Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi yalipotolewa kutoka Costantinopoli hadi mjini Catania kunako mwaka 1126. Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi yalipotolewa kutoka Costantinopoli hadi mjini Catania kunako mwaka 1126.  (@Basilica Cattedrale Sant'Agata_Catania)

Jubilei ya Miaka 900 Tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha Yaliporejeshwa Mjini Catania, Mwaka 1126

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi yalipotolewa kutoka Costantinopoli hadi mjini Catania, Jumatatu tarehe 17 Agosti 2026, Kardinali Pietro Parolin, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin, amewaalika waamini kusali na kuwaombea Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanaoendelea kudhulumiwa, kuteswa na kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Agatha, Bikira na Shahidi kutoka mji wa Catania, huko Sicilia, Kusini mwa Italia. Alizaliwa kunako mwaka 231 BK katika familia tajiri, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu tangu utoto wake, kiasi cha kuifia imani yake kunako mwaka 251 BK wakati wa madhulumu Kaizari Decius baada ya kukataa katu katu kuikana imani yake kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu sanjari na kuivunja nadhiri yake ya ubikira, kielelezo cha uaminifu wake kwa Mungu. Aliuwawa kikatili katika ujana wake. Ilikuwa ni tarehe 17 Agosti 1126 Masalia ya Mtakatifu Agatha yaliporejeshwa mjini Catania, huko Sicilia kwa maandamano makubwa. Hata baada ya Miaka 900, bado ushuhuda wa Mtakatifu Agatha bado ni hai miongoni mwa waamini, kwani ni Mtakatifu ambaye katika maisha yake alibaki akiwa ameungana na Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kuvumilia na hatimaye, kuvuka mateso, majaribu na changamoto za maisha, akaendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika barua aliyomwandikia Kardinali Pietro Parolin, kama Mwakilishi wake wa Kitume katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha yaliporejeshwa mjini Catania anasema, Mtakatifu Agatha ni mfano hai wa uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; hii ni sadaka na upendo wa hali ya juu kabisa alioushuhudia Mtakatifu Agatha, Mama Kanisa anaendelea kuutafakari ushindi huu wa neema na baraka dhidi ya dhuluma na ukatili mkubwa kiasi kile; ushuhuda wa imani thabiti dhhidi ya woga na wasiwasi na upendo dhidi ya kifo. Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayomwezesha mwamini kuwa imara wakati wa majaribu, madhulumu na mateso. “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.” Zab 1:1.

Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi
Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi   (Saint Agatha)

Katika mkesha wa Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha yaliporejeshwa mjini Catania, Kardinali Pietro Parolin, amesema kwamba, katika ulimwengu mamboleo, ukanimungu unaendelea kushika kasi ya ajabu, lakini waamini wanapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yupo na bado anaendelea kutenda na kwamba, watu waaminifu kwa Mungu watapata furaha ya kweli kwa kutekeleza Amri na Maagizo ya Mungu katika maisha yao. Ni katika muktadha huu, Neno la Mungu linakuwa ni chemchemi ya maisha mapya yanayomwongoza mwamini katika uhuru wa kweli na kwamba, kwa njia ya tafakari ya kina, waamini wanaweza kugundua maisha yao na sauti inayowaalika kutafakari na hatimaye, kuweza kupata furaha ya kweli katika maisha. Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi alisimika maisha yake kwa uwepo wa Mungu, kiasi kwamba, aliweza kushinda mawimbi mazito ya hofu, woga na kifo, kumbe, Neno la Mungu linapaswa kuwa ni chemchemi ya imani na maisha mapya katika Kristo Yesu. Masalia ya Mtakatifu Agatha, Bikira na Shahidi yamarejeshwa tena mjini Catania tarehe 17 Agosti 2026 na kuwekwa hadharani kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Jimbo la Catania, tayari kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi yaliporejeshwa mjini Catania. Waamini waliojiandaa kikamilifu wameweza kupokea rehema kamili.

Jubilei ya Miaka 900 tangu masalia ya Mtakatifu Agatha yaliporejeshwa
Jubilei ya Miaka 900 tangu masalia ya Mtakatifu Agatha yaliporejeshwa   (@Basilica Cattedrale Sant'Agata_Catania)

Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa. Huu ni msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba, inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne, asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu Leo XIV. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema kamili. Maadhimisho haya yamewashirikisha viongozi mbalimbali wa Kanisa sanjari na waamini walei kutoka ndani na nje ya Catania.

Kardinali Pietro Parolin, Mwakilishi wa Kitume kwenye Maadhimisho haya
Kardinali Pietro Parolin, Mwakilishi wa Kitume kwenye Maadhimisho haya   (@Basilica Cattedrale Sant'Agata_Catania)

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 900 tangu Masalia ya Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi yalipotolewa kutoka Costantinopoli hadi mjini Catania, Jumatatu tarehe 17 Agosti 2026, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin, amewaalika waamini kusali na kuwaombea Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanaoendelea kudhulumiwa, kuteswa na kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu, Injili na Kanisa lake, lakini jambo la msingi kwa waamini wote ni kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kutembea hatua kwa hatua na waamini wake na kwamba, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu inayolistawisha Kanisa na kwamba, kifodini cha Mtakatifu Agatha ni mbegu ya imani, matumaini na mapendo, chemchemi ya amani na utulivu wa ndani. Kardinali Parolin amewakumbusha kwamba, kuna kifodini ambacho waamini wanakabiliana nacho kila siku ya maisha yao, yaani mwaliko wa kuwa waaminifu na wadumifu katika maisha yao ya Kikristo kama: Wabatizwa, wanandoa, mapadre au watawa. Wanandoa wanapaswa kudumu katika viapo vyao licha ya matatizo na changamoto katika maisha yao; waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya malezi na makuzi ya watoto wao: kiroho na kimwili. Vijana wakite maisha yao katika imani na kamwe wasipotoshwe na utandawazi wa mwonekano; Mapadre na watawa waendelee kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake na wazee waweze kupokea mateso na mahangaiko yao kwa: mapendo, imani na matumaini. Waamini hata katika ukimya wao, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya haki, amani na upendo; msamaha na upatanisho badala ya kuwa na kinyongo na kutaka kulipiza kisasi.

Kanisa Kuu la Jimbo la Catania, Kusini mwa Italia
Kanisa Kuu la Jimbo la Catania, Kusini mwa Italia

Waamini wote katika ujumla wao, watafute na kuambata utakatifu wa maisha, changamoto na mwaliko kutoka katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kardinali Parolin anasema mji wa Catania una urithi mkubwa wa imani, tamaduni, upendo na ibada mbalimbali. Tunu hizi zinapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ili ziweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Watambue kwamba, Injili ya upendo unaobubujika kutoka pale Msalabani ni chemchemi ya mabadiliko katika maisha ya watu wa Mungu. Huu ni upendo unaoweza kuwasaidia waamini kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha hasa umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa usawa; changamoto ya vijana wa kizazi kipya kukimbilia mijini ili kutafuta “malisho ya kijani kibichi” changamoto za maisha ya ndoa na familia pamoja na aina ya mifumo mipya umaskini wa hali na kipato; mambo yanayoendelea kuwaandama watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kumefanyika Maandamani ya Masalia ya Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi kwenye barabara kuu za mji wa Catania.

Mtakatifu Agatha Bikira na Shahidi

 

19 Agosti 2026, 15:39