Kauli mbiu: inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora Mazingira Nyumba ya Wote ni: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Kauli mbiu: inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora Mazingira Nyumba ya Wote ni: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4.   (AFP or licensors)

Ujumbe wa Papa Leo XIV wa Siku ya 12 Ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira 2026

Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira inayoadhimishwa kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili watu wawe na uzima tele Rej. Yn 10:10. Zawadi hii ya uzima ndicho kiini cha utume na wito wa pamoja wa wanafunzi wa Kristo Yesu wa kujenga na kudumisha ustaarabu wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa kuanzia tarehe 1 Septemba 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Hii ni ahadi ya amani kuu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambapo watu wataacha vita na ghasia na kutumia vyombo vya silaha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Itakumbukwa kwamba, siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015, kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, 2015-2016. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya Utunzaji wa Nyumba ya Wote anasema, mazingira ni kito cha thamani kwa ajili ya wote na kwamba, mazingira yana uhusiano wa pekee na maisha ya binadamu. Ongezeko la kiwango cha joto duniani linaendelea kusababisha ongezeko la kina cha maji ya bahari; ukame na mafuriko; dhoruba pamoja na majanga asilia. Hapa mwanadamu anahamasishwa kubadili mtindo wa maisha na maendeleo, kwa kuambata teknolojia rafiki kwa mazingira. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi anasema Baba Mtakatifu Francisko yamepelekea baadhi ya watu kutumbukizwa katika utamaduni wa kutopea kwa imani, kutukuzwa kwa malimwengu na ubaridi wa imani mambo yanayoendelea kusababisha baadhi ya watu kutumbukizwa katika utumwa mamboleo na kazi za suluba; tatizo la kuwatelekeza wazee na kuwanyanyasa watoto, kwa mafao ya mtu binafsi.

Maskini ndio waathirika wakubwa wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii
Maskini ndio waathirika wakubwa wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii   (AFP or licensors)

Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kundi ambalo linaathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mapambano dhidi ya umaskini; kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani, haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa. Baba Mtakatifu Francisko aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji, ni kipindi cha toba na wongofu wa kiikolojia sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, hawa ndio wale “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”

Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote 2026
Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote 2026   (AFP or licensors)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili watu wawe na uzima tele Rej. Yn 10:10. Zawadi hii ya uzima wa milele ndicho kiini cha utume na wito wa pamoja wa wanafunzi wa Kristo Yesu wa kujenga na kudumisha ustaarabu wa upendo. Mama Kanisa anapoadhimisha Siku hii ya Kimataifa ya Kuombea Utunzaji Bora wa Kazi ya uumbaji, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa tena kutafakari juu ya zawadi ya maisha ya uzima na kuithamini dunia inayouendeleza, kwani hizi njia muafaka za kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani. Leo hii, binadamu anashuhudia majanga mengi na mateso makubwa kwa binadamu, kuvurugika kwa kazi ya uumbaji nako kunaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa na kwamba, changamoto kubwa mbele ya binadamu ni kuomba uponyaji na amani inayopata chimbuko lake katika Ulimwengu uliojeruhiwa na kwamba, Mungu wa uzima aliyefunuliwa na Kristo Yesu ndiye kiini cha amani hii ambayo kamwe Ulimwengu hauwezi kuitoa: “Amani nawaachia; amani yangu nawapa” Yn 14:27. Hii ni amani inayobubujika kutoka katika upendo wa kudumu wa Kristo Yesu na utunzaji wake kwa kila mwanadamu. 

Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu. Isa 2:4
Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu. Isa 2:4   (AFP or licensors)

