Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sherehe ya Kuzaliwa Kwa Yohane Mbatizaji: Shuhuda wa Kristo Yesu

Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Watu wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu, na kuwarejesha tena katika imani ya kweli kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI aliwahi kusema kwamba jina la Yohane Mbatizaji kwa lugha ya Kigiriki “Yochanan baptistés” maana yake ni kwamba, "Mungu ni mwenye huruma na pili ni Mbatizaji. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterani, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” ni kielelezo cha upendo, msingi wa maisha ya kiroho na mawe hai ni watu wa Mungu wanaolijenga Kanisa hili. Kanisa hili ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi. Kanisa ni moja: lina Bwana mmoja, laungama imani moja tu, lazaliwa kwa Ubatizo mmoja, lafanywa mwili mmoja, lahuishwa na Roho mmoja, kwa ajili ya tumaini moja. Rej. Efe 4: 3-5, na katika utimilifu wote migawanyiko yote itashindwa. Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mungu aliye mtakatifu sana. Kanisa ni Katoliki latangaza utimilifu wa imani. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya misingi imara ya Mitume kumi na wawili. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la Kitume. Rej. KKK 866-870. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Juni, anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Huyu ni Mtakatifu pekee, ambaye Mama Kanisa anaadhimisha Siku yake ya kuzaliwa hapa duniani, ukiachilia mbali Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bikira Maria. Hizi ni nguzo msingi zinazoaminika katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Yohane Mbatizaji, alitumwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni shuhuda wa nuru, ili watu wasitembee tena gizani, watubu na kumwongokea Mungu. Waamini wanapaswa kujitahidi kumfuasa na hatimaye kufika kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hiki ni kiini cha Habari Njema inayopaswa kutangazwa kwa njia ya unyenyekevu; udugu wa kibinadamu; imani thabiti na utii kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulitegemeza Kanisa kwa nyakati mbalimbali za maisha na utume wake.

Mt. Yohane Mbatizaji: Uhusiano Mubgu na binadamu kwa njia ya Roho Mt.
Mt. Yohane Mbatizaji: Uhusiano Mubgu na binadamu kwa njia ya Roho Mt.

Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni kielelezo makini cha uhusiano wa kina kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo lilinogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5. Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Watu wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu, na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyokita mizizi yake kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo. Mtakatifu Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao. Yohane Mbatizaji akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Kristo Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye.” Mt 17: 5 Kusikiliza ni sanaa inayohitaji majiundo makini, endelevu na fungamani, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu, ili awasaidie kuwa wasikivu wema na wazuri, tayari kumwilisha kile wanachokisikia kutoka katika dhamiri zao nyofu!

Roho Mt. analitegemeza Kanisa
Roho Mt. analitegemeza Kanisa   (@Vatican Media)

Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria alama ya Roho Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana. Hili ni tukio ambalo lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji, kumwona Kristo Yesu akiwa katikati ya kundi kubwa la wadhambi kama wao, lakini kwa ajili yao, ili aweze kubatizwa na kutekeleza haki yote sanjari na mpango wa wokovu wa Mungu. Kristo Yesu akajionesha kuwa ndiye Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Yesu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji ni kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, aliyeishia kukatwa kichwa!

Ni Siku ya Maadhimisho ya Jubile ya Miaka 25 , 50, 60 ya daraja.
Ni Siku ya Maadhimisho ya Jubile ya Miaka 25 , 50, 60 ya daraja.   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waadilifu na waaminifu. Ni katika muktadha huu, Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, katika Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, Jumatano jioni tarehe 24 Juni 2026 anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na utume wa Kardinali Camillo Ruini aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 na ambaye Baba Mtakatifu Leo XIV anamkumbuka kwa: kipaji cha hekima, busara na akili, na kwamba, alikuwa ni mtu aliyejisadaka kwa ajili ya kuhudumia Injili, Kanisa sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu bila kusahau mchango wake kwa Kanisa la Italia kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Alikuwa ni chombo cha majadiliano katika ukweli na uwazi katika ulimwengu wa utamaduni. Sasa kwa sala na maombi ya Bikira Maria, Kardinali Camillo Ruini aweze kupokelewa huko mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele. Hii ni siku maalum kwa ajili ya kusali na kuwasindikiza Maparoko na Wasaidizi wao walioteuliwa hivi karibuni ili kushiriki katika kazi ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la kimisionari na kisinodi.

Kumbukumbu ya Kardinali  Camillo Ruini: Karama na mapaji
Kumbukumbu ya Kardinali Camillo Ruini: Karama na mapaji

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Jubilei ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, upyaisho wa maisha ya kiroho sanjari na ukombozi. Naye Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa ari, moyo mkuu, imani na matumaini zaidi. Ibada hii ya Misa Takatifu ni kwa ajili pia ya kuwashukuru Mapadre wanaoadhimisha Jubilei ya Miaka 25, 50, 60 na mwaka mmoja tangu wapewe Daraja Takatifu ya Upadre.

Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji
23 Juni 2026, 13:58