Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza wanamichezo wote kutazama kwa imani Msalaba, ishara hii ya ukombozi, ambayo inabeba matarajio na matumaini, furaha na changamoto za washiriki wote wa michezo hii. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza wanamichezo wote kutazama kwa imani Msalaba, ishara hii ya ukombozi, ambayo inabeba matarajio na matumaini, furaha na changamoto za washiriki wote wa michezo hii.   (cem)

Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania: Haki, Amani na Udugu

Papa Leo XIV anawahimiza wanamichezo wote kuutazama kwa imani Msalaba, ishara hii ya ukombozi, ambayo inabeba matarajio na matumaini, furaha na changamoto za wanaoshiriki wote. Huku akiwahamasisha kushiriki katika mashindano haya kwa roho ya urafiki, udugu na ushindani wa haki. Papa Leo XIV anapenda kuwahakikishia sala zake ili Michezo hiyo iweze kusaidia kujenga madaraja kati ya tamaduni na watu mbalimbali, ikikuza roho ya ukarimu, upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania, ambayo yanafanyika mjini Taranto, Kaskazini mwa Italia kuanzia tarehe 21 Agosti hadi tarehe 3 Septemba 2026, kwa kuhusisha nchi mbalimbali kutoka Afrika, Asia, na Ulaya zilizoko katika eneo la Bahari ya Mediterania yananogeshwa na kauli mbiu: “Yakumbatie Maisha ya Baadaye." Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, tukio hili la Michezo ya 20 ya Mediterania litakuwa ni ishara ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mataifa. Michezo hii imefunguliwa kwa Ibada ya Misa takatifu pamoja na kusimika Msalaba wa Wanamichezo, Jumatano tarehe 19 Agosti 2026, majira ya jioni, kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Taranto. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa na Askofu mkuu Ciro Miniero wa Jimbo kuu la Taranto kwa ushiriki wa Askofu mkuu Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu.

Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania, huko Taranto
Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania, huko Taranto   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam na matashi mema kwa wanamichezo huko Taranto, katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Ciro Miniero wa Jimbo kuu la Taranto, Italia, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutoa salam zake za dhati kabisa kwa washiriki wa Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania inayoendelea mjini Taranto, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu anawahimiza wanamichezo wote kuutazama kwa imani Msalaba, ishara hii ya ukombozi, ambayo inabeba matarajio na matumaini, furaha na changamoto za wale wote wanaoshiriki katika ulimwengu wa michezo. Huku akiwahamasisha kushiriki katika mashindano haya kwa roho ya urafiki, udugu wa kibinadamu, na ushindani wa haki. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwahakikishia sala zake ili Michezo hiyo iweze kusaidia kujenga madaraja kati ya tamaduni na watu mbalimbali, ikikuza roho ya ukarimu, upendo, mshikamano, na amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewapatia baraka zake za Kitume, ikiwa ni uhakika wa msaada wa daima kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Michezo ijenge urafiki, umoja, upendo na mshikamano
Michezo ijenge urafiki, umoja, upendo na mshikamano   (ANSA)

Askofu mkuu Ciro Miniero wa Jimbo kuu la Taranto, Italia, katika mahubiri yake, amegusia kuhusu changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; umuhimu wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho; kwa kuondokana na woga, wasiwasi na hofu zisizo na msingi, ili kutoa nafasi kwa waamini kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi pamoja na kuthubutu kutenda kwa ari na moyo mkuu. Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania, ambayo yanafanyika mjini Taranto yanawashirikisha wanamichezo 4, 000 kutoka katika nchi 26 zinazozunguka Bahari ya Mediterania, kumbe hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu kutoka tamaduni mbalimbali ili kudumisha ukarimu, mshikamano wa udugu wa kibinadamu sanjari na ujenzi wa misingi ya haki na amani. Msalaba wa Wanamichezo ulianza kutembezwa kunako mwaka 2012, kielelezo cha imani na matumaini; changamoto na mwaliko kwa wanamichezo kutangaza na kushuhudia: haki na amani; Umoja, udugu na mshikamano na kwamba, kimsingi michezo ni amana na utajiri mkubwa wa maisha ya: kiroho, kijamii, kiutu na kimaadili na kwamba michezo inayo nafasi ya pekee katika malezi na majiundo ya watoto na vijana wa kizazi kipya. Michezo licha ya mafanikio yanayoweza kufikiwa na mtu binafsi, lakini ni fursa ya kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa haki na amani; Mshikamano wa udugu wa kibinadamu na maskini pamoja na watu dhaifu katika jamii na kwa njia hii, wanamichezo wanaweza kuisaidia familia ya binadamu kumwilisha ndani mwake Injili ya matumaini.

Michezo
21 Agosti 2026, 15:49