Hata hivyo, ahadi hii ya amani inatofautiana sana na hali halisi iliyopo katika sehemu nyingi duniani. Nabii Isaya alizungumzia wakati ambapo Mataifa “yatafua panga zao ziwe majembe” (Isa 2:4), yakibadilisha kile kinachoharibu maisha kuwa kitu kinachoyategemeza. Lakini ushuhuda unaonesha kwamba, juhudi hizi zinaelekezwa kwenye kinzani, ghasia, vurugu na vita mambo yanayoacha majeraha yanayovuka mipaka ya uwanja wa vita. Husababisha vifo, kutenganisha familia na kulazimisha mamilioni ya watu kukimbia nchi na makazi yao, na hivyo kuzidisha hofu, ukosefu wa haki na migawanyiko. Rej.  Gaudium et Spes, 77-82). Vita pia huacha uharibifu wa kijamii na kimazingira unaodumu kwa vizazi vingi. Zaidi ya hayo, mwingiliano kati ya migogoro ya kivita na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote mara nyingi hujenga mzunguko hatari unaoharibu mifumo ya ikolojia, kuchafua rasilimali muhimu kama vile hewa na maji, na kudhoofisha usalama na uhakika wa chakula. Hali hii huchochea umaskini, ukosefu wa usawa, na mivutano mipya ya kijamii inayoweza kuchangia kuzuka kwa migogoro mingine zaidi. Aidha, vita husababisha majeraha yanayoharibu mfumo mzima wa maisha, yakiathiri si watu binafsi na jamii pekee, bali pia mtandao wao mpana wa uhusiano na familia nzima ya wanadamu, pamoja na uwiano wao na kazi ya Uumbaji. Hali hii inadhihirisha kushindwa kwa kina kuishi kwa sura na mfano wa Mungu, kuheshimu zawadi ya maisha na kutunza dunia ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitunza.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili na kiutu!
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili na kiutu!   (AFP or licensors)

Hili si tatizo la kisiasa pekee, bali pia ni tatizo la kimaadili na la maisha ya kiroho. Kwa kuwa chimbuko lake ni tamaa potofu, matumizi mabaya ya uhuru na mamlaka ya binadamu, na kwamba, vita husimama kama kinyume cha ushuhuda wa Injili ya amani. Kinzani na migogoro iliyotajwa hapo juu haidai tu uwajibikaji bali pia ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani utakao zaa matunda ya uaminifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu, upendo kwa jirani, na heshima kwa zawadi ya uumbaji. Hakika, hali ya kutoelewana iliyoko duniani kama vile: kinzani, vurugu, ukosefu wa haki, na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote si matokeo tu ya mifumo au miundo yenye kasoro; bali ni “dalili ya mgawanyiko wa ndani zaidi wenye mizizi yake ndani ya mwanadamu mwenyewe” kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Rej. GS,10. Kwa kweli, moyo wa mwanadamu ndio mahali ambapo mapambano makubwa zaidi hutokea na ambapo hali ya binadamu ya kuanguka dhambini hujidhihirisha. Moyo si mahali pa hisia pekee, bali ni kiini cha utu wa mtu, mahali ambapo akili, matamanio, utashi, na dhamiri hukutana. Hapa ndipo mwanadamu anapopambana na matamanio yanayopingana ndani yake: kati ya upendo na kutojali, ukweli na udanganyifu, haki na ukosefu wa haki. Rej. Yak 1:14–15.

Waathirika wakuu wa majanga asilia ni maskini
Waathirika wakuu wa majanga asilia ni maskini   (AFP or licensors)

