Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia vijana wa kizazi kipya nchini Perù kamwe wasiogope kuwa mashuhuda na vyombo vya Mungu katika mchakato wa kupyaisha matumaini kwenye mioyo ya watu wengi inayoteseka. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia vijana wa kizazi kipya nchini Perù kamwe wasiogope kuwa mashuhuda na vyombo vya Mungu katika mchakato wa kupyaisha matumaini kwenye mioyo ya watu wengi inayoteseka.  

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV Kwa Siku ya Vijana Kitaifa Nchini Perù

Papa Leo XIV anasema, uwepo hai wa Kristo ndani ya waja wake ndio moto wa ndani unaowachochea kuwa na ujasiri wa kutoka katika uchoyo, ubinafsi na hali ya kujijali binafsi na kutafuta starehe binafsi, ili hatimaye kuwa ni sehemu ya jumuiya ya ndugu wa imani, tayari kujenga na kudumisha urafiki wa kweli, tayari kutangaza na kushuhudia kwamba, inawezekana kuishi katika umoja ndani ya Kristo Yesu. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya kupyaisha matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kitaifa nchini Perù “JNJ Chulucanas 2026” kuanzia tarehe 30 Julai hadi 2 Agosti 2026 ni: "Uwe jasiri, Kristo Yu Hai.” Maadhimisho haya yanafanyika kwenye mji wa Chulucana mahali penye kushika nafasi maalum kwa Askofu Robert Francis Prevost, Baba Mtakatifu Leo XIV kwani ni katika mji huo huo wa eneo la Piura ndipo alipoanza utume wake katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini kunako mwaka 1985 na kwamba, utume huu umedumu kwa zaidi ya miaka ishirini.; ni utume uliomwezesha kuitikia wito wa Upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tukio hili, limeandaliwa na Tume ya Baraza la Maaskofu Perù kwa ajili ya Vijana na Waamini Walei.

Siku ya Vijana Kitaifa Nchini Perù
Siku ya Vijana Kitaifa Nchini Perù   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa njia ya video anawakumbusha vijana hawa kwamba, ule muda waliokuwa wanausubiri kwa hamu kubwa kwa kujiandaa kwa shauku kubwa sasa umewadia na kwamba, anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kutoka katika “sakafu ya moyo wake” kwa kuitikia maadhimisho haya ambayo kimsingi yanalipyaisha na kuliimarisha Kanisa. Kauli mbiu inayonogesha maadhimisho haya ni: “Iweni na ujasiri, Kristo yu hai.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, uwepo hai wa Kristo ndani ya waja wake ndio moto wa ndani unaowachochea kuwa na ujasiri wa kutoka katika uchoyo, ubinafsi na hali ya kujijali binafsi na kutafuta starehe binafsi, ili hatimaye kuwa ni sehemu ya jumuiya ya ndugu wa imani, tayari kujenga na kudumisha urafiki wa kweli, tayari kutangaza na kushuhudia kwamba, inawezekana kuishi katika umoja ndani ya Kristo Yesu.

Vijana ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini Perù
Vijana ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini Perù   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kutoka nchini Perù kufungua mioyo yao kwa mapana ili kupokea zawadi ambapo Kristo Yesu anataka kuwamiminia katika kipindi hiki, tayari kuwamegea na kuwashirikisha vijana wengine, tajiriba watakayojichotea katika maadhimisho haya. Kamwe matukio muhimu katika maadhimisho haya yasibaki yamehifadhiwa kwenye simu za viganjani au kwenye video kwenye mitandao ya kijamii, bali wayashirikishe na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kwani watu wengi wanavutwa na ushuhuda wa Furaha ya Injili yenye kuambukiza na kwamba, ushuhuda huu unatolewa na kijana anayempenda Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaambia vijana wa kizazi kipya nchini Perù kamwe wasiogope kuwa mashuhuda na vyombo vya Mungu katika mchakato wa kupyaisha matumaini kwenye mioyo ya watu wengi inayoteseka. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha ujumbe wake kwa vijana nchini Perù kwa kuwaweka nchini ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Uinjilishaji, Yeye awaombee, ili wapate kuwa ni “Chumvi na mwanga wa Kristo Yesu katika nchi ya Perù. Mwenyezi Mungu apende sasa kuwabariki.

Papa Vijana Perù
01 Agosti 2026, 14:18