Hija ya Papa Leo XIV Nchini San Marino: Jubilei Miaka 100: Rimini Kongamano na Misa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Papa Leo XIV Jumamosi tarehe 22 Agosti 2026 amefanya hija ya kichungaji Jamhuri ya San Marino kama kumbukumbu ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia unaosimikwa katika amana na urithi wa pamoja wa Kikatoliki, ushirikiano katika masuala ya Kimataifa pamoja na uwakilishi wa kidiplomasia kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5:14; amehudhuria na kushiriki Kongamano la Urafiki kati ya Watu; na hatimaye, majira ya jioni, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Bandari ya Rimini, nchini Italia. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa njiani kuelekea San Marino amemtumia ujumbe wa matashi mema Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimwelezea lengo la hija yake ya kichungaji katika Jamhuri ya San Marino ili kukutana na watu wa Mungu nchini humo kama sehemu ya kumbukumbu endelevu ya Jubilei ya miaka 100 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya San Marino na Vatican. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia heri na baraka, ustawi wa maendeleo ya kiroho, kimwili na kijamii kwa watu wa Mungu nchini Italia.
Naye Rais Sergio Mattarella amemshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV kwa ujumbe wake mahususi na ni matumaini yake kwamba, hija hii ya kichungaji huko San Marino italiangazia tukio hili kwa shauku kubwa, kwani linaashiria uhusiano wa kidiplomasia unaosimikwa juu ya tunu za pamoja, majadiliano endelevu kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani; utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kanuni maadili na utu wema yanayotoa uhai kwa Katiba ya Italia. Rais Mattarella anasema, Jamhuri ya San Marino inadhihirisha chimbuko lake la kina la Kikristo kupitia jina lake lenyewe na inahifadhi kwa fahari mila na desturi zake za kale za kitaasisi na kwamba uwepo wa Baba Mtakatifu Leo XIV nchini San Marino utakuwa chanzo kikubwa cha hamasa kwa mamlaka na raia pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaopata faraja kutokana na wito wa Baba Mtakatifu Leo XIV wa mara kwa mara unaotolewa wakati wa hija zake za kitume: changamoto ya ujenzi wa amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Katika kipindi hiki ambapo mfumo wa Kimataifa unakabiliwa zaidi na mielekeo hatari inayopendelea Sheria ya “mwenye nguvu mpishe” uwepo na ukaribu wa Baba Mtakatifu Leo XIV usioyumba wala kuyumbishwa na jamii za Mataifa yote yawe ni makubwa au madogo unatoa matumaini na imani kwa siku zijazo.
Hija za Kitume na Kichungaji zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ndani na nje ya Italia zinalenga pamoja na mambo mengine kuwaimarisha waamini katika fadhila ya imani, matumaini, mapendo na mshikamano, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu chimbuko la maisha na uzima wa milele. Kwa Baba Mtakatifu ziara hizi zinakuwa ni fursa ya kukutana mubashara na watu wa Mungu katika maeneo yao, ili kuhamasisha na kuragibisha mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu; ustawi, maendeleo sanjari na haki msingi za binadamu. Hii pia ni nafasi ya kuangalia changamoto na fursa zinazopatikana katika maeneo husika tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbata maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 22 Agosti 2026 amefanya hija ya kichungaji Jamhuri ya San Marino kama kumbukumbu ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia na kuhudhuria Kongamano la Urafiki kati ya Watu: “Meeting per l'amicizia fra i popoli” na hatimaye, majira ya jioni, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Bandari ya Rimini, nchini Italia. Itakumbukwa kwamba, Jamhuri ya San Marino ni nchi iliyoanzishwa na Mtakatifu Marino tarehe 3 Septemba 301 BK na Mwezi Aprili 1926 ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, uhusiano ulioimarishwa kunako mwaka 1989 kwa njia ya Mkataba kamili “Concordato” na kupyaishwa tena mwaka 1992 kwa kusoma alama za nyakati. Kumbe, hija hii ya kichungaji nchini San Marino ni sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Jamhuri ya San Marino.