Papa Leo XIV: Kanisa Linapaswa Kujibu Kwa Makini Changamoto za Teknolojia ya Akili Unde
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” ulitiwa mkwaju, tarehe 15 Mei 2026, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 135 tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kunako tarehe 15 Mei 1891 na alisema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ina thamani na heshima yake ya asili. Aligusia kuhusu haki msingi za wafanyakazi, mshahara na wajibu wa wafanyakazi; Umiliki wa binafsi wa mali; wajibu wa Serikali, sanjari na kuwalinda wanyonge ndani ya jamii; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV: anaonya kwamba, kamwe katika maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde, binadamu asigeuzwe kuwa kama “mashini, takwimu au biadhaa” bali utu, heshima na haki zake msingi zinapaswa kuzingatiwa na kuheshimiwa. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yawe ni kwa ajili ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi, utu na heshima ya familia ya binadamu; kwa kuwa makini, na hivyo, kuwarejeshea watu imani na matumaini, mambo yanayohitaji ushirikishwaji wa wengi.
Mama Kanisa anataka kujikita katika majadiliano ya kina na mapana mintarafu matumizi ya teknolojia ya akili unde, kwa kumwilisha hekima ya binadamu, dhamiri nyofu, huduma makini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi cha kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kukabiliana kwa pamoja na changamoto zilizoko mbele ya binadamu na hivyo kushirikiana katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu na udugu wa ubinadamu na kwamba, Waraka wa wa Kitume wa “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” kwa kifupi “MH” uwaamshe, watu wote ili wawe ni wajenzi na vyombo vya matumaini, tayari kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kama alivyofanya Bikira Maria kwa utenzi wake wa “Magnificat.”
Ni katika muktadha huu wa Mama Kanisa kukabiliana barabara na changamoto zinazoendelea kuibuliwa na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya akili unde, Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu René Osvaldo Rebolledo Salinas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Chile, kama sehemu ya Maadhimisho ya Semina ya Saba iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kipapa cha Chile kuanzia tarehe 27 hadi 28 Julai 2026, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Changamoto za Teknolojia ya Akili Unde”, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde hayana budi kuelekezwa katika huduma kwa binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujikita katika: utu, heshima, haki msingi pamoja na ukweli. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kuragibisha mawasiliano ya jamii katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde, tayari kulinda, kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, teknolojia ya akili unde iwe ni kwa ajili ya huduma ya ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu aweze kuangaza akili za washiriki na awasaidie kukabiliana barabara na changamoto zinazoibuliwa na teknolojia ya akili unde. Hekima, busara na uwajibikaji ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele, ili kweli mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa yasaidie kuwa ni madaraja ya kuwakutanisha watu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Akifungua semina hii ya Saba, Kardinali Fernando Natalio Chomali Garib, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago de Chile amechambua athari za mitandao ya kijamii na kwamba, mitandao hii inapaswa kujikita katika utu, kwa sababu zinaakisi hisia, mahusiano pamoja na kinzani; kumbe, Baba Mtakatifu Leo XIV katika Waraka wake wa Kitume “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” anakazia mambo makuu manne: “ukweli, wema, uzuri, na manufaa na kwamba, tafsiri ya matumizi ya teknolojia ya akili unde, isitafsiriwe tu kwa kigezo cha maendeleo ya teknolojia, bali kwa kukazia: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na ukweli. Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, kuimarisha mafungamano ya kijamii, ili kujenga mawasiliano yanaodumisha ujenzi wa Yerusalemu mpya na wala si kama ilivyokuwa katika ujenzi wa mji na mnara wa Babeli, kielelezo cha anguko kubwa la binadamu. Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde,” ukizingatiwa katika undani wake, una mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, semina hii iliyowashirikisha wajumbe kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari na kwamba, Kanisa linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza katika kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji.
