Vatican:Mradi wa EACOP,serikali wekezeni katika biashara rafiki wa mazingira&watu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko wa Laudato Si’ (Pentekoste, 24 Mei 2015) kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira, unabainisha wazi juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba yetu ya pamojakuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya imani, iwe kwa Wakristo na wasio wakristo, watu wenye mapenzi mema kwa maana wote tunaishi katika sayari moja inayopaswa kutunzwa na kulindwa. Utume wa Kanisa ni pamoja na kumsaidia mwanadamu wa ulimwengu mamboleo ule uelewa sahihi wa afya ya ulimwengu inavyotegemea na jinsi tunavyoitunza! Taalimungu ya kiekolojia pamoja na mambo mengine inagusa mambo mengi sana na hasa umuhimu kukabiliana na changamotozinazoibuliwa na uchafuzi wa mazingira kila eneo na baadaye kuendelea kusababisha athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi. Katika Ujumbe huo kwa hakika unafafanua hali halisi juu ya utu, hadhi, heshima na haki msingi za binadamu ambazo haziwezi kukiukwa na wale kwenda kinyume na utunzaji bora wa kazi ya Uumbaji. Hata katika Mafundisho jamii ya Kanisa yanahimiza mambo msingi hasa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hasa kwa kutazama mazingira na afya ya wazalendo wanaoishi ndani ya sayari hiyo.
Suala la Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki
Katika muktadha huo wa utunzaji bora wa mazingira, bado linaendelea suala la Afrika kuhusu “Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), lijulikanalo kama Bomba la Mafuta Ghafi la Uganda-Tanzania (UTCOP), ambalo linakusudiwa kusafirisha mafuta hadi Tanga. Kutokana na hilo hata Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu (PIHD) hivi karibuni limeelezea wasi wasi wake na kutokubaliana na ujenzi huo wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) huku likitoa wito kwa serikali zinazohusika kuzingatia hali ya nyumba yetu ya pamoja na kuwekeza katika miradi rafiki kwa ajili ya mazingira inayohifadhi mfumo wa ikolojia. Katika ujumbe ulioshirishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki (AMECEA) kwa njia ya mtandao mwezi uliopita tarehe 26 Machi 2022, vingozi wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu walithibitisha kuwa: “Kanisa Katoliki linasimama pamoja na wananchi wa Uganda na Tanzania kutounga mkono mradi wa EACOP na kuziomba serikali hizo mbili kuangalia uwekezaji katika miradi ambayo inaendana kuhifadhi na kutunza nyumba yetu ya kawaida ya pamoja, maskini, na uchumi.
Mafundisho jamii katoliki yatambua suala la tabianchi kuwa zito sana
Padre Joshtrom Isaac Kureethadam ambaye ni mratibu wa sekta ya Ikolojia ya Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu pia ni mwenyekiti wa falsafa ya sayansi na mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi Jamii na Siasa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesian Roma, na mmoja wa wataalam, mwenye shauku ya kuona vizazi vikichangia kwa kina juu ya hisia ya kustaajabisha mbele ya ukuu wa ulimwengu, lakini pia hisia ya kina ya wasiwasi kwa hali halisi inayozidi kuwa hatari ya makao yetu yaani sayari ya pamoja, alisisitiza kwamba, “dunia na maskini nchini Uganda wanalia dhidi ya maradi wa EACOP, na kama tunataka dunia yenye amani na endelevu, ni lazima tusitishe mradi huo EACOP na mabadiliko ya mafuta yasiyosafishwa kwenda vyanzo vya nishati mbadala”. Katika ujumbe wake alioushirikisha, Padre Kureethadam alifafanua zaidi kwamba Mafundisho Jamii Katoliki yanatambua kwamba mabadiliko ya tabianchi ni suala zito la kimaadili linalotishia kila kiumbe katika nyumba yetu ya pamoja. Pia ina athari mbaya katika juhudi zetu za kulinda maisha ya binadamu, afya, heshima, usalama, daima na chaguo la upendeleo kwa maskini, pamoja na uendelezaji wa manufaa ya kawaida ambayo hali ya hewa ni sehemu yake; kuishi kwa udogo na mshikamano na vizazi vya sasa na vijavyo, ili kupata amani na kutunza zawadi njema ya kazi ya Mungu ya uumbaji.” Akiwageukia wajumbe wa taasisi za kimataifa zinazounga mkono na kuhamasisha matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi katika nchi zinazoendelea barani Afrika na kila mahali, Padre Kureethadam alisisitiza katika ujumbe huo kwamba: “Ni wakati muafaka wa kusambaza fedha hizi kwa sekta inayoweza kurejeshwa.