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake anasema, adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na ni chemchemi ya shughuli zote za kichungaji, mwaliko kwa waamini kupyaisha tena imani yao kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, Mkombozi wa ulimwengu aliyekuja kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Rej. Mt 20:28. Kiri kuu ya imani ya Mtakatifu Petro ni chemchemi ya furaha na matumaini na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa katika ngazi mbalimbali ni kielelezo cha huduma kwa watu wa Mungu. Kumbe, Ufunguo ambao Kristo Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro ni kielelezo cha huduma kwa Kanisa, mwaliko kwa viongozi wote wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao dhana ya uongozi kama huduma, kama alivyoshuhudia Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi, kwa kuendelea kumuiga Kristo: Mtii, Fukara na Mseja, kwa kutoa kipaumbela cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anawaonya viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema mamlaka waliyokabidhiwa na Mama Kanisa ya “Kufunga na Kufungua” kwa kukazia zaidi dhana ya watu: Kukumbatiana, kuunganika pamoja, kuoneshana ukarimu, kusamehe na kuwaokoa wale wanaoelemewa na kongwa la dhambi na mauti pamoja na matokeo yake, kwa kujenga na kudumisha mtandao wa viongozi wenye busara na hekima, ambao Mwenyezi Mungu amewakabidhi watu wake ili kuwaongoza, ili yote hayo yatendeke katika upendo, ustawi na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Nabii Isaya anatabiri lawama kuhusu Shebna kiongozi mkuu wa Mfalme aliyekabidhiwa madaraka ya kufanya upyaisho wa maisha ya kiroho, kimaadili na kijamii mjini Yerusalemu na katika Ufalme wa Yuda, lakini akaelemewa na ubinafsi, uchoyo na ufisadi, akalewa madaraka na kuanza kutumia fursa za kiuchumi kwa ajili ya upendeleo kwa rafiki na ndugu zake na wala si kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama ambavyo Mfalme Hezekia alivyomdhaminisha na matokeo yake, Mwenyezi Mungu akamchagua Eliakim, Mwana wa Hilkia, mtu mwaminifu, mtu huru, mkweli na mwadilifu naye akamweka katika kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake. Baba Mtakatifu anasema, ujumbe wa sehemu hii ya Maandiko Matakatifu ni kuwakumbusha waamini kwamba, kila kitu walicho nacho ni mali ya Mungu, kumbe, wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa wokovu kwa jirani zao. Mtume Paulo katika Somo la Pili anazungumzia kuhusu mpango wa wokovu wa Mungu kwa ajili ya watu wote na kwamba, hukumu zake hazichunguziki na wala njia zake hazitafutikaniki, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni rahisi kwa sababu Yeye ni upendo safi, mwaliko kwa waamini kupenda kwa moyo kama wa Mungu, kwa kulinganisha njia zao na njia za Mungu, mawazo yao na mawazo ya Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, tunu hizi msingi za kimaadili, uaminifu, ukarimu, na wema zinathaminiwa sana na watu wa Romagna, ambao kwa asili ni watu wakweli na wachangamfu; wachapakazi, na wenye kujitolea ili kujenga mshikamano. Huu ni ushuhuda unaopata chimbuko lake kwa watakatifu na wenye heri wengi waliozaliwa katika mkoa huu, ambao walijitahidi kumwilisha tunu za Kiinjili katika maisha yao.
Huu pia ni ushuhuda unaotolewa na Kanisa mahalia na hata kufikia kilele cha watu kufia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kutokana na ukarimu huu, eneo hili limekuwa ni maarufu kwa shughuli za kitalii na likizo kwa watu binafsi, mahali ambapo mtu anakutana na undani wake, tayari kujipatanisha. Kama Jumuiya ya waamini, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu kuwashirikisha wengine mang’amuzi haya ya ndani, kwa kuonesha ukarimu katika Makanisa na makazi yao, ili kuwashirikisha wengine Injili ya upendo. Baba Mtakatifu katika kipindi cha likizo, anapenda kuwahamasisha waamini kukita maisha yao katika sala, ujenzi wa umoja, utamaduni wa kusikiliza, ujasiri, kiasi pamoja na kuwa na moyo wa shukrani kwa uzuri ambao Mwenyezi Mungu anawakirimia na kwamba, wanapotekeleza yote haya, yanakuwa ni chemchemi ya furaha na maisha mapya. Baba Leo XIV ametumia fursa hii, kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari tunu hizi msingi ili kuendelea kuzimwilisha katika maisha yao. Mwishoni amewashukuru kwa mapokezi ya kukata na shoka pamoja na ushiriki wao wa imani na furaha katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu.
