Pad.Pineda:"Sisi ni wahamiaji wanaowahudumia wahamiaji"
Fr. Paul Samasumo – Barcelona.
Kwa kuwa hakuna Kanisa lolote huko Barcelona linaloweza kushindana na ukuu wa usanifu wa Basilika ya Antoni Gaudí ya Sagrada Família, yaani Familia Takatifu, wenyeji waliipatia jina la utani Parokia ya Mtakatifu Agostino kuwa ni “Kanisa Kuu la Maskini.” Lakini kuna umuhimu zaidi kwa jina hili la utani. Kanisa hili la karne ya 18 limetumika kwa muda mrefu kama kimbilio kwa wakazi wa tabaka la wafanyakazi wa Wilaya ya Raval ya Barcelona. Urithi huo unaendelea hadi leo hii, lakini wakati huu, ukihudumia mahitaji ya wahamiaji kutoka Asia, Amerika Kusini, na wachache kutoka Afrika Kaskazini.
Jumuiya ya Waagostinian wa huko Katalonya
Padre Dennis Pineda ndiye Mkuu wa Jumuiya ya Waagostinian huko Katalonya, na Msimamizi mkuu wa Parokia ya Mtakatifu Roque huko Badalona. Anaongoza timu ya Waagostinian (OSA), yenye watawa wanne iliyoko Mtakatifu Agostinian huko Raval ya Barcelona, Parokia ambayo ilimkaribisha Papa Leo XIV alasiri tarehe 10 Juni 2026. Papa alikuwepo huko kukutana na Mashirika ya kutoa misaada ya Jimbo pamoja na Mashirika mengine ya ustawi wa jamii katika kitongoji cha wafanyakazi cha El Raval, mji wa zamani wa Barcelona na alisikiliza ushuhuda wa wafanyakazi watatu.
Siku moja kabla ya ziara ya Papa, Padre Dennis(OSA) alizungumza na Vatican News kwamba kumkaribisha Muagostino mwingine kwa jina la Papa Leo XIV ilikuwa “chanzo cha furaha kubwa.'” Alisema yeye na wenzake ni wahamiaji na wanawahudumia wahamiaji wengine na wale wanaohitaji.
Parokia ni ya watu wenye tamaduni nyingi
“Hili ni Kanisa na Jumuiya mahalum sana, Parokia yenye tamaduni nyingi kweli huko Barcelona," Padre Dennis alielezea. "Tuna watu kutoka nchi na mataifa tofauti. Tunawapatia nafasi ya kusherehekea imani yao ya Kikatoliki na kuwa wamoja katika imani. ‘Kuwa wamoja’, kwa njia hiyo, pia ni utambulisho wetu kama Waagostinian,” alisema Padre Dennis. Aliongeza, “Chini ya Kanisa hili la Mtakatifu Agostino, tunahudumia Parokia mbili, Jumuiya ya Wafilipino na Mkusanyiko mpana kutoka asili mbalimbali. Tunahudumia jumuiya za Waamerika Kusini kama vile Wabolivia, Waperu, Waparaguay, na wengineo.”
Utamaduni na ibada
Padre Dennis anaelewa kwamba watu kutoka mataifa mbalimbali wanapokuja parokiani, mara nyingi huhisi kumbukumbu za zamani kuhusu nchi yao ya asili. “Wanapofika hapa, tunakaribisha utofauti. Tunakubali kwamba wanakosa ibada fulani, watakatifu, au sherehe za Bikira Maria kutoka nyumbani. Mara moja kwa mwezi, tunawapatia nafasi kwa ajili ya sherehe zao, ambapo wanaweza kutoa sanamu za watakatifu wanaowapenda, kuimba nyimbo zao, kucheza muziki, kusali, na kusherehekea kwa njia za kipekee kwa tamaduni zao,” alielezea.
“Jambo jingine ni kwamba, ingawa sisi ni mapadre hapa, tunajua sisi wenyewe ni wahamiaji,” Padre huyo alisisitiza. “Tunaelewa maana ya kukosa kitu kutoka nyumbani. Hicho ndicho tunachokipata hapa kwa Mtakatifu Agostino.” Padre Dennis pia aliakisi juu ya supu inayotayarishwa nyuma ya Kanisa la Mtakatifu Agostino na Masista Wamisionari wa Upendo wa Mama Teresa wa Kalkuta. Jiko hilo wakati mwingine alieleza huhudumia hadi watu 400 kila siku, na mapadre wa kiagostiani hujitolea wakati wowote wanapoweza.
Tumaini lililoongozwa na Papa Leo XIV
Alipoulizwa kuhusu matumaini yake kwa Jumuiya ya Mtakatifu Agostino baada ya ziara ya Papa Leo XIV, Padre Dennis alijibu: “Katika safari zake za kitume, Papa huonesha kila mara kwamba anawajali wahamiaji na waliotengwa.” Alisisitiza kwamba “hawa ni kaka na dada zetu wanaohitaji. Tunaweza kutoka Makanisa, mataifa, na malezi tofauti, lakini mwisho wa siku, ubinadamu ni mmoja. Natumaini kwamba ziara hii ya Barcelona itatukumbusha kwamba chochote tunachofanya kama Kanisa, hatupaswi kamwe kusahau kwamba ubinadamu ni mmoja,” alihitimisha Padre Denis.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
