Kumbukizi ya Miaka 10 Tangu Tetemeko la Ardhi Lilipotokea Katikati Mwa Italia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Msururu wa matetemeko ya ardhi ulioanza usiku wa tarehe 24 Agosti 2016 ulisababisha vifo vya watu 299 na kuacha mamia wakiwa wamejeruhiwa. Maeneo ya Lazio, Marche, Umbria, na Abruzzo yaliharibiwa vibaya; Makanisa yakageuka kuwa vifusi, na maelfu ya familia kulazimika kuhama makazi yao. Eneo lililoathiriwa na tetemeko hili linajumuisha Manispaa 138 zilizoenea katika mikoa ya Marche, Abruzzo, Lazio, na Umbria, likichukua eneo la takriban kilomita za mraba 8,000 linalokaliwa na watu zaidi ya 540,000. Hili ni eneo lenye milima mingi, lililokirimiwa amana na urithi wa mazingira yenye kuvutia, utamaduni, na maisha ya kiroho; ni eneo ambalo linawakilisha sehemu kubwa ya maeneo ya ndani ya nchi ya Italia. Ilikuwa ni janga lililoacha alama ya kudumu katika maisha ya jamii nzima na ambalo, hadi leo hii, linabaki kuwa ni ukumbusho wa huzuni na kumbukumbu endelevu. Hata hivyo, sanjari na majeraha haya hadithi tofauti imeibuka: hii ni hadithi ya ujenzi upya, mshikamano, na kupyaisha upya maeneo haya. Ilikuwa ni tarehe 24 Agosti mwaka 2016 Baba Mtakatifu Francisko akiwa amehuzunishwa na vifo, mahangaiko na maombolezo ya watu walioathirika na tetemeko la aridhi lililotokea katika mkoa wa Marche, Umbria na Lazio hapa Italia, usiku wa kuamkia Jumatano, aliamua kuahirisha katekesi yake kwa mahujaji na wageni na badala yake aliongoza Ibada ya Rosari katika uwanja wa Kanisa Kuu la Makatifu Petro, kwa nia ya kuwaombea waliopoteza maisha katika tetemeko hili na pia kuwafariji wale wote walioathirika vibaya ambao kwa hakika walikuwa wamepoteza makazi na mali. Akitoa maelezo yake kwa watu waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa nia ya kusikiliza katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, aliwaomba radhi akisema, pamoja na kwamba alikuwa ameandaa katekesi yake kama ilivyo kawaida kwa kila siku ya Jumatano katika Maadhimisho ya mwaka wa Huruma ya Mungu.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa anaendelea kuzungumzia uwepo na ukaribu wa Kristo Yesu kwa watu wake, lakini baada ya kupata habari za kutokea kwa tetemeko baya la aridhi lililogonga katikati ya nchi ya Italia na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha, wengine wengi kujeruhiwa, maafa haya yamepiga moyo wake, na hivyo alipenda kuutumia wakati huu wa Katekesi kuonesha huzuni, mshikamano na ukaribu wake kwa watu wote waliopatwa na maafa haya ya kushtukiza. Na hasa kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na wale ambao bado wana mshituko mkubwa na hofu kubwa. Ni katika muktadha wa kumbukizi endelevu ya tetemeko la ardhi lililotokea usiku wa kuamkia tarehe 24 Agosti 2016 na kuathiri vibaya eneo la katikati ya mwa Italia, na hususan mikoa ya: Lazio, Umbria na Marche, Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, aliwakumbusha waamini na mahujaji kuhusu kumbukizi ya tetemeko hili na kusema kwamba anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha pamoja na familia zao pamoja na maeneo yote yaliyoguswa na kutikiswa na maafa haya makubwa. Imani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, viwe ni chemchemi ya ujenzi wa makazi mapya kwa waathirika.
Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 10 tangu Tetemeko la ardhi lilipoteka Katikati ya Italia, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, huko Pescara de Tronto, Arquata del Tronto kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale waliofariki dunia pamoja na wote walioathirika na janga hili. Katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kupyaisha imani na matumaini, bila ya kujikatia wala kukatishwa tamaa na utamaduni wa baadhi ya watu kutaka kujimwambafai kwa kumezwa na uchu wa mali na madaraka na kwamba, hili ni tukio ambalo litaendelea kubaki limeacha alama ya kudumu katika akili na nyoyo za watu na kamwe haliwezi kusahaulika, kwani limeacha mateso makali na machungu ya maisha.Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Italia kujenga maeneo haya kwa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kukuza na kudumisha haki na udugu wa kibinadamu na kamwe wasichelewe kutoa msaada pale unaopohitajika. Watu wote wanapaswa kuwajibika, kwa kujikita katika nguvu ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kama chemchemi ya faraja kwa wale wote walioathirika. Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yawasaidie waathirika kujenga na kudumisha umoja na mshikamano; imani na matumaini bila ya kukatishwa tamaa na matukio ya Ijumaa kuu, bali wawe na matumaini ya Ufufuko na maisha ya uzima wa milele.
Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI amehitimisha mahubiri yake akimwomba Mwenyezi Mungu awashe ndani ya mioyo yao tumaini jipya, hisia ya uwajibikaji, pamoja na moyo wa kujali wengine kwa kuanzia na wale walio katika mazingira magumu zaidi. Mwamba imara wa upendo wa Mungu uwawezeshe kukabiliana na jambo lolote watakakokabiliana nalo huko mbeleni, kwani kwa sasa wanafahamu kwamba, Roho ambaye ni upendo wa Mungu unaokuwa wetu unaokuwa kwao huwabadilisha na kuwapatia nguvu na uwezo wa kuleta upyaisho na ufufuo wa kile kilichoonekana kupotea. Mungu na awabariki na kuwajalia karama ya kuzaliwa upya.