Kwa upande wake Askofu Nicolò Anselmi wa Jimbo Katoliki la Rimini, Italia amesema, tarehe 29 Agosti 1982, miaka 40 iliyopita Mtakatifu Yohane Paulo II aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jimbo Katoliki la Rimini. Hija hii ya kichungaji, imewasaidia kujiandaa kikamilifu kiroho na kimwili na matunda yake yataonekana kwa siku zijazo na kwamba, Ibada ya Misa Takatifu ni zawadi kubwa kwa maisha na utume wa Kanisa. Wanaendelea kuungana na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa ajili ya kusali, ili kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Kama sehemu ya zawadi kwa Baba Mtakatifu, wametia nia ya kuboresha uwanja wa mpira kwa ajili ya wafungwa na watachangia ujenzi wa Hospitali Ukanda wa Gaza na kwamba, wataendelea kuwaonesha upendo na ukarimu wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, tayari kumwilisha Injili ya upendo na mshikamano wa kibinadamu. Amewashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Rimini waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV Jimboni Rimini. Watu wa Mungu wanataka kujenga utamaduni wa upendo dhidi ya utamaduni wa watu kutaka kujimwambafai na kutumia nguvu!
Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa Jimboni Rimini, amepata nafasi ya kuwatembelea wagonjwa, walemavu na maskini wanaohudumiwa na Shirika la Misaada la Jimbo Katoliki la Rimini, Caritas Rimini, amezungumza pamoja nao na kuwapatia neno la faraja, imani na matumaini na kuwakumbusha kwamba, wagonjwa, maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia upendeleo wa pekee kwa kuwaponya, kuwasamehe dhambi zao na kuwarejeshea tena utu, heshima na haki zao msingi. Na watu hawa baada ya kukutana na Kristo Yesu na kuwatendea kwa huruma, ukarimu na upendo mkubwa, waliamua kuwa wafuasi wake na hivyo kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya wafuasi wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika hata wao, kumwachia fursa Kristo Yesu ili aweze kuwagusa, kuwaponya na kuwatakasa; waweze kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili waweze kuonja huruma na upendo wake wa daima, ili hatimaye, pamoja na Kanisa waweze kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na mauti. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu kwa ujasiri, huku wakishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa katika Parokia zao, vyama vya kitume, nyumba za huduma kwa wagonjwa na wazee, ili kuendelea kujifunza kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, hata wao ni watoto wapendwa wa Baba wa milele.
Kongamano la Urafiki Kati ya Watu “Meeting per l'amicizia fra i popoli” ni tamasha kubwa la kimataifa la utamaduni, imani, na majadiliano linalofanyika kila mwaka mjini Rimini, nchini Italia, lilianzishwa na Muasisi wa harakati za “Comunione e Liberazione” Don Luigi Giussani. "Upendo unaolisogeza jua na nyota nyingine" ndiyo kauli mbiu inayonogesha Kongamano la 47 la Urafiki kati ya Watu: “Meeting for Friendship Among Peoples,” ambalo limeanza kutimua vumbi huko Rimini kuanzia Ijumaa tarehe 21 na linatarajiwa kuhitimishwa Jumatano tarehe 26 Agosti 2026. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amesema, Kongamano hili ni mahali pa ujenzi wa amani, watu wanaopendana wanapokutanika; utu, heshima na haki msingi zinalindwa na kudumishwa; watu wanapojenga utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana; hapa ni mahali wanapokutanika watu ili kupanua na kujenga wigo mpana zaidi. Hii ni amana na utajiri ambao Mama Kanisa ameudhaminisha kwa waamini kwa ajili ya huduma kwa wale wenye njaa na kiu ya haki. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Kumbe, Kanisa linapaswa kuendelea kuwa ni chombo cha huduma na sauti ya maskini na wale wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amaonesha mshikamano wa dhati na binadamu wote, changamoto na dhamana kwa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Kamwe, Kanisa lisiridhike na hali yake, kwani litaanza kujitafuta lenyewe na matokeo yake ni kumezwa na malimwengu. Waamini wanaalikwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo, ambayo ni Sheria ya maisha na chombo cha wokovu, kinacho wabidiisha waamini kusafisha na kutakasa: mawazo, maslahi, tabia, uhusiano, mipango na uwekezaji, mambo yanayogusa na kutikisa nyanja zote za maisha ya binadamu kutokana na kuchafuliwa na utamaduni wa uchu wa madaraka.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia umuhimu wa uwajibikaji, huduma na wongofu wa ndani, tayari kutafuta na kuambata utukufu wa Mungu. “Basi, na tuungane ili kuyaweka huru maisha yetu kutokana na mashaka, utamaduni kutokana na kiburi, elimu kutokana na itikadi, kazi kutokana na ibada ya faida, na teknolojia pamoja na fedha kutokana na biashara ya kifo. Tukianzia na mashirika tuliyoyaanzisha na tunayofanyia kazi, na tufichue mifumo isiyo ya haki ya madaraka ambayo ndiyo chanzo cha umaskini, ukosefu wa usawa, vita na majanga ya kimazingira. Na tuizuie teknolojia isiwe na madhara pale inapovuka mipaka na kuwa yenye kuleta uharibifu. Tunahitaji waanzilishi jasiri ambao, kwa kubadili kwanza mwelekeo wa maisha yao wenyewe, wanaweza kufanya mabadiliko yanayotakiwa kwa kila mtu yawe yenye kushawishi na kuaminika.” Anasema Baba Mtakatifu Leo XIV. Kuna haja ya uwepo wa watu wanaopyaisha matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo, ili waweze kuonja ukuu wa Mungu katika maisha yao mintarafu tunu msingi za Kiinjili bila ya watu kuukimbia ukweli wa maisha. Vijana ni ishara ya matumaini na wala si tishio na kwamba, “upendo unaolisogeza jua na nyota nyingine" bado unachochea matumaini. Huu ni usuhuhuda kutoka katika hija za kitume ambazo Baba Mtakatifu amefanya hadi wakati huu. Upendo unawahimiza na kuwazindua kutoka usingizini, unachochea miito mipya na kuwaalika kuchukua tahadhari. Vijana wasiogope kujitoa bila ya kujibakiza, wajifungamanishe kwa roho ya kweli ya ulimwengu mzima, huku wakipanua mitandao yao zaidi ya mipaka yoyote finyu ya hisia ya mali au utambulisho wa kikundi, ni mwaliko kwa vijana kujitosa katika uhalisia wa maisha kwa ukamilifu zaidi.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka vijana wasimame imara kupinga mambo yanayotaka kuwatenganisha na jirani zao, tamaduni, mitazamo na asili tofauti na hasa kwa maskini zaidi miongoni mwa vijana na badala yake, vijana watoke nje, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa ustaarabu wa upendo kwani “Mungu ni upendo.” 1Yn 4:16. Katika upendo, hakuna kulazimishwa wala kulishwa itikadi, wala udanganyifu, hila au ushawishi wa kulazimisha watu kujiunga. Upendo upo tu katika uhuru, katika kukutana kwa dhati na katika kujitoa kwa ukarimu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa kuonesha mwamko wa kutaka kupokea Sakramenti za Kanisa, kielelezo cha uhuru wa kweli, changamoto kwa vijana ni kuendelea kujiaminisha kwa Injili ya Kristo Yesu na kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na kwamba, ni Kristo Yesu anayewanyanyua walioteleza na kuanguka kama mtu binafsi au kama jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kulipenda na kulithamini Kanisa, wajenge na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu na kwamba, wanapaswa kutambua maana ya kuwa ni watu wa Mungu, tayari kujenga na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari linalosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana, kuamua na kutenda kwa pamoja. Vijana wajifunze kutembea kwa pamoja katika umoja; kwa kusikilizana na kushirikishana imani, ambayo ni chimbuko la toba na wongofu wa ndani; uongozi uwe ni kielelezo cha huduma makini kwa watu wa Mungu na kwamba, karama mbalimbali ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wajenge umoja na kudumisha ushirika na Khalifa wa Matakatifu Petro. Roho Mtakatifu awafundishe watu wa Mungu kujenga na kudumisha ushirika.