Umakini wa Vatican kwa ajili ya maisha ya watu nchini Uganda na Tanzania
Nishati mbadala ina uwezo wa kuendesha uchumi mkubwa, kuunda ajira endelevu na kupunguza bili kubwa za umeme zinazoletwa na kuegemea kupita kiasi kwa nishati ya mafuta. Padre Kureethadam aidha alisisitiza kwamba sababu kuu za mabadiliko ya tabianchi “zinachochewa na binadamu na hasa zinajumuisha matumizi ya kupita kiasi na ya haraka ya nishati ya mafuta”. Akinukuu kifungu kutoka kwa Waraka Laudato Si' wa Papa Francisko, juu ya utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja, Padre huyo alifichua kwamba lengo la maisha ya kupita kiasi na ya haraka hayalengi katika kuboresha manufaa ya wote au maendeleo shirikishi na inaweza kuwa chanzo cha mahangaiko, na kusababisha maumivu kwa maskini na watu wote pia.” Ujumbe huo unabainisha kwamba “Nchini Uganda na Tanzania, umakini wetu unatazama shida kubwa inayowasubiri maskini na kuundwa kupitia Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lililopendekezwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Mradi wa EACOP unakadiriwa kuchangia hadi tani milioni 34 za (CO2) yaani hewa chafuzi ya ukaa, kila mwaka, na kuongeza hali ambayo tayari imekwisha imeelemewa”. Kwa maana hiyo , Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu (PIHD) wanayo matumaini kwamba juhudi zote, zikiunganishwa pamoja, zina uwezo wa kukuza mazungumzo ya Laudato Si' kwa kila mtu na kwa njia hiyo wanaongeza kuwa: “Tunaomba umoja huu ulete mabadiliko ya moyo ili ulimwengu ukomeshe upanuzi wa mafuta, kuporomoka kwa viumbe hai, na shida ya hali ya hewa”.
Upinzani wa bomba hilo la mafuta kutoka Hoima Uganda hati Tanga nchini Tanzania
Ikukumbukwe mradi wa Bomba la mafuta la Afrika Mashariki EACOP ni bomba linalopendekezwa la urefu wa karibu kilomita 1,445 litakalosafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania. Bomba hilo linatajwa kuwa refu zaidi duniani lenye joto. Shirika la Taifa la Mafuta la China na kampuni ya nishati ya Ufaransa ya TotalEnergies, sambamba na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda na Kampuni ya Maendeleo ya Petroli Tanzania, zimeendelea kusimama kidete katika kuendeleza mradi wa bomba hilo linalotarajiwa kuanza kusafirisha mafuta mwaka 2025. Hata hivyo hadi sasa Wanaharakati wa mazingira wamezitaka benki zaidi na makampuni ya bima kuondoa ufadhili wao kwa mradi wa bomba hilo. Wiki hii ya mwezi Aprili tu mradi huo ulipata pigo kubwa baada ya kampuni ya bima Allianz Group kujiondoa, ikiungana na benki 15 na makampuni saba ya bima, ambayo ni pamoja na HSBC, BNP Paribas na Swiss Re, ambayo yamekataa kutoa ufadhili wa kifedha kwa mradi huo kufuatia kampeni inayoendeshwa na mashirika kadhaa ya kutetea mazingira, yanayoongozwa na kundi la kimataifa la 350.org.
Shirika la mafuta la TotalEnergies linatetea ujenzi kuwa linazingatia sheria za mazingira
Kwa mujibu wa Shirika la 350.org linadai kuwa ujenzi wa bomba hilo utahamisha maelfu ya familia na kutishia rasilimali za maji katika mabonde ya Ziwa Victoria na Mto Nile. Shirika hilo la mazingira linasema bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi litazalisha takribani tani milioni 37 za hewa ukaa kila mwaka, na hivyo kuchochea mabadiliko ya tabianchi. Kampuni ya mafuta ya TotalEnergies yenyewe imetetea kuwa bomba hilo linazingatia kikamilifu sheria za mazingira ya Uganda na Tanzania. Ripoti ya tathmini ya athari za kijamii kwa ajili ya mazingira iliyofanywa na tume ya Uholanzi ya tathmini ya mazingira iliibua wasiwasi kuhusu hatari kubwa kwa wanyamapori hasa sokwe katika hifadhi za misitu za Bugoma, Wambabya na Taala. Bomba hilo la chini ya ardhi linatarajiwa kuanzia karibu na Ziwa Albert katika wilaya ya Hoima, magharibi mwa Uganda. Litazunguka Ziwa Victoria na kuingia kaskazini mwa Tanzania likielekea rasi ya Chongoleani iliyoko bahari ya Hindi hadi Tanga.