Hivyo, majeraha ya vita na uharibifu wa dunia yana uhusiano wa karibu sana na hali ya moyo wa mwanadamu. Migogoro na kinzani inayomtesa wanadamu, kwa namna nyingi, ni udhihirisho wa nje wa hali ya kutoelewana na mgawanyiko wa ndani. Wakati moyo unapopotoka, uhusiano huathirika, na miundo inayojengwa na mwanadamu huanza kuakisi hali hiyo ya kutotulia na machafuko.Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika hotuba yake wakati wa kuanza rasmi utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alisema: “Jangwa la nje duniani linazidi kupanuka kwa sababu jangwa la ndani limekuwa kubwa mno. Rej. Mahubiri ya tarehe 24 Aprili 2005. Huu ni mwaliko wa kutambua kwamba, kwa namna fulani, kile kilichoharibika katika mazingira pia kimeharibika ndani ya mwanadamu. Kwa hiyo, ili kujenga jamii yenye amani, mwanadamu hapaswi tu kurekebisha miundo bali pia kufanya toba na wongofu wa ndani.  Sababu za ndani kabisa za migogoro na unyonyaji wa kazi ya uumbaji ni matokeo ya kinzani na mgogoro wa kimaadili na kiutamaduni, ikiwa ni pamoja na kupotea kwa hisia ya mipaka, hamu ya kutawala, harakati za kutafuta faida kubwa na ya haraka, na kushindwa kutambua utu, heshima na haki msingi za kila mwanadamu kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Utunzaji Bora wa Mazingira 1 Septemba hadi 4 Oktoba 2026.
Maadhimisho ya Utunzaji Bora wa Mazingira 1 Septemba hadi 4 Oktoba 2026.   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, hivyo, wito wa kinabii wa "kuyageuza mapanga kuwa majembe" Isa 2:4; si maono kwa mataifa pekee, bali ni wito kwa kila mtu na mwaliko kwa kila mtu kubadili uharibifu na kuleta uhai. Hata hivyo, mabadiliko haya hayawezi kupatikana kwa mabadiliko ya nje pekee. Yanahitaji, kwa kushirikiana na neema ya Mungu, wongofu wa kina wa mtu binafsi na wa jamii; yaani kumrudia tena Mwenye Mungu, ambaye atarekebisha matamanio yao, ataponya majeraha yao na kuwasaidia kukua katika fadhila. Bila toba na wongofu wa ndani, amani itabaki kuwa dhaifu na ya muda mfupi. Lakini pale mioyo inapopyaishwa, fursa mpya huanza kujitokeza. Kile kilichotumika kwa uharibifu kinaweza kuelekezwa tena kwenye uhai, kwenye kuwajali maskini, kuwalisha wenye njaa, na kulinda na kudumisha kazi ya Uumbaji. Hii ndiyo njia ya wongofu wa kweli wa kiikolojia, ambapo matokeo ya kukutana na Kristo Yesu yanaonekana wazi katika uhusiano wa binadamu na ulimwengu unaomzunguka. Rej. Laudato si, 217. Hivyo, amani huanzia ndani kabisa ya moyo na kusambaa nje katika uhusiano kati ya binadamu, jamii na ulimwengu katika mapana yake. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, ingawa changamoto zilizoko mbele ya binadamu ni kubwa, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kumwacha binadamu bila njia za uponyaji na mabadiliko. Badala ya silaha za vita, Mungu wa amani anamkirimia mwanadamu nguvu ya kuponya, kupatanisha na kujenga ustaarabu wa upendo. Huu ni mwaliko wa kulinda mifumo mingi ya ikolojia ya uumbaji, ya uhusiano wa kibinadamu na ya moyo wa mwanadamu wenyewe. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Ujumbe wake kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote kwaMwaka 2026 anawaalika watu wa Mungu kufikiria ulimwengu ambapo nguvu zinazotumika sasa kwa ajili ya vita zinaelekezwa kwenye maendeleo kamili ya mwanadamu, kama sehemu ya mchakato wa kutokomeza umaskini, kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kuleta upatanisho kati ya watu waliogawanyika.

Vita ni chanzo cha umaskini, taabu na mahangaiko ya wengi
Vita ni chanzo cha umaskini, taabu na mahangaiko ya wengi   (AFP or licensors)

Mtazamo kama huo unaakisi imani katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Kumbe, zana halisi za kujenga na kudumisha Injili ya amani si silaha za maangamizi, bali ni: Ukweli, majadiliano katika ukweli na uwazi; subira, wema, haki, huruma, uelewa, kujali na upendo. Fadhila hizi hutoka katika mioyo iliyofundwa na Injili na kutegemezwa na neema ya Mungu. Sifa hizi pekee ndizo zenye uwezo wa kubadilisha watu binafsi, kupyaisha jamii na kuponya majeraha ya ulimwengu mamboleo. Hii ni njia ambayo iko mbele ya walimwengu ingawa si rahisi anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kutafuta na kuambata amani sanjari na kujikita katika utunzaji bora wa kazi ya Uumbaji na kuilinda nyoyo yao kwa maana kila wanachokifanya hutoka ndani ya moyo! Rej.  Mithali 4:23. Ikiwa kama wanadamu wataitekeleza kazi hii kwa unyenyekevu na imani thabiti, wataweza kuwa ni washiriki katika kazi ya Mungu ya kufanya mambo yote kuwa ni mapya. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusonga mbele taratibu, lakini kwa uhakika, kutoka jangwani, kuelekea bustanini; kutoka kwenye utengano na kuanza kuelekea kwenye ushirika na umoja; na kutoka kwenye vita na vurugu na kuanza kuelekea kwenye ujenzi wa amani. Mwenyezi Mungu awajalie wanadamu ujasiri wa kutembea katika njia hii katika nyakati hizi, ili panga ziweze kweli kubadilishwa kuwa majembe; ahadi ya Injili ipate mizizi imara zaidi katika Ulimwengu mamboleo na amani ya Kristo Yesu itawale juu ya kazi yote ya Uumbaji.

Ujumbe Siku ya Mazingira 2026
20 Agosti 2026, 16:03