Kwa upande wake Prof. Davide Prosperi Rais “Comunione e Liberazione” amesema, uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika Kongamano hili ni amana na utajiri ambao kamwe hautasahaulika katika akili na nyoyo za watu na kwamba, wakati huu Mfuko huu unaendelea kukua na kukomaa kwa kutambua dhamana na wajibu wake katika huduma kwa Kanisa, yaani uinjilishaji wa watu katika medani mbalimbali za maisha kwa njia ya Injili ya upendo na utamadunisho wa Injili; kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa haki na amani, sanjari na Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” kwa kifupi “MH” uliozinduliwa rasmi tarehe 25 Mei 2026, Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa unazungumzia kuhusu: Mtazamo thabiti wa uaminifu kwa Injili; misingi na kanuni za Mafundisho Jamii ya Kanisa; Teknolojia na utawala. Ukuu wa ubinadamu katika nuru ya ahadi za teknolojia ya akili unde; Kulinda utu wa binadamu wakati wa mabadiliko: na hatimaye ni kuhusu: Ukweli, kazi, uhuru; utamaduni wa nguvu na ustaarabu wa upendo. Mwishoni mwa Waraka wake wa Kitume, Baba Mtakatifu Leo XIV anapendekeza programu ya maisha ya Kikristo inayosimikwa katika kiasi, lakini inayohitaji nguvu ya kuweza kukabili mabadiliko ya teknolojia wakati wowote kwa mwanga wa Injili. Njia hii inawezekana kwa waamini kutafakari mpango wa Mungu katika maisha yao, kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kikanisa kwa ushiriki mkamilifu katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu sanjari na kujikita katika ujenzi wa Ulimwengu unaozingatia wema wa wote na kuendelea kusali katika umoja na Bikira Maria Mama wa Kanisa. Mfuko wa Urafiki Kati ya Watu “Meeting per l'amicizia fra i popoli” unasema umeanza kuufanyia kazi Waraka huu wa Kitume kama sehemu ya malezi, makuzi na majiundo ya wanachama wa Mfuko huu na wanamwomba Baba Mtakatifu Leo XIV awasaidie kutambua na hatimaye kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Wakati huo huo Dr. Bernhard Scholz Rais wa Mfuko wa Urafiki Kati ya Watu “Meeting per l'amicizia fra i popoli” amemwambia Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, Kongamano hili linawashirikisha watu zaidi 3, 000 na kwamba, tangu kuanzishwa kwake, Kongamano hili limekuwa ni mahali pa watu wa Mungu kukutana na kujadiliana; kujenga na kuthamini tajiriba na uzoefu wa watu kukutana, ili hatimaye, kujenga na kudumisha utamaduni na urafiki wa kijamii, tukio ambalo linageuka na kuwa ni hija ya ujenzi wa haki, amani na kudumisha uhuru wa kila mtu. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka wanachama wa Mfuko huu kujenga na kudumisha urafiki na utamaduni wa upendo unaojenga na kusimika maisha na historia ya binadamu.
Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa Nchini San Marino, Jumamosi tarehe 22 Agosti 2026 amebahatika kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu Jimbo Katoliki la San Marino-Montefeltro kwenye Kanisa la Mtakatifu Marino. Amepata fursa ya Kuabudu Ekaristi Takatifu sanjari na kutoa heshima zake kwenye Masalia ya Mtakatifu Marino. Hii ni jumuiya yenye urithi mkubwa wa imani, historia na ujasiri ulioneshwa na kushuhudiwa na Watakatifu Marino la Leo, takribani Karne kumi na nane zilizopita kwa kujitoa bila ya kujibakiza katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, uliopelekea kuzaliwa kwa utamaduni wenye tunu mpya zilizosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na watu wa Mungu wakaitikia wito huu na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kwa uaminifu mkubwa, mwaliko na changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kuishi katika furaha ya kweli, kwa kusikiliza kwa uaminifu sauti ya Mungu anayetaka kuwasaidia kutimiza ndoto zao za maisha. Pili, Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini San Marino kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kuitikia miito mbalimbali ndani ya Kanisa; wakiendelea kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii na kisiasa, kwa kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kikamilifu kushiriki katika kutangaza na kushuhudia Injili ya amani. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi wote wa Kanisa, waalimu na walezi wanaoendelea kujisadaka wa ajili ya majiundo na malezi ya watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo, lakini wazazi na walezi wanapaswa kukumbuka kwamba, wao ndio walimu wa kwanza wa imani, tunu msingi za Kiinjili na utu wema kwa kuwashirikisha kikamilifu wazazi na walezi, ili nao pia waweze kujisikia kwamba, wanahusika kikamilifu katika malezi na majiundo ya watoto wao katika kuwarithisha imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo. Watoto na vijana warithishwe uzuri na utakatifu wa Sakramenti za kuingizwa katika Ukristo, ili kuimarisha hija ya utakatifu wa maisha, kwani kwa njia ya Ubatizo wabatizwa hushiriki ukuhani wa Kristo, utume wake wa kinabii na wa kifalme, ili waweze hatimaye kuwa na ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na kwamba, waamini wachote nguvu kutoka katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga wa Kristo Yesu ulimwenguni.
