Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi tarehe 3 Oktoba 1226. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi tarehe 3 Oktoba 1226.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Msamaha wa Assisi Jubilei ya Miaka 800 Tangu Mt. Francisko wa Assisi Afariki

Watu wa Mungu kwa mwaka 2026 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi. Injili ya Kristo ilikuwa ni mwongozo na dira ya maisha kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi pamoja na wafuasi wake, wakajenga Jumuiya ambayo ilikuwa kama mwili mmoja, roho moja na tumaini moja la wito wao, akiwa ametiwa moyo, alipokuwa akisali huko Porziuncola, na maono ya Kristo Yesu na Bikira Maria wakiwa wamezungukwa na Malaika!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Alhamisi tarehe 30 Julai 2026, maelfu ya wahamiaji walivuka mpaka kutoka nchini Morocco na kuingia katika eneo la Hispania la Ceuta na takwimu zinaonesha kwamba, kati ya watu 1,500 hadi 3,000 walifaulu kuingia siku hiyo, hasa kwa kuogelea kuzunguka kizuizi cha mpaka. Idadi hii inajumuishawatu wengi zaidi waliokuwa wameingia siku chache zilizopita, na takribani jumla ya watu 1,500 hadi watu 2,000 katika siku kumi zilizopita. Serikali ya Ceuta ikatangaza dharura ya kibinadamu na kijamii, ikisema vituo vya mapokezi vimejaa hadi kufurika. Katika patashika hii, wahamiaji zaidi ya 18 walifariki dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 2 Agosti 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali ya kutisha huko Ceuta na kwamba, anamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Afrika, asaidie kupatikana kwa suluhisho la amani, utulivu ili haki ipatikane na kutawala.

Hali inatisha sana huko Ceuta, Hispania
Hali inatisha sana huko Ceuta, Hispania

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, ili vita ikome sehemu mbalimbali za dunia na suluhisho la kidiplomasia lipatikane kwa migogoro hii. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea waathirika wote wa chuki na uhasama na vita na hasa dhaifu na watu wasiokuwa na ulinzi. Hawa ni watoto, wazee na wagonjwa. Kristo Yesu apende kuwafariji wote wanaoteseka na kuibariki kazi ya wale wanaotoa misaada na faraja kwa waathirika.

Wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Morocco limeingia nchini Hispania
Wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Morocco limeingia nchini Hispania   (ANSA)

Msamaha wa Assisi huadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Agosti, ikiwa ni siku maalumu ya kupata rehema kamili iliyoombwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya Kanisa la Porziuncola nchini Italia kutoka kwa Papa Onorio wa Tatu, kunako mwaka 1216. Mafundisho ya imani na ibada ya Rehema katika Kanisa Katoliki yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake, hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake.

Jubilei ya Miaka 800 tangu Mt. Francisko wa Assisi alipofariki dunia
Jubilei ya Miaka 800 tangu Mt. Francisko wa Assisi alipofariki dunia

Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba, inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata Rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza masharti yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa Rehema kamili. Nne; asali Kanuni ya Imani na Sala ya Baba Yetu, kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni, atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa Rehema Kamili. Huu ni muda wa kusali, kutafakari na kuomba rehema na neema ya Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi afariki dunia
Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi afariki dunia   (ANSA)

Watu wa Mungu kwa mwaka 2026 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi. Injili ya Kristo ilikuwa ni mwongozo na dira  ya maisha kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi pamoja na wafuasi wake, wakajenga Jumuiya ambayo ilikuwa kama mwili mmoja, roho moja na tumaini moja la wito wao, akiwa ametiwa moyo, alipokuwa akisali huko Porziuncola, na maono ya Kristo Yesu na Bikira Maria wakiwa wamezungukwa na Malaika. Baba Mtakatifu Leo XIV anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kuu na kuwataka waamini kuithamini na hasa wakati huu wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipofariki dunia huko Porziuncola, tarehe 3 Oktoba 1226.

Msamaha wa Assisi 2026
04 Agosti 2026, 14:43