilia mkazo sana dhana ya "diplomasia ya kukutana," akiongozwa na mafundisho ya Papa Francisko na alisisitiza katika hotuba kadhaa rasmi. Hili si kuhusu mahesabu ya kisiasa, lakini kuhusu sanaa ya Kikristo ya kujenga madaraja: "Sio juu ya kujadili maslahi, lakini kuhusu kuwezesha kukutana kati ya wale ambao wanaonekana kutopatanishwa."

Askofu mkuu aliwasilisha Hernández kama mfano halisi wa diplomasia hii ya kukutana: "Daktari, muumini, raia, mtu wa sayansi na sala, alijua jinsi ya kuunganisha binadamu na kimungu, sayansi na imani, huduma na kutafakari." Wakati wa janga la homa ya Hispania, Mtakatifu wa baadaye alijali kila mtu, bila ubaguzi, akivunja vizuizi vya itikadi au tabaka la kijamii: huduma ya kweli kwa wote. "Mtu anaweza kusema alikufa jinsi alivyoishi: kwenye njia ya huduma, kama ishara ya kukutana na mateso ya wengine," alibainisha Kaimu Katibu wa Vatican.

Kongamano kuhusu Mtakatifu wa Venezuela
Kongamano kuhusu Mtakatifu wa Venezuela

Kutangazwa Mtakatifu kama Ishara ya Upatanisho

Katika tafakari yake ya kitaalimungu na kichungaji, Askofu Mkuu Peña Parra alipendekeza kuelewa kutangazwa kwa Hernández kuwa "ishara kutoka kwa Mungu na fursa kwa wanadamu, kwani inatualika kutambuana kama ndugu, kuponya kutoaminiana, na kujenga upya kuishi pamoja kwa msingi wa ukweli na haki." Pia alisisitiza kwamba "kumtambua kuwa Mtakatifu kunamaanisha kuthibitisha kwamba ubora zaidi katika historia yetu si migogoro au itikadi, lakini uwezo wa huduma na kujitolea ambao alijidhihirisha katika kumwiga Yesu Kristo." Kulingana na Naibu Katibu wa Vatican  tukio hili litakuwa "wakati wa umoja wa kitaifa" ambapo Wana Venezuela wote, waamini au la,  wataweza kujitambua kwa ishara ya pamoja.

Wito wa Kujitolea

Askofu Mkuu Peña Parra alihimiza kuwa watu wasiwe watazamaji tu, bali  wawe wote wahusika wakuu katika safari iliyoanzishwa na kutangazwa kuwa Mtakatifu. José Gregorio, hakuhitaji kuandika mikataba ya kidiplomasia au kutoa hotuba za kisiasa ili kuwa mpatanishi." Maisha yake rahisi yakawa daraja kati ya imani na sayansi, watu na wasomi, dini maarufu na utamaduni wa chuo kikuu, ibada na ushiriki wa raia. Ndani yake, usemi wa Mtakatifu Paulo unatimizwa: ‘Kristo ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote kuwa mmoja’ (Ef 2:14). Maisha yake yalikuwa ishara ya amani ile inayozalisha ushirika. Akihitimisha hotuba yake, alisisitiza kwamba, kuinuliwa kuwa Mtakatifu Hernándéz Cisneros katika madhabahu ni ujumbe unaoenea ulimwenguni kote, kwani Kanisa litawakumbusha walimwengu kwamba, Venezuela ni zaidi ya kile kinachooneshwa na vyombo vya habari: “Ni nchi yenye uwezo wa kuzaa matunda ya utakatifu, na itatangaza kwamba amani inawezekana pale wanaume na wanawake wanapobadilisha maisha yao kuwa zawadi. "José Gregorio anajionesha kama shahidi wa uongozi kwa taifa. Kutangazwa kwake kuwa Mtakatifu wakati huo huo ni kumbukumbu ya shukrani, ishara ya upatanisho na unabii wa siku zijazo," na  alihitimisha akisema kuwa: "Maisha yake na mfano wake hufanya sauti ya Kristo isikike, ikitukumbusha kwamba amani na upatanisho vinawezekana na ambayo huanza daima katika moyo wa kila mtu ambaye anaitikia wito wake.”

Asante kwa kusoma maka hii. Ikiwa unataka kubaki na sasisho, tunakualika ujiendikishe,kwa kubonyeza hapa: cliccando qui

21 Oktoba 2025, 12:12