Waamini wajitahidi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu itakayowawezesha watu wengine waweze kukutana na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Yote haya yafanyike chini ya kivuli cha Injili ya upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema “tunaishi katika ulimwengu uliojeruhiwa na migogoro mingi, tukishuhudia kwa wasiwasi kuongezeka kwa vurugu, kujitenga, na hofu dhidi ya wengine. Tukikabiliwa na hali hizi zinazotia wasiwasi, jibu letu pekee ni kufuata njia ya Injili kwa uthabiti zaidi. Msukumo wake unapatikana katika kiini cha jamii "iliyojengwa juu ya heshima kwa uhuru wa mtu binafsi na ule wa wengine, na zaidi ya yote, juu ya heshima kwa Mapenzi ya Mungu" (Mt. Yohane Paulo II, Mahubiri, San Marino, 29 Agosti 1982) jamii inayofundisha na kuhimiza kujali watu walio katika mazingira magumu na hatarishi; kusameheana, ujenzi wa ushirika, na mshikamano.” Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka watu wa Mungu nchini San Marino kujenga na kudumisha ujirani mwema, kwa kushirikiana na kusaidiana ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazotokana na upungufu wa watu na huduma za kijamii, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kuendelea kujikita katika umwilishaji wa tunu msingi za kijamii na hatimaye, kuondokana na uchoyo pamoja ubinafsi. Jumuiya za Kikristo ziwe ni ishara ya umoja na ushirika, Injili ya matumaini na ujenzi wa udugu wa kibinadamu na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, kipaumbele chake katika shughuli za kichungaji ni ujenzi wa ushirika na umoja wa Kanisa.
Kwa upande wake, Askofu Domenico Beneventi, wa Jimbo Katoliki la San Marino-Montefeltro, amemwelezea Baba Mtakatifu Leo XIV changamoto wanazokumbana nazo katika maisha na utume wa Kanisa, bado wanaendelea kutangaza na kushuhudia Imani, inayomwilishwa katika mshikamano na ujenzi wa ujirani mwema. Wanaendelea kujikita katika kutoa huduma katika sekta ya elimu; kwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, wanaendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Wanataka kujenga Kanisa hai linalotangaza na kushuhudia furaha na Injili ya maisha; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu na kwamba, wanataka kujenga nyumba ya amani.
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 22 Agosti 2026 amefanya hija ya kichungaji Jamhuri ya San Marino kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5:14. Hija hii ilikuwa pia ni sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Jamhuri ya San Marino ilipoanzisha Uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, Mwezi Aprili 1926. Hii ni hija inayofuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetembelea nchi ya San Marino mwaka 1982 na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mwaka 2011. Hii ni nchi ambayo imekita amana na utajiri wake katika uhuru “Libertas” unaopania pamoja na mambo mengine kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; dhamiri nyofu pamoja na kutafuta ukweli. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kulinda na kutunza dhamiri nyofu. Uhuru unawasaidia kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika na majadiliano katika ukweli na uwazi, chemchemi ya upendo katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kumbe, uhuru wa kweli na ushirika ni chanda na pete, ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Kwa Mtakatifu Marino uhuru na utii ni mambo yanayo bubujika kutoka katika Injili na kwamba, Mtakatifu Marino na Leo ni mashuhuda na wajenzi wa miji huru inayosimikwa katika msingi wa amani na kwamba, wananchi wa San Marino wanajipambanua kwa kuwa ni wafanyakazi hodari.
