Kauli mbiu ya Mkutano wa SIGNIS kwa Mwaka 2026 ni “Mawasiliano ya Kidijitali kwa Amani ya Kitamaduni na Ustawi wa Mazingira” Kauli mbiu ya Mkutano wa SIGNIS kwa Mwaka 2026 ni “Mawasiliano ya Kidijitali kwa Amani ya Kitamaduni na Ustawi wa Mazingira”  

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Mkutano wa SIGNIS Kigali, Rwanda

Papa Leo XIV anasema kauli mbiu ya Mkutano wa SIGNIS kwa Mwaka 2026 ni “Mawasiliano ya Kidijitali kwa Amani ya Kitamaduni na Ustawi wa Mazingira” iwasaidie wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutafuta njia za kuragibisha sera za mawasiliano pamoja na nyenzo zake kutafuta na kuambata ukweli unaoheshimu utu na heshima ya mwwanadamu. Na kwa jinsi hii, kazi ya SIGNIS itaelekea katika utamaduni unaoakisi tunu za Kiinjili yaani: Ushirika, amani na mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Ulimwenguni SIGNIS, liliundwa kunako mwaka 2001 na kutambuliwa rasmi na Vatican tarehe 24 Oktoba 2014 baada ya kuunganisha Mashirika ya OCIC, lililoanzishwa mwaka 1928 na UNDA mwaka 1945 kushughulikia masuala ya tasnia ya mawasiliano ya jamii ndani ya Kanisa. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki katika mchakato wa kutetea, kulinda na kudumisha utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi. SIGNIS inapaswa kujielekeza zaidi katika masuala ya haki, amani na upatanisho, kama sehemu ya utume wake ulimwenguni ili kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa kweli na mwanga wa Kiinjili. SIGNIS kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2026 inafanya Mkutano wake mkuu huko Kigali, Rwanda nchi ya kwanza Barani Afrika kuwa ni mwenyeji wa Mkutano wa Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Ulimwenguni, SIGNIS, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mawasiliano ya Kidijitali kwa Amani ya Kitamaduni na Ustawi wa Mazingira.” Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Ubinadamu wa ajabu" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” uliotiwa mkwaju tarehe 15 Mei 2026, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 135 tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kunako tarehe 15 Mei 1891.

Waraka wa Kitume: Maginifica humanitas umezinduliwa ratehe 25 Mei 2026
Waraka wa Kitume: Maginifica humanitas umezinduliwa ratehe 25 Mei 2026   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa washiriki wa Mkutano wa SIGNIS, Kigali Rwanda kwa Mwaka 2026, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, anapenda kuchukua fursa hii kuwatumia salam na matashi mema washiriki wote wa Mkutano wa SIGNIS na kwamba, ni matumaini yake kuwa wajumbe wataweza kuchangia mawazo yatakayoliwezesha Jukwaa la Mawasiliano ya Jamii kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hizi ni nyakati za maendeleo ya teknolojia ya kidijitali zinazomwathiri binadamu katika medani mbalimbali za maisha yake. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Waraka wake wa “Magnifica humanitas” yaani: “Ubinadamu wa ajabu" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” anasema, mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii si tu kwamba, yanapasha habari, lakini yanaunda pia utamaduni kwa sababu mawasiliano yana nguvu na uwezo kutoka katika undani wa dhamiri zao yanaweza kuwaunda watu na kuwa na mtazamo wa ulimwengu kadiri ya dhamiri zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kauli mbiu ya Mkutano wa SIGNIS kwa Mwaka 2026 ni “Mawasiliano ya Kidijitali kwa Amani ya Kitamaduni na Ustawi wa Mazingira” iwasaidie wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutafuta njia za kuragibisha sera na mikakati ya mawasiliano pamoja na nyenzo zake kutafuta, kuenzi na kuambata ukweli unaoheshimu utu na heshima ya mwanadamu. Na kwa jinsi hii, kazi ya SIGNIS itaelekea katika utamaduni unaoakisi tunu za Kiinjili yaani: Ushirika, amani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwaweka wajumbe wa mkutano huu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia sala zake ili mkutano huu uweze kuzaa matumda yanayokusudiwa.

Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Naye Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anayemaliza muda wake wa uongozi katika ujumbe wake kwa washiriki wa Mkutano wa SIGNIS, Kigali, Rwanda anasema, kimsingi mawasiliano yanaanza na watu na wala si teknolojia na kwamba, mawasiliano yana uwezo wa kuwaunganisha watu, lakini kinyume chake mawasiliano ya kidijitali yanaunda mwelekeo wa upweke hasi, mahusiano yasiyo ya kweli kutoka katika undani wa mtu. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano wa kikatoliki wanapaswa kujenga jumuiya inayothaminiana, kwa kuunda mitandao ya kijamii inayolenga kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, teknolojia ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu na kwamba, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde yataendelea kuleta mabadiliko makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, lakini si chimbuko la hekima na busara, uhuru na tajiriba, uwajibikaji na wala upendo, kumbe, binadamu anapaswa kuwajibika na kuwa ni mhusika mkuu katika matumizi ya teknolojia ya akili unde na kwamba, teknolojia iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dr. Paolo Ruffini: Ujumbe kwa Mkutano wa SIGNIS Kigali, Rwanda
Dr. Paolo Ruffini: Ujumbe kwa Mkutano wa SIGNIS Kigali, Rwanda

Kimsingi, SIGNIS inawajibika kuunda mtandao wa mawasiliano ya kijamii, kwa kuwa na wajasiriamali, mafundi na wataalamu wa mawasiliano watakaosaidia kuunda ulimwengu wa kidijitali unaoheshimu na kuthamini ikolojia ya mawasiliano. SIGNIS inaweza kutekeleza dhamana na wajibu huu kwa kujenga mitandao ya mawasiliano ya wataalam wanaoshirikishana imani moja. SIGNIS liwe ni jukwaa la watu kuaminiana, mahali pa watu kupata habari ya kweli na mahali ambapo miradi ya mawasiliano inapangwa na kutekelezwa, kwa ajili ya huduma ya ukweli badala ya kutafuta faida kubwa. Mustakabali wa mawasiliano kwa siku za usoni unategemea sana uwajibikaji na asili ya mawasiliano yanayojikita katika ujenzi wa madaraja kwa njia ya imani, kwa kukutana pamoja na kushuhudia nyuso na sauti za binadamu katika ulimwengu wa maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde.

Teknolojia ya Akili Unde inazidi kuongezeka maradufu.
Teknolojia ya Akili Unde inazidi kuongezeka maradufu.   (REUTERS)

Mawasiliano hayana budi kujikita katika kuhifadhi tunu msingi za kijamii kama vile: Ukweli na uwazi; Uwajibikaji wa kijamii na kwamba, wadau wa tasnia ya mawasiliano wanawajibika kikamilifu kulinda utambulisho wao sanjari na mabadiliko yanayoendelea kuletwa na matumizi makubwa ya teknolojia ya akili unde. Mawasiliano ya jamii hayana budi kusimikwa katika uhuru wa mawazo, uwajibikaji wa kijamii; uhuru wa kupanga na kuchagua; kiu na kuwa na jamii ambayo inasimikwa katika ukweli, uwazi sanjari na hifadhi ya kumbukumbu hai, kwamba, wao ni nani katika Ulimwengu mamboleo! Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yamefungua fursa kubwa ya mawasiliano, kwa kuwawezesha watu kuwasiliana kwa ufasaha zaidi; watu kufahamu mambo kwa kina na mapana pamoja na kujenga ujirani mwema; lakini kwa bahati mbaya haya ni mambo yanaweza kubadilisha mihimili msingi ya ustaarabu wa mwanadamu kiasi cha kugusa na kutikisa undani wa maisha ya mtu; uhusiano wake na jirani zake na matokeo yake ni ukosefu wa usawa sanjari na kuibuka kwa ukosefu wa haki jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema watu wana kiu ya kuufahamu ukweli, ili wapate kuokoka. Huu ni mwaliko kwa wataalam na mabingwa wa matumizi ya teknolojia, na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali sanjari na matumizi ya sayansi ya akili unde kuhakikisha kwamba, yote haya yanakuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu kwa kulinda na kutunza utu na heshima yake. Lakini kwa bahati mbaya, maendeleo haya makubwa ya sayansi na teknolojia yamekuwa yakimong’onyoa utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuathiri mahusiano na mafungamano thabiti ya binadamu, changamoto kubwa ni kwa watu wa Mataifa kuona na kutambua ukuu wa mwanadamu, wenye chapa ya sura ya Mungu na wanadamu.

Papa Leo XIV Ujumbe Signis
04 Agosti 2026, 15:45