Mtakatifu Inyasi wa Loyola: Vipaumbe vya Wayesuit: 2019-2029: Elimu na Vijana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Inyasi wa Loyola (Iñigo López de Oñaz y Loyola) alizaliwa tarehe 23 Oktoba 1491 huko Azpeitia nchini Hispania. Akafariki dunia tarehe 31 Julai 1556 mjini Roma. Ni Askari aliyetubu na kumwongokea Kristo Yesu na Kanisa lake. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 24 Juni 1537 akapewa daraja takatifu ya Upadre. Mtakatifu Inyas wa Loyola pamoja na mapadre wenzake wapya walitumia muda huu kufanya mazoezi ya shughuli za kuchungaji pamoja na kutumia muda mrefu kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu. Kwa kushirikiana na wenzake, akafaulu kuanzisha Shirika la Wayesuit (Jesuits). Alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri na Papa Paulo V kunako tarehe 27 Julai 1609. Papa Gregory wa XV akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 12 Machi 1622. Mama Kanisa anafanya kumbukumbu yake kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai. Yote haya ni kwa ajili ya Sifa na Utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi “Ad maiorem Dei gloriam au Ad majórem Dei glóriam.”
Vipaumbele vya Wayesuit katika kipindi cha miaka kumi yaani kuanzia Mwaka 2019 hadi mwaka 2029 ni msingi wa mahusiano na mafungamano kati ya Wayesuit na Kristo Yesu; mambo yanayomwilishwa katika maisha binafsi na katika Jumuiya inayosali na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Vipaumbele hivi ni sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Wayesuit ambao umefanyiwa kazi katika kipindi cha miaka miwili, ili kuhakikisha kwamba, Wayesuit wanatumia kikamilifu rasilimali watu, vitu na fedha, ili kufikia lengo hili muhimu, daima wakiendelea kusoma alama za nyakati. Hapa kinachohitajika ni kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu, kwa kuwashirikisha watu kutoka katika makundi na medani mbalimbali za maisha, ili kugundua amana na utajiri unaofumbatwa katika mafungo ya kiroho yanayotolewa na Wayesuit. Lengo ni kuhakikisha kwamba, haki jamii inapewa msukumo wa pekee, ili kweli mabadiliko makubwa yanayojitokeza katika masuala ya: kiuchumi, kijamii na kisiasa, yanazingatia haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao ni pamoja na kuyaangalia yale mema, mazuri na matakatifu yanayowazunguka vijana katika “vijiwe vyao”, kwa kusikiliza na kujibu kiu na matamanio yao halali kadiri ya mabadiliko ya jamii; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.
Hii ni changamoto ya kuwapatia vijana fursa ya kuonesha vipaji na ubunifu wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Umefika wakati kwa viongozi wa Kanisa kujifunza kutoka kwa vijana wa kizazi kipya! Mwishoni, ni utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kushiriki katika sera, mbinu na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira, pamoja na kuangalia sera mbadala, ili kuweza kudhibiti uharibifu wa mazingira unaoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu wengi duniani. Hii ni changamoto ya kushirikiana na wadau mbalimbali kama sehemu ya mbinu mkakati wa utekelezaji wa malengo haya katika maisha na utume wa Wayesuit. Baba Mtakatifu Leo XIV hivi karibuni alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu vya Kiyesuit “The Association of Jesuit Colleges and Universities, AJCU. Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu 28 vya Kiyesuit vinaunda Shirikisho la la Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu nchini Marekani sanjari na Taasisi tatu wanachama washiriki kutoka nchini Canada. Vyuo hivi vimekita mizizi yake katika taaluma mbalimbali, tafiti za kina, masomo ya sanaa huria pamoja na masomo ya kitaaluma.
Hii ilikuwa ni fursa maalum kwa wajumbe hawa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha mshikamano wa upendo na Khalifa wa Mtakatifu Petro na viongozi wakuu wa Shirika la Wayesuit ambalo limekuwa mstari wa mbele kwa karne nyingi katika sekta ya elimu na hivyo kujipatia mafanikio makubwa, lakini pia linakabiliana na changamoto mamboleo katika sekta ya elimu, ukanimungu; Serikali nyingi zinashindwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wakimbizi na wahamiaji; vijana wengi wamejikatia tamaa na hivyo kuonekana kama “daladala” iliyokatika usukani; athari za mabadiliko ya tabianchi; uchoyo na ubinafsi; matumizi mabaya ya rasilimali za dunia pamoja na changamoto ya ukuaji wa teknolojia ya akili unde. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV alibainisha vipaumbele vinne wanavyopaswa kuvifanyia kazi, kwa kutoa fursa hata kwa watoto wa maskini kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii zao.
Jambo la kwanza ni kwa Shirika la Wayesuit kuwaonesha watu wa Mungu njia inayokwenda kwa Mungu kwa njia ya mafungo ya maisha ya kiroho; wanafunzi katika tafiti zao wasaidiwe kutafuta na kuufahamu ukweli wenyewe; wasaidiwe kuzima kiu ya kumtafuta na kumfahamu Mungu katika maisha yao. Vijana waoneshwe fursa za kuweza kukutana moja kwa moja na Kristo Yesu katika: Neno, Maisha ya Sala, Sakramenti na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili na viongozi wenyewe wajiweke wazi kwa maongozi ya Roho Mtakatifu katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku. Pili, Baba Mtakatifu anawataka Wayesuit, kutembea na kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi zao kutokana na sababu mbalimbali. Wanafunzi waelimishwe kutambua haki jamii, mafundisho jamii ya Kanisa, wajitahidi kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Kipaumbele cha tatu ni kuhakikisha kwamba, Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinakuwa ni maeneo muafaka ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya; vijana wajenge na kudumisha urafiki wa kijamii; wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watangaze Injili ya matumaini kwa kuwekeza zaidi katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, huduma kwa maskini pamoja na maisha ya sala kwa kukumbuka kwamba, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini ya waamini na kwamba, kwa kushirikiana na kushikamana na Kristo Yesu, kila kitu kinawezekana. Rej. 1Pt 1:3; Mt 19:26. Kipaumbele cha nne kinakita mizizi yake anasema Baba Mtakatifu Leo XIV katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hali hii inatokana na ukweli kwamba, kuna athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, mwaliko kwa Jumuiya zao kuwa makini katika utekelezaji wa ikolojia fungamani ya binadamu. Kumbe, taasisi na vyuo vikuu vinaweza kufundisha dhamana hii ya utunzaji bora wa mazingira kwa kujikita katika uhalisia na wala si katika nadharia peke yake.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde hayana budi kuelekezwa katika huduma kwa binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujikita katika: utu, heshima, haki msingi pamoja na ukweli. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kuragibisha mawasiliano ya jamii katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde, tayari kulinda, kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, teknolojia ya akili unde iwe ni kwa ajili ya huduma ya ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Waraka wake wa Kitume “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” anakazia mambo makuu manne: “ukweli, wema, uzuri, na manufaa na kwamba, tafsiri ya matumizi ya teknolojia ya akili unde, isitafsiriwe tu kwa kigezo cha maendeleo ya teknolojia, bali kwa kukazia: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na ukweli. Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru Wayesuit kwa sadaka na majitoleo yao katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika sekta ya elimu, akawapatia baraka zake za kitume kwao wenyewe, familia pamoja na taasisi wanazoziongoza.