Jubilei ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kiplomasia kati ya San Marino na Vatican ni changamoto ya kusimama kidete kujenga na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia, amani na utulivu dhidi ya “mawasiliano ya kukurupuka, lugha ya uchokozi, na mivutano ya madaraka inayotawala nyakati zetu, wito wa diplomasia ni kukuza majadiliano na kila mtu ikiwa ni pamoja na wale wanaoonekana kuwa “wasiofaa” au wasiotambuliwa kama washirika halali wa majadiliano huku ikionesha unyenyekevu na subira kuu ili kuunganisha hata ishara ndogo kabisa za nia njema kutoka kwa pande zinazohasimiana, kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuleta na kudumisha amani Rej. Magnifica humanitas, 224. Ni katika muktadha huu, San Marino inaweza kuwa ni kielelezo bora cha siasa safi, mahali ambapo kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa zinamwilishwa, ni nchi ambayo inaendelea kutafuta na kutekeleza ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujikita katika kanuni auni, mshikamano na haki jamii na kwamba, kwa sasa San Marino iko kwenye mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, ustawi, ulinzi na utunzaji wa Injili ya uhai katika hatua zake zote kuanzia kutungwa mimba hadi kifo cha kawaida. Ni kipengele muhimu sana cha ubinadamu. Teknolojia inaweza pia kusaidia katika utunzaji wa binadamu kwa mfano, kwa kutoa zana zinazosaidia katika utabiri na upangaji wa mambo lakini bila kuingilia uhuru na uwezo wa binadamu wa kufanya maamuzi, kwani binadamu ndiye kiini cha mahusiano na ndiye mwenye jukumu la kufanya maamuzi. Rej. Magnifica humanitas,114.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, utunzaji na heshima hii kwa jirani imekuwa sifa bainifu ya historia ya San Marino tangu kuanzishwa kwake. Kama ilivyobainishwa, sifa hii imejidhihirisha katika utamaduni wa ukarimu ambao haujawahi kuyumba kwa karne nyingi, kwa wale wanaoteseka na kukabiliwa na changamoto ngumu za maisha. Hivi karibuni, jambo hili limeonekana wazi katika uungaji mkono na ukarimu uliooneshwa kwa watu wa Ukraine, hasa wakati wa kuzuka kwa mgogoro huo, pamoja na katika utiifu wa Sheria za Kimataifa za Kibinadamu katika kipindi hiki cha kihistoria ambapo sheria hizo zinaonekana kupuuzwa, au hata kusiginwa waziwazi, kila siku. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “hali hii ya kujali pia inatokana na utamaduni wa Kikristo wa nchi hii pamoja na ushirikiano endelevu na wenye tija kati ya mamlaka za kisiasa na Askofu mahalia katika kulenga ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu ameishukuru San Marino kwa ushuhuda huu na kuwataka kusimama kidete kulinda kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi.
Kwa upande wao Kapteni Alice Mina na Vladimiro Selva viongozi wakuu wa Jamhuri ya San Marino wamesema, nchi yao imesimikwa katika amani, uhuru unaokazia utu, heshima na haki msingi za binadamu; katika nguvu ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu, heshima na majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba, mizizi ya nchi hii ya San Marino inapata chimbuko lake kutoka kwa Muasisi wake Mtakatifu Marino. Wamekumbuka hija ya kitume iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 29 Agosti 1982 na ile ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI alioifanya tarehe 19 Juni 2011, huu ni mwaliko wa kuendelea kushikamana ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo katika ujenzi wa urafiki wa kijamii, imani na majadiliano; kwa kulinda na kutunza utu na heshima ya kila binadamu. San Marino imekuwa ni kimbilio la wakimbizi na wahamiaji 100, 000 kutoka Ukraine wakati wa vita na Urusi. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hayana budi kujielekeza kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Viongozi hawa wamegusia tema kama vile haki na amani; umuhimu wa kuheshimu Sheria na Mikataba ya Kimataifa.
