Kumesalia mwaka mmoja kabla ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 huko Seoul, Corea ya Kusini kuanza kutimua vumbi. Kumesalia mwaka mmoja kabla ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 huko Seoul, Corea ya Kusini kuanza kutimua vumbi.  

Maadhimisho ya Siku 42 ya Vijana Ulimwenguni, 2027 Seoul, Korea ya Kusini

Papa Leo XIV alitangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 Jimbo kuu la Seoul, Corea ya Kusini, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2027 na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu; “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Matumaini yaliyomo ndani ya waamini ndiyo yanayowapatia nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi wakati wa kufungua maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana Oktoba 2018 yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” aliwataka Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, wanajenga sanaa na utamaduni wa kusikiliza vijana kwa makini na kuzungumza nao kwa ujasiri unaofumbatwa katika ukweli na uwazi. Lengo ni kusaidia mchakato wa wongofu wa kimisionari unaojikita katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu kilio na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya sanjari na kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wanaoonekana kuvunjika na kupondeka moyo! Mama Kanisa katika mbinu mkakati wake wa shughuli za kichungaji anataka kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika: haki, amani; ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Katika maadhimisho ya sehemu ya kwanza, Mababa wa Sinodi ya vijana walikazia umoja na mshikamano wa Kanisa, wajibu na umuhimu wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana katika kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuambatana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya Injili na matumaini!

Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni nchini Korea ya Kusini
Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni nchini Korea ya Kusini   (AFP or licensors)

Viongozi wa Kanisa wajenge sanaa na utamaduni wa majadiliano na vijana katika ukweli na uwazi, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Mababa wa Sinodi walikazia umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, viongozi wa Kanisa hawana budi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kuwa karibu na binadamu mdhambi na hatimaye, akampatia nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu. Kanisa halina budi kujikita katika toba, wongofu wa ndani, unyenyekevu, ari na moyo mkuu; mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda unaoakisi Fumbo la Utakatifu wa maisha na Sakramenti ya maisha hai. Vijana wasikilizwe kwa moyo wa huruma na mapendo. Kanisa linawapokea na kuwasaidia kadiri ya matamanio yao halali, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika hatua mbalimbali za maisha, malezi na makuzi ya vijana: kwenye familia, shule na taasisi za elimu bila kusahau umuhimu wa maisha na utume wa vijana kwenye Parokia. Kuna kundi kubwa la vijana ambalo limejeruhiwa na kwamba, linahitaji kusikia Injili ya matumaini inayomwilishwa katika Katekesi makini na endelevu; katika huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; malezi ya awali na endelevu kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Papa Leo XIV anawakaribisha vijana wote nchini Korea ya Kusini
Papa Leo XIV anawakaribisha vijana wote nchini Korea ya Kusini   (ANSA)

Vijana wafundwe kuthamini na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wasindikizwe kwa imani, matumaini na mapendo, ili waweze kung’amua wito katika maisha yao na hatimaye, kufanya maamuzi magumu na endelevu! Vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Changamoto za maisha ya kifamilia, kiuchumi, kijamii na kitamaduni; mambo yanayoibuka kwa kasi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na hali zao, bila kutafuta njia za mkato katika maisha! Madhara ya vita, njaa, magonjwa, rushwa na ufisadi ni kati ya mambo yanayochangia hali ngumu ya maisha ya vijana, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Kuna haja ya kuimarisha utandawazi wa mshikamano utakaotoa fursa ya ajira, elimu, ustawi na maendeleo endelevu ya vijana kwa kuondokana na utamaduni usiojali wala kuthamini utu, maisha na haki msingi za binadamu. Vijana wajikite katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, mambo yanayohatarisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Taasisi za elimu na vyuo vikuu viwe ni jukwaa la kurithisha imani, maadili na utu wema; kwa kuwafunda vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano; tayari kujisadaka katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Maandalizi ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni yameanza kupamba moto
Maandalizi ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni yameanza kupamba moto   (@Vatican Media)

Itakumbukwa kwamba, baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Vijana mahujaji wa matumaini” Baba Mtakatifu Leo XIV alitangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2027 na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu; “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Matumaini yaliyomo ndani ya nyoyo za waamini ndiyo yanayowapatia nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini hadi miisho ya dunia. Amewakaribisha vijana wengi zaidi huko Seoul, Corea ya Kusini, ili kwa pamoja waweze kuendeleza ndoto na matumaini.

Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana 2025
Maadhimisho ya Jubilei ya Vijana 2025   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, kumesalia mwaka mmoja kabla ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 huko Seoul, Korea ya Kusini kuanza kutimua vumbi. Vijana pamoja na wachungaji wao watakaohudhuria maadhimisho haya wanazidi kuwa ni kiini cha maandalizi ya tukio hili muhimu la Kikanisa. Wimbo Maalum wa tukio hili pamoja na sala rasmi na ushuhuda wa watakatifu watano walioteuliwa kuwa ni wasimamizi na walinzi wa kiroho kwa ajili ya Maadhimisho haya ni nyenzo msingi za kichungaji zinazowasaidia vijana wa kizazi kipya kujiandaa kikamilifu kiroho kwa ajili ya maadhimisho haya na kwamba, maadhimisho haya yamezidi kutajirishwa kutokana na imani, shauku na ushiriki hai wa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mwaliko kwa Maaskofu na viongozi wa Kanisa watakao ambatana na vijana kwenda Seoul watumie vyema amana, utajiri na rasilimali hizi katika maandalizi yao, ili hatimaye, waweze kuiishi siku hii kama tajiriba halisi ya imani, umoja na mshikamano wa Kanisa sanjari na vijana kukutana binafsi na Kristo Yesu Mfufuka.

Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni yameanza kushika kasi
Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni yameanza kushika kasi

Wakati huo huo, Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni nchini Korea ya Kusini inasema, inaendelea kukamilisha maandalizi ya maadhimisho haya kwa kujikita katika ushirikiano wa kimataifa, huduma kwa ajili ya mahujaji, malazi, usafiri, usalama, huduma za afya na mawasiliano. Vijana wote wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya maisha yao ya kiroho. Wimbo rasmi wa maadhimisho haya uko mbioni kuzinduliwa rasmi na umetungwa na Francis Jiyoon Kim kutoka Korea unaochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni: “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33 na kwa lugha ya Kilatini unasomeka hivi: “Confidite, Ego Vici Mundum.” Kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho haya, vijana katika maeneo yao, wanahimizwa kushiriki kampeni ya kupanda miti kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Usajili wa washiriki wa maadhimisho haya utazinduliwa hivi karibuni kwa kutumia kiunganishi kifuatacho: website www.wydseoul.org.

Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni
31 Julai 2026, 15:17